Saturday 27 October 2012

Safu mbili zinazoihujumu serikali ya ubia Zanzibar

NOVEMBA 5 Wazanzibari wataadhimisha kutimu miaka miwili tangu iundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kabla ya hapo Wazanzibari walikuwa wamegawanyika vibaya sana. Hakuna asiyetambua hatari iliyokuwepo siku hizo. Walikuwa haweshi kuzozana kisiasa. Athari ya mzozano wao ni madhara makubwa yaliyotokea katika historia ya karibuni ya nchi yao.
Kwa hakika, mzozano huo si wa jana wala juzi. Ulianza kuchomoza mwaka 1957 pale siasa zilipokuwa zinachacha na watawala wa kikoloni wa Kingereza walipoanzisha mfumo wa siasa za vyama vingi.
Mikwaruzano na mifarakano ya kisiasa iliendelea na kusababisha Mapinduzi ya mwaka 1964. Baada ya Mapinduzi hayo haikuchukua muda Zanzibar ikapoteza mamlaka yake kamili ilipoungana na Tanganyika mwezi wa Aprili mwaka huo wa 1964.
Wakati huo Mapinduzi yalikuwa ya moto lakini yalikuwa bado machanga na hayakutimia hata umri wa Siku Mia Moja. Ndiyo maana kuna wenye kuhoji kwamba Mapinduzi hayo yalinyimwa fursa ya kujiimarisha na kujizatiti ili yaweze kuyatanzua matatizo ya muda mrefu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yaliyokuwa yakiwakabili Wazanzibari.
Moja ya mambo yenye kusikitisha katika historia ya karibuni ya Zanzibar ni kwamba Mapinduzi ya nchi hiyo, ambayo katika siku zake za awali yalitangaza kanuni za kupigiwa mfano za kutaka kuleta usawa na maendeleo kwa Wazanzibari wote, yaliachiwa yapoteze dira na yapotoke.
Serikali ya Muungano, kwa upande wake, iliyakodolea macho tu Mapinduzi na vitimbi vya upotovu vya viongozi wake. Wakati wote huo Serikali ya Muungano haikuchukua hatua yoyote na wala haikuonyesha dalili ya kutaka kufanya chochote kile kuizuia hali ya uonevu na ya utawala mbovu isizidi kuwa mbaya.
Matokeo yake ni kwamba Mapinduzi yalikwenda kombo na yakapotea njia. Hii ndiyo sababu kwa nini hadi hii leo, katika kipindi cha takriban nusu karne, malengo Mapinduzi ya kuleta usawa na maendeleo hayakuweza kutimizwa.
Ni jambo lililo wazi kwamba Wazanzibari wamepata hasara kubwa kutokana na mgawanyiko na mfarakano wao. Ubishani na uhasama wa kisiasa uliendelea kwa muda mrefu mno na kama nilivyokwishagusia, uliidhuru sana Zanzibar. Kwa kweli hali hiyo ya kutokuwako suluhu ya kisiasa ndiyo iliyochangia pakubwa kuifanya Zanzibar iwe kama ilivyo hii leo.
Hivi sasa imekuwa ni nchi yenye uchumi uliodidimia kwa vile uchumi huo ulitupwa kwa miaka na mikaka bila ya kushughulikiwa ipasavyo na bila ya kusimamiwa inavyostahiki. Miaka yote hiyo watawala walipuuza kuwa na mikakati endelevu ya kuupanga na kuukuza uchumi. Matokeo yake yakawa kuanguka kwa viwango vya utendaji kazi katika nyanja zote za utawala na uendeshaji wa sera za kijamii.
Tunapoiangalia hali ya zamani ndipo tunapoweza kuiona hasa thamani na tija ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika nchi iliyokuwa imegawika kama Zanzibar. Serikali aina hiyo ni ya mfumo wa kuwa na ubia katika madaraka ya serikali na hivyo kumfanya kila Mzanzibari ahisi kwamba anashirikishwa katika serikali na anakuwa mtiifu kwa serikali hiyo.
Hali kama hii iliyoko sasa Visiwani haijapatapo kuwako kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hakujawahi kuwako utiifu kama huo kwa serikali kabla ya kuundwa kwa hiyo serikali ya ubia kwani tangu siasa za vyama vingi zirejee Visiwani, takriban nusu ya wakazi wa Zanzibar wakinyanyaswa, wakibaguliwa na wakitengwa na serikali au wakionekana kuwa ni ‘maadui wa taifa’ ambao lazima wadhibitiwe na wagandamizwe.
Hali ya mambo hii leo Zanzibar ni tofauti sana na ilivyokuwa zamani. Hii leo Zanzibar ina serikali iliyoviingiza ndani yake vyama vyote vikuu nchini humo yaani Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF). Matokeo yake ni kupatikana umoja miongoni mwa Wazanzibari na pia utulivu wa hali ya kisiasa. Yote hayo mawili ni mambo adhimu na yanabidi yaendelezwe, yakuzwe na yaimarishwe ili Wazanzibari waweze kutimiza malengo yao.
Kuna jambo moja ambalo ni muhimu kukumbuka. Nalo ni kwamba hii Serikali ya Umoja wa Kitaifa isingaliweza kuundwa bila ya kupatikana maridhiano yaliyoondosha uhasama baina ya vyama vikuu vya kisiasa Visiwani. Kwa hili, ile Kamati ya Maridhiano ya Wazanzibari sita iliyolisuka suluhisho mwanana la Kizanzibari kwa matatizo ya Kizanzibari inastahiki kupewa sifa maalumu katika historia ya karibuni ya Zanzibar.
