Thursday 31 January 2013

SMZ yashtuka idadi ya watu kuongezeka kwa kasi

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imewasisitiza Wazanzibari kutumia uzazi wa mpango ili kupunguza idadi ya watu ambayo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku katika visiwa vya Zanzibar.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakati akiufunga Mkutano wa 10 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Ukumbi wa Baraza hilo uliopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Sensa ya 2002, Zanzibar ilikuwa na watu wapatao 980,000 na katika Sensa iliyofanywa mwaka jana 2012, ambapo ni miaka kumi baadaye, Zanzibar imekuwa na idadi ya watu 1,303,560 jambo ambalo Baloazi Seif alisema Serikali inapaswa kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa wananchi wake.
“Mheshimiwa Spika ongezeko ni watu 323,560. Hili ni ongezeko kubwa sana. Hatuna budi sasa tufanye maarifa ya kupunguza kasi ya kuzaliana ili watoto wetu tuwalee vizuri zaidi,” alisema Balozi Seif mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Balozi Seif alisema idadi hiyo ya watu iliyoongezeka Zanzibar, Serikali haina budi kuwa na mipango madhubuti ya kudhibiti ongezeko la kasi la idadi hiyo ya watu na hivyo kushauri kuongeza bidii katika kufanya kazi na kuzalisha kwa wingi bidhaa zitakazokidhi mahitaji ya watu wake ndani na kupata ziada ya kuuza nje ya nchi.
Alisema wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar jumla ya miradi 53 ya maendeleo iliwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa yenye thamani ya wastani wa Sh97 bilioni katika sekta ya elimu, maji safi na salama, afya, kilimo, uvuvi na miundombinu ya habari, mawasiliano na barabara.
“Hii ni hatua kubwa ya maendeleo ambayo nchi yetu imepiga katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Nachukua nafasi hii kuwashukuru kwa dhati viongozi katika ngazi zote na wananchi wote kwa kushirikiana katika kufanikisha sherehe zetu hizi adimu ambazo zilifana sana,” alisema.
Akizungumzia suala la sheria zinazotungwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa nia ya kuwatumikia wananchi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwasihi watekelezaji wa sheria hizo wazisimamie na kuhakikisha kuwa zinatekelezwa ipasavyo bila ya kumuonea haya au aibu mtu yeyote atakayezikiuka sheria hizo

No comments:

Post a Comment