Saturday 23 February 2013

TUSIPOTUMIA AKILI ZETU VIZURI, WAZANZIBAR TUTAPIGANISHWA KAMA MAKUCHI

Matukio ya kusikitisha, kufedhehesha na yakushangza yamekuwa yakitokea Zanzibar tangu mwaka jana baada ya wazinzabar kuanzisha harakati za kurudisha Zanzibar yenye mamlaka kamili (Zanzibar huru), harakati zilizoanzia kwenye baraza la wawakilishi mwaka 2010, kwa kubadili katiba ya Zanzibar na kuitaja Zanzibar kuwa ni nchi kamili! Vugu vugu lililochagizwa zaidi na jumuia ya mihadhara na ya kiislam ( al maarufu kama UAMSHO)!
Vugu vugu hilo lilipelekea mvutano kati ya jeshi la polisi na wafuasi wa masheikh wanaoongoza jumuia ya UAMSHO. Chakushangaza mvutano au mapambano yalikuwa ni kati ya polisi na wafuasi wa UAMSHO, lakini tukaamka asubuhi nakusikia MAKANISA kadhaa yamechomwa moto! Eti waZanzibar hao (UAMSHO) ambao wamekuwa wakiishi kwa amani na upendo na wakristo kwa karne tele zilizopita, leo hii wameacha nyumba zote za askari wanaopigana nao, wanaCCM, viongozi wa SMZ, na masheha badala yake wameenda kuchoma moto makanisa! Hapa tukaambiwa uchunguzi utafanyika na wahusika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria….watu wakakamatwa kwa nzo, wakatafutwa kila mwenye ndevu akanyolewa, wakahilikishwa, na kwa kutumia technologia (kama alivyosema Kamishna Mussa), wakaangalia kanda za video kubaini walokuwepo kwenye vurugu zile na kuwakamata! Tukasubri majibu , tuambiwe ni nani hasa alochoma makanisa? Ikabaki kuwa “watu wasiojulikana” Jibu mpaka leo hakuna!
Tutakaa tena kidogo, tukasikia Sheikh Farid katekwa, jeshi la polisi likasema hajui alipo, itakuwa kajiteka! Vurugu zikazuka tena, makanisa yakachomwa tena, lakini mara hii wakaongeza na kuchoma maskani za CCM, na polisi mmoja akauliwa kwa kukatwa katwa kwa mapanga! Mkuu wa jeshi la polisi nchini Said Mwema, akasema ametuma makachero wenye ujuzi wa hali ya juu (walobobea) kutoka makao makuu Dar es salaam, kuja Zanzibar kuwatafuta wahusika wote walouwa na kuchoma makanisa ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria…tukasubiri na tunaendelea kusubiri, bila kupata majibu mpaka leo!
Hatujakaa vizuri, tukasikia Sheikh Soraga, kamwagiwa tindi kali usoni, na “mtu asiejulikana”! Kama kawaida tukaambiwa tena, jeshi la polisi linafanya uchunguzi kuwatia nguvuni wahusika….mpaka naandika habari hii hakuna jibu la nani alommwagia Sheikh Soraga tindi kali! Jeshi la polisi bado lafanya uchunguzi tu!
Tukiwa bado tunatafakari hayo, tunasikia tena Padri Ambrose kashambuliwa kwa risasi, na “watu wasiojulikana”! Lengo ilikuwa ni kumuuwa, lakini bahati nzuri yupo hai! Hili likaendelea kutushangaza wengi, eti mara hii wazanzibar wamekuwa wanamiliki silaha za moto, na ni wajuzi wakuzitumia?!! Hapa sasa tukasikia kauli kali zaidi, tena kutoka kwa viongozi wajuu zaidi kisiasa katika nchi yetu, akiwemo Rais wa Tanzania, Kanali, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa serkali ya Zanzibar Biochemist, Dr. Ali Shein, wakilaani nakuvitaka vyombo vyote vya jeshi la polisi, wakiwemo usalama wa taifa kufanya uchunguzi kwa weledi wajuu kabisa ili kubaini na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wahusika! Tukasubiri na tunaendelea kusubiri kuwajuwa wahusika, lakini mpaka sasa hakuna jibu!
Eeeh juzi tena tunasikia Pandri Mushi, ameuliwa kwa risasi na “watu wasojulikana”! Mauaji hayo yanatokea tena ndani ya Zanzibar hiyo hiyo! Mara hii Tanzania zima ikatikisika, kauli nzito nzito, kutoka kila kiongozi wanchi hii, kuanzia rais wa Tanzania, rais wa SMZ, waziri wa mambo ya ndani, n.k…karibu kila mwenye mdomo (access ya vyombo vya habari) alisema na kulaani. Tukaambiwa FBI, CIA, Mossad wote hao wakishirikiana na TISS watakuja kuchunguza na kuwatia nguvuni walomuuwa na walo ratibu mauwaji hayo….tukasubiri nab ado twasubiri!
