Wednesday 30 January 2013

Ufisadi Watikisa Zanzibar


KWA mara nyingine watu wa Zanzibar wameshitushwa na habari za ubadhirifu mkubwa wa fedha uliogunduliwa na Kamati ya Baraza la Wawakilishi katika uchunguzi wake wa Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).
Kwangu mimi hili ni jambo la kawaida, ila ninashangaa kuwa kimepita kipindi kirefu kidogo tokea mara ya mwisho kusikika habari za aina hii, za baadhi ya watu kuchezea wanavyotaka fedha na mali za serikali na taasisi zake.
Nasema hivi kwa sababu bado haijaonekana kwa vitendo watu wanaofanya ufisadi na kuitia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi kuwajibishwa kisheria.
Panapotokea vishindo vya kuwabana wanaodaiwa kuhusika na ufisadi basi wanaokabwa ni dagaa na wale mapapa kubaki wakielea habarini.
Watu hawana wasiwasi kama vile fedha walizochezea ni zao au za familia zao. Huku ndiko kutesa kwa zamu.
Machi mwaka jana, Kamati ya Kuchunguza Mahesabu ya Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) ya Zanzibar ilionya kuwa ingeliwapelekea mahakamani baadhi ya watendaji wakuu wa serikali na wahasibu ifikapo Mei wale waliokiuka sheria za matumizi ya fedha za serikali.
Sasa ni karibu mwaka mmoja na hakuna aliyefikishwa mahakamani kwa wizi au ubadhirifu wa fedha za umma uliogunduliwa wakati ule.
Hii ilitokana na PAC kuona kwamba ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali iligundua kuwa miradi mingi iliyokamilika ilikuwa hailingani na fedha zilizotumika.
Ripoti ile ilieleza kuwa yapo magari ya serikali yaliodaiwa kuwa mabovu, lakini ukweli ni kwamba huo ulikuwa mradi wa kuiba vipuri.
Katika mambo yaliyogunduliwa wakati ule ni kwamba katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2008-09 fedha za masurufu zilizopotea zilikuwa sh mibilioni 5.1.
Mambo mengine yalikuwa na sura ya ufisadi uliokithiri na unaonuka yaliyoelezwa katika ripoti ile ni pamoja na :
Malipo ya dola 94,000 za Marekani yalifanywa bila ya kuwepo stakabadhi.
Fedha zilizopotea katika mikataba ni sh milioni 413.6, vifaa vingi vilinunuliwa na baadhi ya ofisi za serikali bila kutumia zabuni.
Tulielezwa na baadhi ya watu kuamini (si mimi) kwamba PAC haitakuwa tena na muhali au kumuonea huruma mtu yeyote aliyeiba au kutumia vibaya fedha za serikali.
Hivi sasa tunapewa hadithi mpya ya ubadhirifu unaosemekana kufanyika ZECO, lakini ukweli ni kwamba kilichofanyika ni kuendeleza utamaduni wa kuiba na kuvuruga fedha za umma. Wapo wanaosema fedha za umma hazina mwenyewe na ukizipata ni sawa na zile za kuokota! Hivyo ni haki kuzichota.
Tunaambiwa kuwa miongoni mwa madudu yaliyogunduliwa katika Shirika la Umeme ni haya yafuatayo:
Kuwapo tofauti ya malipo kati ya kazi zinazofanana na baadhi ya malipo yaliyopo kwenye risiti yanatofautiana na malipo halisi.
Wapo wateja wanaotumia umeme bure na hawamo kwenye orodha ya shirika. Ipo tofauti kubwa ya ada za malipo zinazotozwa kwa wanaounganishiwa umeme na majina ya watu wanaodaiwa kufaidika kutajwa.
Yupo mteja (ametajwa jina) anayedaiwa kuungiwa umeme wa njia tatu na kuonesha kuwa amelipa sh milioni nane wakati mtu huyo anadai amelipa sh milioni 37, lakini kwenye akaunti ya mtu binafsi.
