Wednesday 16 January 2013

‘Kidau nipeleka Pemba, nina haja nako’

HUKU kwetu Uswahilini kabla ya kuja kwa vyombo vya kisasa vya mawasiliano na yale yaitwayo siku hizi ‘majukwaa ya kijamii’ watunzi wa mashairi au nyimbo walikuwa na dhima kubwa katika jamii. Wao ndio waliojitwika kazi ambayo leo hufanywa na waandishi.
Washairi walikuwa wakitangaza mambo au kupinga mambo yawe mema au mawi. Ilikuwa ni kazi yao kuhadharisha palipohitajika kutolewa indhari, kunasihi palipopasa kutolewa nasaha, kuwakosoa watawala na hata kuwatukana au kuwaapiza maapizo yalipolazimika.
Si mara zote wakinusurika. Nao pia yakiwasibu yanayowasibu waandishi wa leo. Wakipingwa na kuzomewa; mara nyingine wakipigwa na hata kufungwa gerezani.
Mombasa tu kuna mfano wa Suudi bin Said Al-Maamiriy (1810-1878) aliyewahi kufungwa kwa kuandika mashairi yaliyomuunga mkono mpiganiaji uhuru Mbaruku bin Rashid Mazrui. Kifungo cha gerezani hakikumrudisha nyuma Suudi kwani alipofunguliwa aliendelea na harakati zake.
Kwa mfano huo tunaona jinsi washairi wa kale wa Uswahilini walivyokuwa na sifa ambayo kila mwandishi wa leo anahitajika kuwa nayo — sifa ya ushujaa wa kutowaogopa watawala. Sifa ya kuisema kweli japokuwa hiyo kweli yawauma watawala.
Bila ya shaka, kama ilivyo kwa baadhi ya waandishi wetu wa leo kuna baadhi ya washairi wa zama za kale waliokuwa wakinunuliwa na watawala. Ufisadi haukuzaliwa jana.
Hao waliokuwa wakinunuliwa walikuwa ni wachache na hawakumbukwi kama wanavyokumbukwa waliokuwa na ujasiri wa kuisema kweli na waliokuwa wakifuatwa kama wanavyofuatwa waimbaji wa kileo wa muziki wa ‘pop’.
Kuna mfano mwingine. Huu ni wa ushujaa wa mshairi wa Pate, Ali Koti, ambaye alipojitosa katika siasa za Pate hakuchelea kumkosoa mfalme mpya na viongozi wenzake waliompindua Sultani wao.
Mifano hiyo imetajwa na Abdurrahman Saggaf Alawy (Maallim Saggaf) na Ali Abdalla El-Maawy kwenye Dibaji ya kitabu kiitwacho Kale ya Washairi wa Pemba: Kamange na Sarahani. Kitabu hiki kimechapishwa na shirika la uchapishaji la Mkuki Na Nyota la Dar es Salaam. Kimehaririwa na Abdilatif Abdalla, gwiji wa mashairi kutoka Mombasa na mshairi wa Sauti ya Dhiki. Mhariri ametupatia lulu kwa Utangulizi wake wenye kutufunza mengi.
Kale ya Washairi wa Pemba ni mkusanyiko wa mashairi ya Kamange na Sarahani, washairi wa Kipemba waliokuwa wakivuma hadi Unguja na pwani za Tanganyika na Kenya.
‘Kamange’ alikuwa Ali bin Said bin Rashid Jahadhmiy (1830-1910) aliyezaliwa Bogowa, Pemba, na aliyekuwa na lakabu nyingine ya ‘Basha-Ali.’ Lakabu hii ilitokana na cheo cha ‘Basha’ (Pasha) kilichokuwa kikitumika katika majeshi ya Misri na Uturuki.
Sarahani alikuwa Sarahani bin Matwar bin Sarahan al-Hudhry, Hinawy (1841-1926) aliyezaliwa Pondeyani, Chake Chake, Pemba. Sarahani alimpiku Kamange kwa usomi kwa vile pamoja na kubobea katika masomo ya kidini, historia ya Kiislamu na fasihi pamoja na historia ya fasihi ya Kiarabu alijifunza Urudhi (kaida za Ushairi) na Qawafi. Kadhalika alijifunza elimu ya Unajimu.
Sarahani pia alikuwa shekhe aliyekuwa akipigapiga mbizi katika falsafa kama mshairi mwengine wa Pemba, Nassor Muhammad Jahadhmy (Kichumba) ambaye kwa utaalamu wake wa historia akipenda kutoa mifano yake kutoka historia ya Ukristo, ya Yemen na ya Misri.
