Sunday 20 January 2013

NANUSA HARUFU YA ‘GEORGE ORWELL’ MCHAKATO WA KATIBA

Riwaya ya Shamba la wanyama (1945), ni moja kati ya kazi nzuri kabisa za kibunifu katika Tasnia ya fasihi andishi hapa duniani. Riwaya hii ambayo iliandikwa na Muingereza ambaye ni maarufu kwa jina la George Orwell, ni mtiririko wa sitiari (allegory) unaoakisi dhana nzima ya ujamaa wa kidemoskrasia katika tawala mbali mbali za kidunia.
Kazi hii yenye ubora, ladha na mvuto usiochosha, inahusu kisa cha dola la wanyama. Wanyama ambao kwa pamoja walikubaliana kuungana na kuishi kwa misingi ya usawa na haki. Moja kati ya kanuni hizo za usawa, ilikubaliwa kwamba hakuna mnyama mmoja atakemdhuru mnyama mwengine ama kwa kumla, kumpiga, kumdhulumu na hata kumuuwa. Kanuni hii ilipita na ikaandikiwa kauli mbiu (slogan) isemayo ‘Wanyama wote ni sawa’!
Kwa muda baada ya kanuni hii kupitishwa na kukubaliwa na wanyama wote, wanyama wadogo wadogo na wale waliokuwa waathirika wa vitimbi, viteweji na mateso ya wanyama wakubwa, walihisi kupata faraja kubwa kwa kuhakikishiwa usalama wao. Imani yao hii ilichangiwa na kuona kauli ile mbiu ikiimbwa na kuandikwa kila kona ya dola lao lile kiasi ya kumfanya kila mnyama aamini kile anachokiona katika kauli mbiu ile.
Waswahili husema ‘Taa haachi mwiba wake’. Haikutimia wiki, kuna baadhi ya wanyama hasa ndege, walianza kuona dalili mbaya katika jamii yao. Moja ya dalili hio ni kupotea kwa baadhi ya wanyama katika mazingira ya kutatanisha. Kwa lugha nyepesi, kuna baadhi ya wanyama walianza kuwala wengine kimya kimya kila siku.
Wanyama wadogo walipogundua usaliti huu walirudi kwa mkubwa wao kushitaki na kusimulia masikitiko yao juu ya kitendo hiki cha uvunjifu wa amani, na usalama wa wanyama katika dola yao. Kwa bahati mbaya walipofika mahala pa mashtaka na kueleza makosa yao, waliona ile kauli mbiu imebadilishwa kidogo kutoka ilivyokuwa mwanzo.
Awali kauli ilisomeka ‘Wanyama wote ni sawa’, lakini sasa inasomeka ‘Wanyama wote ni sawa, lakini baaadhi ya wanyama, ni sawa zaidi kuliko wengine’! Kisa hichi kikaishia hapo. Kumalizika kwa kisa hiki ndipo tunapopata nadharia hiyo niliyoitumia katika kichwa cha makala hii hapo juu, ambayo ni moja ya nadharia maarufu duniani kwa sasa. Yaani nadharia ya ‘Ki-Orwelli’.
Nimewajibikiwa na kuandika kwa kusema kuwa kwa namna mchakato mzima wa maoni ya katiba unavyokwenda, nanusa harufu ile ile waliyoinusa wanyama wadogo kama mimi katika ‘Shamba la wanyama’. Harufu ya kwamba kuna baadhi ya wanyama ni sawa kuliko wengine. Na hii si tuhuma kutoka katika ombwe la uwazi, bali ina kila aina ya ithibati na visherehesho vya kuutilia shaka mapema mchakato huu wa katiba nchini.
Nilitegemea iwapo maoni ya katiba yalilenga kukusanya maoni ya wananchi, kwa haki na usawa, na ili yanipe imani kuwa haki itatendeka, basi yalikuwa yafanywe kwa wanachi wote bila kuweka tabaka (strata/ social classes). Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika mchakato wa katiba, wananchi wote, wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo, viongozi na waongozwa, mashehe na mapadiri, wanasiasa na majeshi, wote kwa pamoja ni wananchi walio sawa. Na mchakato wa katiba ulikuwa uanze na kauli mbiu hiyo ya ‘ Wananchi wote ni sawa mbele ya haki na sheria’!
Kuwe na usawa kwamba, maoni ya katiba yafanyike kama vile tunavyofanya uchaguzi. Yapitie kimajimbo au maeneo ya ukazi wa wananchi. Sasa maoni yakifika jimbo ambalo kiongozi mkuu wa nchi au mstaafu anapoishi, basi hio ndio iwe zamu yake ya kwenda kutoa maoni hapo kwao. Kwa mfano, ikiwa Rais wa Zanzibar anaishi Mbweni, basi maoni yakifika jimbo la eneo hilo, iwe ndio zamu yake ya kutoa maoni na wananchi sawia, ijapokuwa atapewa nafasi ya kwanza kufanya hivyo, lakini utaratibu uwe hivyo.
Na nilitegemea iwe hivi kwa watu wote nchi nzima. Wa Bagamoyo akatowe maoni kwao, alie Dar es Salaam atatoa maoni hapo jimboni kwake, alie kambini kwa jeshi bila shaka kambi hio haiko angani, aende jimbo ilipo kambi hio akatoe maoni. Na kwa mpangilio kama huu angalau tungeweza kuamini kwamba mchakato wa katiba una sura ya usawa na hivyo haki haichezi mbali.
Lakini ni jambo la kushangaza sana kuona tume ya Katiba inapitia majumbani mwa viongozi na wastaafu, wizara, idara, na mashirika ya Serikali, na halafu pengine hata taasisi za kidini, ili kukusanya maoni. Utaratibu huu unaleta matabaka kwa wananchi. Na asili na maumbile ya mfumo wa kitabaka duniani dumu daima hautendi haki. Huu ndio uhalisia wa nadharia na mifumo yote ya kitabaka duniani.
Kwa mujibu wa mwenendo wa mchakato huu wa katiba unavyoendeshwa, wa kuanza kijumba hodi, unaonesha wazi kuwagawa wananchi na kuwafanya wasiwe sawa mbele ya haki. Binadamu ni mtu aliemumbwa na fikra, akili, na maarifa. Unapomleta mtu kama Mkapa jimboni kutoa maoni na wanachi wengine, hata akizomewa, watu watahisi kuwepo kwa usawa. Na unapompa siku yake pekee tena nyumbani kwake, unaanza kuuumba dudu moja baya mno la ubaguzi na ngazi refu ya utabaka baina ya wananchi na wakubwa wao.
Taswira inayojengeka machoni mwa wananchi hivi sasa, kwa tume kuanza kupitia watu binafsi majumbani kukusanya maoni yao, eti tu kwa sababu ni wakubwa, haina mustakabali mzuri. Haina kwa sababu tafsiri iko wazi ya utaratibu kama huu. Iko wazi hata kwa kujiuliza swali dogo tu. Hivi kweli maoni waliyotoa wananchi wote wa Zanzibar, yanawezajae kuyapindua maoni aliyoyatoa Mkapa na Mwinyi? Sipati picha!
Yaani, hivi kweli maoni ya wananchi wa kawaida yatasikilizwa bora kwa kulinganisha wingi wao kuliko ukubwa na maoni ya wenye cheo, kauli, na nguvu katika nchi hii? Hili si kweli, maana tumeona katika chaguzi nyingi hapa nchini, ambapo sauti ya wananchi walio wengi ikipinduliwa na kauli ya mtu mmoja. Hili liko wazi kama sabuni ya mche!
Na ndio hapa ninapoona kuwa ile kauli mbiu isemayo ‘Watu wote ni sawa mbele ya haki na Sheria’ ikibadilika na kusomeka ‘Watu wote ni sawa mbele ya haki na sheria, lakini baadhi ya watu, ni sawa zaidi kuliko wengine’. Kwa hali hii naanza kukosa imani na kutawaliwa na ruwaza za nadharia ya ‘Ki-Orwell’ ninapautazama mchakato mzima wa katiba hapa nchini unavyokwenda.
Chanzo: Mzalendo.net

No comments:

Post a Comment