Thursday 13 December 2012

Jinsi Nyerere alivyotawala kimabavu

Barazani kwa Ahmed Rajab
KITU kimoja mataifa ya Magharibi yanachojivunia ni Sheria ya Haki za Binadamu (Bill of Rights). Mataifa hayo na mengine yenye kujigamba kwamba ni ya kidemokrasia halisi yameiingiza sheria hiyo katika katiba zao.
Walimwengu kwa jumla huipigania na kuitetea sheria hiyo kwa sababu wengi wao wanataka tuwe na dunia yenye kuwahakikishia binadamu wote kwamba wataishi maisha ya heshima, ya utu, yenye kuwafanya binadamu wote wawe sawa mbele ya sheria na yenye kuwapa wote uhuru.
Sheria ya Haki za Binadamu ni msingi muhimu wa mfumo wa kidemokrasia na utawala bora. Ndiyo maana tunawaona wanasiasa wengi, walio wema na hata wasio wema, wakiipigia debe sheria hiyo.
Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar zote zinaielezea kwa makini Sheria ya Haki za Binadamu. Katiba zote mbili zilifanyiwa marekebisho mwaka 1984 ili iingizwe hiyo Sheria ya Haki za Binadamu katika kila moja ya katiba hizo.
Wakati wa uhuru mwaka 1961 Tanganyika haikuwa na Sheria ya Haki za Binadamu katika katiba yake. Zanzibar, kwa upande mwingine, iliwahi kuwa na mlango mzima wa Sheria ya Haki za Binadamu katika katiba yake ya uhuru ya mwaka 1963. Katiba hiyo ilifutwa baada ya Mapinduzi ya 1964 na Zanzibar ilipoungana na Tanganyika ikawa inaitumia katiba ya Muungano ambayo kama nilivyogusia haikuwa na Sheria ya Haki za Binadamu.
Tanzania iliiingiza Sheria ya Haki za Binadamu katika katiba yake miaka miwili baada ya viongozi wa nchi za Kiafrika kukutana jijini Nairobi na kuuidhinisha Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu (ACHPR) na pia kuunda Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu yenye makao yake makuu mjini Banjul, Gambia.
Kuna sababu ya kwa nini Tanganyika (na baadaye Tanzania) haikuwa na Sheria ya Haki za Binadamu katika katiba yake. Kwa hakika, Mwalimu Julius Nyerere na wenzake waliokuwa wakipigania uhuru wa Tanganyika hawakutaka kwa makusudi kuliingiza suala hilo katika katiba ya Tanganyika huru.
Kisingizio walichotoa akina Nyerere ni kuwa wakichelea majaji wa kikoloni ambao ndio siku hizo wakisimamia mahakama kwamba huenda wakavitumia vifungu vya Sheria ya Haki za Binadamu ili kuzisambaratisha jitihada za serikali mpya ya wazalendo za kuupatia umma maendeleo ya haraka ya kiuchumi.
Nyerere alikataa katukatu kwamba katiba ya Tanganyika ya wakati wa uhuru iwe na Sheria ya Haki za Binadamu. Alifanya ukaidi huohuo wakati katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ilipokuwa inaandaliwa mwaka 1962. Hivyo, katiba zote hizo mbili zilimwezesha Nyerere aitawale nchi kwa mabavu kama walivyofanya wakoloni wa Kiingereza kabla yake.
Taifa jipya la Tanganyika lilifungua macho likijikuta limezirithi sheria za kimabavu. La kusikitisha ni kwamba Nyerere hakufanya jitihada yoyote ya kuzifuta sheria hizo na kuweka sheria zenye kuheshimu haki za binadamu.
Kwa hili Nyerere na Tanganyika hawakuwa peke yao barani Afrika. Nchi nyingi nyingine za Kiafrika zilikuwa na utawala uliojengeka juu ya misingi ya kimabavu na isiyoheshimu haki za binadamu.
Sheria ya Haki za Binadamu iliyoingizwa kwenye Katiba ya Muungano mwaka 1984 ilikuwa isitumike katika mahakama ya kisheria kwa muda wa miaka mitatu ili kuipa Serikali ya Muungano muda wa kutosha wa kuzifuta au kuzibadili sheria zake zote zenye kwenda kinyume na Haki za Binadamu. Hata hivyo, hatua hiyo haikuisaidia Serikali ya Muungano kuzibatilisha sheria zake zote za kimabavu.
Sidhani kama ninakosea nikisema kwamba Tanzania ilikubali kichwa upande kuiingiza Sheria ya Haki za Binadamu katika katiba yake. Nasema hivi kwa sababu ingawa Sheria ya Haki za Binadamu imo ndani ya katiba za Muungano na Zanzibar bado kuna mushkili mkubwa katika utakelezwaji wake. Inavyoonyesha ni kwamba serikali imefanya kusudi iwe ngumu kwa watu binafsi kuzitetea haki zao za kimsingi katika mahakama.
Jingine ni kwamba ingawa katiba zote hizo mbili zinazitambua takriban haki zote za kiraia na za kisiasa hata hivyo kuna nyakati ambapo wananchi wanapata taabu kuzipata au wanazuiwa wasizipate haki zao. Mfano mzuri ni haki ya wananchi ya kuwa na uhuru wa kukusanyika au wa kuandamana wakati wanapotaka. Hizi ni haki za kimsingi za binadamu na uhalali wake si lazima upatikane kwa haki hizo kutajwa ndani ya katiba.
Kwa hali ilivyo Bara na Visiwani haki hizo za kukusanyika na kuandamana zinautegemea sana ukarimu wa Polisi. Wao ndio wenye kutoa kibali cha kufanyika mkutano wa hadhara au maandamano. Wakati wa maandamano Polisi wanatakiwa wawe wanasimamia usalama na amani na si wao kuanza kuichafua amani.
Kesi inayoendelea sasa Zanzibar ya washukiwa wa Uamsho imezidi kufichua jinsi serikali ya huko inavyoikiuka Sheria ya Haki za Binadamu licha ya kuwa imo ndani ya katiba zote mbili, ya Muungano na ya Zanzibar.
Sheria ya Haki za Binadamu inasema kesi ziwe zinaendeshwa kwa haraka. Lakini tukiiangalia hii kesi ya Uamsho tunaona kwamba mahakama yanasotasota katika kuiendesha.
Zaidi ni kwamba washtakiwa ingawa ni watuhumiwa na hawajapatikana na hatia hadi sasa wanatendewa mambo kana kwamba wamekwishapatikana na hatia. Wananyimwa haki zao za kimsingi wakiwa korokoroni na wanafanyiwa mambo ya kuudhalilisha utu wao. Na Bara kuna kesi chungu nzima ambazo kwa miaka mingi baada ya kufunguliwa bado hazijasikilizwa.
Swali la kujiuliza ni: Nani wa kulaumiwa pale wakubwa wa serikali wanapoukiuka huo msingi wa demokrasia halisi? Tumezoea kuwatupia lawama wakubwa wa serikali. Lakini wapo wengine ambao pia wanastahiki kuibeba. Nao ni umma, tukiwemo mimi na wewe.
Umma usiojali serikali inafanya nini au nini haifanyi inachopaswa kufanya ni umma uliopotoka na unaoweza kutiwa shemere na kubururwa kama kondoo na hao wakubwa wa serikali.
Tusitarajie kupewa haki zetu. Lazima wananchi sote tuzipiganie haki zetu zote zikiwa pamoja na zile za kutaka elimu, afya na ajira. Na hatutoweza kufanya hivyo mpaka tujipange. Tuunde jumuiya za kupigania haki zetu, tushurutishe somo la Sheria ya Haki za Binadamu lifundishwe katika maskuli hadi vyuo vikuu. Lengo liwe kuhakikisha kwamba wananchi tusiwe na uwezo wa kusema tu bali pia tuwe na uwezo wa kuamua. Hiyo ndiyo nguvu ya Umma.
Chanzo: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment