Monday 6 February 2012

Zanzibar haina hisa BOT

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ni mmoja wa wateja wakuu wa Benki Kuu Tanzania (BOT) lakini si mwanahisa, Bunge limeelezwa.

Naibu Waziri wa Fedha, Perreira Ame Silima amesema, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pia ni mteja mkuu wa BOT.

“Wateja wengine ni mabenki ya biashara yaliyopewa leseni kuendesha shughuli zake nchini” amesema Silima wakati anajibu swali la Mbunge wa Kojani, Rashid Ali Omar (CUF).

Mbunge huyo huyo alitaka kufahamu kama Zanzibar imeshawahi kupata hisa zake kupitia BOT kwa kuwa kuna taarifa kwamba, SMZ ni mteja wa mwanzo wa Benki Kuu Tanzania.

“Kifungu cha 14 (2) cha sheria hiyo iliyoanzisha Benki Kuu kinaeleza wazi kwamba ni Jamuhuri ya Muungano pekee ndiyo inaweza kisheria kumiliki hisa za Benki Kuu” amesema Silima.

Kwa mujibu wa Silima, Jamuhuri ya Muungano pekee ndiyo itakayotoa na kumiliki mtaji BOT.

Amewaeleza wabunge kuwa, BOT ilianzishwa mwaka 1965, inamilikiwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba hisa zote zinamilikiwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Mtaji ulioanzisha Benki Kuu ilipoanza shughuli zake mwaka 1966 ulitolewa na Hazina ya Jamuhuri ya Muungano na mwenye dhamana ya hisa hizo, kama ilivyo kwa mashirika yote ya umma ni Msajili wa Hazina yaani ‘The Treasury Registrar’

No comments:

Post a Comment