Sunday 9 December 2012

Ukweli kuhusu Uhuru wa Tanzania

SHEREHE ZA UHURU ‘FEKI’ WA TANZANIA…!
• Msimu wa Tanganyika kuizuga dunia wawadia!
• Hufanya sherehe za mamilioni ya walipa kodi dunia nzima!
Tarehe 09 Disemba mwaka huu, yatajwa kitaifa na kimataifa kuwa ndio siku ya Uhuru wa Tanzania ambao hadi siku hio, Taifa hilo la ‘kufikirika’ la Riwaya za Shaaban Robert litatimiza miaka 51, tangu lipate uhuru kutoka kwa Wakoloni wa nchi jirani ya ‘Kusadikika’ pia ya Shaaban Robert.
Kwa wasiokuwa wasomaji wa Riwaya za Mwandishi mahiri, na baba wa fasihi ya Kiswahili hayati Shaabani Bin Ufukwe (Shaaban Robert), nataka niwakumbushe tu kuwa katika Riwaya zake mbili za Kusadikika na Kufikirika, alijaribu kusawili mazingira ya nchi zisizokuwepo kiuhalisia bali kivitendo na muonekano wa kitaswira nchi hizo hufanywa zionekane zipo au huwepo kimawazo. Lakini kiuhakiki nchi hizo zaweza kuwa sawa na nchi yoyote ile yenye sifa zilizotajwa na mwandishi huyo.
Nalazimika kujenga hoja kuwa uhuru wa Tanzania ni wa nchi za Kusadikika na kufikirika kwa sababu dhana nzima ya uhuru na nchi yenyewe haipo kiuhalisia na kimantiki. Kwanza hakuna nchi ambayo inaitwa Tanzania kiukweli hasa na kama ni jina tu, ‘Tanzania’ ni sawa na jina lilibuniwa na watu la Dar es Salaam kuiita ‘Bongo’ na si vyenginevyo. Pili, hata kama nchi hiyo tunalazimishwa kuamini kuwa ipo, basi haihusiani kabisa na dhana ya uhuru na Ukombozi wan chi za Afrika na ndio hata ukifuatilia harakati za uhuru na ukombozi wa bara la Afrika utakutia nchi iitwayo Tanzania haimo kabisa.
Dhana ya uhuru wa nchi haihitaji mtu aliesoma sana kuijua fasili yake. Kwani kimsingi Uhuru ni hatua ya nchi kujipatia nafasi ya kujitawala yenyewe na uwezo wa kujifanyia maamuzi ambapo kabla ilikuwa mamlaka hayo hayakuwa mikononi mwa Wazalendo au wananchi wenyewe, bali yalikuwa chini ya mikono ya wageni waitwao Wakoloni.
Kwa mantiki hii tunarudia kusema kuwa, Tanzania haikuwepo kabla na hata muda mfupi baada ya Uhuru wa bara na Visiwani, itakuwaje iwe nchi huru? Unaposema Uhuru wa Tanzania, kwa wenye akili za kidadisi watakuuliza nchi hio ilitawaliwa na nani? Labda tujikumbushe historia kidogo ya Afrika Mashariki. Zanzibar ilitawaliwa na Muarabu, Kenya Muingereza, Uganda Muingereza, na Tanganyika au German East Africa, ilitawaliwa na Mjerumani.
Hili ni somo la Hitoria ya darasa la sita na la saba hapa kwetu.
Pia tujikumbushe tarehe muhimu za Uhuru wa nchi hizo. Kenya ilipata Uhuru tarehe 10 Disemba 1963, Uganda tarehe 09 Oktoba 1962, Zanzibar 12 Disemba, 1963, na Tanganyika Tarehe 09 Disemba, 1961. Kwa hivyo, hapa hapana cha kuwazuga watu, kwani kwa hakika katika nchi hizi kuu nne za Afrika Mashariki utaona kuwa Tanzania haimo.
Juu ya hayo, hivi sasa kuna mabango kila pahala duniani na katika mitandao ya jamii inayosema na kunadi Sherehe za kufa mtu za Uhuru wa Tanzania kutimiza miaka 51. Wenzetu wa bara wamezoea kuwazuga Wazanzibari kwa sababu ndio ‘mazuzu’ labda au ‘mayakhe’ au ‘mdebwedo’ kama walivyozoea kutuita, na wanafikiria kuwa Wazanzibari waliokuwa ‘mazuzu’ wakati huo watakuwa mazuzu na vizazi vyao vijavyo kiasi ya kutoweza kujua hata hesabu ya kutoa na kujumlisha.
Kwa vile wanaaamini waliweza kuitawala Zanzibar kwa hadaa, ujanja, na kuwazuga wazanzibari kwa kuwapa vyeo na kuwatisha wengine kwa adhabu na mambo mbali mbali, wenzetu hawa bado wanaamini kuwa dunia nzima ina mazuzu kama hivi wanvyowaona Wazanzibari walioshindwa kujuwa hesabu ya Mwalimu ya 1+ 1 = 2 ( Wazanzibari walisema 1+1=3).
Baada ya kuona kuwa hatujui hesabu ndio hapo ukaona kuwa Uhuru wa Tanganyika unatimiza miaka 51 yaani ni sawa na 2012-1961, wao wakidhani na hesabu hii itaushinda pia.Cha kushangaza, hesabu ya darasa la kwanza hadi la tatu tu hii na bado dunia nzima inazugwa ik iamini kuwa Tanzania leo inatimiza miaka 51 ya uhuru wakati nchi yenyewe hata haipo, imeundwa tu kutokana na Riwaya za Shaaban Robert za kusadikika na kufikirika.
Mpaka hapa naamini umeweza kuona kuwa wenzetu wa bara wanatumia hila na mbinu kuudanganya Ulimwengu na huku wakitumia pesa zisikuwa kidogo za walipa kodi ndani na nje ya nchi kwa kusherehekea Uhuru wa nchi isiyokuwepo katika nchi zilizotawaliwa. Huu ni upotoshaji mkubwa wa dunia na kusema kweli unaiondolea hadhi nchi yetu kwa kusema Uongo ulio dhahiri mbele ya kadamnasi ya kimataifa.
Leo hii kuna Sherehe kila pahali: London, Canada, Italia, China, Ufaransa, Ujerumani, Marekani na nchi zote; eti ‘Miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania’. Hii haileti maana wala haina mvuto wowote zaidi ya kuuonesha Umma ufinyu wetu wa mawazo na fikira za kutojua maana ya neno Uhuru na baya zaidi hata kutojua historia yetu na hesabu ya kujumlisha na kutoa tu ambayo kila mtoto wetu wa darasa la kwanza na la pili anaijua.
Nionavyo, Ipo haja tubadilike. Hakuna ubaya kusema ukweli hata kama unauma. Wala haitaibabua sura haiba ya bara kwa kuandika na kujitangazia ‘Miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika’. Si vibaya kwani huu ndio ukweli. Ni afadhali tuseme ukweli tuepuke kuchekwa na kuadhirishwa.
Nakumbuka mwaka jana pale London, kuna Mzanzibari mmoja alifanikiwa kupenya na kuingia katika Sherehe za Miaka 50 ya uhuru wa ‘Tanzania’. Alipofika alimuuliza balozi ‘Hivi Tanzania ilipata uhuru kutoka kwa nani?’. Balozi hakuwa na Jibu. Baada ya hili, tulifikiri watajirekebisha, lakini ndio kwanza wanazidi kujitangaza hivyo ilhali dunia inajuwa kuwa huu wanaoufanya ni Uongo wa mchana, kuzimu hakuna nyota.
Kwa muungwana ni wajibu ukweli usemwe, hakuna uhuru wa Tanzania. Tusidanganyane na kudanganya watu kwani mwisho tutashindwa kwani ukisema uongo, Ukweli haujifichi,na ukiibuka ukweli kinachofata ni kuona aibu tu. Kwani wazungu husema ‘Unaweza kuwadanganya baadhi ya watu, baadhi wa wakati, lakini huwezi kuwadanganya watu wote, siku zote’.

No comments:

Post a Comment