Sunday 5 February 2012

Shamhuna amejisahau au amejaribu ujinga?

KATIKA wadhifa wa Waziri wa Maji, Ardhi, Nyumba na Nishati anaoshikilia, Ali Juma Shamhuna amejisahau. Pengine sivyo. Yawezekana amejaribu ujinga.Ameshiriki kutunga ombi la Serikali ya Jamhuri ya Muungano bila ya kuihusisha serikali iliyompa madaraka kiutendaji – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inayoendeshwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Ombi hilo liliwasilishwa Umoja wa Mataifa 18 Desemba mwaka jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Profesa Anna Tibaijuka.
Tanzania inataka kuongezewa eneo la bahari kuu tengefu la kushughulikia harakati za kiuchumi juu ya eneo la awali la maili 200. Eneo linaloombwa limo katika maji ya Bahari ya Hindi ambayo Zanzibar inayatambua kuwa katika eneo lake la utawala.
Shamhuna mwenyewe alikiri kwenye Baraza la Wawakilishi alipotakiwa kueleza kilichotokea kwa kadri ajuavyo. Kwa sauti ya kujiamini kama ilivyo kawaida yake, alisema:
“Kama mimi waziri ndio serikali, basi nitasema serikali tumeshirikishwa. Lakini kama tafsiri ya serikali ni kwa maana ya Baraza la Mapinduzi, basi niseme hapa kuwa serikali yetu haikushirikishwa katika suala hili.”
Kweli, namna mjadala ulivyokwenda na ulivyohitimishwa, ilithibitika kuwa serikali haikushirikishwa maana BLM, nguzo yake kuu, halikujadili suala hilo. Kiutendaji, BLM ni sawa na Baraza la Mawaziri kwingineko.Laiti jambo lenyewe lingekuwa jepesi kisera na lisilokirihisha wananchi wanapolichambua, nina hakika isingekuwa kitu. Ni jambo zito. Sababu za uzito wake ni nyingi.
Kwa namna hiyo ya kutoishirikisha SMZ, Waziri Shamhuna ameridhia kuandaliwa kwa ombi linalohusu maliasili ya Zanzibar – bahari kuu. Waziri huyu mwakilishi wa jimbo la Donge, Mkoa wa Kaskazini Unguja, anajua fika – sithubutu kusema alisahau yaliyotokea mwaka 2009 – kwamba SMZ inafanyia kazi azimio la Baraza la Wawakilishi la kutaka suala la bahari kuu litolewe katika orodha ya mambo ya muungano.
Anajua kuwa bahari kuu ni moja ya maeneo matatu ambayo baada ya mjadala mrefu ndani ya Baraza yalitungiwa azimio rasmi.Azimio lilitaka serikali ichukue hatua za kuhakikisha maeneo hayo yanatolewa kutoka mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zanzibar imetaka isimamie matumizi ya maliasili hizo peke yake.
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ile iliyoundwa baada ya Zanzibar kupata uhuru 10 Desemba 1963 na mapinduzi siku 33 baadaye – tarehe 12 Januari, 1964, iliungana na Jamhuri ya Tanganyika na kuundwa jamhuri moja ya Muungano wa Tanzania.
Jamhuri hiyo ilisabiliwa mambo 11 mahsusi ya kuyashughulikia kiutendaji, yaliyokuwa yakishughulikiwa na jamhuri mbili kila moja kivyake. Baadaye orodha ya mambo haya iliongezeka. Maeneo haya matatu ni miongoni mwa yaliyoongezwa.
Ni mtizamo wa Zanzibar kuwa hatua hiyo imezorotesha kasi ya matumizi bora ya maliasili hiyo kwa umri wa muungano. Ndipo ilipokuja hoja barazani ya kuielekeza SMZ kuyatwaa ya kuyasimamia mambo hayo.Yote hayo yalitokea wakati SMZ ikiwa chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Lakini mjadala wake uliozaa azimio ulifanyika katika hali iliyothibitisha mshikamano imara wa wawakilishi wa chama hicho na wale wa Chama cha Wananchi (CUF) kilichokuwa cha upinzani.
Kama suala hilo liliunganisha wawakilishi wakati huo 2009, itakuaje kipindi hichi ambacho SMZ inaundwa na vyama hivyo kufuatia maridhiano yaliyohalalishwa kikatiba na wananchi kupitia kura ya maoni ya Julai 2010.
Na hapa ndipo Waziri Shamhuna alipaswa kupazingatia baada ya kuletewa wazo na waziri mwenzake Profesa Tibaijuka la kupeleka ombi la Tanzania Umoja wa Mataifa la kutaka kuongezewa eneo la bahari kuu tengefu la kiasi cha maili 245.
Sema alijisahau. Kwa bahati mbaya amejisahau kwa jambo alilopaswa kulijua vizuri na mapema. Hilo lilikuwa suala lililohusu wajibu wake kama waziri msimamizi wa maliasili za Zanzibar.Haitarajiwi kiongozi mkubwa katika CCM na waziri mzoefu ndani ya Baraza la Mapinduzi kama yeye ajisahau hivi.
Ingawa makosa ni kawaida kwa binadamu, na kila mtu hukosea, inakuwa kituko mtu anapojisahau katika wajibu wake. Ukweli, hilo linakuwa ni kosa la hatari. Na ukweli huo umedhihirika baraza lilipojadili hoja ya Ismail Jussa Ladhu, mwakilishi wa Mji Mkongwe (CUF), kwa wawakilishi wenzake wa CCM kumsulubu.
Sasa Shamhuna yupo katika shinikizo za kutakiwa ajiuzulu uwaziri kwa kutuhumiwa kukiuka maadili ya uongozi na kukiuka mamlaka ya serikali. Shamhuna amekiri kufahamu ombi tangu maandalizi yake, bali amekiri pia kuwa kwa tafsiri ya serikali kuwa ni baraza la mapinduzi, basi serikali haikushirikishwa. Anajua nini hasa maana ya serikali.
Sikiliza asemavyo Ali Mzee Ali, mwakilishi wa kuteuliwa na Rais (CCM): “Mheshimiwa Shamhuna amejitia kitanzi mwenyewe katika kuelezea ushiriki wake katika suala hili ambalo baraza tayari limelitolea msimamo mwaka 2009.”
Hamza Hassan Juma, mwakilishi mwingine kutoka CCM (Kwamtipura), anasema: “Inakuaje waziri anakuja hapa bila ya kuwa na msimamo juu ya masuala nyeti kama haya… inabidi ajiuzulu au rais amuwajibishe.” Katika majadiliano barazani, Hamza alitisha mamlaka aliposema, “Kama hatua (ya kumtimua) haitochukuliwa, tunaweza kutumia kifungu cha 41 kupiga kura ya kutokuwa na imani na serikali.”
Pamoja naye, wajumbe wengine waliochangia hoja ni Hija Hassan Hija (Kiwani, CUF), Mbarouk Wadi Mussa (Mkwajuni, CCM), Asha Bakari Makame (Viti Maalum, CCM), Omar Ali Shehe (Chake Chake, CUF) na Rashid Seif Suleiman (Ziwani, CUF).
Asha Bakari, aliyewahi kuwa waziri katika SMZ na sasa Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM, alisema Shamhuna anapaswa kuwajibika mwenyewe kabla ya kuagizwa na rais. Yote hayo yalianzia kwa Jussa, mwakilishi mpya na anayesifika kwa kuchokono mambo serikalini.
Aliwasilisha hoja yake baada ya kusoma taarifa za suala hilo kwenye vyombo vya habari zikimnukuu Profesa Tibaijuka, alihoji uhalali wa Serikali ya Muungano kuwasilisha ombi hilo bila ya kushirikisha Zanzibar kikamilifu na katika hali ya kupingana na azimio la baraza.
Jussa alipendekeza ombi hilo lisitishwe na iwapo Serikali ya Muungano itapuuza, SMZ iandike barua rasmi ya malalamiko na kuiwasilisha Umoja wa Mataifa. Akitoa msimamo, kiongozi wa serikali barazani, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema suala hilo litajadiliwa kwenye BLM kwa kuangalia athari za hatua hiyo ya ombi la kuongezwa kwa eneo la bahari kuu linaloihusisha Zanzibar, na kuja kutoa kauli rasmi mbele ya Baraza.
Kama wawakilishi wametishia kupiga kura ya kutokuwa na imani na serikali, ina maana hasa jambo hili ni zito na limewagusa wananchi. Ni mtihani kwa serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein
Chanzo: Zanzibar Yetu

No comments:

Post a Comment