Tuesday 13 November 2012

Baharia Karume Aegesha Chombo Bandarini

Rais Mstaafu wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM (Zanzibar), Mhe. Amani Karume, amewapa darasa zuri la uongozi na demokrasia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama chake na wananchi kwa ujumla hasa kuhusiana na mwelekeo wa siasa Zanzibar. Alisema hali ya kisiasa Zanzibar ni ya kuridhisha na yenye amani na utulivu ambapo fujo na ghasia za hapa na pale zinatokana na wanaharakati na siyo wanasiasa. Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikubaliwa kupitia vikao vya CCM lakini iliamuliwa kwa kupitishwa na Wazanzibari ambao kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ndiyo waamuzi wa mwisho wa mustakbali wa kisiasa wa Zanzibar. Viongozi wa CCM Zanzibar wasipowatendea wema wananchi watawakumbuka wakati wa uchaguzi ukifika. Ubaguzi, ubabe na kuchochea mfarakano si katika malengo ya ASP. Kila mtu aachiwe kuwa huru kutoa maoni anayoyataka kuhusiana na Mjadala wa Katiba Mpya na watu wasiitwe majina mabaya kwa sababu tu maoni wanayotoa hayaungwi mkono na baadhi ya watu. Tumewataka watu watoe maoni yao, basi tuheshimu mawazo yao. Wanaotaka Muungano uendelee ni haki yao, wanaotaka Serikali mbili kama zilivyo, wanaotaka Serikali mbili za Mkataba, wote waheshimiwe. Tume ya Katiba ndiyo iliyopewa kazi ya kukusanya maoni ya wananchi, iachiwe ifanye kazi yake. Hatimaye maoni ya walio wengi yaheshimiwe. Uongozi ni kazi nzito, na mimi nina asili ya ubaharia kupitia kwa baba yangu. Leo nakiegesha chombo salama bandarini na nina-sign off. Ni jukumu la wenzangu sasa kukipeleka chombo salama. Muhimu tujifunze kuvumiliana. Hapa kwenye Mkutano Mkuu huu, Mwenyekiti kaalika viongozi wa vyama vya upinzani na wametwambia maneno ya maana ya kutushauri. Ingekuwa Zanzibar kumefanyika yale tungeitana kila majina mabaya. Tujifunze kuvumiliana.
Chanzo: Mzalendo

No comments:

Post a Comment