Maridhiano haya hayakuwa matokeo ya kauli ya asilimia 65 ya Wazanzibari waliyoyaridhia katika kura ya maoni lakini ndani ya CCM yalipata ‘baraka’, kama isemwavyo siku hizi, za Mwenyekiti wake Jakaya Kikwete.
Bila ya shaka maridhiano hayakuuyayusha kabisa kabisa uhasama wa kisiasa uliokuweko. Kama tukitaraji hayo yatokee katika kipindi kifupi kama hiki basi tukitaraji miujiza. Mabaki ya uhasama huo yangaliko. Lakini juu ya kuzuka kwa mikwaruzano ya kisiasa ya hapa na pale, kwa jumla Wazanzibari hii leo wana umoja wasiowahi kuwa nao kwa muda mrefu sana.
Wengi wao wenye kuuonja uhondo wa amani na utulivu hawakubali tena kubabaishwa au kutiwa fitna na kuletewa tena migawanyiko ya kuwafanya wananchi wawe na utengano. Kadhalika, juu ya rabsha za hapa na pale kwa jumla Zanzibar hii leo ni kisiwa cha amani.
Wazanzibari wanatambua umuhimu wa kuhakikisha kwamba amani na hali ya utulivu inaendelea kudumu ili waweze kufanikisha juhudi zao za kupigania pawepo na mfumo mpya wa ushirikiano kati ya Zanzibar na Tanganyika wakati wa mchakato wa sasa wa kuitunga upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Hawatoweza kamwe kuyapata matlaba yao bila ya kuwa watu wamoja waliosimama pamoja na wenye kuamini kwamba kuwa watiifu kwa nchi yao na kuyapigania maslahi ya nchi yao ni jambo la wajibu na lililo muhimu na adhimu kushinda utiifu kwa chama chochote cha kisiasa au itikadi yoyote ya kisiasa.
Kuhusu suala hili, Wazanzibari wanaelewa vilivyo kwamba ikiwa hali ya amani itachafuliwa basi hali ya ndani ya nchi haitokuwa tulivu wala imara na itaitia nchi yao jina baya ulimwenguni. Kwa hakika, hali hiyo itakwenda kinyume na maslahi ya Zanzibar kwani baadhi ya watu wataanza kuwa na shaka ikiwa Zanzibar yenye mamlaka yake kamili itaweza kuhifadhi amani na hali ya utulivu na wakati huohuo kuwapatia Wazanzibari maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii.
Kwa hivyo, katika kuuadhimisha mwaka wa pili wa uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni muhimu Wazanzibari wa itikadi tofauti za kisiasa wahakikishe tena kwamba wamejitolea kuyatetea Maridhiano pamoja na umoja wao wa pamoja. Hizo ndizo nguzo mbili zitazowawezesha kutimiza lengo lao la kuwa na Muungano wa aina mpya na Tanganyika.
Kwa hili pia Wazanzibari wako macho na wanatambua kwamba kuna vitimbakwiri ndani na nje ya nchi wenye nia ya kuwababaisha wasishiriki kikamilifu katika mchakato unaoendelea wa kulipatia taifa katiba mpya. Zoezi hili ni muhimu kabisa kwa mustakbali wa vizazi vijavyo vya Wazanzibari. Suala hili ni kubwa kushinda masuala yote mengine ambayo hayana manufaa kwa ustawi na ufanisi wa Zanzibar.
Huu si wakati wake lakini nina hakika iko siku hao wenye kuleta chokochoko ama watafichuliwa na Wazanzibari wenzao au watajifichua wenyewe kwa njama zao. Itafika siku umma utachoka na chokochoko zenye lengo la kuubabaisha na kuutoa kwenye mstari wa kupigania pawepo mashirikiano mapya na Tanganyika.
Kuna safu mbili za wenye kuleta chokochoko hizo. Ya kwanza ni ile ya wahafidhina wa CCM/Zanzibar ambo tangu mwanzo walijitokeza wazi kuyapinga maridhiano. Hawa bado wanaendelea na vitimbi vyao.
Safu ya pili ni ya wale wanaojaribu kuihujumu Serikali ya Umoja wa Kitaifa bila ya kutanabahi kwamba nao pia wanaangukia kulekule kwa wahafidhina wa CCM. Wanachofanya hawa ni kuwatia mitegoni vijana wenye jazba nyingi lakini wasio na uweledi wa kisiasa.
Baadhi ya vitendo vya vijana hao tulivishuhudia wiki iliyopita wakati wa siku tatu za machafuko mjini Unguja. Hivi ni vitendo vya kulaaniwa kwani vina hatari ya kuweza kuudhuru umoja uliopo miongoni mwa wananchi. Aidha vitendo hivyo vinawapa nguvu wahafidhina wa CCM wathubutu kujaribu kupendekeza hatua ambazo zitaichafua hali ya amani na utulivu wa kisiasa uliopo na pingine kuudhoufisha msimamo wa kuwa na umoja wa pamoja wa kuipigania Zanzibar.
Hadi sasa dalili zilizopo zinaonyesha kwamba Wazanzibari wamevinjari kuendelea na umoja wao pamoja na Serikali yao ya Umoja wa Kitaifa. Hili ni jambo la kutia moyo. Wazanzibari wote kwa pamoja wana jukumu la jumla la kuidumisha amani na hali ya utulivu wa kisiasa mpaka na baada ya kuupata muradi wao.
chanzo: raia mwema

No comments:

Post a Comment