Thursday 15 November 2012

Wapeni uongozi wapenzi wa busara

Hekima za Barazani kwa Ahmed Rajab
HUU ni wakati wa Wazanzibari kusimama na kuwashika masikio viongozi wao. Chokochoko zinazofanywa chini kwa chini na matamshi ya uchochezi tuliyoyasikia hivi majuzi yakitamkwa hadharani, tena kinaganaga, na viongozi wachache wa CCM/Zanzibar ni mambo ambayo hayawezi kuvumiliwa katika karne ya 21.
Hotuba zilizojaa chuki za kikabila na vitisho vya kutumia nguvu na zenye lengo la kuichafua hali ya utulivu iliyopo nchini tangu papatikane Maridhiano ni mfano wa matamshi ya uchochezi (‘hate speech’).
Kanda za video za hotuba hizo ni ushahidi madhubuti wa kuweza kuwafungulia kesi wenye kuyatoa matamshi hayo. Inasikitisha kuona kwamba viongozi wakuu wa chama cha CCM wamekaa kimya wakiwasikia viongozi wa ngazi za chini wakitoa matamshi ya usaliti na uchochezi. Inasikitisha zaidi kuiona Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hasa vyombo vyake vya kisheria pia imekaa kimya bila ya kuwachukulia hatua wanaohusika au hata angalau kuwakemea.
Nina hakika kwamba lau matamshi kama hayo yangekuwa yametamkwa nchini Kenya basi wanasiasa hao wangelikwishajikuta mahakamani wakijibu mashtaka ya uchochezi.
Ingekuwa hivyo kwa sababu Kenya ya leo ina katiba ambayo, ingawa ina madosari yake, haivumilii mambo ya kipuuzi lakini yenye hatari kama hayo. Kadhalika Kenya ina asasi za kiraia pamoja na vyombo vya habari vilivyo macho vinavyokemea dalili zozote zinazoweza kusababisha mauaji ya raia.
Vivyo hivyo, vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, vitendo vinavyofanywa na vyombo vya dola kuwadhalilisha wananchi navyo pia haviwezi kuvumiliwa katika jamii inayojinasibisha na mfumo wa demokrasia.
Katika mfumo wa demokrasia tunaosema kuwa tunauiga dola lazima iwe na uhalali. Na uhalali huo unaweza kujengwa juu ya mihimili mitatu: utawala bora, uongozi stadi na ufanisi katika kuwakidhia wananchi mahitajio yao.
Katika hali hii iliyopo sasa utawala bora maana yake ni kuvifanya vyombo vya kisheria vya dola vichukue hatua zinazostahiki bila ya upendeleo. Uongozi stadi maana yake ni kuwa na viongozi wanaojitokeza wazi na kuchukua hatua au kukemea pale mambo yanapoonekana kuwa na dalili ya kwenda kombo bila ya kujali iwapo wenye kusababisha hayo ni watu wa chama chao au la. Na kuwakidhia wananchi mahitajio yao ni kuwapatia raia wanachokihitaji kwa ustawi wao.
Wazanzibari wamechoka kuhasimiana kisiasa. Wameona jinsi uhasama wa kisiasa ulivyowahasirisha kwa kipindi cha miongo kadhaa. Ndiyo maana zaidi ya thuluthi mbili yao walioshiriki katika kura ya maoni ya kihistoria wakakubali pawepo Maridhiano na paundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa baina ya vyama vikuu viwili vya kisiasa Visiwani humo yaani CCM na CUF.
Wazanzibari wengi walikuwa na matumaini mema ilipoundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Novemba 2010. Walihisi kwamba kupatikana Maridhiano na kuundwa kwa serikali ya aina hiyo kutaipatia Zanzibar amani, utulivu wa kisiasa, maendeleo na umoja wao. Kwa sababu hizo waliiunga mkono moja kwa moja serikali mpya ilipoundwa.
Zanzibar ilipiga hatua kubwa ya kuelekea mbele yalipopatikana Maridhiano na ilipoundwa serikali hiyo. Sasa kuna wasiwasi kwamba inaweza ikarudi nyuma. Hivyo ni jambo la busara kwamba viongozi wa Kizanzibari na waliomo kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa wakabiliane vilivyo na changamoto iliyopo na waendelee kuyatafutia ufumbuzi matatizo yote ambayo lazima yataendelea kuzuka.
Msimamo wao uwe ni wa kuangalia mbele, na si nyuma. Tena uwe ni msimamo wa kujitolea kuziondosha tofauti zote zilizo ndani ya jamii kwa njia ya kindugu ili waweze kuyatetea maslahi ya Zanzibar na ya watu wake wote.
Haya yote ni muhimu hasa kwa vile mustakbali wa Zanzibar huenda ukaamuliwa katika kipindi cha kasoro miaka miwili ijayo kufikia 2014 pale utapomalizika huu mchakato wa sasa wa kulipatia taifa katiba mpya.
Kwa hivyo, ni muhimu kwamba mawaziri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa wawe wanayatetea na kuyapigania matakwa ya raia waliowachagua na wasiende kinyume nao kwani endapo zoezi hili la katiba halitokuwa na matokeo ya kuwaridhisha wengi wa Wazanzibari basi kutaendelea kuwako na manung’uniko ya kisiasa. Tena zoezi hilo litakuwa limeshindwa kuutafutia ufumbuzi ule mgogoro wa muda mrefu kati ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.
Kwa hili ni muhimu kwamba Wazanzibari wawasihi viongozi wao wa vyama vyote vya kisiasa wafanye mambo kwa busara na wavumiliane kisiasa. Kama kuna tofauti zozote zinazozuka ndani ya Serikali basi watumie njia za mazungumzo na za kidemokrasia ili wapatane na kuhakikisha kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa inafanikiwa katika utekelazaji wa sera zake, hasa zile zinazohusika na maslahi ya Zanzibar na ustawi wa Wazanzibari wote bila ya kujali mielekeo yao ya kisiasa.
Inafaa Wazanzibari wawakumbushe viongozi wao wasia wa Plato, yule mwanafalsafa wa Kiyunani, aliyewahi kusema kwamba: “Wanadamu kamwe hawatoona mwisho wa matata mpaka pale wapenzi wa busara wataposhika madaraka ya kisiasa, au pale wenye madaraka watapokuwa wapenzi wa busara.”
Wawakilishi wa Kizanzibari ndani ya vyombo vyote vya maamuzi kuhusu suala la katiba wanabeba jukumu kubwa. Hawa ni wale wenye kuiwakilisha Zanzibar ndani ya Serikali ya Muungano, ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hata wale wawakilishi 15 wa Kizanzibari walio katika Tume ya Katiba.
Ikiwa watafanya kazi zao bila ya kuuzingatia uzalendo wao na kwa maslahi ya Zanzibar na badala yake wakijiachia waongozwe na mazingatio ya maslahi yao binafsi au ya vyama vyao basi wataiangusha Zanzibar na Wazanzibari wenzao na watasababisha madhara makubwa yatayohitaji vizazi kadhaa kuyaondosha.
Chanzo: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment