“Mimi sitafuni maneno kwamba ni muumini wa Zanzibar yenye mamlaka kamili
kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na mashirikiano kati yake na Tanganyika
kupitia Muungano wa Mkataba. Namshangaa leo anakuja kiongozi wa Zanzibar anasema
tuna bendera na muhuri na wimbo wa taifa, hayo yanatosha. Hivi huyu anajua
anachokisema au anatumikia maslahi ya waliomtuma? Una bendera gani hii ambayo
mwisho wake Chumbe? Mimi nataka niione bendera ya Dola ya Zanzibar inapepea
Umoja wa Mataifa, New York pale. Nataka tuwe na Paspoti ya Zanzibar, nikisafiri
nitoe Paspoti ya nchi yangu. Nataka tuwe na Ofisi za Kibalozi za Zanzibar katika
nchi za nje.
Leo hata mamlaka ya kiuchumi hatuna. Tumeamua rasilimali yetu ya mafuta na
gesi asilia yasiwe mambo ya Muungano, mpaka leo Tanganyika wamekwamisha,
wanatuzuia tusinufaike na rasilimali zetu tukajenga uchumi wetu. Wanasema tuna
viwango na mfumo mmoja wa kodi lakini bidhaa zikitoka Zanzibar wanazitoza ushuru
tena. Lengo ni kuua uchumi wetu ili hatimaye tudhoofike na tusalimu amri kwao.
Yaguju! Wasahau hilo. Leo hata katika mikutano ya kimataifa, viongozi wetu wa
Zanzibar hawapewi heshima ya uwakilishi wa nchi yetu.
Inafika mahala hata Naibu Waziri tu wa Bara anaongoza ujumbe wa Tanzania
wakati kuna Waziri kamili kutoka Zanzibar lakini haheshimiwi. Tutarejesha
mamlaka yetu kamili. Tuwe na Benki Kuu, tuwe na sarafu yetu ya Zanzibar, tupange
uchumi wetu kwa maslahi ya watu wetu. Tunataka tuwe na uanachama katika jumuiya
na mashirika yote ya kimataifa. Tuwe na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zanzibar. Tuwe
na uwezo wa kuingia mikataba na nchi za kigeni. Hayo ndiyo tunayoyataka.
Tukisema hivi hatuna maana tunataka ugomvi na Tanganyika. Hapana! Tunataka tuwe
majirani wema na Tanganyika kama tutakavyokuwa na ujirani mwema na Kenya. Hayo
yatafikiwa kupitia Muungano wa Mkataba wa Madola mawili huru kamili.”
Chanzo: Mzalendo
No comments:
Post a Comment