Wednesday 23 January 2013

Mishahara hewa yaitesa Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ) katika kukabiliana na wimbi la wafanyakazi hewa imekusudia kufanya uhakiki kwa baadhi ya taasisi zake za ulinzi ili kujua idadi kamili ya watumishi wake.
Hali hiyo imekuja kufuatia matukio ya ubadhirifu wa fedha na kukabiliana na tatizo la kulipa mishahara kwa watumishi hewa.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheri wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM), Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua Serikali imekabiliana vipi na tatizo la mishahara hewa kwa kikosi cha KMKM.
Katika swali lake, Jaku alisema kwamba katika kikosi cha KMKM Serikali inalipa watumishi hewa waliostaafu zaidi ya Sh18 milioni kwa mwezi jambo ambalo linaipa Serikali wakati mgumu wa kutoa mishahara isivyo stahiki.
Akijibu swali hilo Waziri Kheri alikiri kuwapo kwa ubadhirifu huo ambao umegunduliwa kutokana na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu wa Hesabu za Serikali na ambapo kwa sasa tukio hilo linafanyiwa kazi na wahusika. ”Waheshimiwa tumepokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu upotevu mkubwa wa fedha za umma katika Kikosi cha KMKM ambao hulipwa wastaafu hewa...Hatuna wasiwasi na taarifa ya mkaguzi, lakini ripoti hiyo hivi saa inafanyiwa kazi,” alisema waziri huyo.
Alisema ni marufuku kwa watumishi wa umma kulipwa fedha wakati wanapostaafu utumishi wa umma serikalini na kitendo hicho ni kinyume na sheria za utumishi wa Serikali na kuwataka watu ambao wanawatambua wenye kufanya hayo waripoti.
katika vyombo vya sheria.
Akijibu swali la nyongeza la mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake (CUF), Omar Ali Shehe aliyesema kwamba zipo taarifa katika Kikosi cha Mafunzo tatizo kama hilo lipo, Kheri alisema Serikali itafanya ukaguzi wa taasisi zake vikiwamo vikosi maalumu vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment