Friday 20 April 2012

Waandamana kutaka kura ya kuamua Muungano

Salma Said, Zanzibar
JESHI la Polisi Zanzibar limewatia mbaroni zaidi ya watu 10 wakiwemo viongozi wa kundi la wanaotaka kuitishwe kura ya maoni kuhusu Muungano, baada ya kukataa kutii amri ya jeshi hilo iliyowataka kuondoka katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi jana.

Kundi la watu zaidi ya 40 lilifika katika viwanja hivyo vya Baraza la Wawakilishi huko Chukwani wakitaka kuonana na Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho.

Spika alimuagiza Katibu wake, Yahya Khamis Hamad kuongea na wananchi hao.
Wakizungumza nje ya viwanja hivyo, wananchi hao walisema lengo lao ni kuonana na Spika Kificho ili kuwasilisha ombi lao la kutaka kupelekwa hoja binafsi ya kuitishwa kura ya maoni ya kutaka au kukataa Muungano.

Katibu wa Baraza hilo alisema sio vibaya wananchi hao kuwasilisha mapendekezo hayo kwa Spika, lakini aliwataka wananchi hao kufuata utaratibu unaokubalika wa majadiliano na siyo kujikusanya katika viwanja hivyo jambo ambalo linatishia usalama.

“Waheshimiwa pengine mmekuja hapa kwa nia njema kabisa lakini kwa utaratibu huu nimelazimika kuja hapa nje na kukuombeni muondoke ili muache shughuli za baraza ziendelee kwa sababu sipendi kuona mkipambana na polisi katika viwanja hivi,” alisema Katibu huyo.

Aliongeza, “Hata Spika alisema kwa utaratibu kama huu hataweza kuwaruhusu kuonana naye lakini kama mtafuata utaratibu mzuri ambao umewekwa na tumeuainisha ndani ya barua zenu basi mnaweza kukutana na kuongea naye."

“Lakini kwa hali kama hii haitawezekana kwa sababu shughuli za Baraza zinaendelea lakini pia wananchi wanashindwa kupita hapa na kufanya shughuli zao kwa kuwa mmefunga njia, waheshimiwa wanataka kuja hapa lakini wanashindwa kutokana na hali hii,” alisema Katibu Hamad.

Mapema, wananchi hao wakiongozwa na Rashid Salum Adiy walifika katika viwanja hivyo kwa wingi wakiwa na mabango yao yenye ujumbe wa kutaka kuitishwa kwa kura ya maoni kuamua mustakabali wa Zanzibar ambapo walitaka kuingia ndani na kuonana na uongozi wa baraza hilo.

Hata hivyo jeshi la polisi lilitoa tahadhari na kuwataka waondoke katika viwanja hivyo na kuelekea nyumbani ili kupisha viongozi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwasili katika baraza hilo ili waendelee na shughuli za Baraza hilo ambalo jana limeakhirishwa.

Rashid Sulum Adiy ni kiongozi wa kundi hilo la wazanzibari wenye kudai kuitishwa kura ya maoni juu ya mustakabali wa Zanzibar ndani ya Muungano na anataka Baraza la Wawakilishi liitishe kura ya maoni ya kuwauliza wazanzibari iwapo wanautaka Muungano au hawautaki.

Katika barua yao walioiwasilisha kwa Spika Kificho ya Aprili 18 mwaka huu inasema “Sisi ni wananchi 1825 miongoni mwa watu 300,000 sote wazanzibari na ni watu wazima wenye akili timamu kutoka majimbo 50 ya Unguja na Pemba tunakutaka utuwasilishie mbele ya Baraza la Wawakilishi ombi la hoja yetu binafsi ya kuwepo kwa kura ya maoni juu ya suala la Muungano wa Tanzania,” ilisema barua hiyo.

Wakitilia mkazo hoja hiyo katika barua yao walisema baada ya kipindi cha miaka 48 ya Muungano hoja yao hiyo ya kuitisha kura ya maoni ni muhimu sana kwa wazanzibari na vizazi vya baadae.

“Hatukubali kama tutapigwa mabomu, marungu au kukamatwa kwa sababu ya hatari inayotukabili mbele yetu. Kwa hivyo kwa heshima na tunaliomba baraza nalo lishirikiane na sisi kwa kutumiza wajibu wake na kulikubali ombi letu la kuwa na kura ya maoni juu ya Muungano,” ilisema barua hiyo ambayo Mwananchi inayo nakala yake.

Barua hiyo imesema Muungano huo umekosa misingi ya kisheria ya kitaifa na kimataifa na ndio sababu ya kuongezeka kero na kasoro kadhaa, lawama na matatizo mbali mbali yanayoshindikana kutatuliwa kwa pande mbili hizo.

Walisema kwa kuwa Muungano huo unahusu nchi mbili tofauti, za Zanzibar na Tanganyika ni vizuri wananchi wakapewa nafasi ya kuhojiwa iwapo wanautaka uendelee au uvunjike kwani maamuzi ya wananchi ndio yanayotegemea kuendeleza usalama na utulivu uliopo.

Hivi karibuni Rais Kikwete aliteua tume ya kukusanya maoni juu ya Katiba mpya na tayari wajumbe wa tume hiyo wameshaapishwa na wataanza kazi rasmi mwanzoni mwa mwezi ujao lakini malalamiko juu ya suala hilo yamekuwa yakijichomoza kila siku hapa Zanzibar.

Makundi mbali mbali yamekuwa yakifanya mikutano ya wazi kuelezea suala hilo huku idadi kuwa ya wazanzibari wakiunga mkono hoja ya kuwepo kura ya maoni kwanza kabla ya tume kuanza kufanya kazi zake.Kamishna wa polisi Ali alisema watu hao watafikishwa mahakamani Jumatatu kwa kosa la kusababisha uvunjifu wa amani.

Alisema ingawa sheria inawapa watu haki ya kudai wanachotaka, bado watu wana wajibu wa kufuata taratibu ili kulinda haki za wengine na badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment