Thursday 10 May 2012

Zanzibar siyo taifa kamili

Mhariri wa gazeti hili ameamua kuichapicha makala hii kutokana na umuhimu wake nchini wakati huu wa kuelekea kuandika Katiba mpya. Ni makala iliyoandikwa na aliyekuwa Mbunge wa Chunya, Njelu M. Kasaka, miaka 19 iliyopita (1993) na kuchapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Mwananchi.
WAKATI uchunguzi unafanywa na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu uhalali wa Zanzibar kujiunga na Organization of Islamic Conference (OIC) na wakati wa mjadala bungeni kuhusu suala hili mambo mengi yaliyojitokeza. Moja ya mambo yaliyojitokeza kwa nguvu kabisa lilikuwa ni nafasi ya Zanzibar katika Muungano wa Tanzania.
Madai yalitolewa kuwa kwa Bunge kuchunguza suala la Zanzibar kujiunga na OIC ni kuionea Zanzibar kwani hiyo ni nchi huru na taifa kamili (independent sovereign state) lenye uwezo wa kuingia mikataba na mataifa mengine. Viongozi wengi wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na Alhaji Aboud Jumbe, Wolfgang Duarado na Ali Nabwa, mwandishi wa habari wa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, wote walisisitiza kuwa Zanzibar ni nchi huru na taifa kamili.
Hakuna mtu aliyetazamia suala kama hili kuzuka na kupata umuhimu lililoupata. Watanzania wengi hasa Bara, walidhani wanauelewa Muungano na kwamba Zanzibar na Tanganyika zilishaungana na kuwa Tanzania. Lakini hoja zilianza kutolewa ambazo zimeturudisha nyuma miaka 29 iliyopita ili kuangalia upya maana ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni nini.
Kuna swali la kujiuliza. Hivi ni kweli Zanzibar ni nchi huru na ni taifa kamili ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, au ni sehemu tu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyo na uhuru wa kushughulikia mambo yake ya ndani? Ili kupata jibu la swali hili yatupasa kuangalia makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Ibara ya kwanza ya makubaliano ya Muungano (Articles of Union) inasema hivi “Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitaungana na kuwa taifa moja ambalo ni Jamhuri”. Kutokana na makubaliano hayo Jamhuri ya Tanganyika ilitoweka, kadhalika Jamhuri ya Watu wa Zanzibar nayo ilitoweka tukapata Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taifa jipya la Tanzania likazaliwa.
Je, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inasemaje juu ya suala hili? Ibara ya kwanza ya Katiba inasema: “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano,” na ibara ya pili, ibara ndogo ya kwanza inaeleza kuwa, “Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar.”
Katiba hii ndiyo ambayo viongozi wote wa Jamhuri ya Muungano (pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) huapa wanapopewa madaraka, kuiheshimu na kuilinda wakati wote wanapokuwa kwenye madaraka.
Kutokana na maelezo hayo hapo juu ni dhahiri kuwa katika Jamhuri ya Muungano tunayo nchi moja tu na taifa moja tu nalo ni Tanzania. Hakuna taifa jingine ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo kauli ya viongozi wa Zanzibar kuwa Zanzibar ni taifa kamili, ni kauli ya kukana makubaliano ya Muungano (Articles of Union), ni kauli ya kuikana Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kwa hiyo ni kauli ya kutaka kudhoofisha Muungano na hatimaye kuuvunja.
Muungano wa Tanzania ni Muungano wa nchi mbili yaani Tanganyika na Zanzibar. Kuwepo kwa Muungano wa namna hii kunategemea sana nchi zote mbili kubaki kikamilifu ndani ya Muungano.
Nchi moja ikitoka, basi Muungano husambaratika mara moja Kwa maana hiyo basi, iwapo Zanzibar inadai kuwa yenyewe ni nchi kamili, basi Muungano haupo kwa sababu makubaliano ya Muungano hayakutoa nafasi ya Zanzibar kuwa taifa kamili ndani ya Muungano.
Wala Tanzania Bara haiwezi kuwa peke yake ndiyo Jamhuri ya Muungano kwa kujivika jaketi la Muungano. Kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha makubaliano ya Muungano na kinyume cha Katiba inayosema Tanzania ni pamoja na Tanzania Bara na Zanzibar.
Hakuna Rais wa Zanzibar?
Ukisoma makubaliano ya Muungano (Articles of Union) hakuna ibara inayozungumzia juu ya Rais wa Zanzibar, Kulingana na makubaliano hayo hakuna Ofisi ya Rais wa Zanzibar bali Ofisi za Makamu wawili wa Rais. Moja wa Makamu hao wa Rais ambaye kwa kawaida atakuwa mtu mkazi wa Zanzibar, atakuwa ndiye Kiongozi msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa masuala yanayohusu Zanzibar.
Kwa hiyo kuwepo kwa Ofisi ya Rais wa Zanzibar kama inavyofahamika sasa ni moja kati ya mambo mengi yaliyopenyezwa ndani ya mfumo wa Muungano nje ya makubaliano ya Muungano ya 1964.
Moja ya matatizo makubwa yaliyoufikisha Muungano kwenye mgogoro wa sasa ni muundo wa Serikali mbili. Serikali mbili katika Muungano wa nchi mbili una matatizo.
Hivi sasa Serikali ya Muungano ndiyo hiyo hiyo Serikali ya Tanzania Bara wakati Serikali ya Mapinduzi ni kwa ajili ya Zanzibar tu.
Katika kuendesha Serikali hizi kumezuka hisia kwa Wazanzibari kuwa Serikali ya Muungano ni Serikali ya Tanzania Bara. Kwa mtazamo huo, kila utakapoongeza uwezo zaidi kwa Serikali ya Muungano maana yake unaongeza uwezo Tanzania Bara dhidi ya Serikali ya Zanzibar, na Wazanzibari watakataa.
Unaporuhusu Serikali ya Zanzibar iwe na uwezo zaidi katika masuala ambayo Watanzania Bara wanayaona kuwa ni ya Muungano, maana yake unadhoofisha Muungano.
Serikali ya Muungano inapokuwa hiyo hiyo ndiyo Serikali ya Bara inashindwa kuchukua hatua za kinidhamu Zanzibar inapokiuka makubaliano ya Muungano kwa kuogopa itaonekana inaionea Zanzibar kwa kuwa ni nchi ndogo kwa kila hali ukilinganisha na Tanzania Bara. Pia itatafsiriwa kuwa Tanganyika inataka kuimeza Zanzibar.
Hali kadhalika Zanzibar hushindwa kuchukua hatua yoyote Serikali ya Muungano inapokwenda kinyume cha makubaliano ya Muungano kwa vile serikali ile ni ya Muungano. Lakini pia Zanzibar yaweza isichukue hatua yoyote kwa vile haileweki kama kitendo cha Serikali ya Muungano kimefanywa kama Serikali ya Muungano au kama Serikali ya Bara.
Kibaya zaidi ni hisia zilizojengeka sasa kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar ni sawa, hakuna iliyo na kauli juu ya mwenziwe katika jambo lolote. Kwa hiyo mambo inayofanya Serikali ya Muungano huonekana kuwa yanahusu Bara na Zanzibar haijishughulishi nayo.
Madai ya Serikali Tatu
Hivi sasa watu wengi Zanzibar na Bara wanadai Serikali tatu ili mambo ya Muungano yajulikane waziwazi na mambo yasiyo ya Muungano yajulikane pande zote mbili za Muungano. Wasioafiki hoja ya Serikali tatu wametoa sababu tatu:-
  • Kwa vile hakuna muundo usiokuwa na matatizo, basi tuendelee na muundo huu ingawa una matatizo mengi. Wenye hoja hii wanasahau kuwa ingawa muundo wowote ule haukosi matatizo, aina moja ya Muungano yaweza kuwa na matatizo makubwa zaidi. Huu ni muundo ambao hauruhusu hata nchi nyingine kujiunga bila ya muundo wenyewe kubadilika.
  • Muundo wa shirikisho yaani Serikali tatu utaifanya Serikali ya Muungano kutokuwa na nguvu na waweza kusababisha Muungano kuvunjika. Hapa swali la kujiuliza ni kwamba serikali kutokuwa na nguvu kwa upande gani? Kwa hali ilivyo sasa, Serikali ya Muungano ina nguvu Bara lakini Zanzibar haina nguvu kabisa. Afadhali Serikali ya Shirikisho kwa mambo ya Muungano itakuwa na nguvu pande zote ukilinganisha na hali ya sasa ya muundo wa Serikali mbili.
  • Kwa vile Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume walikubaliana kuwa na serikali mbili, basi hakuna sababu ya kubadilisha sasa. Sababu hii haina maana yoyote bali ni ubabaishaji tu na hakuna haja ya kuzungumzia zaidi. Mimi nakubaliana na Muungano wa Serikali tatu ambao ulipendekezwa na Tume ya Nyalali. Muundo huu unaleta usawa na haki kwa pande zote mbili za Muungano. Kudumu kwa Muungano wowote ule hakutegemei muundo wake bali hutegemea nia thabiti ya kisiasa ya kutaka Muungano uendelee. Kama nia haipo bila ya kujali muundo wake, Muungano husambaratika.
Nia ikiwepo nchi shiriki huheshimu makubaliano ya Muungano. Je, makubaliano yetu ya Muungano yanaheshimiwa? Nadhani wakati umefika kwa makubaliano yetu ya Muungano kuangaliwa upya.
Suala la kuhusu uwezo wa Bunge na Serikali ya Muungano juu ya Zanzibar, ibara ya nne ya makubaliano ya Muungano inayataja mambo yafuatayo kuwa chini ya mamlaka ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; Mambo ya Nchi za Nje, Ulinzi, Polisi, Madaraka ya kutangaza hali ya hatari, Uraia, Uhamiaji, Biashara ya Nje na Mikopo, Utumishi katika Serikali ya Muungano, Kodi ya Mapato, Kodi ya Mashirika; Ushuru wa Forodha na Kodi ya Mauzo; Bandari; Mambo ya Usafiri wa Anga; Posta na Telegraphs.
Katika mambo haya makubaliano yanatoa madaraka yote (exclusive authority) kwa Bunge na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa nchi nzima. Ni kutokana na ukweli huu nashindwa kukubaliana na wale wanaosema Bunge halina madaraka kuhoji suala la Zanzibar kujiunga na OIC.
Kadhalika nashindwa kuelewa baadhi ya viongozi wetu wanaposema Katiba ina utata na haikuwa wazi katika kuonyesha yapi ni mambo ya Muungano na yapi ni mambo ya ndani ya Zanzibar. Ninaloliona hapa ni kushindwa kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano na yapi ni mambo ya ndani ya Zanzibar. Ninaloliona hapa ni kushindwa kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano kutekeleza Makubaliano ya Muungano ya 1964, basi.
Pia sikubaliani na hoja kwamba kujiunga na OIC si suala la Muungano. Suala hili linagusa Katiba na mambo ya Nchi za Nje ambayo yametajwa na makubaliano ya Muungano kuwa ni mambo ya Muungano. Kwa hiyo iwapo tafsiri ya Zanzibar kwamba mambo haya si ya Muungano itakubaliwa na Serikali ya Muungano, basi hakuna mambo ya Muungano na ndiyo kusema hakuna Muungano!
Ningependa pia kuzungumzia suala jingine ambalo linajitokeza katika makala ambazo amekuwa akizitoa Alhaji Aboud Jumbe aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Katika makala hizo Alhaji Jumbe amelalamikia vitendo kadhaa ambavyo anadai vilitendwa na Serikali iliyoongozwa na Mwalimu Julius Nyerere lakini vilikuwa kinyume na msimamo na maadili ya taifa hili.
Malalamiko ya Jumbe yanachukua sura ya mtu ambaye yeye mwenyewe hakuwepo ndani ya Serikali hiyo. Lakini kama Watanzania wote wanavyojua ni kwamba Alhaj Jumbe alikuwa kiongozi wa ngazi ya juu katika taifa hili tangu Muungano mwaka 1964. Ameshika nyadhifa mbalimbali za juu katika Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kipindi cha miaka 20.
Yeye alishiriki
Leo kwangu mimi linakuwa ni jambo la kushangaza ninapoona Jumbe amekaa kando analaumu vitendo vya Serikali ambavyo yeye mwenyewe alishiriki kwa namna moja au nyingine! Ni vigumu kuamini kuwa Jumbe hakuhusika na uandaaji na utekelezaji wa sera mbalimbali wakati wa Serikali ya Mwalimu Nyerere.
Katika kuzungumzia suala hili, si madhumuni yangu kumshambulia Alhaji Jumbe bali ni kutaka kuonyesha mambo mawili ambayo yamejitokeza katika makala zake. Kwanza ni maamuzi ya pamoja ambayo Serikali yetu imekuwa ikisisitiza kuwa ndiyo msingi unaofuatwa katika kufikia maamuzi muhimu ya kitaifa. Maamuzi ya pamoja mara nyingi hufikiwa kwenye vikao ambavyo Mheshimiwa Jumbe alikuwa ni mshiriki kwa miaka ishirini.
