Hoja 18 za Baraza la Katiba, juu ya
Kwa Nini Tuujadili Muungano ni hizi zifuatazo: Tutakuwa tunawaletea hoja moja moja ili kuongeza ufahamu wa nini tufanye kama wazanzibari katika kuchangia katiba mpya ijayo
1.
Kuundwa kwake
Kuundwa kwa Muungano wa Tanzania kuna udhaifu wa kisheria kama ambavyo imeshawahi kuelezwa mara kadhaa na
wanasheria na wanasiasa kadhaa wa kadhaa. Ni Muungano ambao ulianzishwa kwa
utashi wa viongozi wawili wa kisiasa wakiwa ni Marais wa nchi mbili huru,
lakini mambo ya msingi yakiwa hayajazingatiwa.
Ni utaratibu unaokubalika
kimataifa na kisheria hata kufuatwa na nchi za Jumuia ya Madola, ambazo kwa
kuwa Zanzibar na Tanganyika zote zilikuwa kwa njia moja au nyengine chini ya
Himaya ya Uingereza, kwamba viongozi wakuu wa nchi wanaweza kuingia Mikataba ya
Kimataifa kwa niaba ya nchi zao.Hivyo viongozi wakuu wawili marais Aman abeid
Karume na Julius Nyerere wakaingia mkataba wa kuunganisha nchi zao
Utiaji huo wa saini ulishuhudiwa
na viongozi kadhaa wa kila upande wakiwamo kwa upande wa Zanzibar Ali
Mwinyigogo, Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na kwa upande wa Tanganyika
walikuwepo akina Ali Mwinyi Tambwe, Bhoke Munanka na Osca Kambona. Utiaji saini wa Mkataba wa Muungano haukuhalalisha
kukubaliwa na kuridhiwa kwa Muungano na watu wa Zanzibar.
Na ndipo Rais Abeid Amani Karume
wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar akaingia mkataba na Rais Julius Nyerere wa
Serikali ya Tanganyika, lakini ilikuwa lazima hatua hiyo ifuatiwe na ile ya
kuridhia Mkataba huo, na Mabunge ya nchi zao - hili ni sharti kwa mujibu wa
mfumo wa kisheria, lakini pia lilifanywa ni sharti ndani ya Mkataba wa
Muungano, (Kifungu cha 8) ambacho kilisema wazi kuwa baada ya kusainiwa na
viongozi hao Mkataba huo ulilazimika upate ridhaa ya mabunge ya nchi zao.
Upande wa Tanganyika ulitimiza
sharti hilo kwa kupitishwa Sheria Namba 22, 1964, ambapo nakala kivuli ya
Mkataba wa Muungano iliambatanishwa, na huku sote tunajua kuwa hadi hivi leo
nakala halisi ya Mkataba wa Muungano haijaonekana hadharani.
Nakala halisi ya Mkataba wa
Muungano imeshindwa kutolewa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, ambaye alisema
katika Hati ya Kiapo kwenye kesi Namba 20, 2005 iliyofunguliwa na Rashid Salim
Adi na wenzake katika Mahkama kuu ya Zanzibar, kwamba Serikali ya Zanzibar
haina hati halisi ya Muungano.
Bila ya shaka hili ni suala sio
tu la kushangaza lakini ni la aibu kwa Serikali kukosa kuwa na Mkataba halisi
wa kimataifa wa Muungano, na kwa hivyo si
suala ambalo linafaa liendelee kufunikwa daima dawamu.
Kama ambavyo tumesema wakati Tanganyika iliridhia Mkataba huo Zanzibar haikufanya hivyo
jambo ambalo Rais wa Pili wa Zanzibar Aboud Jumbe katika kitabu chake cha The
Partnership amesema ni mgogoro kamili wa kisheria.
Zanzibar ikiwa ndio kwanza
inatoka kwenye Mapinduzi na kusimamishwa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1963,
ilitunga Sheria iliyoitwa Legislative Powers Decree, Namba 1, 1964 ambayo
ilitoa mamlaka ya kutunga sheria kwa Baraza la Mapinduzi, na kwa hivyo Baraza
hilo la Mapinduzi lingeweza kuwa Bunge la kuridhia Mkataba wa Kimataifa
uliokuwa umetiwa saini baina ya Karume na Nyerere na sharti hilo likiwa limetajwa
kwenye Mkataba wenyewe.
Lakini watu waliokuwa na dhamana
ndani ya Serikali wakati huo pamoja na Jumbe wamesema Baraza la Mapinduzi halikuridhia
Mkataba huo. Ikumbukwe wakati huo Baraza la Mapinduzi lilikuwa na mamlaka ya
kikatiba ya kutunga sheria.
Wolfgang Dourado, aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kwa wakati huo, kauli yake ni hiyo hiyo na zaidi
ananukuliwa akisema hivyo katika Mkutano wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika
(TLS) 1985, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Baraza la Mapinduzi kwa wakati huo, Salim Rashid amesema katika Hati ya Kiapo
kwenye kesi ya Rashid Salim Adi na Wenzake kuwa Mkataba wa Muungano
haukuridhiwa na Baraza la Mapinduzi.
Halafu pia msomi anaeheshimika
katika uwanja wa Katiba, Professa Issa Shivji amethibitisha kupitia vitabu
vyake viwili kile cha 1990 Legal Foundations of the Union of Tanganyika and
Zanzibar na kile cha 2008 Pan-Africanism
or Pragmatism. Lessons of the Tanganyika-Zanzibar Union kuwa hakuna
pahala popote pale ambapo Mkataba wa Muungano inaonyesha umeridhiwa na mdau wa
pili yaani Zanzibar.
Ila bila ya shaka hoja inakuja
kuwa hakuna ambae amechukua hatua moja mbele ya kusaili uhalali wa Muungano
ambao unakosa sifa muhimu na awali kabisa ya kuridhiwa au tuseme kwa usahihi
zaidi kukosa kuridhiwa na upande mmoja na kwa hivyo ukaruhusiwa kusonga mbele
hadi leo.
No comments:
Post a Comment