WIKI iliyopita waziri mkuu wa zamani wa Angola Marcolino Moco, akiwa
ziarani Ureno, alimshambulia vikali Rais José Eduardo dos Santos kwa
namna anavyoyatumia madaraka yake kuwatajirisha jamaa zake. Moco
anamuelewa vilivyo dos Santos na anaujua nje ndani utawala wake.
Mbali ya kuwa waziri mkuu (1992 hadi 1996) aliwahi kwa muda wa mwaka,
kuwa katibu mkuu wa MPLA, chama kinachotawala nchini humo. Nyadhifa
hizo alizishika chini ya Dos Santos. Hali kadhalika, Moco ni katibu
mtendaji wa kwanza wa Jumuiya ya Nchi Zizungumzazo Kireno (CPLP).
Moco, ambaye bado ni mwanachama wa MPLA, alisema kwamba ayafanyayo
Dos Santos yanastahili kulaaniwa kwa sababu ni mambo ya fedheha na ni ya
kashfa.
Dos Santos si kiongozi pekee barani Afrika mwenye kushtumiwa kwa
kuyatumia vibaya madaraka yake kwa minajili ya kupora mali ya taifa au
kwa kuvitumia vyombo vya dola kwa kujitajirisha yeye na wanawe na jamaa
zake na wengine walio karibu naye.
Nchini Tanzania tumeshuhudia jinsi Ikulu ya Dar es Salaam
ilivyogeuzwa na kuwa pahala pa kufanyia biashara wakati wa utawala wa
Rais (Mstaafu) Benjamin Mkapa. Tunashuhudia pia jinsi ufisadi
unavyozidi kushamiri nchini hadi leo.
Maovu hayo ya Angola na ya Tanzania yameweza kutendwa kwa sababu ya ukosefu wa ‘utawala bora’ na kutopevuka kwa demokrasia.
Inapofuatwa kikwelikweli, demokrasia huwa ni mfumo wa serikali ya
watu, iliyoundwa na watu na kwa ajili ya watu. Tunapoutaja mfumo wa
‘serikali ya watu’ tunaikusudia serikali yenye kuwashirikisha wananchi
kupitia wabunge waliowachagua.
Tunaposema kuwa serikali ya kidemokrasia ni ile iliyoundwa na watu
tunakusudia serikali inayoendeshwa na waliochaguliwa na wale walio
wengi. Huchaguliwa katika uchaguzi mkuu.
Na tunaposema kuwa serikali ya kidemokrasia ni ile iliyopo kwa ajili
ya watu huwa tunaikusudia serikali yenye kuwatumikia wananchi.
Hadi sasa tumeizungumzia demokrasia kwa mkato.
Serikali ya kidemokrasia huhimiza na huruhusu haki za uraia kama vile
uhuru wa kusema, uhuru wa kuabudu au kutoabudu, uhuru wa kutoa maoni na
wa kushiriki katika harakati mbalimbali nchini.
Serikali aina hiyo, kadhalika, husisitiza na hulinda utawala wa sheria pamoja na kuheshimu haki za walio wachache katika jamii.
Kwa jumla, jamii inayoelezewa kuwa ni ya kidemokrasia ni ile jamii
ambamo watu wake huonekana kuwa ni sawa mbele ya serikali na mbele ya
sheria.
Yapo mengine pia katika mfumo wa kidemokrasia, kwani demokrasia si
dhana au mfumo wa kisiasa tu, bali pia ni mfumo wenye kanuni ya kiuchumi
na ya kijamii. Serikali inayofuata mfumo huo huwashughulikia wote
katika jamii, hasa walio masikini na wengine wasio na hali nzuri za
kimaisha.
Serikali hiyo huhakikisha kwamba inatoa huduma nzuri za kijamii ikiwa
ni pamoja na huduma ya afya na elimu ya bure, kuwapatia wasiojiweza
nyumba za kuishi kwa bei nafuu kama si bure. Huwa ni haki ya kila
mwananchi kupata huduma zote hizo; wananchi wote huwa ni sawa na
hawabaguliwi si kwa itikadi zao za kisiasa, za kidini, za kikabila, za
kijinsia au kwa visingizio vyovyote vile.
Nchi ya kidemokrasia huwaona raia wake wote kuwa watu walio sawa
mbele ya sheria. Na hii ina maana kwamba katika utumishi wa serikali
watu huwa wanaajiriwa serikalini kwa mujibu wa vigezo maalumu, vikiwa
pamoja na sifa za masomo na uzoefu wa kazi. Watu huwa hawaajiriwi
serikalini au kupandishwa vyeo kwa sababu ya utiifu wao wa kisiasa au
kwa sababu wamekifadhili chama kinachotawala.
Katika mfumo kama huo, ajira serikalini au katika taasisi nyingine za
umma huwa hazirithiwi wala huwa hakuna kupendeleana kwa sababu watu
wana udugu au ujamaa au usuhuba au kwa sababu muajiriwa ni mtoto wa
fulani.
Kwa ufupi, huo ndio msingi wa mfumo wa kidemokrasia.
Jingine lililo muhimu ni kwamba katika mfumo aina hiyo kunakuwa na
utenganisho wa madaraka au mamlaka kati ya Baraza la Kutunga Sheria
(Bunge), Mahakama na Serikali (Rais). Hakuna mtu mmoja pekee anayekuwa
na madaraka au mamlaka ya utendaji.
Badala yake kunakuwa na Katiba ya Kidemokrasia inayohakikisha kwamba
vyombo vya dola vina taratibu za kudhibitiana ili kuepusha matumizi
mabaya ya madaraka.
Hivyo, Bunge linakuwa na mamlaka ya juu dhidi ya tawi la Utendaji la
serikali (yaani Rais) na Mahakama yanakuwa na uhuru kamili na huwa
hayawezi kuingiliwa ama na Bunge au na Rais.
Sehemu muhimu ya mfumo aina hii ni kuheshimu haki za kimsingi za
binadamu, kama zilivyotajwa na Umoja wa Mataifa katika Tangazo lake la
Haki za Binadamu. Tangazo hilo linaharamisha kila aina ya ubaguzi na
linasema kwamba wanadamu wote ni sawa na wana hadhi sawa ya utu.
Ili kuustawisha mfumo wa demokrasia ni muhimu kwamba wananchi wawe na
uhuru wa kusema, uhuru wa kutoa maoni yao na uhuru wa kukusanyika na
kuunda vyama wavitakavyo.
Watu wasioridhika na hali ya mambo ilivyo pia wawe na uhuru wa
kueleza manung’uniko yao. Vyombo vya habari navyo lazima viwe huru
pamoja na njia nyingine za mawasiliano na visiwe vinazuiwa au vinajizuia
vyenyewe kueneza habari zisizopendwa na wakubwa.
Ikiwa hizi ndizo kanuni za kimsingi za demokrasia, basi tunaweza
kuzipima nchi na kuangalia iwapo katiba zao zinazikumbatia kanuni hizi
au la. Hili ni suala linalostahiki kutiwa maanani nchini kwa vile kuna
mchakato utaopelekea kuandikwa kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania.
Tunaweza kujiuliza maswali kadhaa. Kwa mfano, kwa kiwango gani hii
katiba ya sasa ya Tanzania inakidhi kanuni za kuifanya iwe ‘nchi ya
kidemokrasi’, na hasa katika mfumo wa Muungano kati ya Tanganyika na
Zanzibar. Kwa vile huu ni Muungano wa nchi mbili zilizo huru
inavyotakiwa ni kwamba serikali yake iendeshwe kwa msingi wa usawa baina
ya sehemu hizo mbili.
Swali jingine ni iwapo katiba ya sasa inaupa upande mmoja wa Muungano
madaraka makubwa sana kushinda upande mwingine, labda kwa sababu ya
ukubwa wake au wingi wa watu wake.
Tunaweza pia kujiuliza iwapo ni sawa katika jamii ya kidemokrasia
kuwa na Rais Mtendaji aliye na madaraka yasiyo na kikomo? Katiba ya sasa
ya Tanzania ina vifungu vyenye kumpa Rais nguvu kubwa mno bila ya kuwa
na taratibu za vyombo vingine vya dola za kumdhibiti asiyatumie vibaya
madaraka yake.
Ili kuweza kuipima nchi na kuingalia kama ni ya demokrasia changa au
ya udikteta unaoendelea itatubidi tuyaangalie madaraka ya Rais, ya Bunge
na uhuru wa Mahakama pamoja na ubora wa sheria za nchi na nguvu
zisizoshindika za taasisi za serikali, urasimu ambao unapalilia hongo na
ulaji rushwa.
Kuna kigezo kingine ambacho tunapaswa kukizingatia. Nacho ni jinsi Jumla ya Pato la Taifa (GNP) linavyogawiwa kwa wananchi.
Ni muhimu pia kuangazia jinsi fedha chafu, yaani zile zinazopatikana
kwa njia mbalimbali za kifisadi, zinavyokuwa na dhima katika uchumi wa
taifa na jinsi ‘zinavyofuliwa’ na kusafishwa kwa kuingizwa katika
uchumi.
Kwa hiyo, tukiyaangalia yote hayo tutaona kwamba demokrasia ni mfumo
wa kikatiba na wa kiserikali wenye kuhimiza pawepo maridhiano katika
siasa pamoja na utaratibu wa kuihalalisha serikali.
Tunapoutaja ‘utawala bora’ tunakuwa tunauzungumzia uhalali wa
serikali kutawala na mahusiano yaliyopo baina ya serikali na
wanaotawaliwa. Utawala bora ni sehemu muhimu ya utawala wenye kujigamba
kwamba ni wa kidemokrasia. Na ni lazima huo utawala bora uwe unakwenda
sambamba na utawala wa sheria na uwaridhishe wananchi kwamba serikali
ipo ili iwatumikie wananchi na si wananchi wapo kuitumikia serikali.
Katika jamii yenye utawala bora, serikali hupata uhalali wake kutoka
kwa wapigaji kura. Kwa hakika, uchaguzi ni kijenzi muhimu cha ‘utawala
bora’. Uchaguzi huwa unafanywa baada ya vipindi maalumu, unakuwa wa
ushindani, unakuwa wazi, na unakuwa ‘huru na wa haki’ na washindani au
wagombea wote wanapata fursa sawa. Chaguzi zinazofanywa namna hiyo
aghalabu huwa na matokeo ambayo wagombea wote huyakubali wakitambua
kwamba hakujapita mizungu yoyote wakati wa uchaguzi.
Nchi nyingi za Kiafrika zisemazo kwamba zina misingi ya demokrasia na
utawala bora zimeunda wizara au idara za serikali zenye kushughulikia
masuala haya pamoja na shughuli za kikatiba.
Wizara kama hiyo ipo Zanzibar. Huo ni mwanzo mwema; lakini si
kuanzishwa kwa wizara aina hiyo kutakoifanya nchi iwe na utawala bora au
muovu. Nchi itakuwa ni yenye utawala bora pale wananchi wake watapokuwa
na uhuru wa kimsingi, maisha mazuri na watapokuwa wanalindwa na sheria
bila ya ubaguzi au mapendeleo.
No comments:
Post a Comment