Friday 13 April 2012

Wazanzibari wa Tume watashikana ama wataangushana?

Barazani kwa Ahmed Rajab
 
WATANZANIA sasa wanatambua kwamba mchakato wa Katiba umeanza kwa dhati. Pia sasa wanajua nani yumo na nani hayumo kwenye Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Mabadiliko ya Katiba.
Tume hiyo, ambayo kwa mkato inaitwa Tume ya Katiba, ni chombo chenye umuhimu mkubwa katika mchakato mzima wa kutunga Katiba mpya na kinahitaji kuwa na uadilifu wa hali ya juu wa kuweza kuwakilisha maoni halisi ya wananchi kuhusu Katiba waitakayo na hivyo kuhusu aina ya Muungano wautakao.
Majina 30 ya wajumbe wa Tume hiyo yalitangazwa Ijumaa iliyopita na Rais Jakaya Kikwete pamoja na ya mwenyekiti wa tume na makamu wake.
Wajumbe hao (15 kutoka Bara na 15 kutoka Visiwani) wataapishwa baadaye mwezi huu kama inavyotakiwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 ambayo ndiyo iliyosababisha kuundwa kwa Tume hiyo ya Katiba. Mwenyekiti wao, Jaji Joseph Warioba ametoka Bara na Makamu wake Jaji Mkuu mstaafu Augostino Ramadhani ni Mzanzibari.
Kuteuliwa kwa Tume hiyo ni hatua ya mwanzo katika mchakato uliopangwa uendelee kwa muda wa miaka miwili na kufikia kikomo Aprili mwaka 2014.
Inatarajiwa kwamba kufikia hapo, Jamhuri ya Muungano ya Tanzania itakuwa imepata Katiba mpya itayotungwa na Bunge la Katiba na kupigiwa kura ya maoni na wananchi.
Yote hayo yatatendeka kwa mujibu wa Sheria Kuhusu Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni. Sheria hiyo ndiyo iliyomwezesha Rais kuunda hiyo Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni Kuhusu Katiba Mpya.
Sheria hiyo ina vifungu vingi vilivyo muhimu sana kama kile chenye kutaka pawepo na idadi sawa ya wajumbe kutoka Zanzibar na kutoka Bara katika Tume ya Katiba. Hilo limetekelezwa.
Labda kifungu kilicho muhimu zaidi ni kile chenye kusisitiza kwamba mchakato huo uwe unaongozwa na kuamuliwa na wananchi. Ndiyo maana pakawa na haja ya kupigwa kura mbili tofauti za maoni — moja kwa upande wa Bara na nyingine kwa upande wa Zanzibar.
Zoezi hilo la kura ya maoni lina umuhimu wa aina yake — pingine kama wa kufa na kupona — kwa Zanzibar. Lakini hata kabla ya Wazanzibari kupiga kura hiyo ya maoni juu ya iwapo wanaikubali au wanaikataa Katiba itayopendekezwa Tume ya Katiba itakuwa na jukumu la kukusanya maoni ya Wazanzibari katika kila shehia ya Unguja na Pemba. Hapo Tume itakuwa na kazi ya kweli.
Kwa mara ya mwanzo Wazanzibari watapata fursa ya kutoa maoni yao bila ya woga wowote na bila ya vikwazo vyovyote kuhusu mustakbali wa nchi yao na namna wanavyotaka kujipatia malengo yao ya kitaifa.
Kwa vile mchakato huo umeanza, ni muhimu kukumbushana kwamba hili si jaribio la kwanza la kutunga Katiba mpya ya Tanzania. Kabla ya mchakato huu wa sasa kulikuwa na Tume za Nyalali na Kisanga zilizotoa mapendekezo ya kimsingi kuhusu Katiba mpya ya Tanzania. Mapendekezo hayo lakini yalipingwa na kutupiliwa mbali na Serikali ya Muungano.
Miongoni mwa mapendekezo ya Tume ya Nyalali lile la kuwa na mfumo mpya wa vyama vingi vya kisiasa lilikubaliwa lakini mapendekezo yake kuhusu mageuzi ya kimsingi ya kisheria na kikatiba yalikataliwa ingawa yalikuwa muhimu ili mfumo wa kidemokrasia uweze kumea vizuri katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Ni taabu kutabiri matokeo ya huu mchakato wa sasa yatakuwaje. Ninasema hivi kwa sababu kwa upande wa Zanzibar kumetokea mageuzi makubwa ya kifikra miongoni mwa wananchi kuhusu Muungano wa Visiwa hivyo na Tanganyika. Na wanapoyajadili masuala yanayohusika na Muungano utawakuta kuwa hawana tena woga wa kudhaniwa kuwa ni mahaini.
Natuombe salama kwa sababu jinsi Wazanzibari wanavyotoa hoja za kuunga mkono maoni yao sitostaajabu endapo mchakato huu utasimamishwa kabla ya wakati wake pale wajumbe wa Kamati ya Tume watapoyasikia rasmi maoni hayo.
Jambo jingine lililotokea huko Visiwani hivi karibuni ni Wazanzibari wengi vya vyama na itikadi tofauti za kisiasa kuwa na sauti moja kuhusu ile wanayoiita Ajenda ya Zanzibar. Tunachosubiri kuona ni iwapo wajumbe 15 wenye kuiwakilisha Zanzibar katika Tume ya Katiba nao wataibuka kuwa na sauti moja na msimamo mmoja wenye kuyawakilisha matakwa halisi ya Wazanzibari wenzao au la.
Ikiwa watakuwa na msimamo huo patakuwa salama. Lakini ikiwa wataonekana kuwa kama nyumba iliyogawika kama hali ya mambo ilivyokuwa katika tume zilizopita, ikiwa watakuwa wanazozana wenyewe kwa wenyewe na kupingana kwa misingi ya kichama na kupuuza matakwa ya Wazanzibari basi wenzao wa Visiwani hawatowasamehe wala hawatokuwa na imani nao.
Hivi sasa takriban kila wiki kunafanywa mikutano na mihadhara mbalimbali katika sehemu tofauti za Zanzibar ambapo Wazanzibari wanakusanyika bila ya kujali mielekeo yao ya kisiasa kuutafakari mustakbali wa Zanzibar ndani na nje ya Muungano wake na Tanganyika.
Kilichojitokeza ni kwamba mikutano hiyo inaandaliwa na kudhaminiwa na jumuiya zisizo za kisiasa. Kwa hakika, vyama vikuu vya kisiasa huko Zanzibar vimekaa kimya, havisemi lolote kuhusu suala hili. Sababu zilizovifanya vyama hivyo visithubutu kufungua midomo yao zinaeleweka. Hiyo ni kheri pia kwani wananchi wa Visiwani wamepata uwanja wa kuyasema yaliyo kwenye nyoyo zao bila ya kufungika kwa maagizo au misimamo rasmi ya vyama hivyo.
Ninafikiri labda sababu iliyovifanya vyama vya CCM na CUF vikae kimya ni kwamba mapendekezo yao rasmi kama yalivyo kwenye ilani zao yamepitwa na wakati na hayakubaliwi na idadi kubwa ya Wazanzibari wenye kuamini kwamba hayatoweza kulitatua tatizo lao la kimsingi.
Pendekezo rasmi la CCM/Zanzibar ni la kuendelea na mfumo uliopo wa serikali mbili (ya Zanzibar na ya Muungano) na kutia virakapale palipochanika au kufumka. Lile la CUF ni la kutaka pawepo serikali tatu (ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya Muungano).
Ukizungumza na Wazanzibari na ukisoma wanayoyaandika katika mitandao yao utaona kwamba wengi wao, bila ya kujali ni wafuasi wa chama gani, wanataka nchi yao iwe na mamlaka kamili ya kidola. Wanataka iwe na mamlaka yatayoiwezesha nchi hiyo iendeshe shughuli zake za ndani na za nje. Muhimu kushinda yote wanataka iwe na serikali yenye uwezo kamili wa kusimamia mambo yake ya kiuchumi, ya kijamii na ya kisiasa. Tukitaka tusitake hii ndio hali halisi ilivyo Zanzibar hii leo.
Ikiwa vile vyama viwili vikuu vya kisiasa huko Zanzibar pamoja na tabaka zima la wanasiasa wa huko hawatoona umuhimu wa kuiangalia upya misimamo yao kuhusu Muungano basi nao pia watakuwa wamepitwa na wakati na hawatokuwa na maana yoyote kwa nchi yao.
Lazima watambue kwamba kuna mambo mawili makuu yenye kuwafanya Wazanzibari wawe kila mara wanakuna vichwa vyao. Nayo ni namna ya kujipatia tonge na suala la Muungano. Ndiyo maana tunaona kwamba wananchi wa kawaida wa Zanzibar wamewapiku viongozi wao wa kisiasa, kutoka vyama vyote. Wananchi wako katika safu za mbele kabisa katika kudai haki zao na ndiyo maana pia tunaona kwamba ni asasi zisizo za kiserikali pamoja na vikundi vingine ndivyo vilivyo mbele katika kuuongoza mjadala na kuelimishana kuhusu Katiba mpya.
Wazanzibari wanajua walitakalo. Siku hizi hawakubali tena kubabaishwa au kutishwa na yeyote yule waridhie wasilolitaka.
Kadhalika, ni dhahiri kwamba leo Wazanzibari wana umoja wasiokuwa nao kwa muda mrefu sana. Wameazimia kwamba vizazi vyao vijavyo viwe na maisha bora kuliko waliyokuwa nayo wao. Kwa hilo tu pana haja kubwa ya viongozi wa Zanzibar — wa CCM na wa CUF — wawe wanashirikiana na kufanya kazi pamoja ili wawe na msimamo ambao utayawakilisha kikweli matakwa halisi ya wananchi wenzao. Wakifanya hivyo watakuwa wanalipigania lengo la kitaifa la Wazanzibari.
Vivyo hivyo wale wajumbe 15 Wakizanzibari katika Tume ya Katiba wanawajibika kushirikiana na kuwa kitu kimoja katika kuyatetea maslahi ya Zanzibar. Lazima waiweke mbele Ajenda ya Zanzibar na wasiyumbishwe na ajenda za vyama au zao wao wenyewe binafsi au tamaa ya kunufaika wao.
Wajumbe hao wametwikwa jukumu kubwa. Wasipoitumia vyema fursa waliyoipata ya kuiwakilisha vilivyo nchi yao basi watajikuta wanalaaniwa si na wananchi wenzao tu bali historia nayo daima itakuwa ikiwalaani.

No comments:

Post a Comment