WANANCHI wa kijiji cha Chwaka, Kusini Unguja
wamewaomba Rais Jakaya Kikwete na Dk Ali Mohamed Shein, kushughulikia
suala la Katiba ili kuweza kuirejeshea Zanzibar mamlaka yake kamili kama
ilivyokuwa kabla ya kuungana na Tanganyika.
Ombi hilo lilitolewa juzi kwenye mkutano wa wazi wa
Baraza la Katiba Zanzibar (BAKAZA) wakati likitoa elimu ya Katiba kwa
wananchi wa kijiji hicho. Huo ni mfululizo wa Baraza hilo katika kutoa
elimu ya Katiba kwa wananchi wa Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano huo mmoja wa Wazee wa
Chwaka, Fadhil Mussa Haji alisema suala la kuunganisha nchi lilifanywa
na watu wawili, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume na wote hawapo tena.
Alisema ni jukumu la viongozi waliopo madarakani kulishughulikia suala
hilo.
“Mwalimu Nyerere na Mzee Karume waliunganisha nchi
kwa kuamua wao wenyewe na kisha Mzee Karume akaja uwanjani kutuuliza
mnakubali union watu wakaitikia…kwa kuwa alijua hakuna atakayeweza
kupinga kwa wakati ule,” alisema na kuongeza:
”Lakini sisi hatujakubaliana na hayo tokea wakati
huo…sasa kilichobaki tunamuomba Rais Kikwete na Rais Shein wao ndio wapo
madakarakani waturejeshee mamlaka na hadhi ya Zanzibar,” alisema Mzee
Fadhil, huku akishangiriwa na vijana waliohudhuria mkutano huo.
Mzee Fadhil alisema yapo baadhi ya mambo ambayo
yameingizwa katika orodha ya mambo muungano bila ya ridhaa ya
Wazanzibari, lakini baadhi ya mambo Wazanzibari wenyewe walishiriki
kuizamisha nchi yao kutokana na tamaa na kupenda madaraka, jambo ambalo
alisema hivi sasa linawafanya wajute:
“Ni sisi wenyewe tumefanya na tumetaka tutendewe
hivi kwa sababu sisi tulikuwa tumeshapata uhuru wetu hapa mwaka 1963
lakini ni Wazanzibari wenyewe wakaleta mapinduzi na kuukataa ule uhuru
halali,” alisema na kufafanua:
”Sasa tunasema hizi tamaa na kupenda madaraka sasa
hivi ndivyo vitu vinavyotuadhibu sote katika nchi yetu kwa tamaa za hao
wachache waliyokuwa wakituamulia,” alisema Mzee Fadhil.
Alitoa mfano kwa viongozi wa Wazanzibari
walivyojikaanga kwa mafuta yao wenyewe: “Ni tamaa ndizo zilizosababisha
nchi kutokuwa na hadhi na mamlaka kamili ya kujiamulia mambo yake,”
alisema Mzee Fadhil.
Alisema ni tamaa ndiyo zilizofanya kuporwa mamlaka
kamili ya Zanzibar na hivyo kubakisha nchi kukosa uwakilishi hata kwa
yale mambo ya Zanzibar, ambayo sio ya muungano yanavyokosa uwakilishi wa
Wazanzibari katika nchi za nje:
”Wakati umefika sasa kwa kila mmoja kufahamu kwamba
mamlaka ya Zanzibar yanahitaji kuheshimiwa na kupiganiwa na kila raia
ili hadhi ya Zanzibar irudi,” alisema Mzee Fadhil.
Akitoa maoni yake alipendekeza Katiba mpya iweke
bayana mamlaka ya Zanzibar na rais wake, kwani alisema hivi sasa rais wa
Zanzibar, hana hadhi ya kweli kama itakiwavyo kwa rais wa nchi.Chanzo: Mzalendo
No comments:
Post a Comment