Benki moja inasemekana kuwa ilitozwa sh 3,718,000 kuungiwa umeme, lakini vifaa hasa vilivyotumika kwa kazi hiyo vina thamani ya sh milioni 14.
Baadhi ya wateja, zikiwamo hoteli za kitalii, hawamo kwenye orodha ya malipo ya shirika, nguzo feki zimetumika kuunga umeme, mafaili ya wateja wakubwa 147 yamekosekana.
Ipo kampuni iliyokodishwa mnara na haijawahi kulipa tangu ilipokodishwa. Hakuna maelezo yanayoeleweka juu ya ununuzi wa jenereta 32 ya akiba ya shirika yaliyopo hapo Mtoni. Hapakuwepo na zabuni za ununuzi wa majenereta haya.
Kwa kweli yapo madudu mengi katika ripoti hii na tuhuma zilizoambatanishwa na madai haya ya ufisadi ni nzito na zinaunguza kuliko huo umeme wenyewe.
Ni mahakama tu, kama ipo huru na inaachiwa kufanya kazi yake inayotarajiwa kufanya, ndiyo inayoweza kutoa uamuzi wa haki na ukweli kujulikana. Inawezekana pia tuhuma hizo ni majungu, lakini mahakama ndiyo itakayosema kama ni jungu au sufuria.
Lakini kwa Zanzibar ninayoijua, labda ibadilike kama ilivyo kwa usiku na mchana, hili suala litamalizikia hewani kama lile la kugunduliwa zaidi ya wafanyakazi hewa 3,500 katika serikali miaka mitatu iliyopita.
Kikwazo kikubwa kilichopo ni utamaduni wa kulindanana na kuwaonea muhali watu wanaosemekana wamewiba fedha za umma na kuharibu mali za serikali.
Mafisadi huonewa huruma kama vile wameiba kwa bahati mbaya na rungu la dola siku zote huwaaangukia wanaoiba embe, ndizi, chapati na mandazi au kutoa kauli za kisiasa, kama juu ya Muungano, zisiowafurahisha wakubwa.
Tuliwahi kuambiwa katika miezi ya mwisho ya utawala wa Rais Amani Abeid Karume kuwa Zanzibar haina mafisadi na kwamba viongozi wake ni wasafi na sasa tunaendelea kuuona usafi huo wa viongozi!
Ukweli ni kuwa ufisadi unanuka Visiwani na kama maelezo yaliyotolewa na Kamati ya Baraza la Wawakilishi yana ukweli basi ufisadi uliopo unatisha.
Tusijidanganye na kutaka kuwafanya malaika viongozi wetu na watumishi wa ngazi za juu wa serikali. Wapo miongoni mwao ambao ni wezi wakubwa na wabadhirifu na haifai kuwafumbia macho wala kuwazibia masikio.
Tuache kulindana kwa mambo maovu kwani watu wazuri ni wale wanaolindana kwa mema na si uchafu. Mwenendo huu wa kuwalinda mafisadi utaiponza Zanzibar.
Ukiangalia matokeo kama ya wakubwa kudaiwa kupora mali, ardhi na mashamba ya watu na hata kuua, japokuwa si kwa makusudi, utaona wanakingiwa kifua na kulindwa.
Kwa bahati mbaya waandishi wa habari wanaofichua haya kwa kuwapa nafasi ya kusikika wale wanaodai kudhulumiwa huandamwa kama wao ni wahalifu na hata kuhatarishiwa maisha yao.
Sasa waandishi wa habari wamekaa pembeni na kupumua huku wakiiangalia kwa masikitiko Zanzibar inakwenda mrama na badala yake wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wapo mbele kufichua ufisadi.
Sijui kwa uoza huu ulioanikwa katika Baraza la Wawakilishi serikali itasemaje au itachukua hatua gani kwa wanaotuhumiwa au vyama vyao vitaambiwa wawashughulikie wawakilishi wao walioweka mambo hadharani.
Tunasubiri kitakachotokea na wakati ndio utatupa jawabu. Maskini Zanzibar. Au sasa ndiyo tuseme Zanzibar ni njema, atakaye aibe?
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment