Tuesday 6 November 2012

Tume huru ndiyo itakayoeleza ukweli Z’bar

Na Salim Said Salim
MARA nyingi ninaposomesha waandishi wa habari nawaeleza kuwa kuandika uwongo au kuzua jambo sio vibaya na kwamba hiyo ni haki ya msingi ya kila mtu.
Lakini huo uwongo ukishaandikwa, huyo mwandishi anatakiwa ausome mwenyewe, pia si vibaya kama ataamua kuuamini na sio kuuuchapisha katika gazeti au kuutangaza katika redio au kituo cha televisheni.
Njia nzuri ya kuusoma uzushi huo na kujifurahisha ni kwa huyo mwandishi kufanya hivyo akiwa amejifungia chumbani peke yake.
Kuupeleka katika jamii ni kinyume cha maadili ya taaluma ya habari na ni dhambi.
Ninasikitika kuona baadhi ya wanasiasa, viongozi wa serikali na Jeshi la Polisi wanazua uongo wa dhahir shahir na kuja hadharani kuueleza umma na kuwataka watu wauamini na kuukubali.
Katika miaka yangu ya zaidi 45, nimeshuhudia kauli nyingi za uwongo, zikiwemo zile zisizokuwa na kichwa wala miguu kutoka kwa waandishi wa habari, wana siasa, viongozi wa serikali na hata wa dini.
Ninakumbuka katika utumishi wangu wa karibu miaka 10 kama mjumbe wa Baraza la Habari la Tanzania (MCT), nilishuhudia waandishi wakibuni habari za aina kwa aina na mojawapo ni kusingizia mtu mmoja kuwa kabaka na kupelekwa mahakamani.
Katika habari ile alitajwa kwa jina la mwendesha mashitaka na hakimu aliyesikiliza ile kesi na kumpa dhamana.
Kumbe yote yale yaliyoandikwa baada ya kuyafuatilia yalikuwa ni uzushi uliokuwa na lengo la kumpaka matope yule aliyedaiwa kubaka ambaye alikuwa ana lengo la kugombea udiwani katika eneo la Ubungo, Dar es Salaam.
Uwongo mwingine ambao kama ungeliingizwa katika mashindano ungenyakuwa medali ya dhahabu kama sio ya lulu au almasi ni wa taarifa ya Jeshi la Polisi baada ya polisi kuuwa na kujeruhi wengine kule Pemba katika Kijiji cha Shumba Mjini, Micheweni wakati wakipandisha bendera ya tawi la Chama cha Wananchi (CUF) baada ya mfumo wa vyama vingi kuingia.
Polisi walidai, tena bila ya aibu, kuwa ati risasi zilipigwa hewani. Jamani toka lini risasi iliyopigwa hewani inateremka chini na kuumiza makalio au mgongo wa mtu. Toka siku ile nimekuwa na wasi wasi na kauli zinazotolewa na maafande wa Jeshi la Polisi.
Katika vurugu zilizotokea Zanzibar hivi karibuni na kusababisha viongozi wa Jumuiya ya Uamsho kukamatwa na kunyolewa ndevu hata kabla ya kesi kuhukumiwa, tunasikia kila aina ya uwongo, uzushi na unafiki kila pembe. Kwa kifupi unaweza kusema yapo mashindano Zanzibar ya kudanganya umma.
Watu hawa wananyosheana vidole na wengine kutajana majina ya watu na kuwahukumu utafikiria wao wamepewa kazi ya uhakimu kama ndio waliohusika na vurugu za hivi karibuni.
Kwa maana nyingine, wamejifanya mabingwa wa upelelezi na watu wanapaswa kuwaamini na wasiwahoji.
Hawa ndio wale tunaowaita limbukeni wa siasa kwa sababu wanafikiri siasa ni kusema uongo na kupakazana matope.
Hakuna ubishi kwamba vurugu zimetokea na watu kuuawa na wengine kujeruhiwa. Lakini kuwataka watu wayaone mauaji ya askari polisi, Koplo Said Abdulrahmani, katika eneo la Bububu ndio pekee yaliyotokea sio sahihi na sio haki katika dunia hii na hata mbele ya Mungu.
Roho zote zilizopotea zina thamani sawa na anayeelewa ni roho gani ilikuwa bora zaidi ni mwenyewe aliyetuumba.
Mauaji yote yanapaswa kulaaniwa na sio ya Polisi tu kwani haikuandikwa kwenye msahafu kwamba askari ni kiumbe kitukufu na wengine ni viumbe dhaifu.
Mauji ni mauaji na yote yanapaswa kulaaniwa, yawe ya askari, mfanyabiashara, mchunga ng’ombe au mfuga kuku au mvuvi.
Yote lazima yachunguzwe na wahusika (sio waliosingiziwa) wafikishwe mbele ya vyombo ya sheria.
Jeshi la Polisi na wanasiasa wa chama tawala wa CCM wanalaani mauaji ya askari tu. Wapi imeandikwa katika Kuran au Biblia kwamba akiuawa afande ndio mauaji na akiuawa mtu mwingine ni sadaka?
Zipo shutuma nyingi. Wapo wanaodai kuwa wafuasi wa uamsho wanahusika na mauaji na hata kuvunja maduka ya pombe na kulewa na wapo wanaosema vyombo vya dola vilisababisha vurugu.
Baadhi ya viongozi wa CCM wamewanyooshea vidole viongozi wa chama cha CUF kuwa chanzo cha vurugu na CUF wanadai waliosababisha maafa na wizi ni Janjaweed ambao chama hicho kinadai ni watoto wa CCM.
Lakini pia, zimesikika kauli, tena zenye nguvu, zinazotaja kuwepo kwa makundi yanayojiita Ubaya Ubaya, Mbwa Mwitu, Nguruwe na kadhalika kuwa ndio waliofanya vurugu na hata kuua.
Hapa unajiuliza ukweli hasa ni upi? Nani anasema kweli na nani anasema uwongo.
Njia pekee ni kufanya uchunguzi, lakini kwa kuwa Jeshi la Polisi nalo linanyooshewa vidole, basi njia pekee ni kuwa na uchunguzi wa tume huru. Inawezekana, japokuwa ni tabu kuamini, kuwa polisi wanaweza kufanya uchunguzi wa haki kutokana na tayari makamanda wao kuwashutumu uamsho moja kwa moja huku wakisema upelelezi unaendelea na haujakamilika.
Kama polisi hawajakamilisha uchunguzi inakuwaje leo wawalaumu uamsho?
CUF nao wanasema hawa vijana wanaodaiwa kuhusika na vurugu ni wale wanaowaita Janjaaweed ambao CUF inadai walikusanywa na CCM kwa ajili ya kufanya ghasia na kupiga kura mara mbili mbili katika uchaguzi na kutokana na kukosa ajira sasa wameamua kufanya uhalifu.
Sijui CUF wamepata wapi uthibitisho huo wa kukinyooshea CCM kidole cha lawama.
Lakini lililo baya zaidi ni hizi hukumu zinazotolewa. Sijuwi kwa nini polisi haitaki kuiachia mahakama kuhukumu au ndiyo tuseme kazi hiyo sasa wamekabidhiwa wao?
Nimesema na ninarudia kwamba ni tume huru tu, tena ile itakayopata imani ya wananchi, ndiyo inaweza kutoa jawabu na si vinginevyo.
Hawa vijana wa Ubaya Ubaya wamekuwa wakilaumiwa muda mrefu kwa vitendo vya uhalifu kabla ya vurugu za hivi karibuni, lakini wamekuwa wakiendeleza ubaya wao kama vile wamepewe leseni ya kufanya hivyo. Inasikitisha, tena sana.
Kama kweli Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo viongozi wake sasa wanaonekana kugawanyika mapande mawili, moja la CCM na jingine la CUF, linataka kutafuta ukweli basi iundwe tume huru ya uchunguzi.
Si vibaya hata kama wajumbe wa tume hiyo watatoka Tanzania Bara au katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na si Zanzibar ambapo inaonekana utashi wa kisiasa, uongo, unafiki na uzandiki unatumika kufunika ukweli.
Kama hawa waongo, wanafiki na wazandiki wanafanya haya wakiwa ndani ya majumba yao ni sawa, lakini wanapeleka uovu wao huu hadharani na kutaka watu wauamini.
Watu wa Zanzibar sio mbumbumbu kama hao wazushi, waongo na wanafiki. Wanaujua ukweli na siku zote ukweli haufichiki, hasa katika zama hizi za ukweli na uwazi.
Wapo watu waliopiga picha na kuchukuwa video na wapo wanaodai kuona yaliyotendeka. Kinachongojewa ni nafasi ya kuyaweka hadharani. Kama hapana hofu ya ukweli kujulikana kwa nini serikali iwe inaona vigumu kuunda tume huru ya uchunguzi?
Tume hii pia itafute ukweli juu ya hao wanaoitwa Janjaweed. Je, kweli wapo watu hawa? Nani aliwakusanya, waliwekwa wapi, nani aliwahudumia na kama walikuwepo nini yalikuwa makusio ya kuunda kikosi hiki?
Yapo maeneo ambayo yanadaiwa ndipo walipowekwa na wanadaiwa kwamba vijana hawa walitumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu uliofanyika karibuni.
Kwa kweli shutuma zinazosikika ni ndefu na jawabu ni kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi. Kutoifanya hivyo hakutatoa tafsiri yoyote ile isipokuwa kutaka kuficha ukweli.
Hatukatai kuwa kazi ya kutafuta wahalifu imekabidhiwa Jeshi la Polisi, lakini lazima tukumbushane kwamba hawa maafande sio manabii au malaika na upo ushahidi kwamba polisi katika nchi nyingi wamekuwa wakitoa taarifa za uongo.
Mfano mmoja tu wa hivi karibuni ni namna ambavyo Jeshi la Polisi la Uingereza lilivyofanya uubunifu wa kuwasingizia mashabiki wa timu ya Liverpool kuwa ndio waliofdanya vurugu zilisababisha vifo vya watu wengi katika uwanja wa mpira.
Baada ya miaka 19 ya uongo wa Jeshi la Polisi ukweli umepatikana na sasa wanaohusika wanawajibishwa kisheria, Au na sisi tunangojea itimie miaka 20 ndio tuungojee ukweli?
Jaribio lolote la kuficha ukweli linaweza kuvumiliwa leo na kesho, lakini ipo siku watatokea watu wataifichua kama ilivyofanyika kwa uwongo wa polisi wa Uingereza.
Wazanzibari au Watanzania kwa jumla wanataka kuujuwa ukweli na nafasi nzuri ya kutimiza kiu yao ni kuiachia tume huru kuifanya kazi hiyo.
Katika makala yangu ya hivi karibuni niliuliza; Zanzibar inaelekea wapi?
Sasa nimeipata ishara zinazonipa hisia za jawabu ya suala langu. Nazo ni kwamba visiwa hivi vinarudia kule tulikotoka ambapo siasa za mvutano, unafiki na uzandiki zilitawala na kusabaisha watu kuuawa na wengine kuwa vilema.
Kama siasa hizi zitaachiwa basi yale maridhiano ya kisiasa yalioleta umoja wa Wazanzibari na kusababisha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa yatakuwa hayana maana wala faida tena kwa Wazanzibari.
Wanaohusika wasije kusema wanaonewa wakihukumiwa kwa haya maovu wanayoyatenda hivi sasa.
Wenzao katika nchi mbali mbali walijifanya majabari, walitukana watu ovyo pembezoni na hadharani na wakapika majungu ya uovu na kuacha wengine kuyapakua.
Leo wanatiwa kamba ya shingo, wanalia na kutaka wahurumiwe. Ninawakumbusha kuwa sheria haina huruma, kwani humhurumia asiyetenda kosa na humuadhibu anayetenda maovu.
Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment