Na Salim said Salim
KATIKA mwisho wa mwezi Aprili, mwaka 2005 nilieleza katika gazeti hili namna
nilivyosikitishwa na kushitushwa na baadhi ya watu katika nchi mbali mbali
walivyodhalilishwa, kuteswa na hata kuuliwa na vyombo vya dola kwa visingizio
mbali mbali.
Vyombo vya dola ambavyo ndio dhamana vya usalama wa raia vilikataa kuhusika
na kuishia kulaumu wahuni.
Lengo la makala ile lilikuwa kuieleza serikali ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar,
komandoo Salmin Amour, kwamba historia haitafumbia macho mwenendo wake wa
utawala na kumtaka achukue haraka zitakazowapa nafasi watu wa Visiwani kuiona
serikali kuwa ni yao na ipo kwa masilahi yao.
Hivi sasa komandoo anakumbukwa zaidi kwa vitendo vile kuliko mengine. Leo
ninakusudia kurejea simulizi ile kwa vile yanayotokea Zanzibar hivi sasa yana
muelekeo unaotaka kufanana na tuliyoyaona wakati wa utawala wa komandoo.
Katika makala yangu ile ya zaidi ya miaka saba iliyopita nilieleza kuwa
nilipokuwa kijana mdogo ninasoma Czechoslovakia, sasa imegawika na kuwa nchi
mbili za Czech na Slovak, katika mwaka 1964 nilitembelea kijiji kimoja cha
Slovakia, nje kidogo ya mji wake mkuu wa Bratislava.
Nilielezwa namna ambavyo kijiji hiki kilichopo kando kando ya Mto Danube,
kilivyoshuhudia halaiki ya aina yake wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia
(1939-45).
Maelezo niliyoyapata kutoka kwa watu walioshuhudia halaiki ile na kupoteza
ndugu, jamaa na marafiki ilinipelekea kukosa usingizi kwa karibu wiki nzima.
Maelezo yale yalikuwa juu ya namna askari wa kinazi wa Adolf Hitler, dikteta
wa Kijerumani aliyesababisha vita walivyotesa watu na kutia moto nyumba huku
watu wakiwamo ndani usiku na mamia kupoteza maisha.
Furaha yangu ya kutembelea Slovakia ilinitumbukia nyongo, lakini nilipata
mafunzo ya namna mbavyo madikteta wanavyokuwa hawathamini maisha ya watu.
Hadithi za kusikitisha za watu wale sitazisahau daima. Sikujua kwamba ipo
siku nitakaporudi nyumbani nitasikia hadithi zinazofanana kwa kiasi fulani na
zile.
Nilieleza mara kadhaa nilipokuwa Addis Ababa, Ethiopia, wakati wa utawala wa
Mengistu Haile- Mariam, ambaye sasa anaishi Zimbabwe kama mgeni wa rafiki yake
Rais Robert Mugabe.
Niliwaona askari wa mgambo waliokuwa wakiitwa Kabele walivyokuwa wakipiga
watu barabarani na majumbani. Walichokuwa wakifanya waliiga askari wa dikteta wa
Haiti Papa Doc waliojulikana kama Tom Tom Makut.
Siku moja nilipokuwa Addis Ababa, katika eneo linaloitwa Markato, yaani
markiti (sokoni) vijana hao waliwapiga watu wawili mpaka wakafa hapo hapo na
siku ya pili yake vyombo vya habari vya serikali vilieleza kuwa vijana wale
walikuwa wapinga mapinduzi na wachochezi.
Kosa lao ni kuwa vijana wale hawakuitikia na kukaa kimya pale mwanamgambo
mmoja wa Kabele aliposema kwa sauti ‘Maisha marefu kwa Mengistu’.
Kila mtu alitarajiwa ajibu : ‘Aishi’. Baadaye nilikuja kupata habari kwamba
mmoja alikuwa amelewa na mwingine alikuwa hasikii vizuri.
Nilikwenda Arusha ambapo nilifanya kazi kama mwandishi wa magazeti ya
serikali ya Daily News na Sunday News kabla hayajataifishwa mwaka 1971.
Huu ni mji nilioufurahia sana kwani maisha yalikuwa mazuri kwa kipindi cha
karibu miaka saba niliyokuwepo huko tangu mwaka 1967, mara tu baada ya kuundwa
jumuiya ya kwanza ya Afrika Mashariki.
Lakini nilipotembelea Arusha mwaka 2000 kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari
nilijikuta nakumbuka Czechoslovakia. Hii ilitokana na siku moja kwenda
kusikiliza kesi za mauaji ya halaiki ya Rwanda ya 1994.
Sikustahamili na nilitoka nje mapema kutokana na maelezo yaliyotolewa
kuonesha binadamu anavyoweza kupoteza utu wake na kuwa mnyama, katili kama
nilivyowaona wanyama pindi nilipotembelea mbuga za Manyara, Ngorongoro,
Serengeti na Momella nilipokuwa ninaishi Arusha.
Mashahidi walielezea mauaji na mateso yaliyofanywa na vijana wa Interahamwe
yaliyoandamana na uchomaji nyumba moto huku watoto wadogo wakilia ndani
walivyokuwa wakijiona wanapoteza maisha yao wakiwa hawana la kufanya.
Wakati nilipoandika makala ile kwa gazeti hili nikiwa Zanzibar nilishuhudia
mambo ambayo sikutaka kuyaamini.
Siku moja baada ya kutoka Ofisi ya Tume ya Uchaguzi Kilimani, nilipigiwa simu
kwenda Hospitali ya Al-Rahma iliyokuwepo masafa ya mita 300 toka mahali
nilipokuwepo.
Nilipofika hapo niliona watu waliokatwa katwa mapanga kichwani, miguuni na
wengine kupigwa nondo, huku wakimiminika damu. Wawili walikuwa wamepoteza
fahamu. Ilinikumbusha mbali na kutoamini niliyoyaona. Picha na video za matukio
yale zipo.
Jumla ya watu waliofikishwa pale wakiwa majeruhi walikuwa 10, wote taabani na
nilielezwa kuwa walipigwa mapanga na nondo wakati wakingojea kujiandikisha kuwa
wapiga kura katika kituo cha Kijiji cha Kinuni.
Wakati ule watu wengi walichomewa moto nyumba zao na kulazimika kwenda kuishi
porini na kupoteza mali zao. Visima na maskuli yalitiwa kinyesi na kina fulani
ili papatikane visingizio vya kukamata watu.
Baadaye komandoo aliamrisha kuvunjwa nyumba kadha hapo Mtoni Kidatu na wapo
waliopoteza maisha yao kwa mshituko wa moyo na ufukara waliotiwa na komandoo kwa
sababu za kisiasa. Kinara wa uvunjaji nyumba zile alidaiwa kuwa ni Mkuu wa Mkoa
wa Mjini Magahribi, Abdulla Rashid.
Watu wengi, hasa wenye asili ya Kisiwa cha Pemba, walifunguliwa kesi bandia
za madai ya kuwa wazembe na wazururaji au kumtukana rais. Ilikuwa balaa ya aina
yake.
Kwa hakika hali hii si tu kuwa ilikuwa inasikitisha, bali pia ilikuwa ya
kutisha. Wakati ule nilisema: Hii ni hali ambayo haipaswi kunyamaziwa kimya na
aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Omar Mahita.
Nilimueleza Mahita, kuwa baadhi ya hao waliopigwa vibaya sana ni maofisa
wastaafu wa Jeshi la Polisi ambao wakati ule walikuwa mara kwa mara wakikamatwa
na kupigwa panapotokea mtafaruku wa kisiasa Visiwani.
Nilieleza kuwa uzoefu wangu wa kufanya kazi kwa karibu na aliyekuwa Rais
Benjamin Mkapa alipokuwa Mhariri Mtendaji wa Daily News ulinipa mashaka kama
hali ile ya mateso waliokuwa wanapata Wazanzibari ilikuwa inamsumbua.
Wakati mmoja Mkapa alisema baadhi ya mambo ya Zanzibar yalikuwa yanamkosesha
usingizi, lakini nikaeleza wasiwasi wangu kama alikuwa na nia hasa ya kumaliza
balaa ile iliyokuwepo wakati ule. Sikushangaa alipomuachia urithi wa maovu yale
Rais Jakaya Kikwete mwaka 2000.
Nimeeleza haya hii leo kuonesha wasiwasi wangu kwamba ile hali mbaya ya siku
za nyuma huenda ikarudia Zanzibar kama hapatakuwepo ustahamilivu, kuondosha
uonevu na kuachana na mtindo wa kubuni kesi bandia.
Panapotokea mzozo sheria iachiwe ichukue mkondo wake na siyo kudhalilisha
watu kwa kuwapiga bakora, kuwanyoa ndevu, kuwanyima chakula na haki ya kukoga na
kubadili nguo wakati wakiwa mahabusu kama tunavyoona hivi sasa. Jamani tukumbuke
Mungu yupo!
Hivi sasa tayari watu wamekuwa na mashaka makubwa na hali iliyopo Zanzibar na
baadhi ya nchi zimeshaanza kulalamika juu ya vitendo vya uvunjaji wa haki za
binadamu Visiwani.
Sura iliyopo sasa Zanzibar ya serikali ya umoja wa kitaifa ni chafu na
inanuka na inahitaji kusafishwa na kufukizwa ubani na udi. Kweli Polisi
wanaosema hawahusiki wanashindwa kuwadhibiti hao tunaoambiwa ni vikundi vya
Ubaya Ubaya na Mbwa Mwitu?
Au Zanzibar ya leo ina vikundi vya mafia kama tunavyoona katika baadhi ya
nchi za Amerika ya Kusini?
Dunia inatuangalia na tayari taasisi za kutetea haki za binadamu kama Amnesty
International zinasema hakuna utawala bora Zanzibar.
Mahakama zetu lazima zifanye kazi ya kuonekana kuwa huru na si zinavyoonekana
hivi sasa. Hatutaki baadaye kuwasikia mahakimu na majaji wanajikosha kama
ilivyofanyika katika miaka ya karibuni kwamba walikuwa wanapelekewa vikaratasi
kuelezwa wazishughulikie vipi kesi mbali mbali.
Siasa ni mchezo wa mbinu nyingi za wazi na za siri, lakini huu mchezo mbaya
wa kupiga watu majumbani, kuchezea miili yao kwa kuwanyoa ndevu na kuifanya
dhamana kama siyo haki ya mshitakiwa ni wa hatari.
Viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Rais Ali Mohamed Shein na
Makamu wake wawili, Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Iddi, wajue wao ni
dhamana na hawawezi kukwepa dhamana hiyo watakapotakiwa watoe maelezo kwa nini
waliruhusu maovu yanayofanyika sasa.
Huu mchezo wa kunyamazia maovu, kama utaachiwa kuendelea, utatoa sura mbaya
katika kumbukumbu za historia kama ilivyo kwa iliyokuwa Czechoslovakia, Ethiopia
wakati wa utawala wa dikteta Mengistu, Chile wakati wa utawala wa Agostino
Pinochet na mauaji ya halaiki yaliotokea Rwanda.
Zanzibar haiwezi kukaribia huko lakini kila jambo lina mwanzo wake . Wakati
wa utawala wa komandoo Salmin Amour hali mbaya ilianza kama hivi na baadaye
tukashuhudia watu wengi wakipoteza maisha yao na kuwa vilema.
Orodha ya majina ya watu waliouawa, kujeruhiwa na kufungwa jela kwa maonevu
inajaza ukurasa huu. Huo ndio ukweli na waliofanya kama hawataki yaelezwe
wasingethubutu kutenda maovu yale.
Ni vizuri hatua zikachukuliwa haraka kuzuia hali tete iliyojaa hasama na
maonevu yaliopo sasa kudhibitiwa. Moto huanza na cheche na tayari cheche
tunaziona na zikiachiliwa watatokea watu kuzimwagia petroli.
Tusingojee moto kupanda juu ya paa na ndipo tukaanza kufanya juhudi za
kuuzima. Tukumbuke ule wimbo wa Malindi usemao: Moto ukija kuwaka mzimaji
nani?
Wale wenye kupanga njama hizi za maovu na kutaka kuirejesha Zanzibar
ilipotoka wasipewe mwanya wa kupumua. Mchezo wao utatuponza sote na kuja
kujutia.
Tukumbuke ni rahisi kubomoa kuliko kujenga na wazee walituasa kwa
kutuambia….majuto ni mjukuu na tukifanya masihara majuto yetu yanaweza kuwa ya
vilembwe na vitukuu.
Tushirikiane kuirejesha Zanzibar katika hali ya utulivu na kama mtu anataka
kupiga watu anunue ngoma na apige mpaka ipasuke, si kupiga migongo ya watu na
anayetaka kunyoa ndevu anunue beberu na ajifunze kunyoa ndevu na si za watu
wengine.
No comments:
Post a Comment