Thursday 14 February 2013

Uchama usiruhusiwe kuyapiku maslahi ya Zanzibar

AGHALABU umma unapoachiwa na kupewa uhuru kamili wa kujiamulia wenyewe mambo yao hujiamulia mambo yenye kheri nao.
Tuliyashuhudia hayo Zanzibar, Julai 31, 2010 pale wananchi wa huko walipopiga kura ya maoni wakipendelea nchi yao iwe inaendeshwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Ulikuwa ni uamuzi wa busara, wa kujiepusha na shari.
Ulikuwa pia uamuzi uliozusha matumaini mengi na makubwa hasa baada ya Serikali hiyo kuundwa Novemba 1, 2010 baada ya uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka huo. Wazanzibari wakitaraji kwamba angalau watumishi wakuu wa serikali watateuliwa kwa kuzingatia sifa zao za utendaji wa kazi na si mengine.
Watu wakidhani kwamba mambo ya zamani yatatupiliwa mbali, kwamba wakuu serikalini watateuliwa kwa mujibu wa ustahili wao na si kwa mapendeleo — yawe ya kisiasa, ya kikabila au ya kujuana.
Kadhalika, wengi wakitumai kwamba hatimaye Zanzibar inaelekea ndiko — kwenye maendeleo. Wengine wakihisi kwamba angalau kutawekwa msingi madhubuti wa kuzitengeneza huduma zilizo muhimu sana na miundombinu imara pamoja na kuufanya uchumi ustawi. Alhasili wakiamini kwamba mambo yataanza kutengemaa.
Walikosea. Tunaelekea mwaka wa tatu tangu iundwe hiyo Serikali ya ubia na wengi wa Wazanzibari wanaona kuwa hali zao za maisha zimezidi kuwa ngumu. Siku hizi, kwa mfano, wakitaka kununua chakula inawabidi wanunue kwa bei za kuruka juu sana kushinda zile walizokuwa wakilipa katika 2010. Ukizilinganisha bei za vyakula zilivyokuwa miaka miwili iliyopita na zilivyo sasa hutoshangaa ukiwaona wanalia.
Isitoshe zile idara au wizara zilizo chini ya udhibiti wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama vile za afya na elimu hazikufanya mengi ya kutia moyo.
Ni muhimu Wazanzibari wote wawe wanaitafakari hali hii hasa wakiwa katika mchakato wa kuandikwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni muhimu pia wajiulize wamefanikiwa kwa kiasi gani hadi sasa, na wajiwekee mkakati wa kuuhitimisha mchakato huu wakiwa wameungana, wakiwa na msimamo mmoja kuhusu Katiba mpya waitakayo.
Tunavyoambiwa ni kwamba Katiba hiyo mpya itakuwa tayari Aprili 2014 wakati ambapo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utatimia miaka 50.
Mswada wa Katiba hiyo mpya utapigiwa kura ya maamuzi Tanganyika na Zanzibar chini ya usimamizi wa tume za uchaguzi za sehemu hizo mbili za Jamhuri ya Muungano.
Ili waweze kuupata muradi wao Wazanzibari hawana hila ila waungane; wawe na msimamo mmoja wakati wa kupiga kura ya maamuzi wakitambua kwamba uchama au itikadi za kisiasa haziwezi kuyapiku maslahi ya Zanzibar.
Ninaamini kwamba wamekwishajifunza vya kutosha kutokana na makosa ya zamani ya viongozi wao wa kisiasa, ambao badala ya ushirikiano wakipingana, wakizozana na wakizusha mgawanyiko katika jamii.
Viongozi wenyewe waligawanyika na waliwagawanya wafuasi wao kiasi cha kuwafanya baadhi yao wayaone maslahi ya nchi yao kuwa ni duni yakilinganishwa na maslahi ya vyama vyao vya kisiasa.
Wazanzibari waligawika vibaya sana tangu miaka ya 1950 Waingereza walipoanzisha siasa za ushindani wa vyama na chaguzi hadi 2010 palipopatikana Maridhiano na baadaye Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Wazanzibari waligawika hata walipokuwa chini ya mfumo uliohalalisha chama kimoja tu cha kisiasa kutoka 1964 hadi 1995 kwani takriban nusu yao hawakuwa na imani na Serikali ya Mapinduzi.
Si tabu kung’amua kwa nini hawakuwa na imani na serikali hiyo. Sababu kubwa ni kwamba awamu zote za Serikali ya Mapinduzi zilikuwa zikihubiri na zikifuata siasa za kibaguzi. Kwa hizo siasa zao chafu awamu zote hizo ziliwatenga na kuwafanya si kitu Wazanzibari wasiovaa mashati ya kijani na kuimba nyimbo za CCM.
Ndiyo maana kuna haja ya kuwa tangu sasa Wazanzibari wawe na mtazamo mmoja kuhusu jinsi nchi yao itavyotawaliwa baada ya kupatikana Katiba mpya. Mtazamano huo lazima uhakikishe kwamba jamii itayoibuka itakuwa ya haki na usawa, itayowapa Wazanzibari wote fursa sawa bila ya ubaguzi au upendeleo wa aina yoyote.
Ili waweze kuijenga jamii waitakayo yenye kuwapa wote haki sawa, Wazanzibari wanapaswa wawe na mdahalo juu ya mapendekezo yote yaliyotolewa wakati Tume ya Katiba ilipokuwa ikikusanya mawazo ya wananchi kuhusu Katiba waitakayo kazi ambayo ilimalizika karibuni tu Visiwani.
Sasa tukiwa tunazisubiri hatua za mchakato huo zitazotufikisha Aprili 2014 ni muhimu Wazanzibari wote waungane na wautetee mfumo wa Muungano utaojengwa juu ya msingi wa Mkataba.
Huo ndio mfumo pekee utaoirejeshea Zanzibar mamlaka yanayoiwezesha iendeshe shughuli zake za ndani na nje ya nchi bila ya kuomba ruhusa Bara au kutoka nchi yoyote ya kigeni.
Ni muhali hii leo kumpata mzalendo wa Kizanzibari asiyetaka Rais wa Zanzibar na Serikali ya Umoja wa Kitaifa warejeshewe mamlaka yao kamili pamoja na Baraza la Wawakilishi kuwa na uwezo wa kutunga sheria kuhusu mambo yote na si yale yasiyo ya Muungano tu.
Wapo, bila ya shaka, wenye kutaka mfumo wa sasa uendelee. Lakini Wazanzibari aina hiyo, ambao wenzao wanawaita vibaraka, si wengi na hata hao nao wanataka Zanzibar irejeshewe ‘mamlaka’ yake ingawa hawaelezi jinsi mamlaka hayo yanavyoweza kurejeshwa chini ya mfumo uliopo wa serikali mbili.
Wengi wanaiunga mkono kauli iliyotolewa Jumamosi iliyopita huko Nungwi, Unguja, na Ismail Jussa ambaye ni mwakilishi wa Mji Mkongwe. Jussa alisema kwamba Wazanzibari hawana sababu ya kuendelea na mfumo uliopo wa Muungano kwa kuwa ‘unaididimiza Zanzibar, kiuchumi na kijamii’. Kwa mujibu wa Jussa mfumo pekee utakaoipa Zanzibar fursa ya kusonga mbele ni mfumo wa Muungano wa Mkataba.
Hayo ndiyo maoni ya baadhi ya Wazanzibari na Serikali ya Muungano inawajibika kuyaheshimu maoni hayo. Kwa kufanya hivyo tu ndipo tatizo hili tata la Muungano litavyoweza kutanzuliwa ili nchi hizo mbili ziweze kusonga mbele bila ya kubughudhiana.
Chanzo: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment