Na Salim Said Salim
TUNAAMBIWA kuwa hapa nyumbani na nje katika mfumo wa utawala bora wa haki na
sheria dhamana kwa mshitakiwa ni haki, japokuwa mahakama ndiyo yenye uamuzi wa
mwisho juu ya suala hili.
Nchi nyingi zenye utawala wa demokrasia zimeweka utaratibu unaojaribu kwa
kiasi fulani kuhakikisha mahakama hazitumii vibaya mamlaka yake katika suala la
dhamana.
Hii ni kwa sababu ipo dhana yenye nguvu inayosema kumuwekea mshitakiwa
masharti magumu ya dhamana yanatoa tafsiri ya kuwa sawa na kumnyima dhamana au
kuanza kumuadhibu mtuhata kabla hajatiwa hatiani.
Katika baadhi ya kesi zinazoendelea Zanzibar hivi, hasa zile zenye harufu ya
kisiasa, kuchimba almasi au dhahabu ni rahisi kuliko kupata dhamana.
Hali hii imesababisha baadhi ya watu,Visiwani na nje, kuuliza kwa kiasi gani
mahakama za Zanzibar zipo huru?
Mimi ukiniuliza jibu langu ni kwamba nasikia kuwa zipo huru, lakini sizioni
kuwa huru.
Baadhi ya watu Visiwani, hasa wanasheria, wanasema panapokuwepo kesi zenye
mashiko ya kisiasa ya aina moja au nyingine mahakama za Zanzibar huwa
zinendeshwa kwa kitufe cha mbali (remote control).
Maelezo haya yamepata nguvu kutokana na mahakimu na majaji kueleza mara
nyingi kuwa wamekuwa wakipewa amri na wakubwa, baadhi ya wakati kwa kutumiwa
vikaratasi, juu ya namna wanavyotakiwa kuendesha kesi.
Unapokuwa na mtindo wa aina hii, hata ikiwa kwa kesi chache sana, basi
majumuisho unayopata ni kuwa mahakama hazipo huru na kwamba zimegeuzwa kuwa
sehemu ya utawala badala ya kuwa eneo lililo huru na linalotoa na kulinda
haki.
Mahakama za Zanzibar hivi sasa zimekuwa zikitoa masharti ya dhamana ambayo
unaweza kusema magumu sana au hayatekelezeki na hali hii imezusha wasi wasi juu
ya huo uhuru wa mahakama unazungumzwa.
Zanzibar imekuwa na sifa ya kuweka masharti magumu ya mtuhumiwa kupewa
dhamana na baadhi ya masharti haya ni ya aina yake na ya kipekee ambayo husikii
kuwekwa Tanzania Bara au katika nchi yoyote ile inayojinadi kuwa na mazingira ya
utawala wa haki na sheria.
Baadhi ya masharti haya, kama nilivyoeleza siku za nyuma, yana sura chafu ya
kuwabagua raia na kuwaweka katika madaraja mawili, moja la watukufu na lingine
ni la watu ambao mahakama haitaki kuwaamini. Hawa watukufu ni wale wanaofanya
kazi serikalini na wasiostahiki kuaminiwa na kuheshimiwa ni wale ambao sio
wafanyakazi wa serikali.
Siku hizi imekuwa kawaida kusikia mshitakiwa anaambiwa kwamba wadhamini wake
lazima wawe watumishi wa serikali wakati inajulikana wazi kuwa mtumishi wa
serikali hawezi kuhatarisha ajira yake kwa kukubali kuwa mdhamini katika kesi
ambayo watuhumiwa wake wamekuwa wakizungumzwa na viongozi wakuu wa nchi.
Mfano mmoja ni wa kesi inayowakabili viongozi wa jumuiya ya Kiislamu ya
Uamsho. Hivi mfanyakazi gani wa serikali atajitokeza kuwawekea dhamana?
Tusidanganyane, huu sio mchezo mzuri na ndio maana wananchi wengi na hata hao
tunaowaita washirika wetu wa maendeleo wanauona hauonyeshi haki kutendeka.
Au vipi kijana ambaye hana hata kiwanja utamtaka aweke dhamana waraka wa
nyumba wakati hata hivyo viwanja hugawiana wakubwa na watu wanaohusika na
ugawaji hujigawia wao, watoto, wake zao na hata wajukuu? (angalia ripoti ya tume
ya uchunguzi juu ya ugawaji wa viwanja).
Kama majina ya kweli na sio ya bandia ya watu waliopewa viwanja yatawekwa
hadharani utaona watu hoe hae kama akina Salim Said Salim ambao hawapo tayari
kuwaabudu viongozi kwa ajili ya kutaka vyeo au kulinda urafiki hutayaona.
Majina ya waliopewa viwanja yatawekwa hadharani. Sasa vipi mtu masikini
utamtaka aweke kaburi la mzee wake.
Jamani zama za kuifanya Zanzibar kuwa na haki ya kufanya tutakalo, licha ya
kutia saini mikataba ya kimataifa ya kuheshimu haki za binaadamu, ikiwa pamoja
na za washitakiwa, zimepita. Siku hizi nchi haziruhusiwi na hzivumiliwi ukiukaji
wa haki za binaadamu au za washitakiwa.
Mtindo huu wa kuwabagua watu wa Zanzibar kwa mafungu ni wa hatari na
utaiathiri Zanzibar. Fikiria serikali itahisi vipi kama watatokea watu na kusema
wanaoruhusiwa kuingia katika hoteli au maduka wanayoyamiliki ni wale tu ambao
sio watumishi wa serikali?
Kama serikali kupitia mahakama, ina wabagua watu kwanini na wananchi nao
wasiwe na haki ya kuendeleza sera hii ya ubaguzi kwa kutumia mali zao?
Lakini kama serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar inataka kurejea tulikotoka
ambapo kulikuwepo mahakama za wananchi (mahakimu wazee wanaosinzia hovyo) na
kutojali uhuru wa mtu na hata kutoa hukumu kabla ya kesi kusikilizwa basi
serikali isione aibu kutamka hivyo.
Kinachosikitisha ni kuona haya yanafanyika wakati Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali na ile ya Mkurugenzi wa Mashitaka inaongozwa na watu wenye
kuheshimika katika fani ya sheria, lakini wamekaa kimya kama vile kutoa masharti
magumu au kumnyima mshitakiwa dhamana ni jambo zuri na linalofaa kupongezwa.
Nilitegemea wanasheria wenye kuheshimika kama hawa wawili wanaoongoza taasisi
hizi muhimu za serikali, wangejitokeza kupinga mwenendo huu wa kibaguzi, lakini
inaonekana wameweka maslahi yao mbele kuliko yale ya kulinda haki na sheria.
Wazanzibari waache utamaduni wa kulindana kwa maovu. Watu anaojiita waungwana
hulindana kwa mambo mazuri na sio mabaya, hasa yale yanayoitia nchi dosari.
Lakini hata jumuiya za kiraia zimekaa kimya, labda kwa kuhofia msajili kuzifuta,
lakini ukweli lazima usemwe, potelea mbali liwalo na liwe.
Wazanzibari wanataka kuwa na utawala wa haki na sheria za kweli na sio bandia
kama inavyojitokeza sasa.
Wazanzibari wengi walikuwa na imani na matumaini makubwa na serikali ya umoja
wa kitaifa katika kusimamia haki na sheria, lakini kinachoonekana hivi sasa ni
kwamba ndoto yao haikuwa ya asubuhi, mchana wala usiku.
Hakuna kitu kibaya katika nchi inayojigamba kuwa na utawala wa kidemokrasia,
halafu zikaweopo dalili za vyombo vya dola na mahakama kutumika vibaya na hasa
kuridhia kile kinachoonekana kama utashi wa kisiasa.
Mpaka sasa viongozi wa Uamsho hawana kosa mpaka pale itapothibitishwa bila ya
wasi wasi wowote na mahakamani kuwa shutuma zinazowakabili ni za kweli na sio za
kusingiziwa au kubunia.
Watu waliokabiliwa na mashitaka ya kuingiza dawa za kulevya ambazo zinaathiri
maisha ya mamia ya watu, waliodaiwa kuiba mabilioni ya fedha, waliodaiwa kufanya
uzemba wa meli kuzama na watu wengi kufa na wanaosemekana wameajiri wafanyakazi
hewa na kuitia hasara serikali wamepata dhamana.
Ni muhimu kuelewa kwamba dunia ina tuangalia na kutucheka. Tufanye mambo
mezani na kutumia hekima na busara.
Vile vile tuelewe kwamba dunia inatuangalia na hapo tutakapolaumiwa kwamba
tuliziendesha mahakama zetu hovyo tusije tukasema tunaonewa.
Tujuwe kuwa hatimaye tutapanda tunachovuna, lakini historia itatukumbuka
baadhi yetu kuwa tulikataa kupalilia mbegu mbaya.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment