Friday 22 February 2013

Viongozi wetu na urongo wausemao

MWANDISHI George Orwell aliwahi kuandika kwamba kutamka ukweli huwa ni kitendo cha kimapinduzi pale udanganyifu unapozagaa na kuenea pote kwa watu wote.
Nadhani alikusudia kusema kwamba katika nyakati za uongo, kama hizi tunazoziishi sasa, kutamka ukweli huwa ni kitendo cha kishujaa kinachoweza hatimaye kusababisha mapinduzi.
Huenda pia ikawa alikusudia ya kuwa katika nyakati za uongo panahitajika shujaa kusema kweli kwa sababu jamii huwa imekwishazoea kudanganywa na hufuata tu inachoambiwa na wakubwa wake.
Jamii inakuwa kama ng’ombe aliyetiwa shemere. Na hao wakubwa hujifanya kuwa wao ndio wenye kujua kila kitu na kwamba walisemalo ndo ndilo. Ndio ukweli usiopingika.
Siku hizi uongo umeenea kote hasa katika ngazi za utawala na unahatarisha mfumo wa utawala bora tunaouengaenga. Uongo ni hatari kwa utawala bora kwa sababu unatumiwa kuwa visingizio pale haki za binadamu zinapokiukwa au viongozi wanapojiingiza katika ufisadi.
Uongo huo unaanzia juu kwa wanasiasa na viongozi wetu na kutiririka kwa maofisa wa ngazi za chini. Viongozi wetu, na wanasiasa wetu kwa jumla, wameugeuza ulaghai na kuufanya uwe sanaa pendwa. Wao wenyewe wamebobea katika kudanganya danganya na wamekuwa mafanani wa uongo. Na wala hawana haya.
Hii ndiyo sababu kwa nini viongozi wetu wanathubutu kutueleza chochote watakacho hata ikiwa wanajua kwamba sisi tunajua ya kuwa hicho wanachokieleza ni cha kubuni, ni ghiliba tupu.
Iko mifano mingi. Wa karibuni ni ule wa kiongozi mmoja wa taifa aliyesema kwamba nakala halisi ya Hati ya Muungano ipo ilhali ulimwengu mzima unajua kwamba hakuna kitu kama hicho. Haipo nchini wala haipo makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York.
Mfano mwingine ni wakati wa tukio la mauaji ya 2001 huko Pemba. Rais wa wakati huo Benjamin Mkapa alidanganya kuhusu idadi ya waliouawa na pia alidanganya kuhusu waandamanaji akisema walikuwa ‘magaidi’ waliotaka kuipindua serikali.
Baadaye tume aliyoiteua yeye mwenyewe kuchunguza tukio hilo ikiwa chini ya Kanali Hashim Mbita ilitoa ripoti iliyokuwa tofauti na aliyoyasema Mkapa.
Mfano mwingine ni hotuba aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete kwa Bunge Desemba 30, 2005 kulifungua baada ya uchaguzi wa mwaka huo. Alisema anashangazwa na Wazanzibari hao hao wanaofaidika na fursa za Muungano kuwa ndio haohao wanaoonyesha hisia za kujitenga.
Ni wazi kwamba aliwakusudia wapigaji kura wa Pemba waliokibwaga chama cha CCM. Lakini kusema kwamba wasiokitaka chama cha CCM hawautaki Muungano si kweli kwa sababu wakati wa uchaguzi huohuo takriban Kilimanjaro nzima ilipiga kura dhidi ya CCM.
Ukweli ni kwamba wapo wasiokitaka chama cha CCM na wasioutaka Muungano lakini pia wapo wanaoutaka Muungano na wasiokitaka chama cha CCM. Ukweli lazima usemwe.
Viongozi wetu wanasahau kwamba kusema kweli ni jambo lililo adhimu katika siasa. Ni jambo la uadilifu. Linampambanua kiongozi anayestahili kuheshimiwa na yule anayedharauliwa anayeonekana kuwa ana sifa za kihuni, za kijambazi, ili ajipatie muradi wake. Lengo lake huwa ni kujipatia alitakalo potelea mbali ikiwa ukweli atautupa jaani.
Inanijia hapa kuutaja ushairi na kuuhusisha na siasa kwani kuna wenye kuiona fani ya ushairi kuwa ni fani ya kisiasa. Wenye kuuangalia ushairi kwa mtazamo huo na kuufananisha na siasa hufanya hivyo kwa sababu wanasema ushairi humfanya mshairi aseme kweli.
Viongozi wetu pia wanasahau kwamba wananchi wengi hawataki kujiingiza katika mambo ya siasa kwa sababu wanaziona siasa kuwa ni chafu na kwamba chanzo cha uchafu huo ni uongo.
Ipo sababu inayowafanya viongozi wetu wazoee kusema uongo na kuifanya hali hiyo iwe hulka yao. Sababu yenyewe ni kwamba mara nyingi uongo huwafaa ingawa manufaa wayapatayo huwa ni ya muda mfupi tu. Hatimaye huo uongo huja kuwasuta.
Historia ina mifano mingi yenye kuonyesha jinsi uongo unavyokuwa hauna mwisho mwema kwa viongozi wausemao.
Athari zake ni nyingi. Moja na labda ni athari iliyo ndogo ni ile inayoathiri afya yake kiongozi mwenye kusema uongo.
Nakumbuka mwaka jana kulifanywa utafiti wa kitaalamu kuhusu athari ya uongo kwa afya ya waongo. Waliofanya utafiti huo walikuwa wataalamu wa Chuo Kikuu cha Notre Dame waliogundua kwamba kusema uongo kuna athari mbaya sana kwa afya ya wasemaji uongo kiasi cha kuwafanya waingiwe na wahaka, fadhaa ama huzuni. Wengine huingia kichaa na kuwa majnuni kwa uongo wasiokwisha kusema.
Hizo ni athari zinazowapata watu wa kawaida tu. Zinazidi kuwa mbaya kwa kiongozi mwenye majukumu makubwa na hasa wa nchi kama za kwetu. Hawa ni viongozi ambao aghalabu hutaka waonekane kuwa wao ni wababe wanaopaa angani wakiitia dunia katika kwapa zao.
Nadhani Orwell alipofananisha kusema kweli na ‘kitendo cha kimapinduzi’ alikusudia mapinduzi ya kifikra au ya hali halisi ya mambo ilivyo. Mapinduzi ya kifikra ni yale yanayoubiruwa mfumo wa jinsi jamii ilivyozoea kufikiri.
Mapinduzi ya aina hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya jamii. Kuselelea kuitakidi fikra au dhana zilizojaa kutu zisizopigwa msasa ili ziyasibu mazingira yaliyobadilika ni kujitakia balaa. Ni kuutia pingu uwezo wetu wa kufikiri na kutufanya tufanye mambo yasiyoelekea katika wakati ambapo dunia, kwa jumla, huwa imepiga hatua mbele.
Fikra zetu hazitoweza kuchanua ikiwa sisi na wale tuliowachagua watuongoze tutakuwa na tabia ya kudanganyana.
Hapa ninawakumbuka watu wawili wasiojulikana ni nani (pengine alikuwa ni mtu huyohuyo mmoja) lakini waliotoa wasia ambao tunafaa tuuzingatie kwa makini.
Mmoja alisema: Siku zote sema kweli, hata kama itakubidi uubuni (huo ukweli).
Mwengine alisema: Sikuzote sema kweli. Na kama huwezi kusema kweli sikuzote, basi usiseme uongo.
chanzo: Raia mwema

No comments:

Post a Comment