Wednesday 23 January 2013

Umoja wa Ulaya na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Leo tunaendelea na mjadala wetu kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa muktadha wa kutazama muundo wa Umoja wa Ulaya (EU).
Kama tunavyofahamu kuwa Umoja wa Ulaya si Muungano wa Kikatiba, ni wa mkataba ambao haujavunja zile dola za nchi wanachama.
Umoja huo umekubaliana kuwa na baadhi ya mambo katika ushirikiano wao ambapo wameunda vyombo vya Umoja ikiwemo Halmashauri ya Ulaya.
Halmashauri hii ni mkutano wa Wakuu wa nchi na viongozi wa Serikali za nchi wanachama. Wanakutana mara mbili kwa mwaka na kutoa maazimio muhimu.
Nafasi ya Urais wa EU hubadilika kila baada ya miezi 6, ifahamike kuwa Urais uliokusudiwa hapa si ule wa dola kwa maana ya ukuu wa nchi.
EU pia ina Baraza la Mawaziri ambapo ni katika yale mambo tu waliyokubaliana kushirikiana kwa pamoja ndiyo hukutana kupanga mipango ya utekelezaji katika Mataifa yao.
Tofauti kubwa ni kwamba katika Muungano wa Kikatiba kwa mfano wa Tanganyika na Zanzibar kuna Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo linajumuisha mawaziri wote wa SMT wanaosimamia mambo ya Muungano na yasiyokuwa ya Muungano.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ni mjumbe katika baraza hili. Hapa napo kuna msongo wa kazi kwa mfano ni wakati gani Baraza la Mawaziri inajadili mambo ya Muungano na yasiyokuwa ya Muungano kwa kutumia baraza hilohilo?
Wenzetu wa EU wana Kamati ya Ulaya ambayo majukumu yake ni kusimamia utekelezaji wa maazimio ya Halmashauri na Bunge ambayo ina makamishna 24 na mwenyekiti. Ingawaje inaonekana kama ni Serikali, lakini haimo hasa katika mfumo wa Serikali kwa maana haina madaraka.
Chombo kingine cha Umoja wa Ulaya ni Bunge la Ulaya ambalo lina wabunge 732 wanaochaguliwa na wananchi. Ikiwa muundo wa Muungano wetu utakuwa katika mfumo wa aina hii malalamiko mengi ya upande mmoja kuona unaonewa hayatakuwepo.
Hii haina maana kwamba ndiyo matatizo hayatakuwepo, lakini kwa sehemu kubwa utakuwa si kama muundo wa sasa wa Serikali mbili ambao tume zote zilizoundwa na Serikali zimeukosoa kwa kushauri kutafutwa kwa muundo muafaka wenye kufaa.
Tazama tatizo la msingi la mfumo wa muundo katika utekelezaji wa mambo ya Serikali, kwa mfano, Katiba ya Tanganyika imelindwa kwenye mkataba wa Muungano na pia ilipaswa kuwepo na Serikali yake, pamoja na viongozi wake kuwepo na kusimamia mambo yasiyo ya Muungano.
Tunaona pia Katiba na sheria za Tanganyika ndizo zilizotakiwa zitumike katika eneo la Tanganyika kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano kwa upande wa Tanganyika kama ambavyo Katiba na sheria za Zanzibar zinavyotumika katika eneo la Zanzibar kwa yale mambo ambayo si ya Muungano.
Watanganyika wanaodai Tanganyika yao wana hoja katika hili maana licha ya kufutwa kwa Serikali hiyo, lakini kuendelea kutambua kuwepo kwa sheria zisizo za muungano ni kutambua kuwepo kwa mamlaka ya Tanganyika ambako sheria hizo kwa mambo yote yasiyo ya Muungano ziliendelea na zinaendelea kutumika hadi leo kwa Tanzania Bara.
Kwa mfano kifungu cha 3 (1) cha Provisional Transitional Decree kinatajwa kuwa ni miongoni mwa kero pale kilipohalalisha wafanyakazi wa iliyokuwa Serikali ya Tanganyika kugeuzwa kuwa watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Utaona hali hiyo katika kifungu cha 6 (i) cha Decree kinasema mara tu baada kuanza Muungano, Mahakama ya Tanganyika na Majaji wake wote nao watakuwa ndiyo Mahakama na Majaji wa Jamhuri ya Muungano kinyume na Makubaliano ya Muungano. Mpaka leo Katiba zote mbili hazitambui Mahakama kama ni suala la Muungano. Nembo ya Tanganyika inatumika kama nembo ya Serikali ya Muungano na Idara ya Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika inachukuliwa kama Idara ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano.
Kwa mifano hiyo michache utaweza kubaini udhaifu wa msingi wa mfumo wa muundo wa Muungano ambao bila shaka kama utafanyia marekebisho kwa kutafuta mfumo mujarab utaondoa zile zinazoitwa kero za Muungano.
Hoja ya waumini wa muundo wa Muungano wa mkataba inaonekana kuwa na nguvu zaidi hasa wakiitazama Umoja wa Ulaya ambao umepata mafanikio na kufanya Mataifa mengine ya Ulaya ambayo hapo awali hayakuwa wanachama kuweza kujiunga.
Leo Umoja huo una nguvu kubwa kiuchumi, tumeona wakati wa msukosuko wa kifedha kama Taifa la Ugiriki lilivyokuwa katika hali mbaya na linavyosaidiwa na wanachama wenzake wa EU hasa Ujerumani.
Ingawa ziko Tume zilipendekeza muundo wa Serikali tatu, lakini yafaa kukumbuka kuwa tatizo si idadi ya Serikali, tatizo ni muundo au maumbile yake Muungano huu ambao kiasi kidogo unafanana na ule wa Marekani na Uingereza.
Imeelezwa mara nyingi juu ya ripoti ya Tume ya Jaji Nyalali iliyosema muundo muafaka wa Muungano ni Serikali tatu.
Jaji Mstaafu Francis Nyalali, alieleza wazi katika ripoti yake kuwa muundo wa Serikali mbili una matatizo mengi, muundo muafaka ni wa serikali tatu.
Wakubwa ndani ya CCM walipokutana Mjini Dodoma wakasema haiwezekani kutekeleza maoni ya Tume, lakini kwa ushauri uleule, Tume ya Jaji Robert Kisanga nayo ikaeleza udhaifu wa muundo wa Muungano, lakini kama ilivyo kwa mtangulizi wake, Tume ya Kisanga ikaambiwa hapana sera ya Chama Cha Mapinduzi hazibadiliki.
Ni muhimu kuelewa kuwa msingi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukujengeka kwa sababu ya hisani ya kisiasa, kiuchumi kiutamaduni au jiografia pengine utashi wa utawala, lahasha. Huu ni mkataba wa Kimataifa kama ilivyo mikataba mengine ambayo Washiriki wote wana haki sawa.
Mapenzi ya haki hufanya maisha kuwa matamu hasa ikiwa haki yenyewe mtu huweza kuifahamu na kusadiki. Ni vigumu sana kuijua haki pasipo kuitenda na watu wengine hawawezi kufaulu kwa sababu ya kupuuza haki na ukweli.
Haki na kweli ni sawa na watoto pacha, mtu na awe na wingi wa akili wa kushinda mchwa, lakini iwapo ana mazoea ya kupuuza mambo mawili haya, basi anafanya ujinga ulio mkubwa wa fikra na fahamu.
Kuelekea kwenye mchakato wa kutoa maoni katika Tume ya Katiba ni lazima kila mtu kuheshimu haki na uhuru wa mwingine si vyema kubeza maoni ya wengine, kama unatofautiana kimtazamo salia na wako waache wengine waeleza mitazamo yao.
Chanzo: Rai

No comments:

Post a Comment