Asili za koo za washairi Kamange na Sarahani ni Omani lakini ziliingia Uswahilini miaka mingi sana iliyopita, zikaoana na Waswahili na vizalia vyao vikawa ni Waswahili.
Kamange na Sarahani wakipenda kutaniana na kujibizana hata watu wakifikiria kwamba wanagombana. Ukweli ulidhihirika alipokufa Kamange pale Sarahani kwenye ubeti mmoja wa kuomboleza kifo cha mwenzake alipoandika:
“Twali tukitukanana, watu wasitudhaniye
Kama hawa wapatana, ya ndani tusiwambiye
Kufurahisha fitina, kusudi watuzomeye
Naliya leo sinaye, ya mawadda na swafawa.”
Hawa ni washairi ambao zama zao Washairi wa Pemba waligawika mapande mawili: pande la Kamange na la Sarahani. Kamange ndiye aliyekuwa malenga na shaha; mshindani wake alikuwa mmoja tu, Sarahani.
Baadhi ya mashairi ya Kamange yanamuibuwa kuwa ni mtu aliyekuwa tayari ilipohitajika kuwakaripia na kuwapinga wakuu wa serikali. Alikuwa heshi kusuguana roho na wakuu wa Pemba. Aliwapinga kwa mwendo wao mbaya wa ubadhirifu wa mali ya umma na kwa kula rushwa.
Katika shairi lake ‘Doriya Kapatikana!’ lililokuwa likimsema na kumlaani Doriya, askari wa gereza Kamange alisema:
“Naende mbele afike, Pemba asirudi tena
Jamii wanusurike, yawaondoke mahana
Khuduma waitumike, pasiwe kusukumana
Doriya kapatikana, naende mbele afike…
Hajuwi Pemba peremba, haufai ujagina?
Mashumu yakikukumba, haukutoki mdhana
Nenda kamwulize Simba, dola ilivyombana
Doriya kapatikana, naende mbele afike…”
Kamange alikuwa pia stadi wa mashairi ya mapenzi. Katika shairi ‘Muwacheni Anighuri’ anakisifu hivi kichwa cha mwanamke:
“Kichwa chake mviringe, ndiyo mwanzo wa khabari
Hakuumbwa vungevunge, kama hawa khantwiri
Hana pazi hana tenge, sawasawa mdawari
Muwacheni anighuri, ndiye Badii Jamali.”
Serikali ya kikoloni ilipopiga marufuku uwindaji na ikatoa hukumu ya viboko 50 kwa apatikanaye anawinda, Sarahani akijua kwamba Kamange akipenda kuwinda, alimpelekea ubeti ufuatao:
“Mwenye kuondowa miko, ilani tumeletewa
Ni khamsini viboko, na mnyoo akatiwa
Basha uwinja hauko, natule vya kununuwa
Ndege wamerufukuwa, wawinja tahadharini!”
Kale ya Washairi wa Pemba kinawazungumza pia washairi wengine wa kale ya Pemba miongoni mwao wakiwa akina Bahemedi wa Sinawi (Hemed bin Seif Al-Ismaily), Ruweihy (Bwana Muhammad bin Juma Al-Kharusy) na Hemedi bin Khatoro.
Kitabu hiki kinawazindua wenye kuidhania Pemba kuwa ni debe tupu kifasihi, kwamba haina urathi wa ushairi wa kupigiwa mfano. Chaonyesha jinsi ushairi wa Pemba, kwa lahaja ya Kipemba, ulivyo na ladha ya aina yake ingawa washairi wa Pemba walikuwa na tabia pia ya kuchanganya Kipemba na lahaja nyingine kama za Kimvita, Kiamu, Kimrima, Kivumba na kutumia maneno yenye asili ya Kiarabu.
Kiswahili chetu kimeporwa. Walokipora sasa watamba kwamba wao ndio wenye kuitamalaki lugha hii. Wanajipurukusha na kujitia kusahau kwamba Kiswahili kina wenyewe na kina mila na utamaduni wake.
Maallim Saggaf na El-Maawy wanatukumbusha kwenye Dibaji yao kwamba: “Ushahidi wa kihistoria waonyesha wazi kuwa pwani ya Afrika ya Mashariki kulikuwa na Waswahili kabla ya kuzaliwa Nabii Isa...”
Swali wanaloliuliza na wanalohoji kuwa lahitaji utafiti zaidi ni: nani aliyewaita watu hao ‘Waswahili’, na lugha yao ‘Kiswahili’ na utamaduni wao ‘Uswahili’? Inavyoonyesha hawaridhiki kwamba asili ya ‘Swahili’ ni neno la Kiarabu saahil, yaani pwani
Raia Mwema

No comments:

Post a Comment