Maamuzi mengi kiserikali hupitia kwenye Baraza la Mawaziri ambako Mheshimiwa Jumbe kwa wadhifa wake kama Makamu wa Kwanza wa Rais, alikuwa anapata nafasi ya kuwa Mwenyekiti wakati Rais hayupo. Ni dhahiri Mheshimiwa Jumbe alikuwa na nafasi nzuri ya kuzuia vitendo vya serikali vilivyoonekana kuwa havifai. Kwa mantiki hii kama kuna vitendo vyovyote vya kulaumiwa katika Serikali iliyopita, basi Jumbe hawezi kuzikwepa lawama hizo.
Pili, inawezekana kweli kwamba mambo yaliyokuwa yanafanywa na Serikali iliyopita Jumbe au kiongozi mwingine yeyote hakuwa na uwezo wa kuzuia au kubadili mwelekeo. Hapo napo inabidi tujiulize kwa nini? Moja ni kwamba Mheshimiwa Jumbe alishindwa kutumia vema madaraka aliyopewa na hivyo kuacha sera mbovu ziendelee kutekelezwa ingawa yeye mwenyewe alikuwa haziafiki. Kama hivyo ndivyo ni kosa la nani?
La msingi ni pale ambapo kiongozi kama Mheshimiwa Jumbe anashindwa kufanya lolote kwa sababu Rais wa nchi ana madaraka makubwa yanayomruhusu kufanya lolote bila kuulizwa na mtu yoyote. Na hili nadhani ndilo tatizo lililokuwepo (na bado lipo) wakati Alhaji Jumbe alipokuwepo madarakani.
Wakati viongozi walikuwa wanahubiri uongozi wa pamoja, viongozi hao hao kwa kupitia chama kinachotawala na Bunge waliendelea kurundika madaraka makubwa kwa Rais wa nchi kiasi kwamba hatimaye vyombo vingine vyote vilibaki bila madaraka kabisa.
Katika mazingira ya namna hiyo ingawa maamuzi mbalimbali huwa ni ya vikao, hali halisi ni kwamba maamuzi yote hufanywa na mtu mmoja. Kiongozi wa namna hiyo baadaye huacha hata kuwasikiliza viongozi wenzake na wao wasiwe na la kufanya kwa kuwa madaraka yote yako mikononi mwake.
Kiongozi mwenye madaraka makubwa hivyo aweza kuliyumbisha taifa bila ya kujijua. Matakwa yake binafsi huchukuliwa kuwa ndiyo matakwa ya taifa. Akimchukia mtu yeyote, basi taifa zima humchukia mtu huyo! Msimamo wake juu ya suala fulani basi huo ndiyo utakaokuwa msimamo wa taifa.
Kwa kifupi ni kwamba kila atakaloamua kulifanya kiongozi wa nchi litafanyika hata kama halifai. Viongozi wenzie ambao ndio waliompa madaraka hayo makubwa, hunung’unikia pembeni lakini hadharani wanamuunga mkono katika kila jambo analolifanya.
Inawezekana Alhaji Jumbe alijikuta katika mazingira ya namna hiyo. Kama kuna mambo ambayo yalikuwa yanafanyika ndani ya Serikali na yeye binafsi alikuwa hapendi, alishindwa kuzuia kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa amepewa kiongozi wa Serikali, yaani Rais.
Wakati huo huenda Alhaji Jumbe hakuweza kutoa malalamiko yake hadharani kwa kuogopa. Lakini leo kwa kuwa hakuna la kuogopa, anatoa malalamiko yake hadharani na kulaumu!
Nimezungumzia suala la Mheshimiwa Jumbe kwa kirefu ili kuonyesha hatari iliyopo kwa taifa kukabidhi madaraka yote kwa mtu mmoja na kuviacha vyombo vingine (Bunge, Mahakama, Halmashauri Kuu ya Taifa) kutokuwa na madaraka.
Rais siyo taifa…
Madaraka yanapaswa kusambazwa kwa madhumuni ya kuleta uwiano wa madaraka na uwezo, kwa taasisi mbalimbali ili kutotoa mwanya wa vishawishi kwa Rais kutawala kwa kadiri anavyopenda. Utaratibu huu huviwezesha vyombo vingine kumzuia Rais kufanya jambo ambalo ni kinyume cha Katiba au hata maadili tu ya taifa yaliyojengeka kwa muda mrefu.
Taifa lazima liwe na uwezo wa kumzuia kiongozi wa nchi siyo tu anapofanya mambo kinyume cha Katiba, bali hata anapotumia uwezo wa Ofisi yake vibaya. Uwezo kama huo unapotolewa kwa taasisi za taifa isitafsiriwe kuwa una lengo la kumwandama kiongozi fulani, bali yote yanafanywa kwa manufaa ya taifa hili la leo, kesho na kesho kutwa.
