Na Ahmed Rajab
KUFIKIA mwanzoni mwa mwezi wa Aprili mwaka 1964, kama miezi mitatu
baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, mambo Visiwani humo yalikuwa shwari.
Hali ya kisiasa ilikuwa thabiti na hivyo mazingira ya kijamii nayo
yalikuwa mazuri.
Mandhari ya kisiasa ya wakati huo yalikuwa ya kimapinduzi. Hata
steshini ya Redio ya Serikali iliacha kupiga nyimbo za taarab
zilizokuwa na maudhui ya kimapenzi. Badala yake ikipiga nyimbo kuwaenzi
wakwezi na wakulima na nyingine kuhusu Mapinduzi ya Januari 12, 1963.
Serikali ya Mapinduzi, ikiongozwa na Sheikh Abeid Amani Karume,
ilikuwa Serikali iliyokuwa na umoja. Wakati huo ilikwishaanza kuchukua
hatua mbalimbali zilizokuwa na lengo la kuleta usawa katika jamii.
Hatua hizo, zikiwa pamoja na kutoa huduma bure za afya na elimu bure
kwa watoto wote na kutaifisha ardhi, ziliwavutia wananchi wengi wa
kawaida katika nchi nyingine za Afrika ya Mashariki.
Iwapo kuna wataosema kwamba hatua hizo hazikufanikiwa, ni swali
jingine. Ukweli ni kwamba hatua hizo zilizitia homa serikali fulani.
Haikustaajabisha kwamba mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12 wanajeshi
waliasi nchini Tanganyika (Januari 20), Uganda (Januari 23) na Kenya
(Januari 24). Uasi huo haukushangaza kwa vile serikali za nchi hizo
hazikuonyesha ari ya kuchukua hatua kama zile za Zanzibar ambazo
zingewanyanyua watu wao.
Lakini labda waliotishika zaidi walikuwa wakubwa wa serikali za
Kimagharibi. Pamoja na mengine walitishika na jina jipya la ‘Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar.’ Nchi hiyo haikuwa Jamhuri tu ya kawaida baada ya
kuondoshwa usultani lakini ilijitambulisha rasmi kuwa ni ‘Jamhuri ya
Watu wa Zanzibar.’
Kulikuwa tofauti kubwa kiitikadi kati ya nchi iliyokuwa ikijiita
‘Jamhuri’ na ile iliyokuwa ikijinata kuwa ni ‘Jamhuri ya Watu.’
Isimu hiyo ya pili ikitumiwa na serikali zilizokuwa zikijigamba
kwamba zinatawala kwa maslahi ya wengi wa watu wao. Kinyume na Zanzibar
lakini nyingi ya serikali hizo zikifuata itikadi ya kisiasa ya Kimarx
na Kilenin au ya Kikomunisti.
Kufikia mwanzoni mwa Aprili 1964 wengi wa Wazanzibari walikuwa
wamekwishayakubali Mapinduzi kuwa ni kudura ya Mungu. Watu wakiendelea
na shughuli zao kama kawaida.
Vituko vya watu kufukuzwa kazini kwa sababu za kikabila au za
kisiasa vilizuka baadaye pamoja na visa vya kamatakamata na misiba ya
mauaji.
Serikali ikiwapeleka nchi za nje kwa masomo ya juu wanafunzi wa kila
kabila na ikiendesha shughuli zake kwa nidhamu. Hakukuwa na segemnege
katika uendeshaji wa vyombo vya dola.
Ingawa mazingara yalikuwa tofauti na yale ya serikali
iliyopinduliwa, watumishi wakuu wa serikali waliiendesha nchi kwa
mujibu wa sheria zilizokuwapo na mpya zilizotungwa na Baraza la
Mapinduzi.
Hali hiyo iliyodumu kwa muda mfupi iliwafanya wengi wawe na
matumaini na mustakbali wa taifa lao jipya. Leo tukikaa na kuipima hali
ya mambo ilivyokuwa hatuoni ushahidi kwamba utawala wa Karume
ulikabiliwa na kitisho kikubwa cha kutaka kuuangusha.
Sisemi kwamba hakujakuwako watu waliokuwa wakiiapiza serikali yake
na waliokuwa wakiomba isambaratike au ipinduliwe moja kwa moja.
Walikuwepo. Lakini nguvu zao za kuandaa mapinduzi ya kuyapinga
Mapinduzi ya Januari 12 zilikuwa dhaifu. Hakuna mpinga Mapinduzi
aliyethubutu kufurukuta wakati huo.
Tarehe Aprili 13 Karume alimwambia Katibu wa Baraza la Mapinduzi,
Salim Rashid, kwamba Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Tanganyika,
alimpigia simu akimtaka ende Dar es Salaam. Siku ya pili yake Karume na
Salim Rashid wakafunga safari kwenda kwa Mwalimu.
Walipofika Ikulu, Dar es Salaam, Mwalimu huku akimuangalia Salim
Rashid aliwaambia wasaidizi wake: ‘Mpeni gari (Salim) akanyoe ndevu.’
Ni wazi kuwa Nyerere hakutaka Katibu wa Baraza la Mapinduzi asikie
aliyokuwa amepanga kumwambia Karume. Ndipo Salim Rashid akashika njia
kwenda kwa kinyozi akimuacha Karume na Mwalimu. Mbali ya Marais hao
wawili hakuna mtu anayejuwa kwa uhakika nini hasa kilijiri kati yao
sebleni Ikulu.
Kuna wanaoshikilia kwamba Nyerere alimtisha Karume kwa kumwambia
kulikuwa na njama za kumpindua na kwamba muungano wa nchi zao utampa
himaya.
Na kuna wasemao kwamba wakati huohuo Nyerere alisema atawarejesha
kwao askari polisi 300 Wakitanganyika waliokuwa na silaha na
waliopelekwa Zanzibar kusaidia kuzuia fujo.
Miaka michache kabla ya hapo Karume aliwahi kutaja nia yake ya
kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika na kuifanya iwe jamhuri. Kauli
hiyo, aliyoitoa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na iliyoripotiwa
kwenye gazeti la Mwongozo la chama cha Zanzibar Nationalist Party
(maarufu kwa jina la Hizbu), ilimchongea baadaye amuangukie na kumtaka
radhi sultani wa wakati huo Seyyid Khalifa bin Haroub.
Ingawa tangu hapo Karume alikuwa na ndoto ya Muungano wa Zanzibar na
Tangayika hatujui akitaka uundwe kwa masharti gani au uwe wa aina
gani. Tunachoweza kufikiria ni kwamba matamshi ya Nyerere ya Aprili 14
yalimtia hawafu kubwa Karume kiasi cha kumfanya ampe mwenzake
aliyemzidi akili uhuru kamili wa kuziunganisha nchi zao.
Aliporejea Zanzibar Karume aliwaficha memba wenzake wa Baraza la
Mapinduzi alichokubaliana na Nyerere. Siri ya Muungano ilikuwa yake
peke yake Zanzibar. Hakulishauri Baraza la Mapinduzi, hakuishauri
serikali wala hajakishauri chama cha Afro-Shirazi Party (ASP).
Wadadisi na wataalamu wengi wenye kuitalii kwa kina historia ya
Muungano wanaamini kwamba ingawa Nyerere alikuwa mtetezi wa umoja wa
Afrika na ingawa Karume alikwishadokeza kwamba angependelea Zanzibar na
Tanganyika ziungane, Muungano ulioundwa Aprili 26 mwaka 1964
uliandaliwa ili kuliridhia matakwa ya dharura ya Marekani.
Wakati huo Marekani kwa kweli ilikuwa hamnazo, majununi kabisa,
kuifikiria Zanzibar kuwa ngome ya ukomunisti upande wa Afrika ya
Mashariki na kitisho kwa maslahi yake. Marekani ikawa mbioni kutafuta
njia au mamba wa kuyameza Mapinduzi ya Zanzibar.
Siku tatu au nne baada ya huo mkutano wa siri wa Marais wawili
Karume alipelekewa Hati za Muungano kutoka Dar es Salaam. Hati hizo
alikabidhiwa Ikulu ya Zanzibar na aliyekuwa waziri mdogo wa mambo ya
kigeni wa Tanganyika.
Hii leo mustakbali wa Zanzibar uko njia panda kama ulivyokuwa pale
Karume na Nyerere walipoziunganisha nchi zao. Lakini hali halisi za
Aprili 1964 na za leo zimebadilika sana. Hii ni kwa sababu kwanza
hali ya ndani ya Zanzibar kwenyewe imebadilika; pili, mahusiano yake na
nchi zilizo ngeni kwake yamebadilika na tatu, mazingara ya ulimwengu
pia yamebadilika.
Mnamo Aprili 1964 mustakbali wa Zanzibar uliamuliwa kwa njama
zilizoandaliwa na Marekani pamoja na madola mengine ya Kimagharibi,
ambayo tunaweza kuyabandika lakabu ya ‘wapishi wa kimataifa’. Mpishi
mwengine alikuwa jirani Tanganyika.
Kama inavyokumbushwa mara kwa mara Muungano uliopo leo sio ule
ulioelezwa na Hati za Muungano, zilizokuwa na mambo 11 tu ya Muungano.
Kwa muda wa miongo kadhaa Zanzibar ikiachiwa ijiendeshe yenyewe.
Kwa mfano, ilikuwa na uhuru kamili wa kisiasa toka 1964 hadi 1972 alipouliwa Sheikh Karume.
Kwa upande wa uchumi serikali za Zanzibar ziliendelea kuwa na uhuru
kamili mpaka ilipoingia ile ya awamu ya tano ya Rais (Mstaafu) Salmin
Amour. Serikali hiyo ilishindwa nguvu na shinikizo za Bara. Ikabidi
isalimu amri na kuchanganya sera yake ya fedha pamoja na kodi na ushuru
na ile ya Bara (yaani ya serikali ya Muungano).
Tukiuzingatia umoja walio nao Wazanzibari na matarajio yao kwa
Serikali yao ya Umoja wa Kitaifa, halitokuwa la ajabu iwapo mchakato
utaopelekea kupatikana kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania utayathibitisha matakwa yao.
Matakwa hayo yatabainika watapotoa maoni yao kwenye Tume ya Katiba
na yataonyesha kuwa wengi wao watataka pawepo Muungano wa Mkataba na si
wa Katiba.
Ushahidi kwamba hali ya mahusiano ya Zanzibar na Muungano ni tofauti
na ilivyokuwa zamani ni ile migogoro isiyokwisha kati ya pande hizo
mbili. Shtuma zilizoko Visiwani ni kuwa Serikali ya Muungano yenyewe
ndiyo inayoianzisha migogoro hiyo, kama kwa mfano kwa kuandikiana
mikataba na jumuiya za kimataifa kwa niaba ya Zanzibar au kwa kuwa na
makubaliano ya kibalozi kwa niaba ya Zanzibar na madola ya nje, mfano
Norway.
Serikali ya Tanzania haina haki ya kufanya hivyo hata ikiwa sekta
zote zinazohusika za utawala ziko chini ya mamlaka yake. Na hivyo sivyo
ilivyo. Tena haina haki hiyo kwa sababu mfumo wa Muungano uliopo sasa
si wa kudumu kwa vile kuna huu mchakato wa kuamua kuhusu majaaliwa ya
Muungano wenyewe pamoja na mfumo wake na katiba yake.
Wakuu wa Bara watapata taabu Zanzibar na huenda hata wakahatarisha
usalama endapo watajaribu kushikilia kwamba mfumo uliopo sasa wa
Muungano uendelezwe kama ulivyo.
Hatimaye tukumbuke kuwa ulimwengu nao pia umebadilika. Tujuavyo,
tena kwa uhakika, ni kuwa kinyume na mwanzoni mwa 1964 hii leo nchi
kadhaa za Kimagharibi ziko tayari kuiunga mkono Zanzibar ikiwa itadai
mamlaka yake kamili kutoka Serikali ya Muungano. Tumeyadaka haya
faraghani yakidondoka kutoka ndimi za wanabalozi wa nchi fulani
wasiotaka kutajwa.
Chanzo: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment