HATIMAE
waya mpya wa umeme utakaolazwa baharini kutoka Ras Fumba Zanzibar hadi
Ras Kiromoni Dar-es-Salaam umewasili Zanzibar na kupokewa rasmi pamoja
na kukaguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Ali Mohamed Shein, huko katika bandari ya Malindi mjini Unguja.Waya huo
utakaotumika katika mradi wa uwekaji wa waya wa pili wa umeme kutoka
Ras-Fumba hadi Ras Kiromoni Dar-es-Salaam, shughuli zake za ulazaji
zinatarajiwa kuanza siku ya Juamatatu majira ya asubuhi.Akitoa
maelezo yake huku akionesha furaha kubwa Dk. Shein alitoa pongezi kwa
Kampuni iliyotengeza waya huo pamoja na Wakandarasi waliotengeza waya
huo alieleza kuwa licha ya kuwa kazi hiyo ni ngumu lakini imefanywa
vizuri.Dk. Shein
alisema kuwa kuja kwa waya huo kutapunguza usumbufu wanaoupata hivi sasa
wananchi wa kupata umeme kwa mgao kwani waya huo utakuwa na umeme wenye
megawati 100 ambazo zitatosheleza kwa kiasi kikubwa na nyengine
kubakia.
Alisema
kuwa matumizi ya umeme kwa kisiwa cha Unguja ni megawati 45 tu kwa hivi
sasa lakini waya una megawati 100 ambazo zitasaidia kutoa huduma hiyo
pamoja na kuweza kujipanga vizuri kwa shughuli nyengine za maendeleo
hapo baadae.Aidha, Dk.
Shein alisema kuwa waya huo ambao pia, utasaidia kutoa huduma nyengine
za mawasiliano yakiwemo mtandao wa intaneti utawezesha kutoa huduma za
e- Government pamoja na huduma za mkonga wa taifa kama ulivyo kwa waya
uliolazwa kisiwani Pemba.Rais Dk.
Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa ulazaji wa waya
huo katika hafla itakayofanyika siku ya Jumaatatu asubuhi.Akipata
maelezo kutoka kwa jopo la wakandarasi wa waya huo Kampuni ya VISCAS, na
mhandisi mdogo pamoja na Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya ESB
International pamoja na Msaidizi Mtendaji Mkuu wa MCA-T kwa upande wa
Zanzibar Bwana Ahmed Rashid, walieleza kuwa shughuli hizo za ulazaji wa
waya zitafanywa si zaidi ya siku 12 kwa kutumia meli na vifaa
walivyonavyo kwa kushirikiana na meli nyengine.Walieleza
kuwa waya huo wenye urefu wa kilomita 37 na uzito wa tani 2000, shughuli
za ulazaji pamoja na zile za kuunganisha katika vituo maalum vilivyopo
Mtoni na vile vya Dar-es-Salaam zinatarajiwa kumalizika na kutoa huduma
ya umeme unatokana na waya huo mpya mnamo mwanzoni mwa mwezi wa Novemba.Aidha,
uongozi wa MCA-T ulitoa shukurani kwa uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi
kwa mashirikiano makubwa ya mazungumzo na viongozi wa dini katika
mchakato mzima wa kuvunjwa nyumba, madrasa na baadhi ya nyumba za ibada
kwa lengo la kupitisha waya mpya wa umeme kutoka Fumba hadi Mtoni.Uongozi
huo wa MCA-T pia ulieleza kuwa kuna hakiba ya waya upatao mita 450 ambao
utawekwa katika kituo cha Mtoni kwa ajili ya dharura pale
itakapohitajika na kusisitiza kuwa tayari nguzo maalum za ardhini
zimeshawekwa katika baadhi ya sehemu.Walieleza kuwa waya huo mpya utalazwa sambamba na waya huu uliopo hivi sasa na kusisitiza kuwa shughuli hizo za ulazaji zinatarajiwa kuanza siku ya Jumatatu asubuhi.Nae Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Bwana Hassan Ali Mbarouk alisema kuwa waya huo unauwezo wa kuishi zaidi ya miaka 30.Mradi wa
waya huo wa umeme umenza miaka mine iliyopita ambao umetengenezwa na
Kampuni ya VISCAS kutoka Japan ambao mbali ya kutengeneza pia, watakuwa
na jukumu la ulazaji wa waya huo ambao utasimamiwa na Wahandisi washauri
wa Kampuni ya ESB International kutoka Ireland.Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Changamoto la Milenia (MCC) kutoka Marekani.Baadhi ya
wananchi ambao walikuwepo katika hafla hiyo fupi huko katika bandari ya
Malindi mjini Unguja wakizungumza na mwandishi wa habari hizi walieleza
kufarajika kwao na juhudi zinazochukuliwa na Serikali yao inayoongozwa
na Dk. Shein katika kuwatatulia kero zao.Walieleza
kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza
huduma za maendeleo kwa wananchi sambamba na kuimarisha sekta za
maendeleo zikiwemo mawasiliano pamoja na sekta ya utalii ambayo ndio
sekta inayoipatia fedha nyingi serikali.
No comments:
Post a Comment