Friday 21 December 2012

‘Katiba inayoandaliwa ni ya watawala’

JUKWAA la Katiba limesisitiza kuwa Katiba mpya haiwezi kupatikana Aprili 26, 2014 na endapo itafanyika hivyo litazunguka nchi nzima kuhamasisha wananchi kuikataa rasimu ya Katiba hiyo kwa njia ya kura.
Jukwaa hilo limesema litafikia hatua hiyo kwa kuwa Katiba itakayopatikana itakuwa ni ya watawala kwa kuwa wananchi wengi hawajapata fursa ya kutoa maoni yao.
Kauli hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deus Kibamba, alipozungumza na waandishi wa habari alipokuwa akitoa tathmini ya mchakato wa Katiba kwa mzunguko kwa kwanza.
Alisema endapo nchi inahitaji Katiba ya demokrasia haiwezi kupatikana ndani ya kipindi hicho na kumuonya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji mstafuu, Joseph Warioba, na wenzake kulitilia maanani suala hilo.
“Dharura imewahi kuligharimu taifa letu na katika nchi nyingine kushindwa kufanya maandalizi kunaweza kusababisha machafuko kwa kutokamilika kwa Katiba mpya huku muafaka ukiwa umeshuka na jamii kutokubaliana kwa mambo mengi ya msingi.”
Pamoja na hayo, jukwaa hilo limetoa hati chafu kwa wakuu wa wilaya wawili, Rosemary Kirigini (Meatu) na Jokiwa Kasunga (Monduli), kwa madai kuwa ni maadui wa mchakato wa Katiba kwa mwaka 2012.
Alisema Kirigini alizuia kumfanyika mkutano wa Katiba ulioandaliwa na asasi ya kiraia ya Mongonet akitaka wasijadili masuala ya Katiba bali mambo mengine wakati Kasunga alizuia mikutano ya uhamasishaji uliokuwa ukifanywa na taasisi ya Pingo’s Forum ambayo ilikuwa na lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya mchakato wa Katiba mpya kwa madai ya kutaka taarifa zaidi za taasisi hiyo kabla ya kuruhusu kufaya kazi katika wilaya yake.
“Kutokana na ukubwa wa makosa yaliyofanywa na wakuu hawa wa wilaya na hatari yake katika kufifisha mchakato wa Katiba, Jukwaa la Katiba leo tunatoa hatia maalumu kwa viongozi hawa kama ishara ya kuwatangaza kuwa maadui wa Katiba mpya. Utaratibu huu utaendelea katika muda wote wa uundaji wa Katiba mpya hadi kukamilika,” alisema Kibamba na kuongeza nakala za hati hizo zitapelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete.
Alisema kwa mwaka ujao wanatarajiwa kuwapeleka watu wa aina hiyo mahakamani kwa kuwa wanavunja Katiba ibara ya 18.
Akielezea dosari zilizojitokeza katika mzunguko wanne na wa mwisho wa awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni ya Katiba ni fursa finyu ya utoaji maoni kwa wananachi.
“Jukwaa la Katiba Tanzania tulishuhudia watu wakijitokeza kwa wingi huku muda uliotengwa ukiendelea kuwa mdogo kwa idadi ya watu wengi waliojitokeza katika mzunguko huu.
“Watazamaji wetu walishuhudia wananchi wakishauriwa kutoa maoni yao kwa njia ya maandishi kwa kuwa wengi wao walikosa fursa ya kuzungumza katika mikutano ya tume,” alisema na kutoa mfano suala hilo limejitokeza eneo la Segerea na Temeke, kata ya Pemba Mnazi.
Alisema suala hilo liliwakatisha tamaa watu wasiojua kusoma na kuandika, ni kinyume na lengo kuwa Katiba itaandikwa na Watanzania wote hata kama hawawezi kusoma wala kuandika.
Aidha alisema wakati mwingine tume ilionekana kuwa na haraka ya kuondoka kutokana na muda waliopangiwa kuwa finyu na walikuwa wakiwahi mikutano mingine.
Alieleza kuwa dosari nyingine waliyoibaini ni kwa vyama kuendelea kuingilia mchakato wa Katiba, jambo linalosababisha kutokea kwa fujo kwa wafuasi kupigana na kutolea mfano vurugu zilizotokea Zanzibar.
Kutokana na hali hiyo, jukwaa hilo limeshauri kuwapo na majadiliano aina ya taifa tunalohitaji kulijenga ikiwa ni pamoja na kukubaliana mipaka ya Katiba tunayoiunda.
“Tujadiliane kwanza tunaunda Katiba ya Muungano? Kama ndiyo tunataka Muungano wa aina gani wa serikali mbili, tatu au wa mkataba,” alisema.
Aidha wanapendekeza mchakato wa Katiba mpya lazima utenganishwe na michakato ya uchaguzi ujao, kwani kuna hatari ya mchakato mmojawapo kuvurugwa.
“Hii itatoa fursa kwa mchakato wa Katiba mpya kuendelea taratibu na bila kuhitaji kukimbizwa hata kama utahitajika kuendelea mpaka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,” alisema.
Aidha alisema jukwaa hilo litaendelea na kampeni ya kugawa Katiba ya sasa kwa kila Mtanzania na kwamba mpaka sasa kwa kushirikiana na asasi mbalimbali wameshasambaza nakala zaidi ya 300,000 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nakala 10,000 za Katiba ya Zanzibar.
Alisema katika mwaka ujao, jukwaa limejipanga kuendelea na kampeni ya kuongeza nakala za Katiba nukta nundu kwa ajili ya watu wasioona
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment