Thursday 29 November 2012

Karume “mpuuzi”, lakini ukweli wake mchungu

MAKALA hii itahitimisha tathmini yangu kuhusu Mkutano Mkuu wa 8 wa CCM uliofanyika Dodoma tangu Novemba 11 hadi Novemba 14 mwaka huu.
Kwa kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ni chama dola, vimbwanga vyake huwa vinachanganya watu na kuamini kuwa kila baada ya Mkutano Mkuu, CCM huwa inazaliwa upya.
Imani hii imejengeka kutokana na ukweli kuwa, kabla ya Mkutano Mkuu, huwa kuna dalili za migawanyiko na mipango kadhaa ya makundi kutaka agenda zao zishinde.
Kutokana na udhibiti wa vyombo vya dola pamoja na ushabiki uliopitiliza, mipango hiyo huwa inakwama na kuwafanya watu wengi kuamini kuwa CCM ina wenyewe, na wenyewe hao huwa wanaifanya izaliwe upya kila baada ya Mkutano Mkuu!
Historia ya dhana hii ni ndefu, na wahanga (victims) wa mkakati huu kwa miaka ya karibuni ni Salmin Amour (Komandoo), Mzee John Malecela, Dk. Gharib Bilal, Samuel Sitta na sasa Edward Lowassa.
Kwa miaka ya nyuma wanakumbukwa Mzee Aboud Jumbe na Sharrif Hamad. Kwa sababu zilizo wazi, mkakati huu wa kuipa uhai mpya CCM huwa unawaathiri sana Wazanzibari kuliko Watanganyika.
Rais Karume na “upuuzi” wake
Kama Makamu Mwenyekiti anayemaliza muda wake, rais mstaafu Amani Karume alikaribishwa kutoa nasaha zake siku ya kufunga mkutano. Alitoa hotuba, ambayo hivi sasa inaitwa ya kipuuzi huko Magogoni na mtaa wa Lumumba.
Hakuna aliyetarajia kuwa Karume angesema maneno aliyoyasema siku hiyo kiasi cha Mwenyekiti Jakaya Kikwete kukiri kuwa “hajawahi kumwona amefurahi kiasi hicho” kama alivyomwona siku hiyo.
Mara kadhaa hotuba yake ilikatishwa na watu waliomzomea na kumtaka amalize na kukaa. Hii ikakumbusha enzi za uenyekiti wa Benjamin Mkapa wakati wanamtandao wa Kikwete walipokuwa wakimzomea kila mtu aliyetaka kuhoji matumizi ya rushwa katika mkutano huo.
Mzee Joseph Butiku anaikumbuka hii na aliiandikia barua rasmi kwa Mwenyekiti Mkapa. Hii itukumbushe kuwa zomea zomea haikuanza na CHADEMA katika mikutano.
Alipozomewa sana, Rais Karume akawafananisha wazomeaji na vinywa vya samaki! Wapo waliodai, Rais Karume alikuwa kalewa sana konyagi siku hiyo. Awe alilewa au hakulewa; ni mpuuzi au si mpuuzi; kwangu mimi si habari. Habari muhimu ni yale aliyoyasema kwa dakika alizopewa.
Karume alizungumzia kadi yake ya ASP (Afro Shiraz Party); akaelezea madhumuni ya ASP; akamwuliza Dk. Shein ikiwa yeye anayo kadi yake ya ASP. Moja ya madhumuni ya ASP akakumbusha kuwa ni kulinda uhuru wa Zanzibar na watu wake. Ndipo akahoji wale wanaowazuia wenzao wasitoe maoni yao kuhusu Muungano.
Akamkumbusha Rais Kikwete kuwa alitoa ruhusa kila mtu aseme anachotaka wakati wa mchakato wa kutoa maoni ya katiba mpya. Akahoji iweje sasa wengine wanakamatwa kwa kutoa maoni yao. Karume akakumbusha jinsi CCM ilivyopoteza baadhi ya majimbo kwa sababu ya kupuuzia maoni ya wananchi. Akakumbusha suala la zamu kati ya mbunge na mwakilishi katika jimbo fulani. Wazomeaji hawakutaka kusikia haya wakamwimbia taarabu ya “uamsho uamsho”.
Niseme wazi hata kama nilichoka nikakaa nje ya ukumbi wakati anaongea, Karume alisema mambo ya maana kuliko hotuba za masaa zilizotolewa na waheshimiwa wengine. Kwa muda mfupi, Karume aliuzodoa udikteta unaoabudiwa ndani ya CCM; alibainisha hatari zinazoukabili Muungano; alikumbusha habari za zamu za kuongoza nchi hii iliyotokana na nchi mbili; na zaidi sana alisema kutoka moyoni kuwa ASP haijafa kwa sababu waliokuwa wanachama wake wangali bado hai. CCM tumeze au tuteme, huo ndio ukweli kutoka kwa Karume, ambao sasa unaitwa ni upuuzi na akina Nape Nnauye.
Kulialia na kulalama kulizidi mno
Kwa siku tatu, Watanzania walishuhudia wajumbe zaidi ya 2000 wakilialia na kulalamika ndani ya ukumbi. Mwenyekiti alizindua uliaji huo na kupokewa na wajumbe kwenye vikao visivyo rasmi katika nyumba za kulala wageni na kwenye magari. Kivuli cha Chama cha Denokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliwatesa sana wajumbe na kuwafanya viongozi kupoteza mwelekeo na kuanza kutukana ovyo ovyo.
Haikutarajiwa kuwa Mwenyekiti naye angeingia katika mtego huo, pale alipojikuta anawatukana wapinzani na hasa CHADEMA kwa kuwaita “watu wazima ovyo”, au pale ndani ya NEC alipojikuta anatumia muda mwingi kumpamba Nape Nnauye kwa kuwa anajua kutukanana na CHADEMA. Hata pale alipokumbushwa na rafiki yake kuwa kuitukana CHADEMA si lazima kuijenge CCM, yeye aliishia kusema “wamezidi acha Nape awashughulikie”. Kazi inayomshinda yeye, anaona ni bora aifanye Nape. Kama Mzee Rashidi Kawawa alivyokuwa kwa Mwalimu, Nape ndivyo kwa Kikwete!
Mzee mkorofi kutoka Nyanda za Kusini alihoji, inakuwaje CHADEMA iwe tishio kwa CCM kuliko ufisadi na rushwa ulivyo tishio? CHADEMA inakuwaje tishio kuliko “unduguneizesheni” unaotafutiwa nafasi ya kutambuliwa kwenye katiba ya chama chetu?
Akasema, inakuwaje washauri wakuu wa Mwenyekiti wa chama chetu kuhusu masuala ya chama, si vikao bali ni wanausalama waliojaa fitina? Huyu naye alikuwa analalama sawa tu na wengi waliokuwa wanalalamika kwa siku tatu za mkutano.
Membe: Alimzamisha Mangula; Amemuibua tena.
Nafasi ya Bernard Membe kwa siasa za taifa hili kwa siku za usoni ilikuwa katika mtihani mgumu sana. Kambi ya rafiki yake wa zamani Edward Lowassa ilipania kumzamisha lakini akaokolewa na Kikwete na familia yake.
Kikwete alimsaidia kwa kubadili ratiba za upigaji kura, wakati familia yake (mkewe na mtoto wake) walihaha kila kona kumtafutia kura Bernard Membe. Taifa hili siku moja litadai kujua ukweli wa uhasama na urafiki wa watu hawa watatu – Membe, Kikwete na Lowassa. Jina Kikwete limekaa katikati kwa makusudi. Yeye ni ufunguo wa kitendawili hiki. Hili tuliache kwa sasa.
Mzee Philip Mangula, akaibuka ghafla kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara. Ni huyu huyu ambaye kundi la mtandao lililomwingiza Ikulu Kikwete lilidai alilitesa sana wakati wa kampeini na kuamua kumtosa mara baada ya Kikwete kuapishwa.
Yasemekana, Benard Membe, kachero mzoefu na kiini cha mikakati ya wana mtandao asilia, alimwambia Kikwete kuwa Mangula aliwapa taabu sana hivyo aondolewe kwenye nafasi ya ukatibu mkuu wa chama. Haikuishia hapo, Mzee Mangula alipojaribu kuibukia Iringa kama Mwenyekiti wa Mkoa alishughulikiwa vikali na kuangushwa na mtu asiyefanana na CCM kwa vigezo vyote.
Mzee Mangula alikiri baadaye kuwa ndani ya CCM uongozi uko mnadani na wapiga kura hawataki tena vipeperushi vya wagombea, bali wanataka “vipeperushwa”. Mzee Mangula, kila anapokumbushwa harakati za wana mtandao, huwa anatania kuwa yeye aliponzwa na “faili maalumu”.
Kuna habari kuwa Mzee Mangula kaibuka kwa mkono wa Membe. Kwamba, vikao kadhaa vilifanyika Makambako kati ya wawili hawa. Iwe kwa Membe kujituma au kutumwa, ni kwamba walikutana na agenda ilikuwa ni uchaguzi katika Mkutano Mkuu wa 8.
Aliombwa radhi au hakuombwa, hilo sasa si habari. Habari ni kuwa, Mkutano Mkuu umempitisha Mzee Mangula kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM lakini mshenga mkuu alikuwa Membe. Kama ushenga huu ulikuwa ni kwa manufaa ya chama au kwa manufaa ya mtandao wake anaouunda kwa ajili ya 2015, ni suala la wakati.
Ikiwa ni kweli, basi itakuwa vigumu kukemea mitandao ndani ya chama hiki kikongwe. Kama mtandao wa Membe ni halali, wa Lowassa hauwezi kuwa haramu. Kama Kikwete aliingia kwa mtandao, ni vigumu kuifikiria CCM na urais bila mtandao. Na tumejifunza kwa uchungu kuwa mtandao hauishii katika uchaguzi kwa sababu, baada ya mtu wao kuchaguliwa, kinachofuata ni kufaidi jasho na matunda ya kazi.
Kwa walioshindwa, kuna kazi ya kutathmini ni wapi wamekwama na kuazimia aluta continua. Ni ndoto kuambiana kuvunja makundi wakati anayeshinda na kuingia Ikulu anaendelea na kundi lake.
Jambo moja tu Mzee Mangula alizingatie. Membe anayedaiwa kumzamisha baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 mbele ya Kikwete, hawezi kugeuka leo na kumtetea kuwa ni mtu mzuri anayekifaa chama. Kwa nini hakufaa mwaka 2005 chini ya Mwenyekiti huyuhuyu? Membe ni yule yule, Mwenyekiti ni yule yule, chama ni kile kile na Mangula ni yule yule! Ni kitu gani kimebadilika kumfanya Mangula asiyefaa mwaka 2005, afae mwaka 2012?
Kinachoonekana lakini hakizumguziwi waziwazi, ni ukweli kuwa Kikwete na Membe wanamwona swahiba/hasimu wao Lowassa kuwa sasa ni zaidi ya mgombea urais wa CCM 2015. Kwao, Lowassa amegeuka kuwa chama; ameiteka CCM mbele ya macho yao na wanadhani Mangula atawasaidia kuiokomboa CCM iliyo mateka mikononi mwa Lowassa. Kikwete na Membe hawajiulizi ni kitu gani kimemjenga Lowassa na kumfanya kuiteka CCM.
Kitendo cha kumkimbilia aliyekuwa “adui” yao na chama chao kuwa aje kuwasaidia kukijenga chama walichokibomoa kwa mikono yao, hakieleweki. Wengi tulidhani, Mkutano Mkuu ungepata nafasi ya kutathmini hali hii, badala yake tukaambulia kulialia na vijembe visivyo na mpangilio. Tusubiri Mkutano Mkuu mwingine maalumu au ule wa 2017.
Chanzo: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment