Tuesday 29 January 2013

Misri yarejesha mabilioni ya dola ya mafisadi yaliyofichwa nje ya nchi

CAIRO WAKATI Serikali ya Tanzania ikiendelea kupiga kimya katika kuwashughulikia mafisadi papa ambao wamebainika kuficha mabilioni ya dola za kimarekani katika mabenki ya Uswisi, Serikali ya Misri tayari imeshaanza kutaifisha na kurejesha mabilioni ya dola yaliyokuwa yamefichwa na viongozi wa enzi za utawala wa Hosni Mubarak. Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali ya Misri amesema kuwa, nchi yake imefanikiwa kurejesha dola bilioni moja na milioni mia nane za serikali ya nchi hiyo zilizokuwa zimeporwa na viongozi wa utawala uliong’olewa madarakani nchini humo.

Adel al Saeed, alibainisha kuwa vyombo vya sheria vya Misri bado vinaendelea na uchunguzi wake dhidi ya mafisadi na wale wote waliopora mali za Baitul Maal, wakati wa utawala wa Hosni Mubarak. Aliongeza kuwa uchunguzi uliofanywa kuanza Februari 2011 hadi 31 Oktoba mwaka huu, umeweza kubaini na kukusanya dola bilioni moja na milioni mia nane zilizoporwa na Hosni Mubarak, familia yake, na idadi kadhaa ya mawaziri na wafanyabiashara wakubwa nchini humo.
Amesema kuwa serikali ya Cairo inaendelea kuwasiliana na nchi nyingine kwa njia za kidiplomasia lengo likiwa ni kuzuia na hatimaye kurejeshwa mamilioni ya dola ambayo yalitoroshwa na viongozi wa zamani wa nchi hiyo. Utawala wa kiimla, ufisadi uliokithiri na ukandamizaji dhidi ya wananchi wa Misri ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha wananchi wa Misri kuanzisha harakati za kuiondoa mamlaka ya Hosni Mubarak
Chanzo: Annur

No comments:

Post a Comment