Jambo jingine ambalo Watanzania wanapaswa kulizingatia ni kutofautisha kati ya taifa na Rais. Rais si taifa lakini taifa si Rais. Tofauti hii ni muhimu kwani ndiyo itakayowezesha Watanzania kujua ni wakati gani vitendo vya Rais havilingani na maadili na matakwa ya taifa. Ni kwa mtazamo huo Wamarekani walikataa vita ya Vietnam ambayo waliiona haina umuhimu wowote kwao.
Kutenganisha kati ya Rais na taifa ni muhimu pia katika kuamua kama kiongozi aliyepo aendelee au hapana uchaguzi unapofika. Vigezo muhimu ni kama vile kutekeleza matakwa ya taifa na si yale anayotaka yeye, mwenendo na tabia zake kuendana na maadili ya taifa na kama Katiba inaheshimiwa.
Kimsingi yaliyomo kwenye Katiba ndiyo matakwa na msimamo wa watu na kwa hali hiyo si suala la kiongozi wan chi kuamka na kusema “Nimefanya hivi kwa kuwa Katiba ina kasoro, tutasahihisha baadaye.”
Mwenendo kama huu haukubaliki. Kila kitendo anachotenda kiongozi wa nchi lazima Katiba iwe inaruhusu. Pale ambapo Katiba hairuhusu lakini ni lazima hatua zichukuliwe, basi hurekebishwa kwanza ili kumpa uwezo halali kiongozi wan chi kutekeleza wajibu wake ipasavyo, mambo ya dharura ni suala jingine.
Uchaguzi unapofika kiongozi wa nchi huchaguliwa tena au kutochaguliwa kulingana na alivyotekeleza majukumu yake kipindi kilichopita. Kiongozi wa nchi aliyeshindwa kutekeleza matakwa ya wananchi na taifa huangushwa. Madhumuni ya kufanya hivyo ni kutaka kumpata kiongozi anayeweza kuliongoza taifa vizuri, kwa mafanikio na bila ya kukiuka Katiba.
Kadhalika, wananchi humchagua kiongozi mpya ili aweze kusahihisha na kurekebisha makosa aliyofanya kiongoziu aliyetangulia. Wananchi hawachagui kiongozi mpya wa nchi ili kuendeleza makosa aliyofanya kiongozi aliyetangulia.
Mwanzo potofu
Kwa mantiki hii sikubaliani na mawazo ya Alhaji Jumbe. Katika makala zake kwa gazeti hili hivi karibuni Alhaji Jumbe alidai kuwa Mwalimu Julius Nyerere alichanganya siasa na dini kwa kuwapendelea Wakristo. Kwa hiyo, na Rais Ali Hassan Mwinyi afanye hivyo hivyo kwa kuwapendelea Waislamu! Mawazo haya ni potofu.
Msimamo wa taifa letu tangu uhuru ni kutochanganya siasa na dini, na Katiba yetu inasema hivyo. Kama kuna ushahidi kuwa Nyerere alichanganya siasa na dini wakati wa utawala wake, hilo ni kosa. Alichofanya ni kinyume cha Katiba na kinyume cha maadili ya taifa.
Tunachokitazamia kutoka kwa utawala wa sasa si kurudia makosa bali kuyasahihisha na kulirudisha taifa kwenye msimamo wake. Kosa ni kosa hata lingetendwa na nani.
Kuna mifano katika nchi kadhaa. Serikali mpya inashika madaraka na ikigundua kuwa viongozi waliopita waliendesha Serikali yao bila kufuata Katiba au walitumia madaraka vibaya, huwa wanakamatwa na kufikishwa mahakamani. Wanapopatikana na makosa huadhibiwa. Itakuwaje basi Serikali ya sasa ya Tanzania badala ya kurekebisha makosa yaliyotendwa na Serikali iliyopita (kama yapo) ijitumbukize katika makosa ya aina ile ile?
Ningependa kumaliza kwa kuwaomba Watanzania wote na hasa viongozi kujiepusha na kauli au vitendo vinavyoweza kusababisha uhasama na vurugu kati ya jamii moja na nyingine ya kitanzania.
Lakini si rahisi kurudisha amani na utulivu kati ya jamii hizo bila ya gharama kubwa kwa maisha ya watu na mali zao.
Na baya zaidi ni kwamba upendo na kuaminiana ambavyo vimejengeka baina ya jamii mbalimbali za Watanzania vinaweza visipatikane tena hata baada ya karne moja kupita. Mifano ya namna hiyo imezagaa ndani na nje ya Afrika, hatuhitaji kuambiwa
Chanzo: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment