Saturday 22 December 2012

Wazanzibari tunayajuwa haya???


The Partnership
Na Aboud Jumbe
"Njia haikuwa rahisi na siku zote iliibuka ile shaka ya Zanzibar kumezwa na Tanganyika kwa kupitia Muungano huo. Kama vile Mwalimu alivyoonesha katika hotuba yake ya Sherehe za miaka 10 ya Muungano kuwa watu walikuwa na wasiwasi na "nchi ndogo kama Zanzibar kumezwa na nchi kubwa kama Tanganyika". Khofu hii haikuwa kwa watu wa Zanzibar tu. Kwa wafuatiliaji wengi hali hii ya zimwi kushirikiana na kibushuti kumeifanya dunia siku zote ikae ikisubiri ni kipi kitatokea. Picha inayoonekana ukitizama kipindi cha miaka thelathini ya Muungano huu ni ya kutisha. Inatia mashaka na masuali juu ya yale madhumuni halisi ya Muungano huu huku kukiwa kuna dalili za wazi za kukimbia matakwa ya Mkataba wa Muungano.

Inaweza kuwa jambo jema iwapo tutajiuliza: Kwa nini hapo 1963 nchi za Afrika Mashariki zilikuwa zimejifunga kukubali kuunda Shirikisho zikashindwa kujiunga na Muungano wa Tanzania? Hakuna moja iliyofanya hivyo. Jee, hii ni kutokana na mtiririko wa matukio kuanzia Aprili, 1964 kushindwa mbali ya kudhihirisha khofu ya kumezwa.
Ingefaa hapa nitaje kuwa miezi minne tu baada ya Muungano, marehemu Jomo Kenyatta alinukuliwa na gazeti la Times of London hapo Agosti 3, 1964 akisema hayuko tayari kumpigia magoti Nyerere na Tanganyika. Kitu gani basi kilichomfanya Kenyatta akatae kabisa Muungano ikiwa ni mwaka mmoja tu tokea atoe tamko la kuwa tayari kushirikiana na Obote na Nyerere? Historia imekuwa shahidi upande wake. Jee, hilo ndilo lililokuwa tukilifanya wakati wote?"

Hayo si maneno yangu. Ni maneno ya Sheikh Aboud Jumbe, aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alikuwa pia Katibu Mipango wa ASP na baadaye Rais wa ASP. Huyu si HIZBU na sidhani kama anaweza kutuhumiwa kuwa mpinga Mapinduzi au anataka kurudisha Usultani Zanzibar. Hizo ndizo tafakuri zake.

Langu mimi ni moja tu ninalotaka kuongeza. Nalo ni kwamba aina pekee ya Muungano itakayoondoa khofu ya nchi moja kumezwa na nyingine ni ile ambayo kila nchi shiriki itabaki na mamlaka yake kamili kitaifa na kimataifa na kisha kushirikiana kupitia Muungano wa Mkataba (Treaty based Union). Hivyo ndivyo ulivyo Muungano wa Ulaya (European Union) ambao umeendelea kukua na kufikia kuwa na nchi shiriki 27 na ambao mwaka huu umepewa tuzo ya Nobel. Insha'Allah hiyo ndiyo njia ya kufuatwa katika kujenga mahusiano mapya kati ya Tanganyika na Zanzibar yatakayovutia na nchi nyingine kujiunga na kuondoa khofu kama zile za Jomo Kenyatta alizozitoa Agosti 3, 1964.

No comments:

Post a Comment