Thursday 19 April 2012

Wawakilishi Zanzibar wailipua familia ya Karume

Salma Said, Zanzibar
KAMATI Teule ya Baraza la Wawakilishi imegundua ufisadi wa kutisha katika maeneo tofauti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), huku familia ya Rais mstaafu wa visiwa hivyo, Aman Abeid Karume ikitajwa kukiuka sheria kwenye umiliki wa ardhi.

Wakati familia hiyo ya Rais mstaafu Karume ikituhumiwa kukiuka sheria za ardhi, mfanyabiashara maarufu nchini Said Salim Bakharessa ambaye naye ametajwa kujipatia kiwanja cha Serikali kwa bei ndogo, alijitetea mbele ya kamati na kumlipua waziri aliyekuwa na dhamana ya ardhi akisema, "Mimi nilipigiwa simu na waziri akiniambia kuna kiwanja kinauzwa."
Akisoma ripoti hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Omar Ali Shehe, alitaja maeneo ambayo yalibainika kuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria ambayo mbali na sekta ya ardhi ni ajira katika utumishi Serikali, mikataba katika maeneo nyeti na ukiukaji wa sheria za ununuzi.
Akizungumzia uhalali wa mikataba ya nyumba ya Serikali iliyopo Kiponda inayodaiwa kwamba alipewa mwananchi na baadae kuiuza kwa mtu mwingine, Shehe alisema Kamati imebaini kwamba, mikataba yote ya mauziano iliyofungwa baina ya Serikali na Juma Ali Kidawa na baina yake na Amina Aman Abeid Karume, ni batili na ya udanganyifu.
Shehe alisema kumekuwapo uvamizi wa fukwe na uharibifu wa mazingira kwenye hoteli inayopakana na Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar, Maruhubi, kwenye Hoteli ya Zanzibar Ocean View, Kilimani-Zanzibar na Hoteli ya Misali iliyopo Wesha, Chake Chake-Pemba.
Aliongeza kwamba Kamati imejiridhisha kwamba Ramadhan Abdallah Songa na Mama Fatma Karume walishiriki katika udanganyifu wa mkataba wa mauziano uliofungwa baina ya Serikali na Kidawa.
"Aidha, hati ya matumizi ya ardhi aliyopewa Karume na Mansour Yussuf Himid, (Akiwa Waziri wa Ujenzi, Nishati na Ardhi), imekiuka taratibu za kisheria na kiutawala), " alisema mwenyekiti huyo.

Shehe alisema Kamati inapendekeza nyumba hiyo ambayo sasa imeshajengwa Hoteli ya Amina Aman Karume, hati zote za umiliki wake, zifutwe na apatiwe tena hati ya umiliki wa ardhi husika na baadae atakiwe kumsaidia Kidawa kwa kiwango cha fedha kisichopungua Sh20 milioni, kujinasua na maisha.

"Hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wananchi wote waliohusika katika udanganyifu uliojitokeza katika upatikanaji wa mikataba ya mauziano kutoka katika mamlaka ya Serikali na kumuuzia Kidawa na mauziano baina ya Kidawa na Amina Aman Abeid Karume,"alisema Shehe.

Shehe alisema pia kwamba imegundulika Machano Othman Said akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Miundombinu na Mawasiliano) katika Serikali ya awamu hiyo ya sita, anamiliki asilimia 10 ya hisa katika mradi wa Hoteli ya Misali Sunset Beach, iliyopo Wesha Pemba.

Alisema kwa nafasi yake wakati huo akiwa waziri, Machano (ambaye kwa sasa ni Waziri asiye na Wizara Maalumu), alitumia nafasi yake kuisaidia kuendeshwa hoteli hiyo bila kibali cha mazingira wala leseni ya utalii kutoka Pemba, ambako ndiko kwenye mradi huo hivyo awajibishwe.

Katika ripoti hiyo, Shehe alibainisha kuwa uchunguzi uliofanyika kuhusu uhaulishwaji wa kiwanja cha Wizara ya Miundombinu na Mawasililiano ambacho kipo kwenye eneo ilipokuwepo Karakana na wizara hiyo, eneo la Mtoni, Mjini, Zanzibar, umeonyesha kuna ukiukwaji mkubwa sheria na taratibu za uuzaji wa mali za Serikali.

Shehe, alisema wamejiridhisha kwamba wizara hiyo ya Miundombinu na Mawasiliano haikufuata taratibu za uuzaji wa kiwanja hicho ilichokuwa inakimiliki na kuamua kukiuza kwa kampuni binafsi bila ya kufuata taratibu za kiutawala na taratibu za kisheria.

"Hali hiyo imepelekea wasi wasi mkubwa wa kuwepo kwa harufu ya ubinafsi na harufu ya rushwa, zaidi ukizingatia thamani ya kiwanja hicho kuwa ni sawa na Sh200 milioni bei ambayo ni ndogo kwa mujibu wa bei ya soko na kwa kuzingatia ukubwa wa kiwanja chenyewe na eneo kilipo,"alisema Shehe.

Alisema kulikuwa na matumizi mabaya ya madaraka ya Ofisi ya Rais kwani walipokuwa wakiangalia namna gani ulitolewa uamuzi mzito wa kuuza kiwanja hicho cha Serikali, ilibainika iliruhusiwa na Ofisi ya Rais.

"Katika utafiti wetu, tuligundua kuwa, maombi ya ruhusa ya kuuzwa kwa kiwanja hicho, yametoka kwa Katibu wa Rais, Haroub S. Mussa, ambaye aliandika barua, tuliyoifanya kielelezo Namba. 9 cha Ripoti yetu," alifafanua.

Shehe alisema Haroub hana mamlaka ya kuruhusu uuzwaji wa kiwanja, wala kusimama katika nafasi ya kupeleka uamuzi wa Rais kwa mtu mwengine yeyote kwani kazi hiyo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, kifungu cha 49(1), inafanywa na Katibu Mkuu Kiongozi.

Kutokana na hali hiyo, kamati imependekeza aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mawasiliano na Uchukuzi (2008-2010, Machano) na watendaji wote waliohusika katika kuingia mikataba na Kampuni ya Coastal Fast Ferries Ltd, wawajibishwe kwa misingi ya sheria.

Kuhusu kuchunguza suala zima la Uwanja wa Ndege wa Zanzibar, alisema ulipaji wa fidia kwa watu ambao mali zao zimeathirika kutokana na ujenzi wa uzio wa uwanja huo umegubikwa na utata.

"Matatizo ya ununuzi wa jenereta, mikataba ya ukodishwaji wa sehemu za biashara kwenye eneo la uwanja na utaratibu wa ajira na utoaji wa huduma mbali mbali kwenye maeneo ya uwanja na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa ujumla, haukuzingatia sheria," alisema Shehe.

Alisema kamati imegundua na kujiridhisha kwamba, kumefanyika uzembe wa makusudi na Wizara zote mbili zimehusika katika uzembe huo yaani Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na matokeo yake zaidi ya Sh300 milioni, zinaelekea kupotea huku jenereta lililonunuliwa kwa fedha zote hizo, limeshindwa kujaribiwa kwa kipindi chote cha muda wake wa majaribio (warrant period).

"Aidha, kitendo cha jenereta kukaa bila ya matumizi ya muda mrefu pia ni sehemu ya uharibifu wake. Kwa mantiki hiyo, Kamati inafahamu kwamba, jenereta hilo limetelekezwa," alisema.

Alisema kamati inapendekeza hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa watendaji wote waliohusika na uzembe wa ununuzi wa jenereta hilo, huku msisitizo ukiwekwa kwa makatibu wakuu wa Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano; Mkurugenzi na Meneja wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege.

"Kuhusu mikataba, kamati inapendekeza mikataba yote inayohusiana na ukodishwaji wa biashara mbali mbali katika eneo la uwanja wa ndege ipitiwe upya ili iendane na mabadiliko ya biashara na msisitizo ukiwekwa katika gharama za kodi husika,"alisema.

Katika utoaji ajira kwa upendeleo, Shehe alieleza kuwa Waziri wa Wizara Miundombinu na Mawasiliano, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, wamekuwa wakiwaajiri watoto, ndugu ama jamaa zao, huku wakiwapa fursa nyingi za upendeleo kinyume na utaratibu.

"Spika, naomba kwa makusudi wajumbe wako wapate taarifa hizi katika mfanyakazi, Aisha Msanif Haji, mtoto wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, ambaye ameajiriwa na bado akiwa katika kipindi cha majaribio, tayari amepewa ruhusa ya kusoma, huku akiwa anaendelea kupokea mshahara kama kawaida."

Alisema imethibitika kwamba, kuna mfanyakazi analipwa mshahara wa ngazi ya mtaalamu (msomi wa shahada) wakati bado hajafikia elimu hiyo.
"Huyu si mwengine isipokuwa mtoto wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano,"alisema.
Shehe alisema kutokana na hali hiyo, Kamati imependekeza viongozi na watendaji wakuu wa wizara zote mbili (Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora) waliohusika na kadhia hiyo wawajibishwe kisheria.
Pia uajiri wa wafanyakazi wote ambao kamati imeona hawana sifa za kuajiriwa, ufanyike upya kwa kufuata muongozo wa sheria zilizopo.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment