Thursday 31 January 2013

Tanesco yaidai Zanzibar mabilioni

Shirika la Umeme Zanzibar, (Zeco) linadaiwa Sh. bilioni 22.6 na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Hayo yalielezwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya kuchunguza Hesabu za serikali na Mashirika ya Umma (PAC) Ali Omar Shehe, alipokuwa akiwasirisha ripoti maalum ya kuchunguza utendaji wa Zeco.

Alisema kabla ya kufanyika mazungumzo baina ya Wizara ya Ardhi Makazi, Maji na Nishati Zanzibar na Wizara ya Nishati na Madini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, jumla ya deni lilikuwa la Sh. Bilioni 62.3 hadi mwaka 2010.

Mwenyekiti huyo alisema baada ya mazungumzo ya Viongozi wa pande mbili za Muungano waliafikiana kuwa Serikali ya Muungano itasadia kulipa Sh. bilioni 39.7 kupunguza mzigo wa deni hilo.

Shehe ambaye Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake, alisema baada ya deni kupunguzwa, Zeco inatakiwa kulipa Sh. bilioni 3 kwa mwezi kupunguza deni la matumizi ya umeme.

Shehe alisema kwamba viwango vya umeme vimeathiri Zeco kwa kiwango kikubwa na kushindwa kumudu kulipa gharama deni kwa muda mwafaka.
Chanzo: Nipashe

No comments:

Post a Comment