Thursday 1 November 2012

Indhari kwa watawala na watawaliwa Zanzibar

ALBIUS Tribullus alifariki dunia kama miaka 19 hivi kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (YesuKritso). Tribullus alikuwa Mlatini na mshairi maarufu aliyebobea katika fani ya uandishi wa maombolezi.
Mshairi huyu wa huba na huzuni aliwahi kuandika: “Matumaini daima hutwambia kwamba kesho mambo yatakuwa mazuri zaidi.” Matumaini kama hayo wanayo Wazanzibari wa leo. Yanawaambia kesho mambo yatakuwa mema zaidi lakini kwa sharti.
Sharti lenyewe ni kwamba wajichunge. Watawala na watawaliwa; wale wenye silaha nzito nzito na wale wenye mawe na vibiriti wote wajichunge na wajifunze kutoka historia.
Historia ya kisiasa ya Zanzibar inaonyesha kwamba kwa kipindi cha zaidi ya miongo mitano, tuseme tangu zilipoanza siasa za vyama mwaka 1957 visiwa hivi vimeshuhudia visa vingi vya vurugu, umwagaji wa damu, kuteswa kwa raia na kuuawa kwa mamia ya watu.
Kuna raia walioteswa na waliolemazwa au waliofanyiwa mambo hata akili zao zikaharibika. Hawakuathirika wao tu bali hata familia zao na jamii nzima kwa jumla.
Vitendo hivyo vya kinyama na kikatili viliwezekana kwa sababu watu hawakuweza kuvumiliana kisiasa. Kwa kawaida visa kama hivyo havitokei katika jamii zilizostaarabika ambako watu wenye maoni au itikadi tofauti za kisiasa hupambana kwa njia za amani. Wanapambana kwa mujibu wa kanuni za kidemokrasia, za utawala bora na kwa kuzifuata sheria za nchi.
Bahati nzuri hii leo Zanzibar juu ya vurugu za kusikitisha zilizotokea Unguja majuzi bado kuna hali ya amani na utulivu wa kisiasa. Si hayo tu bali wengi wa Wazanzibari wanataka hali hii ya amani iendelee na matatizo yote ya kisiasa ya tanzuliwe bila ya umwagaji damu, machafuko ya raia au hatua yoyote itakayozua balaa.
Lengo lao ni kuvifanya visiwa hivi viendelee kuwa visiwa vya amani. Hayo ndiyo matakwa ya wananchi. Ninaamini kuwa hayo pia ni matakwa ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Ni muhimu lakini serikali ionyeshe kwamba inakubaliana na wananchi wake kuwa matatizo yote yatanzuliwe kwa kufuata sheria za nchi.
Kama kuna watu wenye kushutumiwa kwa kufanya mambo yasiyokubalika au wanaoshutumiwa kwa vitendo vya uhalifu basi lazima wahakikishiwe na wapewe haki zao zote za kikatiba wanaposhikwa na vyombo vya dola. Yasipofanyika hayo basi hivyo vyombo vya dola na hatimaye serikali yenyewe ndio wanaokuwa wahalifu wa sheria.
Jamii zilizoendelea kimaadili kwa kawaida huwapa wananchi wao haki za kimsingi za binadamu zikiwa pamoja na uhuru wa kusema, uhuru wa kukusanyika na wakujiunga na jumuiya yoyote waitakayo. Visiwani Zanzibar haki zote hizi zipo kwenye katiba lakini hazijatolewa tu hivi hivi na serikali. Zilipiganiwa na Wazanzibari wengi. Kuna baadhi yao walioyasabilia na kuyatolea mhanga maisha yao kwa nchi yao na watu wake wote.
Katika mazingira ya sasa ya Zanzibar lazima pawepo na amani endelevu na ilikuipata amani aina hiyo panahitajika utamaduni uliokomaa wa kuvumiliana kisiasa pamoja na siasa za ukinzani wa amani.
Hizi ni sifa muhimu za kuukuza mfumo wa kidemokrasia. Na hapa tunautafsiri mfumo huo kuwa ni ule wenye kusababisha kupatikana kwa maridhiano juu ya mambo kadhaa ya kimsingi kama vile kwa mfano kutokiukwa kwa uhuru wa nchi, umoja wa watu wake na msimamo wao wa kuiunga mkono serikali yao inapotetea maslahi ya nchi yao.
Ninavyohisi ni kwamba utaratibu huu wa amani na wa pande zote kuweza kukaa pamoja na kubadilishana mawazo ndio suluhisho pekee kwa matatizo yote ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar ya leo. Na kwa hakika tukiyaangazia masuala makuu yanayoikabili Zanzibar hii leo, tunaona kwamba suala kubwa kabisa linalowashughulisha wengi ni lile la mchakato unaoendelea wa kulitafutia taifa katiba mpya. Kuna haja kubwa ya kuhakikisha kwamba mengine yanayotokea kwenye ukingo wa medani ya siasa, ingawa yanaudhi, yasiubabaishe umma na kuufanya upoteze dira.
Hivyo ni muhimu kwamba pawepo busara na watu wajizuie kuongozwa na hamasa zao. Agizo hili ni muhimu hasa kwa viongozi wote wa kisiasa, viongozi ambao lazima wakate maamuzi yao kwa kulingana na mahitaji ya halisi ilivyo ili ule msingi wa ‘nguvu ya hoja’ na siyo ‘hoja ya nguvu’ uwe ndio wenye kuongoza mahusiano baina ya Wazanzibari na baina yao na serikali yao.
Hatutoweza kuiendeleza demokrasia endapo hatutambui kwamba ‘serikali ya kidemokrasia’ inadhamana ya, na inawajibika kwa, watu wote. Inatupasa pia tutambue kwamba serikali aina hiyo haipaswi kuwabagua wale waliovipigia kura vyama vingine na wala haipaswi kuvihodhi vyombo vya dola au idara ya utumishi wa serikali kwa sababu za kiitikadi.
Iwapo serikali itayafanya hayo isiyopaswa kuyafanya basi itawanyima haki za kiraia na kuwatenga wale wasionufaika na fadhila za utawala.
Katika hali nyeti inayoibuka sasa Zanzibar kuna umuhimu kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuonekana kwamba inafanya kazi pamoja kwa ushikirikiano wa wabia wake wote katika kuendesha shughuli za nchi. Serikali sharti iwaonyeshe wananchi wake kwamba sera zake zote zinakubaliwa na wabia wote wawili katika serikali hiyo (yaani chama cha CCM na kile cha CUF) na kwamba wote wanachukua dhima ya pamoja kuhusu maamuzi yote ya serikali. Hiyo ndiyo njia ya pekee ya kuhakikisha kwamba pataendelea kuwako umoja, amani na utulivu wa kisiasa katika nchi yetu.
Raia Mwema

No comments:

Post a Comment