Tukiwa bado tumehamanika na matukio hayo, tukiwa bado tunanyoosheana vidole, na kutupiana lawama, tukiwa tunazidi kuandamwa na wingo zito…leo tunasikia imamu sheikh Ali Khamis huko kitope (kaskazini Unguja), ameuliwa kwa kukatwa katwa mapanga na “ watu wasiojulikana”! Nategemea kauli zitakuwa hizo hizo “Uchunguzi utafanyika…” Na sisi ni kama vifaranga vya kuku…tutanyonya kesho, nabado twasubiri kunyonya!
Kwa kweli ukiangalia ukubwa wa visiwa vyetu (Zanzibar) na population yake na ukilinganisha na matukio haya, utaona kwamba ni matukio mengi sana na yametokea katika kipindi kifupi sana, matukio yakusikitisha na kulaaniwa na kila muungwana! Matukio yasiyopaswa kutokea katika jamii ya watu walostaarabika kama Zanzibar.
Chakusikitisha na kutisha ambacho ndicho kilichonisukuma kuandika haya, ni kuwa matukio yote haya, yamekuwa yakiishia kuhukumiwa na jamii kwa hisia tu, huku serkali ikiishia na jibu la “watu wasojulikana upelelezi unaendelea”, lakini jamii, na hata viongozi wa serkali na dini wamekuwa wakitumia hisia zao, utashi na mihemko yao kushutumu na hata kuhukumu baadhi ya kikundi au kundi katika jamii.
Mwanzaoni wapo walojaribu kuhusisha matukio hayo na CUF, lakini walipoona wazanzibar wa hivi sasa hawatopigana wala kuuwana kwa sababu ya vyama vya siasa, wakakosa nguvu! Lakini mara zote kundi la UAMSHO, likawa ndio kitambaa chao (leso) cha kufutia mafua, jasho, mate, n.k., kila tukio likitokea, basi utaskia UAMSHO hao, kauliwa padre “UAMSHO” , Kamwagiwa tindi kali sheikh -“UAMSHO”, limechomwa kanisa-“UAMSHO”! Khaa, mengine enhe, lakini mengine nkinehe!
Serkali imeacha kufanya kazi yake (Jeshi la polisi) kama walivyoafanya kule mwanza alipouliwa RCO , badala yake imeachia jamii ihukumu kwa hisia, ni hatari! Maana sasa viongozi wa UAMSHO wako ndani, UAMSHO hajulikani ni nani, lakini mauwaji yanaendelea! Sasa akiuliwa padri au kuchomwa kanisa utaskia ni waislam hao, naam hisia hisia, waislam hao wa Zanzibar sasa washakuwa magaidi! Si ndo alivyosema Nchimbi! Na sasa akiuliwa sheikh au ikichomwa misikiti, kwa hisia tu watasema “ WAKRISTO hao” na wakristo nao washakuwa magaidi! Tunako kwenda siko!
Siamini na kamwe sitoamini kwamba eti matukio haya yanafanywa na mzanzibar wakawaida, awe mkiristo au muislam, kamwe siamini kama mzanzibar wakawaida anamiliki silaha ya moto, na amekuwa mjuzi wakuitumia kiasi kwamba anaweza kulenga shabaha kwa ustadi mkubwa huku akiwa kwenye vespa na kumuuwa padri! Siamini kabisa, kama kweli mzanzibar anaweza kumvamia sheikh na kumkata kata mapanga! Nani basi anae fanya haya? Na anafanya haya kwa nini? Na Kwanini mapaka leo Kamishna Mussa hajatoa majibu ya walofanya matukio haya?
Inasikitisha na kushangaza sana, waziri mwenye dhamana na ulinzi wa taifa hili, anaibuka akiwa na maruwe ruwe (hangover) ya mapombe yake alokunywa “Rose garden” anasema eti wanaofanya matukio hayo ni MAGAIDI, huyu ni msomi wa PhD, eti daktari wa falsafa! Kwa falsafa ya aliepata Div 0 matokeo ya mwaka huu ya form 4, basi inatosha kumwambia waziri wakati unatanganza hayo, hukupaswa kuendelea kuwa waziri wa wazara hiyo tena! Ikiwa umeshindwa kudhibiti magaidi mpaka wameweza kuingia ndani ya nchi yako, lakini kama haitoshi, wakaweza kumiliki silaha, wakaweza kupanga na kutekeleza mauwaji na uharibifu wa nyumba za ibada wakati wewe ndie mwenye dhamana ya kulinda hayo yasitokee, sijui alikuwa au bado anangoja nini kwenye ofisi yake? Lakini pia angetwambia hawa magaidi wana demand (madai) nini?
Maana ya neno gaidi (terrorist), ni mtu anaeletea madhara katika jamii au anaefanya mashambulizi au utekaji kwa lengo la kugofya mamlaka au mtu husika ili atekelezewe madai yake! Kwa misingi hiyo gaidi huwa akishatenda huwa hutokeza wazi wazi na kusmema, mimi ndio niliofanya jambo kadhaa, ili unipe, au utekeleze masharti kadhaa, usipotekeleza ntafanya tena jambo kadhaaa…! Sasa matukio yote haya hakuna kikundi, wala mtu alojitokeza kukiri kufanya na kusema amefanya ili apewe nini au anadai nini. Sasa Dr. Nchimbi atwambie magaidi wake hawa wana mdai nini? Atwambie, wanauwa mapadri ili wapewe nini na kanisa katoliki? Wanauwa masheikh ili wapewe nini na waislam?
Nakumbuka, nilipokuwa na miaka 12, ilikuwa tukifunga skuli (nilikuwa skuli ya Jadida, Wete), nikienda kwa bibi yangu Pandani kwa mwewe, kuna mengi niliyapenda huko pandani ikiwemo kuchota maji kwenye kisima cha ndoo kwa kutumia “roda”, lakini jambo jengine ilikuwa lilonifanya niamke mapema sana ni “mchezo wa kupiganisha kuku” ! Niliupenda sana mchezo huu! Walipiganishwa majongoo wakila aina kuanzia makuchi, majogoo upanga n.k. Lakini ugomvi wa makuchi ulikuwa mtamu sana, hawachoki haraka, wajuzi wakupigana, hawakubali kushindwa, si woga na wepesi wakupiganishwa!
Walipiganishwa makuchi wale bila wenyewe kuwa na sababu ya msingi yakupigana! Walipiganishwa bila kujuwa kwanini wanapigana? Walipigana sababu tu wametumwa kupigana! Kupigana kwao makuchi hawa ndo furaha ya wapiganishaji, pengine wapiganaishaji hucheza kamari, na mwenye kuchi alieshinda akapata malipo!
Historia ni mwalimu nzuri, tunasoma kwamba kule India wakati wa harakati za kudai Uhuru zilizokuwa zikiongozwa na Mahtma Gandhi, wakati huo India ikiwa koloni la British, wakoloni hawa walikuwa wakiwapiganisha waislam na wahindu, ili kujenga hoja ya kutowapa uhuru! Walikuwa wakichinja nguruwe kasha wakiwatupa kwenye misikiti ya waislam…kwa hisia waislam wakiwashutumu wahindu kwa kuwatupia nyama haramu, najisi kenye nyumba zao tukufu za ibada, kisha wakoloni hawa wakichnja ng’ombe na kuwatupa kwenye mahekalu ya wahindu, wahindu nao kwa hisia tu, wakawashutumu waislam, kwamba ndio wanaowauwa miungu yao (wahindu wanaabudu ng’ombe kama mungu wao), kisha wanawatupa kwenye nyumba zao za ibada! Kwa hisia wakaishia kupigana na kuuwana….mkoloni akazidi kutawala!
Hali hii ndio nnayo iona Zanzibar, matukio ya kumwagia mavi visima vya maji, kuchomwa moto nyumba za masheha, kulipuliwa mabomu ofisi za CCM, tuliyaona mageni yalipoanza miaka 90 kule kisiwani Pemba, tukawa twaambiwa ni wapinzani, wafukuwa hadi barabara na kuvunja mabomba ya maji! Lakini kisha tukayazoea, na jamiii ikamjuwa hasa anaefanya hayo ni nani! Sasa kuna kumezuka jipya, lakini safari hii si Pemba, ni kwa dada yake, Unguja, kumezuka fasheni ya sampuli yake ya kuwauwa viongozi wa dini, wanauliwa mapadri leo, na kesho wanauliwa masheikh, kwa zamu!
Ni lazima tutumie akili zetu vizuri katika kutafakari mambo haya! Tuweke hisia zetu na misukumo ya kiimani pembeni! Tumuombe Mungu wetu atupe hekima ya kuangalia matukio haya kwa jicho la 3, atupe hekma ya kuwa waadilifu katika kuchambuwa matukio haya! La sivyo, basi, leo atauliwa Padri John, kwa hisia upande mmoja utasema –“WAISLAM hao”, kesho atauliwa Sheikh Abdalllah, kwa hisia upande mwengine utasema – “WAKRISTO hao”, kitakachofuata sihitaji kukieleza hapa, maana wote tunajuwa! Mungu atunusuru!
Wapiganishaji watakuwa wamekaa pembeni wakitutazama tunavyouwana kwa ujinga wetu! Watakuwa wanasubiri kuleta misaada ya kibinaadam” (kama wanavyoita wenyewe), watasubiri kuleta majeshi yao kusimamia amani, watapa habari za kutanganza kwenye vyombo vyao vya habari kama vile CNN, BBC, Al jazeera n.k Zanzibar itakuwa maarufu kama ilivyo afghanstan, Iraq, Syria, n.k! Watapata sababu za kutosha za kuifanya Zanzibar kuwa mkoa wa Tanzania! Utamaduni na asili ya Zanzibar sasa ndo itapotea kabisa!
Tusikubali kufanywa makuchi tukapiganishwa sie kwa sie….!
Chanzo: Mzalendo

No comments:

Post a Comment