Na Salma Said
TUME ya mabadiliko Katiba mpya nchini Tanzania, imeelezwa kuwa Baraza la
Mapinduzi halikushauriwa wala kushirikishwa katika Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar, uliyoundwa Aprili 26, 1964.
Wanasiasa wakongwe waliyokuwa katika Serikali ya Mapinduzi, wakati wa
kuundwa kwa Muungano huo, Bw Salum Rashid na Bw Hassan Nassor Moyo waliiyambia
Tume hiyo, walipokuwa wakitoa maoni yao Maisara, mjini Zanzibar.
Katika maoni yao walisema: Tangu awali ya kuundwa Muungano huo,
kulikosekana uhaliali wake, licha ya kuwa umedumu kwa miaka hamsini huku kukiwa
na malalamiko kadhaa ya wananchi.
Wakizungumza kwa pamoja, Wanasiasa hao waliunga mkono kuwepo kwa Muungano,
lakini walishauri mfumo mpya wa Muungano wa Mkataba, ili kila nchi kuwa na
mamlaka yake kamili:
“Kwa hali ilivyo miaka 50 ya Muungano kushindwa kutatua mambo mbali mbali,
mfumo pekee unaofaa kwa sasa na kwa kizazi hiki ni Muungano wa Mkataba.
Utaratibu wake utajulikana baadae,” walisema Wanasiasa hao.
Bw Moyo alisema Serikali ya Muungano, isiogope maoni ya wananchi kwani kwa
takriban miaka 50 matatizo ya Muungano yameshindwa kutatuliwa na njia pekee kwa
sasa ni kukubali kubadilisha mfumo wa Muungano huo:
“Tukiwa na mfumo mpya wa Muungano, utakwenda sambamba na wakati huu ambao
idadi kubwa ya wananchi wameamka na kuona kuna matatizo katika Muungano wetu,”
alisema Bw Moyo.
Bw Moyo ni Waziri wa kwanza wa Sheria wa Serikali ya Muungano, na Bw Salum
Rashid alikuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi.
Kwa pamoja walishauri kuwepo kwa Muungano lakini walisisitiza, ili
kuimarisha Muungano kwa nchi zote mbili, ni kusikilizwa kwa maoni ya wananchi
ambao wanataka aina mpya ya Muungano wa Mkataba:
“Sisi ndiyo tulikuwa na dhamana wakati ule na tulitakiwa tuunganishe
Serikali kwa kuimarisha udugu na kuimarisha uchumi wetu, bahati mbaya sasa kuna
kero, mimi siziiti kero naita ni matatizo, ni wakati wake kuondoshwa” alisema na
kubainisha:
“Msimamo wangu ni Serikali ya Mkataba na ndiyo ninavyoamini na naamini
kwamba huu muungano tuliyonao ni Muungano wa Mkataba, hili siyo jambo jipya,
Mwalimu Nyerere na Mzee Karume walitia saini ya Mkataba,” hili sio jambo jipya,”
alisisitiza Mzee Moyo.
Bw Moyo alitaka kurudishwa kwa utaratibu wa zamani, ili Rais wa Zanzibar
aendelee kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, akimaanisha Muungano huo ni
wa Tanganyika na Zanzibar.
Naye, Katibu Mkuu wa Kwanza wa Baraza la Mapinduzi, Bw Salum Rashid ambaye
alikuwa Dar es Saalm na Mzee Karume siku ya kusainiwa Mkataba wa Muungano,
alisisitiza kuwepo kwa Muungano wenye maslahi kwa wananchi wa nchi zote
mbili:
“Serikali ya Muungano isiwe na woga wa kuvunjika kwa Muungano. Hilo sio
jambo kubwa na wala siyo jambo geni, baadhi ya nchi za Afrika ziliwahi kuungana,
na Muungano ukavunjika,” alisema na kufafanua zaidi:
“Sioni jambo zito kuvunjika kwa Muungano, mbona Muungano wa Senegal na
Gambia ulivunjika na wote walikuwa ni wanachama wa Umoja wa Afrika na hakuna
jambo lolote lililotokea,” alisema Bw Salum Rashid.
Alisema wananchi wanaotaka Muungano wa Mkataba, hawamaanishi kuvunja
Muungano, bali wanataka mfumo mpya wa Muungano ili kuirudishia Zanzibar, mamlaka
na madaraka yake kamili.
Alisema ifahamike kwamba, kuwa nje ya Serikali siyo sababu ya kuwa ni fursa
ya kuzungumza hayo, lakini wakati ule likizungumzwa suala la Muungano, ilikuwa
inaonekana ni uhaini:
Alisema kwa sasa haiwezekani tena kuburuzwa na hasa vijana. Hivyo matumaini
yake kwa tume hiyo ni makubwa: “Naamini watafanya kazi zao kwa uadilifu mkubwa
na maoni ya wananchi ambayo wameyatoa kwa Tume, yatatekelezwa,” alisema Bw Salum
Rashid.
Alisema Muungano wa Mkataba ndiyo sahihi kwa sasa na hakuna sababa ya
viongozi kuogopa hilo, Wazanzibari na hasa vijana wanataka nchi yao kuwa na
mamlaka kamili.
Bw Moyo na Bw Rashid wote wawili kwa pamoja wamewatoa hofu Wazanzibari
kuhusu utendaji wa Tume hiyo, na walisema wanaiamini kwamba itafanyakazi yake
kwa uadilifu, bila upotoshaji.
Tume hiyo inayongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba na Katibu wa
Tume, Assa Rashid tayari imeshachukuwa maoni ya baadhi ya viongozi wakuu, pamoja
na Marais wastaafu wa Seriakli ya Zanzibar.
Viongozi waliyokwisha toa maoni yao ni pamoja na Makamo wa Kwanza wa Rais
Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Rais Mstaafu Dk Salmin Amour, Dk Amani Abeid
Karume na baadhi viongozi wengine wa Serikali ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment