HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. MAALIM
SEIF SHARIF HAMAD KWA WAANDISHI WA HABARI KATIKA UTARATIBU WA VIONGOZI
KUKUTANA NA WAANDISHI KILA BAADA YA MIEZI MITATU KUZUNGUMZIA UTENDAJI
SERIKALINI HUKO HOTELI YA GRAND PALACE MALINDI MJINI ZANZIBAR TAREHE 6
OKTOBA 2012
Waheshimiwa Waandishi wa habari
Kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa
kutuweka katika hali ya uzima hadi kukutana tena leo kuzungumzia
utendaji na majukumu yetu tuliyokabidhiwa na wananchi wa Zanzibar katika
serikali yetu ya awamu ya saba ya uongozi ambayo imetimiza takriban
miaka miwili sasa.
Pili natoa shukurani zangu za dhati kabisa kwenu nyinyi wanahabari
mliotenga muda wenu kuja kuhudhuria kwa wingi kuitikia wito wetu wa
kutusikiliza, na baadaye kupata fursa ya kuomba ufafanuzi wa masuala
mbali mbali yanayohusu maendeleo ya nchi yetu katika nyanja za kiuchumi,
kijamii, kisiasa na mambo yote yanayogusa jamii ya Wazanzibari kwa
jumla.
Waheshimiwa Waandishi wa habari
Nianze sasa, kuzungumzia mafanikio kwa jumla tuliyoweza kuyapata na
changamoto tunazokabiliana nazo katika kipindi hichi cha mwaka wa pili
wa serikali ya awamu ya saba. Waheshimiwa katika nchi yetu tunaendelea
kujivunia hali ya amani na utulivu katika nchi yetu ya Zanzibar.
Wananchi wote wanapata fursa na uhuru wa kufanya shughuli zao za
kujiletea maendeleo na kuendeleza mshikamano miongoni mwao. Hali hii
hatuna budi kudumisha kwa kuenzi misingi ya maridhiano ya kisiasa
yaliyofikiwa Novemba 5, mwaka 2009 na baadaye kuwa msingi wa kupatikana
serikali hii shirikishi yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa.
Kutokana na nchi yetu kuendelea kudumu katika hali ya amani, utulivu
na maelewano, wananchi wamekuwa wakiitumia kikamilifu fursa na neema
hiyo kushiriki katika shughuli za kujieletea maendeleo, ambapo pia
serikali inaendelea kusimamia majukumu ya wananchi kikamilifu, ikiwemo
kukuza uchumi wake kwa mintaarafu ya kuwapunguzia wananchi ugumu wa
maisha yao.
Katika mwaka 2011 uchumi wetu ulikuwa kwa asilimia 6.8 huku matarajio
katika mwaka huu wa 2012/2013 yakionesha dalili njema kutokana na
tulivyojipanga, ambapo uchumi huo unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 7.5.
Vile vile pato la Mzanzibari limekuwa kutoka T.SHS 782,000 kwa mwaka
hadi kufikia TSHS 960,000 ambazo ni sawa na dola za Marekani 615 kutoka
560 mwaka 2010.
Kwa vyovyote vile, bila ya kuwepo hali ya amani na utulivu na
maelewano miongoni mwetu tusingeweza kujenga imani kwa wawekezaji
vitegauchumi ambao hadi sasa wanaendelea kujitokeza kwa wingi na
kutuunga mkono kwa kuwekeza miradi yao. Bila shaka hali hiyo inatokana
na kuridhishwa kwao na amani na utulivu uliopo.
Hata hivyo, lazima tukiri kuwa bado tunayo kazi nzito mbele yetu ya
kuzidisha bidii kwa kila mmoja wetu, kuiunga mkono serikali katika
kuhakikisha nchi inaendelea kubaki katika hali ya amani na utulivu na
kusaidia kukuza kasi ya kuimarika uchumi wetu.
Kwa kufanya hivyo ndipo tutaweza kuyafikia malengo ya Milenia, ambapo
nchi zote zinatakiwa ifikapo mwaka 2015 pato la wananchi wake liwe
limefikia T.SHS 884,000. Hata hivyo tunapaswa kuzidi kuwajengea
matumaini wananchi wetu, ambao wanaamini hali ya kukua kwa uchumi wa
nchi, haina budi kuambatane na fedha kuonekana mifukoni na sio kwenye
makaratasi.
Sekta za Kilimo, Biashara na Huduma zimeendelea kupewa msukumo mkubwa
na kuendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi na mapato ya wananchi
wetu. Kwa mfano katika Huduma, utalii umeendelea kutoa mchango wa
kipekee katika uchumi wa Zanzibar. Sekta hii inachangia asilimia 80 ya
fedha za kigeni na asilimia 70 ya wananchi wetu wanafaidika katika sekta
hii kwa njia moja ama nyengine.
Mwelekeo wa Serikali yetu ni kuzidi kuiimarisha sekta hii ya Utalii,
ili iendelee kutoa mchango mkubwa zaidi kwa wananchi. Na katika
kuhakikisha lengo hilo tunalifikia, hivi sasa serikali imekuja na
mkakati mpya wa “Utalii kwa Wote”. Mkakati huu tayari umezinduliwa
rasmi, na lengo la kuanzishwa kwake ni kuhakikisha kila mwananchi
Mzanzibari popote pale alipo Unguja na Pemba ananufaika na sekta hii ya
utalii.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kama nilivyogusia hapo awali mafanikio ya mikakati na malengo yote
hayo tuliyoyaeleza yatatokana na nchi yetu kuendelea kudumu katika hali
ya amani, utulivu na maelewano miongoni mwa wananchi wake.
Katika nchi yetu ni ukweli uliowazi kwamba wapo baadhi ya wananchi ama
hawajaelewa, au wameamua kukataa hali hii ya maridhiano na maelewano
miongoni mwetu. Watu hao wakiwemo miongoni mwa baadhi ya watendaji
serikalini wamekuwa na mwenendo ambao matokeo yake yanaweza kuleta
mgawanyiko na kuvuruga hali hii ya mshikamano na amani tunayojivunia.
Serikali itaendelea kuchukua juhudi kubwa kuwaelimisha juu ya umuhimu
wa maridhiano yetu na kuwafahamisha kwamba wananchi walio wengi hivi
sasa hawako tayari kurudi nyuma tulikotoka kwenye hali ya mifarakano na
chuki miongoni mwa jamii.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Katika mkutano kama huu na waandishi wa habari mwaka jana, nilijikita
zaidi kuzungumzia changamoto za kiuchumi ambazo zimesababisha ugumu wa
maisha kwa Wazanzibari walio wengi, zikiwemo mfumuko mkubwa wa bei za
bidhaa muhimu kama vile, mchele, sukari, unga wa ngano na nyenginezo na
kueleza mipango tuliyokuwa tumejipangia. Leo nimepanga nizungumzie zaidi
kwa kifupi changamoto za ndani zinazojitokeza katika utendaji wa kila
siku serikalini.
Waheshimiwa
Katika utendaji wetu serikalini katika kipindi hiki cha miaka miwili,
bado tunakabiliwa na changamoto nyingi. Kati ya hizo ni kudhibiti
matumizi holela ya fedha za umma miongoni mwa watendaji wetu. Ripoti ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mwaka 2010/2011 inaonesha
bado kuna watendaji ambao wamedhamiria kujinufaisha binafsi kupitia
fedha za serikali. Wanafanya hivyo, licha ya hatua na juhudi kubwa
zinazochukuliwa kuwakataza na kuhimizana kujali misingi ya Utawala Bora.
Pamoja na marekebisho katika baadhi ya maeneo lakini bado kila
zinapotoka ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu, zinaonesha suala la
matumizi yasiyofuata taratibu linaendelea kujitokeza.
Kuna udhaifu mkubwa wa kukosekana baadhi ya vielelezo muhimu katika
ukusanyaji na matumizi ya mapato. Aidha, kumegundulika kujitokeza
udanganyifu katika utayarishaji wa mafao ya baadhi ya wastaafu.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameanza utaratibu
wa kukagua miradi ya maendeleo na kujiridhisha kuwa kazi iliyofanyika
inalingana na thamani ya fedha zilizotumika. Imegundulika katika baadhi
ya miradi, fedha zilizolipwa ni nyingi sana ikilinganishwa na kazi
iliyofanyika pamoja na ubora wa kazi wenyewe kuwa haulingani kabisa na
fedha zilizolipwa.
Napenda kutoa wito maalum kwa watendaji serikalini kuacha tabia ya
udokozi wa fedha za wananchi, na wahakikishe wanafuata taratibu na
kanuni za matumizi ya fedha za umma. Aidha, serikali haitavumilia kuona
baadhi ya watendaji wanaendelea kukiuka sheria zilizopo na kuchukua
fedha za wananchi kujinufaisha wao binafsi.
Sote tunaelewa ni kwa kiasi gani serikali inavyojibana katika matumizi,
ili kuhakikisha mapato hayo kidogo yanayopatikana yanatumika katika
shughuli za maendeleo na za kijamii.
Hivi sasa serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha inapata
usafiri wa uhakika wa baharini, kwa azma ya kuwaondolea usumbufu
wananchi na wageni wanaohitaji kusafiri kati ya Unguja na Pemba na
Tanzania Bara. Jambo hilo linahitaji fedha nyingi katika kufanikiwa
kwake; fedha ambazo zitatoka katika mfuko wa serikali. Sasa pale
wanapojitokeza watendaji wa serikali kurudisha nyuma juhudi kama hizo
kwa kufanya udanganyifu kwa kweli hilo si jambo zuri na si jambo la
kuvumiliwa.
Serikali inachukua bidii kutafuta meli kubwa ya kisasa au za kisasa
kwa kuamini kwamba hatua kama hiyo ndiyo itakayotuwezesha kuwa na
usafiri wa uhakika na kuepuka maafa ya baharini, kama yaliyotokea mwezi
Julai mwaka huu kwa kuzama meli ya MV. Skagit katika eneo la Chumbe na
Septemba mwaka jana, yalipotokea maafa kama hayo ilipozama meli ya MV.
Spice Islander katika eneo la Nungwi.
Changamoto nyengine ya muda mrefu inayotukabili ni baadhi ya
watendaji wetu kulalamikiwa kuviza kwa makusudi haki za wananchi. Hali
hiyo imejitokeza zaidi katika suala la utoaji wa Vitambulisho vya
Mzanzibari Mkaazi (ZANID).
Pamoja na ahadi na kauli mbali mbali za watendaji na viongozi kuahidi
kila mwananchi aliyefikia umri wa miaka 18 na mwenye sifa zote za
kupata kitambulisho hicho kuwa atapatiwa, bado malakamiko ni mengi
katika jamii kuwa kuna watu wananyimwa haki hiyo kwa makusudi kabisa.
Serikali inajitahidi kutafuta ufumbuzi wa haraka changamoto hii kwa
kutambua kuwa vitambulisho hivyo ndio utambuzi wa Wazanzibari Wakaazi na
vinahusika moja kwa moja katika upatikanaji wa huduma na haki mbali
mbali za msingi.
Kuwa na kitambulisho hicho ni jambo la lazima la kisheria na kwamba
kumkosesha mtu au mtu kushindwa kuwa nacho ni kosa ambalo mhusika
anaweza kuhukumiwa kifungo na faini. Na kwa umuhimu huo huo, napenda
kuwanasihi wananchi ambao vitambulisho vyao viko tayari, lakini bado
wamekuwa na ajizi kwenda kuvichukua wakavichukue haraka.
Kwa upande mwengine kutokana na umuhimu wa kitambulisho hicho na kwa
kuwa kimehusishwa moja kwa moja katika upatikanaji wa huduma na haki za
msingi, kumejitokeza mahitaji makubwa ya watu kuvitafuta na hata
wasiohusika, yaani baadhi ya wageni wanavitafuta kwa udi na uvumba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduizi Mhe. Dk. Ali
Mohammed Shein kwa kuendelea kuwasisitiza wahusika wanaolalamikiwa
kuwanyima wananchi vitambulisho hivyo kuacha tabia hiyo. Kwa mara ya
mwisho Rais Shein alitoa wito wiki iliyopita kule Pemba wakati wa semina
maalum kwa watendaji wa Serikali za mitaa. Ni imani yangu kwamba
watendaji na viongozi wa serikali za Mitaa, Wilaya na Afisi ya Msajili
wa Vitambulisho, watatii agizo hilo la Rais.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Nimelazimika kulizungumza kwa kirefu kidogo suala hili la
vitambulisho vya Ukaazi kutokana na umuhimu wake kwa wananchi. Lakini
pia tumeona namna baadhi ya watu na vikundi wanavyoweza kutumia udhaifu
wa utoaji vitambulisho hivyo kuuhusisha na masuala mengine muhimu ya
Kitaifa.
Tumeona wakati wa zoezi la Sensa ya Kuhesabu watu na Makaazi hivi
karibuni, baadhi ya watu walivyo tumia udhaifu wa utoaji vitambulisho
hivyo kukaidi amri ya kuhesabiwa. Wamefanya hivyo, licha ya kuwa jambo
la kuhesabiwa lina umuhimu wa kipekee katika maendeleo na ustawi wa
wananchi. Hivyo basi ni vyema hatua zichukuliwe kila mwenye haki ya
kitambulisho hicho asiwekewe kikwazo chochote, ili kuziba mianya kama
hiyo inayotumiwa na baadhi ya watu kurejesha nyuma maendeleo na umoja
wetu.
Waheshimiwa Waandishi
Jambo jengine ambalo napenda kuwahimiza tena wananchi, ni juu ya
umuhimu wa kushiriki kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume ya Mabadiliko ya Katiba
inayoendelea kufanya shughuli za kuratibu maoni ya wananchi nchi nzima
tayari imefanya kazi hiyo katika mikoa ya Kusini Unguja na Kusini Pemba
kwa hapa Zanzibar. Na katika mikoa hiyo wananchi waliweza kujitokeza
vizuri kutoa maoni yao.
Nawasihi wananchi wote wa mikoa ya Kaskazini Unguja, Kaskazini Pemba
na Mjini Magharibi wajitokeze kwa wingi kwenda kutoa maoni yao, wakati
tume hiyo itakapofika katika maeneo yao. Hatua hiyo ndiyo
itakayotuwezesha kupata Katiba tunayoitaka yenye maslahi kwa Zanzibar.
Hii ni fursa adhimu ambayo tumekuwa tukiililia kwa siku nyingi juu ya
haja ya Watanzania kupata fursa ya kutoa maoni yetu, juu ya masuala
yote yanayohusiana na Muungano. Wananchi wawe huru kutoa maoni yao kwa
uwazi na pawepo na uvumilivu. Hata kama mtu hakubaliani na maoni, hoja
zinazotolewa na mwengine, inabidi asikilize kwa uvumilivu. Naye akipata
fursa aseme yake kwa uwazi pia.
Na mwisho wa yote hayo, ni kama ambavyo tunatarajia, maoni ya wengi
ndiyo yatakayo heshimiwe baada ya wale wachache kupewa haki yao ya
kusikilizwa kwa kikamilifu. Na sisi viongozi tunawajibu wa kusimamia
hilo.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Sasa naona tugusie masuala ambayo imekabidhiwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Kama ambavyo mnafahamu ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais pamoja na mambo
mengine, imekabidhiwa majukumu mazito, majukumu ambayo kwa lugha ya
siku hizi yanaitwa Masuala Mtambuka (Cross Cutting issues), yakiwemo;
Masuala yanayohusu Watu Wenye Ulemavu, Mapambano dhidi ya Madawa ya
Kulevya, Uhifadhi wa Mazingira pamoja na Ugonjwa wa Ukimwi.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Katika suala la mapambano dhidi ya UKIMWI, Wazanzibari tunapaswa sote
tufahamu kuwa ukimwi bado upo na unaendelea kuwaathiri watu wetu.
UKIMWI ni tatizo linalotugusa sote, wanawake, wanaume, vijana na watoto
na ni janga ambalo linasababisha matatizo makubwa katika ngazi za
familia hadi serikali.
Serikali kwa ushirikiano na wadau mbali mbali inachukua hatua kubwa
katika kuweka mazingira mazuri ya kupiga vita janga hili, lakini bado
kuna maambukizi mapya ya UKIMWI yanatokea.
Pia wale walioathiriwa na maambukizi bado wanakabiliwa na vikwazo
vingi, ikiwemo kunyanyapaliwa na baadhi ya wanajamii. Aidha wanakumbana
na hali ya umasikini na uhaba wa dawa na huduma nyengine wanazozihitaji.
Kiwango cha maambukizi ya ukimwi miongoni mwa watu wenye umri wa miaka
15 hadi 49 kimeendelea kusimama kwenye 0.6, ikiwa ni sawa na watu 7,200
wanaokadiriwa kuishi na virusi vya UKIMWI. Visiwani humu hali ya
maambukizi ni mbaya zaidi kwa watu wa makundi maalum, ambayo inakadiriwa
kupita kiwango kilichopo katika jamii nzima.
Kwa Zanzibar makundi maalum yanajumuisha; Watu wanaojidunga sindano
za madawa ya kulevya, Wanawake wanaouza miili yao, Wanafunzi katika vyuo
vya Mafunzo na Wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja.
Hata hivyo, tafiti mbali mbali ndogo ndogo hivi sasa zinaendelea, ili
kujua hali halisi ya maambukizi ya UKIMWI Zanzibar, pamoja na mwenendo
mzima wa maradhi hayo na kuweza kuandaa mikakati thabiti kwa mujibu wa
hali ilivyo katika kudhibiti maambukizi mapya, na kuwasaidia wale ambao
tayari wameambukizwa.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imeweza kufuatilia na
kutathmini program mbali mbali za UKIMWI. Mwaka jana jumla ya vikundi 24
vyenye miradi 36 ya kujiongezea kipato vilifuatiliwa. Jumla ya shilingi
milioni 15 kwa mfano walipatiwa jumuiya ya ZAPHA+ kwa ajili ya
kutekeleza shughuli zao mbali mbali zinazolenga utekelezaji wa Mkakati
wa Pili wa Taifa wa UKIMWI Zanzibar.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Nadhani bado mnakumbuka Disemba Mosi mwaka jana tulizindua Mkakati wa
Pili wa Taifa wa UKIMWI wa Zanzibar. Mkakati huo umeandaliwa maalum
kuongoza muitikio wa kitaifa wa mapambano dhidi ya ukimwi kwa mwaka
2011/2016. Lengo kuu ni kuzuia kuenea maambukizi ya virusi vya UKIMWI
miongoni mwa Wazanzibari, kukabiliana na athari mbaya za kiafya, ustawi
na za kiuchumi zinazompata mtu mmoja mmoja , familia zao, makundi maalum
na Taifa kwa jumla.
Aidha, Sera ya Taifa ya UKIMWI ya 2005 imejenga msingi mzuri wa
kufanikisha mapambano dhidi ya ukimwi. Sera hiyo imeweka mfumo wa
utawala wa kisheria kwa ajili ya mipango na harakati zote
zitakazofanywa, ikiwemo kuzuia maambukizi mapya, kutibu, kutunza na
kuwasaidia walioambukizwa pamoja na kuimarisha uwezo wa taasisi katika
kutayarisha na kutekeleza program za ukimwi kwa kuzingatia jinsia na
haki za binaadamu wote.
Katika kufanikisha mapambano dhidi ya UKIMWI Zanzibar tunaendelea kutoa
wito kwa jamii, wakiwemo wazazi na viongozi wa kidini waendelee kutoa
nasaha na kuwakataza vijana wetu na jamii kwa jumla, kuepuka matendo
ambayo yatasababisha watu kuambukizwa virusi vya UKIMWI.
Vijana katika umri wao huiona dunia kama mahali pa uwezekano
usiomalizika. Vijana waliopewa miongozo na malezi mazuri ndio wenye
mwelekeo mzuri wa kusalimika na matatizo kama haya. Familia hazina budi
kuwapa mawaidha vijana wao wa kike na kiume tena kwa uwazi mkubwa kabisa
juu ya ukimwi, ili wajiepushe.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kuhusu Masuala ya Watu Wenye Ulemavu, katika jamii ya Wazanzibari
kama zilivyo jamii nyengine, miongoni mwetu kuna Watu Wenye Ulemavu.
Aidha, katika harakati za kimaisha za siku hadi siku kuna sababu tafauti
zinazopelekea idadi ya watu wenye ulemavu kuongezeka. Kutokana na
ukweli huo pamoja na wajibu wetu wa kibinaadamu, hatuna budi kuwa na
mipango na mikakati imara ya kuwasaidia watu wenye ulemavu. Kujitolea
kwetu kuwasaidia watu wenye ulemavu ndipo tutawawezesha wenzetu hawa
kuishi kwa furaha na kuondokana na vikwazo vingi vinavyowakabili hivi
sasa.
Watu wenye ulemavu wana haki sawa na watu wengine katika jamii.
Wenzetu hawa wana kila haki ya kushirikishwa katika mipango yote ya
kimaendeleo, pamoja na huduma za kijamii. Lakini kwa bahati mbaya sana
hadi sasa watu wenye ulemavu wana kilio kikubwa cha kutopatiwa haki zao
stahiki ipasavyo, pia wana malalamiko mengi ya kunyanyaswa na
kudhalilishwa ikiwemo kijinsia.
Lakini pia katika jamii zetu tunaona ni namna gani hata mwamko juu ya
watu wenye ulemavu ulivyo mdogo. Hadi leo kuna watu bado wanawaficha
watoto na ndugu zao kwa sababu tu wana ulemavu. Kutokana na hali hiyo
ndio maana tukaamua kuanzisha zoezi la makusudi kabisa kushajiisha jamii
kuwafichua na kuwasajili watu wenye ulemavu.
Katika zoezi hilo linaloendelea ambalo lilitanguliwa na mafunzo kwa
Masheha na wakusanyaji taarifa, tumeweza kusajili jumla ya watu 6,445
wenye ulemavu katika mikoa yote miwili kisiwani Pemba. Awali zoezi hilo
lilifanyika kwa majaribio katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako jumla
ya watu wenye ulemavu 3,002 walisajiliwa.
Aidha, katika kukuza na kuendeleza mwamko juu ya masuala ya watu
wenye ulemavu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imefanya kazi kubwa
kuhakikisha masuala ya watu wenye ulemavu yanaingizwa katika mipango ya
taasisi za za Serikali. Hadi sasa ofisi imeweza kusimamia uanzishwaji wa
mpango huo na Maafisa Waratibu 16 tayari wapo katika wizara mbali mbali
kwa ajili ya hatua hizo na tayari wamepatiwa mafunzo maalum.
Kwa upande mwengine, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imehakikisha
inajenga uwezo kwa Idara ya Watu wenye Ulemavu pamoja na Baraza la Watu
Wenye Ulemavu Zanzibar, kwa kununua vifaa vya ofisini pamoja na vifaa
vya utendaji kwa wafanyakazi wake. Vile vile jumuiya tisa za Watu wenye
Ulemavu zimeweza kupatiwa ruzuku pamoja na visaidizi, yaani viti vyenye
magurudumu mawili kwa watu 31 Unguja na Pemba, ili kuwasaidia katika
harakati zao za kimaisha.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Wajibu wetu kwa watu wenye ulemavu ni mkubwa, lakini wakati ukweli
ndio huo uwezo na nyenzo zetu hazitoshi kuweza kuwajengea uwezo
kikamilifu kwa mujibu wa mahitaji yao. Lakini kwa kuthamini maisha na
maendeleo yao, haki, fursa na usawa kwa watu wenye ulemavu, wajibu wetu
wa kuwawezesha kukabilina na umasikini uliokithiri na upatikanaji mdogo
wa huduma za afya tumeona kuna haja kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Watu
Wenye Ulemavu.
Mfuko wa Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar umeanzishwa kama
Sheria No. 9 ya mwaka 2006 inavyoagiza. Kama ambavyo waandishi wa habari
ni mashihidi, Mfuko huo tayari umezinduliwa rasmi wiki iliyopita na
Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed na kwakweli naona fahari
kusema tumeanza vizuri.
Tunawashukuru mwananchi mmoja mmoja, mashirika, jumuiya, taasisi za
kiserikali na watu binafsi, kwa namna walivyojitokeza na kuonesha moyo
wao wa dhati kuwasaidia watu wenye ulemavu Zanzibar. Moyo wao huo
umewezesha mfuko huo kuanza na kiasi cha T.SHS milioni 285. Tunaendeela
kukuhimizeni wananchi na taasisi mbali mbali kuendelea kuchangia mfuko
huu kwani uchangiaji wa mfuko unaendelea.
Matumaini yetu Mfuko huu utaweza kutoa mchango mkubwa kusaidia utatuzi wa changamoto nyingi ambazo baadhi tumesha zianisha.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kwa upande wa Madawa ya Kulevya, Suala hili pia ni changamoto
nyengine kubwa inayotukabali katika nchi yetu. Na ukweli ni kwamba
tatizo hili sio tu kwa Zanzibar, bali kwa Dunia nzima. Kutokana na
ukubwa wa tatizo la madawa ya kulevya mataifa yanaungana kupambana na
wazalishaji, wafanyabiashara na walanguzi wa madawa haya ambao nao
wamejidhatiti vilivyo. Katika baadhi ya nchi tunashuhudia hata nguvu za
kijeshi zikitumika kukabiliana na tatizo hili.
Athari za madawa ya kulevya zipo wazi na Zanzibar tunashuhudia hilo.
Maisha ya watu wetu hasa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa yamekuwa
hatarini. Lakini kwa upande mwengine madawa ya kulevya yamekuwa chanzo
kikuu cha maambukizi ya maradhi ya ukimwi, ambayo nayo yanachukua nafasi
kubwa kuteketeza maisha ya binaadamu na kudhorotesha uchumi wa nchi.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imekuwa ikifanya kazi kubwa ya
kuratibu na kudhibiti utumiaji, biashara na usafirishaji wa madawa hayo.
Kazi hizo zimekuwa zikifanywa kwa karibu na wananchi pamoja na wadau
mbali mbali katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, vikiwemo vyombo
vya ulinzi na usalama, azma yetu ikiwa ni kuinusuru Zanzibar kuwa kituo
cha madawa ya kulevya na wananchi wake kuathirika na madawa hayo.
Mikakati yetu juu ya jambo hili imelenga zaidi kuwa na sheria
zinazokwenda na wakati ambazo zinakidhi haja ya kudhibiti madawa ya
kulevya kwa wakati uliopo.
Katika utekelezaji wa hatua hiyo tayari sheria Nam. 9 ya mwaka 2009
ilipitiwa na wadau mbali mbali na baadaye kuwasilishwa katika kikao cha
Baraza la Wawakilishi na kurekebishwa. Aidha, uandaaji wa Sera ya Madawa
ya Kulevya Zanzibar inaendelea na hivi sasa kazi za kukusanya maoni ya
wadau inafanyika.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Juhudi kubwa katika kudhibiti madawa ya kulevya Zanzibar
tumezielekeza katika kutoa taaluma kwa jamii juu ya madhara yake, lakini
pia kuwasaidia vijana walioingia kwenye matumizi ya madawa haya, kwa
kuwanasihi waache, pamoja na kuwashauri na kuwasaidia njia
zitakazowawezesha kupata kazi za kujiongezea vipato na kuondokana na
tabia ya kukaa bila ya kazi, tabia ambayo huwapa msongo wa mawazo na
kuwafanya waendelee kutumia madawa hayo.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika mwaka wa fedha uliomalizika,
iliweza kutoa ushauri nasaha kwa familia 984 za watumiaji wa madawa ya
kulevya, wakiwemo wanawake 510 na wanaume 474, ambapo kati yao, 97
walikuwa watumiaji wa madawa ya kulevya.
Aidha, ahadi ya kuzisaidia angalau fedha kidogo taasisi zinazotoa
huduma za makaazi ya vijana wanaoacha kutumia madawa ya kulevya (Sober
Houses) ilitekelezwa na shilingi 9,900,000 zilitolewa, pamoja na
televisheni na redio Unguja na Pemba.
Rasimu ya muongozo wa nyumba za marekebisho za makaazi ya vijana
wanaoacha matumizi ya madawa hayo imekamilika. Aidha, suala la taaluma
kwa jamii juu ya kupiga vita madawa ya kulevya limeendelea kupewa
umuhimu wa kipekee kwa kuandaa vipindi mbali mbali vilivyoweza kurushwa
hewani kupitia televisheni na redio. Vile vile Shehia mbali mbali
zilifanyiwa ziara za uhamasishaji na taaluma juu ya athari za madawa
hayo Unguja na Pemba.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kuhusu suala la Kuyahifadhi na kuyalinda mazingira yetu, pia hili
nalo ni muhimu katika kudumisha Uhai na Ustawi wa nchi yoyote ile. Hata
hivyo changamoto inayojitokeza katika nchi nyingi, ikiwemo Zanzibar ni
uharibifu na uchafuzi mkubwa na wa makusudi wa mazingira yetu. Kasi
tunayoishuhudia ya ukataji ovyo wa misitu na uchimbaji wa mchanga na
mawe, kwa ajili ya kutengeneza matofali ni ya kutisha na iwapo
haitadhibitiwa nchi yetu ya Zanzibar kipindi kifupi kijacho itakabiliwa
na janga kubwa la kimazingira.
Aidha, upoteaji wa bioanuwai za nchi kavu na baharini kwa jumla,
utupaji ovyo wa taka na maji machafu, uvunaji usioridhisha wa maliasili
zisizojirejesha, hali inayosababisha kuachwa kwa mashimo mengi, pamoja
na ile tabia ya kuingizwa kwa wingi nchini vifaa chakavu vya
elektroniki, umeme na mifuko ya plastiki inaongeza ukubwa wa hatari hiyo
ya kimazingira.
Kwa upande mwengine suala la mabadiliko ya tabianchi limekuwa ni
tishio kubwa kwa dunia, na nchi zinazoathirika zaidi ni zile za visiwa
vidogo kama vyetu vya Zanzibar. Hali inayojitokeza katika baadhi ya
maeneo ya visiwa vyetu ambako maji ya bahari yamevamia mashamba ya
kilimo cha mpunga inatosha kuwa onyo kali kwetu na kufanya kila
linalowezekana kuyalinda mazingira.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika kukabiliana na changamoto
hizo za kimazingira, ikiwemo suala la athari za mabadiliko ya tabianchi
bado inaamini utoaji wa elimu na kuzidi kukumbushana ndio njia muafaka
na yenye umuhimu wa kipekee.
Hata hivyo hatua za kisheria zimeendelea na zitaendelea kuchukuliwa
kwa wananchi au miradi ya kiuchumi ambayo inaonekana kwa makusudi
kupinga au kudharau sheria na kanuni za uhifadhi wa mazingira.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Miongozi mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni kutoa taaluma kwa
njia ya semina, vipindi vya televisheni na redio, pamoja na kuandaa
ziara za kimasomo katika maeneo mbali mbali, ili wananchi, viongozi wa
maeneo na wanachama wa jumuiya zisizokuwa za kiserikali, waweze
kujifunza na baadaye kusaidia jamii kukumbusha na kuhamasisha suala zima
la kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira ya nchi yetu.
Hatua hizo zinajumuisha mafunzo juu ya mabadiliko ya Tabianchi na
mwelekeo wa Zanzibar katika kusimamia jambo hilo, yalitolewa kwa Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi. Aidha wafanyakazi 12 kutoka Idara ya
Mazingira, Baraza la Manispaa Zanzibar, Halmashauri za Wilaya ya
Magharibi na Mabaraza ya Miji ya Chake Chake, Mkoani na Wete na baadhi
ya wawakilishi wa Jumuiya zisizokuwa za kiserikali waliwezeshwa kufanya
ziara za kujifunza huko Moshi na Arusha, ili waweze kupata uzoefu juu ya
usimamizi wa taka.
Ziara za kujifunza za aina hii, pia ziliwahusisha viongozi 10 wa
Kamati za Machimbo ya Uwandani waliokwenda Mjini Mombasa Kenya kujifunza
njia bora za shughuli za uchimbaji na urejeshwaji wa maeneo
yaliyochimbwa na kuepusha athari za kimazingira.
Hatua hizo zilichukuliwa kwa makusudi, ili kudhibiti kasi ya uchafuzi
wa maeneo na kuyaweka katika hali ya usafi, pamoja na kudhibiti athari
za uchimbaji mawe kwa ajili ya kazi za uchongaji matofali, maeneo ambayo
yanahatarisha sana hali ya mazingira hapa Zanzibar.
Eneo jengine ambalo linaonekana ni sugu katika uharibifu wa mazingira
yetu ni kwenye fukwe na miradi ya hoteli za kitalii. Katika siku za
hivi karibuni miradi 110 ya kitalii ilifanyiwa ufuatiliaji kuona
inavyozingatia masuala ya kimazingira. Taarifa ya ufuatiliaji huo si ya
kufurahisha kwa sababu kati ya miradi mingi ambayo ilionekana kukiuka
kanuni ya kudhibiti matumizi ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji ya mwaka
2006.
Miradi hiyo ilitakiwa kubomoa sehemu zilizojengwa kinyume na kanuni,
lakini ni mradi mmoja tu wa hoteli ya Zanzibar Ocean View ambao umetii
amri hiyo.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ilichukua hatua ya kuwasilisha majina
ya miradi hiyo iliyoshindwa kufuata agizo hilo, Idara ya Mipango Miji na
Vijiji kwa ajili ya hatua za kisheria kwa mujibu wa kanuni.
Hata hivyo, lazima tukiri kwamba ipo haja kubwa ya kuimarishwa Sheria
na kanuni zetu za Mazingira, ili ziweze kukidhi haja kwa mujibu wa
wakati.
Kuhusu usimamizi wa marufuku ya mifuko ya plastiki, baada ya Kanuni
kufanyiwa marekebisho, mafanikio makubwa yameweza kupatikana ambapo hadi
unakamilika mwaka wa fedha uliopita, watu 192 walikamatwa na
kushitakiwa mahakamani na jumla ya shilingi 7,650,000 zilizotokana na
faini ziliingia katika mfuko wa serikali.
Ni dhahiri changamoto ya kimazingira ni kubwa, hivyo ni jukumu la
kila mmoja wetu kutekeleza wajibu wake wa kulinda na kuyahifadhi
Mazingira yetu ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa
kizazi cha sasa na kijacho.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Baada ya kusema hayo natanguliza shukurani zangu nyingi, kwa viongozi
na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwemo Waziri wangu
wa Nchi mchapakazi na muadilifu, Mheshimiwa Fatma Abdulhabib Fereji.
Vile vile shukurani hizo ziende kwa Katibu Mkuu makini mwenye uzoefu na
ujuzi wa taratibu za serikali ambaye ndiye anayenishauri mimi na Waziri
wa Nchi kuhusu masuala ya kitaalamu, mbali kuwa Mtendaji Mkuu wa
shughuli zote zilizochini ya ofisi hii. Huyo ni Dk. Omar Shajak
akisaidiwa na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Islam Seif Salum, pamoja na
Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa Kamisheni zilizo chini ya ofisi hii.
Wote hao nawashukuru kwa msaada mkubwa wanaoendelea kunipa kwa muda wote
huu.
Ahsanteni sana.
No comments:
Post a Comment