KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod
Slaa, ameeleza kushtushwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete inayolenga kuzuia
wananchi kujadili kuhusu Muungano wakati wa mchakato wa marekebisho ya
Katiba.
Dk. Slaa aliye katika ziara ya kichama kukagua uhai wa chama hicho ikiwa ni
pamoja na kukijenga, alitoa dukuduku lake hilo jana wakati akihutubia mkutano
mkubwa wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shycom, mjini Shinyanga.
Katibu mkuu huyo wa CHADEMA alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tu tangu
Rais Kikwete alipowaapisha wajumbe 30 wa Tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya
inayoongozwa na mwanasheria na mwanasiasa anayeheshimika, Jaji Joseph
Warioba.
Wakati akizindua tume hiyo juzi, pamoja na mambo mengine, Rais Kikwete
alisema tume hiyo katika kazi yake haitahusika katika kuhoji kuhusu kuwapo ama
kutokuwapo kwa muungano.
Kwa upande wake Dk. Slaa aliwataka Watanzania kuachana na maneno ya watawala
na kutobweteka baada ya kuundwa kwa tume hiyo ya Jaji Warioba.
“Jamani Watanzania wenzangu wa Shinyanga, naomba tuzungumze kidogo hili la
Katiba mpya, kwanza nawaomba msibweteke eti kwa sababu tume imeundwa, kuundwa
tume hakuleti katiba mpya na bora. Pia tunataka Kikwete ajue kuwa Watanzania
hawatengenezi katiba ya Kikwete wala ya CCM. Wanataka Katiba mpya na bora ya
kwao.
“Nami namuomba ni bora akajitahidi kujiepusha na matamko ya ajabu, maana
anaendelea kutupatia ajenda. Anasema suala la muungano lisijadiliwe wakati wa
mchakato wa utoaji maoni. Hapa anataka kutuma ujumbe gani…” alisema Dk. Slaa na
kushangiliwa.
Akiuchambua muungano, Dk. Slaa alisema ni haki ya Watanzania kwa maana ya
wale wa Zanzibar na wa Bara kujadili muungano wanaoutaka kwani kufanya hivyo
hakuna nia ya kuuvunja.
“Sisi CHADEMA tunasimamia nini? Tunataka Watanzania wajadili wanataka
muungano wa aina gani, tunataka Zanzibar ipate haki zake kama ilivyokuwa mwaka
1964.
“Hapa hoja si muungano uwepo ama usiwepo, hoja ni aina gani ya muungano wa
kisiasa Watanzania wanautaka. Tunaamini kuwa hakuna mwanasiasa mwenye akili
timamu anaweza kuhubiri kuvunja muungano.
“Mwanasiasa anayezungumzia kuvunja muungano huyo ni mwendawazimu, maana
muungano wa kweli wa Watanzania uko kwenye damu zao. Lakini katika suala la
kiutawala wananchi waachwe waamue wanataka aina gani, hii ndiyo hoja hapa,”
alisema Dk. Slaa.
Akifafanua, Dk. Slaa alisema wanazo taarifa kwamba tayari CCM kupitia katika
Halmashauri Kuu yao ya Taifa wameshafikia hatua ya kuwatumia makada wao,
wakiwamo viongozi wa kiserikali kama wakuu wa mikoa na wilaya katika kuhakikisha
yale ambayo chama hicho tawala kinayataka, yanaingizwa katika Katiba mpya.
“Napenda kumwambia haya huku akijua kuwa, mkononi kwangu au ofisini kwetu
tayari tunao uamuzi wa Halmashauri Kuu ya chama chao, ambayo imewaagiza viongozi
ambao ni makada wao, kuhakikisha masuala ambayo chama hicho kinataka yanaingia
katika Katiba mpya, hii ni hatari,” alisema Dk. Slaa.
Akifafanua, alisema chama hicho kitaendelea kuwa mstari wa mbele kuwaongoza
Watanzania waandike Katiba mpya inayozingatia haki za msingi kama vile masuala
ya ardhi, huku pia akisisitiza kuwa suala la mamlaka ya rais linapaswa
kuangaliwa upya na kurekebisha.
Aliongeza kuwa, moja ya mwarobaini wa kuachana na wateule wengi wa rais ni
kuwa na serikali za majimbo ambako viongozi wake sharti wachaguliwe na watu
badala ya sasa wananchi kutawaliwa na mkuu wa mkoa au wilaya wasiyemjua
No comments:
Post a Comment