Thursday 17 May 2012

Hatuwezi kuijadili Tanzania bila kuujadili Muungano

Na generali Ulimwengu
KATIKA muktadha wa mjadala kuhusu kuandika katiba mpya, nimekuwa nikisema kwamba yapo masuala ya kikatiba ya aina mbili: aina ya kwanza ni yale ambayo, hata kama yanaumua hisia kali miongoni mwa wanasiasa, bado yanaweza kupata ufumbuzi wake ndani ya muda mfupi.
Aina ya pili ni ile ya masuala ambayo, hata kama hayaibui hisia kali miongoni mwa wanasiasa na watawala, lakini yana umuhimu mkubwa, ufumbuzi wake hauwezi kupatikana kirahisi au katika muda mfupi.
Aina ya kwanza, kama naruhusiwa kukariri yale niliyokwisha kuyasema, ni ile inayohusu matatizo ya kiutawala na yanayogusa mgawanyo wa madaraka katika ngazi mbalimbali za utawala.
Kuna mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mitatu ya dola (Utawala, Bunge na Mahakama); ukomo wa madaraka ya ofisi za watawala; ukomo wa madaraka ya Bunge; ukomo wa mamlaka ya Mahakama; maingiliano kati ya mihimili hiyo, na kadhalika.
Katika kuyaandikia vipengele vya kikatiba, masuala ya aina hii yatapatiwa majibu kwa kufuata utashi wa kisiasa wa wale walio madarakani pamoja na raia wenzao wenye ujuzi wa mambo na ari ya kuchangia katika maendeleo ya taifa lao.
Mara nyingi maoni yao yatatokana na ujuzi wa kitaaluma katika nyanja za siasa, sheria na historia, na jinsi wanavyoiangalia jamii wanamoishi na mahitaji yake ya wakati huo.
Wajuzi hawa watadurusu mifumo mingi duniani na katika historia, ili kuona kama wanaweza kujifunza namna wenzao walivyoshughulikia hoja zilizo mbele yao. Katika nchi nyingi za Jumuia ya Madola (Commonwealth), mara nyingi wataalamu watajikita zaidi katika historia ya kikatiba ya Uingereza na mfumo unaoitwa wa ‘kibunge”. Lakini wakati mwingine wataenda nje ya mfumo huo na kufanya majaribio ya kuchanganya dhana za mfumo wa kibunge na mfumo unaoitwa wa ‘kirais.’
Ndivyo tulivyofanya sisi kwa kuchanganya dhana hizo mbili, na ndiyo maana tumejenga ofisi zenye utata, kama ile ya ‘waziri mkuu’ asiyekuwa waziri mkuu kwa maana ya mfumo wa ‘kibunge.’
Wanaofuatilia masuala haya watajua kwamba waziri mkuu wa Uingereza ni kiongozi wa wabunge wa chama chake na serikali yake, lakini si bosi wa mawaziri wake. Anaitwa ‘primus inter pares’ (first among equals, ama kiongozi wa walio sawa).
Hata hivyo, inapobidi waziri mkuu achukue uamuzi au abebe lawama, yeye ndiye mkuu wa kufanya hivyo. Hawezi kumwachia malikia majukumu hayo.
Tutaona kwamba hiyo ni tofauti kabisa na jinsi tunavyoendesha mambo yetu kikatiba nchini, na mifano ya hivi karibuni imedhihirisha, kwa mara nyingine tena, utata wa ofisi ya waziri mkuu na mambo mengine yanayotokana na kuchanganya dhana hizi mbili.
Hata hivyo, mimi naamini kwamba haya ni mambo yanayowezwa kurekebishwa iwapo kuna utashi wa kisiasa na uangavu wa mawazo, na utambuzi wa uzoefu wetu kihistoria utakaotuwezesha kuona ni wapi tulipata usumbufu wa kimuundo na ni vipi tunaweza kurekebisha.
Haya ni masuala ya kimpangilio ambayo hayahitaji muda mrefu mno wala tafakuri ya kuchosha kuyapatia ufumbuzi. Utashi wa kisiasa na umahiri wa wajuzi wa mambo vinatosha kuyaangalia, kuyajadili na kuyaweka bayana, kuonyesha njia kadhaa zinazoweza kufuatwa, na hatimaye kuchagua njia mwafaka kwa wote, au kwa walio wengi kwa wakati tulio nao.
Tunaweza kuteua utaratibu wa ‘kibunge’ au ule wa ‘kirais,’ au tunaweza kuteua kuendelea na mseto wetu wa hivi sasa, pamoja na utata wake.
Wakati tukifanya hivyo, tunaweza pia kuamua mambo kama vile mawaziri kutokuwa wabunge; madaraka ya rais kupunguzwa na kukabidhiwa kwa asasi mahsusi; matokeo ya kura za rais kupingwa ndani ya kipindi kilichopangwa, na mambo kama hayo. Haya yote, na mengine kama haya, tunayamudu katika kipindi cha miezi 18.
Sasa tuangalie masuala ambayo ni mazito , nyeti na tata, ambayo yanahitaji tafakuri ya muda mrefu na ambayo hayatatuliki kwa watawala kuwa na utashi wa kuyatatua ama kwa wajuzi wa mambo kuwa na weledi na umahiri uliojipambanua.
Haya ni yala masuala ambayo yanahitaji maridhiano ndani ya jamii ambazo zinaweza kuwa na maslahi yanayokinzana, na wakati mwingine maslahi hayo yakiwa yamejenga uhasama ndani ya jamii hizo, hususan kwa sababu bado jamii hizo hazijapata, au hazijajitengenezea, wasaa wa kuyajadili kwa kina masuala muhimu.
Sina budi kuanza na suala la Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, ambayo ndiyo Tanzania. Juhudi yo yote inayolenga kuwaambia wananchi kwamba wanaweza kuandika katiba mpya kujadili masuala yote yanayohusu nchi yao bila ya kujadili kwa kina sula la Muungano ni kazi bure.
Maana ya juhudi kama hizo ni sawa na kuwaambia watu wajadili kila kitu kadri wanavyotaka lakini wasiijadili Tanzania yenyewe, jambo ambalo halieleweki.
Katiba haina budi kusimama juu ya misingi ya aina ya Tanzania tunayotaka kuijenga, na hiyo ni pamoja na kile kinachoifanya Tanzania kuwa Tanzania, na hicho ni Muungano. Sasa inawezekana vipi kuijadili Tanzania kwa kutoijadili Tanzania?
Sote tunaelewa kwamba yapo maoni yanayopishana mno kuhusu Muungano kama muungano, na pia muungano kwa maana ya mifumo yake na michakato yake. Ni kusema kwamba wapo watu wanaoamini kwamba Mungano, pamoja na kwamba una matatizo kadhaa, ni jambo jema na ambalo linafaa kuendelezwa huku matatizo yake yakirekebishwa ili kukidhi maslahi ya wana-Muungano wote.
Wapo wanaoamini kwamba Muungano hauna haja ya kuendelea kuwapo kwa sababu mbalimbali. Wengine wanazitaja sababu hizo, na wengine hawautaki kwa sababu tu hawautaki.
Kisha wapo watu ambao wanauona Muungano kama kitu kilichopo na ambacho wamekizoea, lakini hawajui kama una manufaa au hauna manufaa, na wala hawaoni ni kwa nini watu wanasumbua akili zao juu ya jambo kama hilo.
Baina ya misimamo hii, naamini kwamba kila mmoja una mantiki yake, na si busara kuenenda kama vile upande mmoja lazima umebebwa na mantiki nzito zaidi kuliko mwingine. Busara inasema tuujadili Muungano, na tuujadili katika marefu na mapana yake na pia kina chake katika kila eneo.
Itakuwa hasara kubwa iwapo tutaingia katika zoezi la kuandika katiba mpya (kama kweli tumedhamiria kuandika katiba mpya, na si kugongagonga iliyopo) bila kujadili kwa kina asasi hii muhimu kuliko zote.
Kitakuwa ni kichekesho cha gharama kubwa iwapo tutajidai tumeandika katiba mpya halafu baada ya miaka miwili au mitatu tuanze kuunda tume, mara “Tume ya Bakari”, mara “Tume ya Yohana” eti “kuangalia kasoro za Muungano na kupendekeza marekebisho ya kuuboresha.”
Tume hizi tumeziona, mapendekezo yake tumeyasoma, lakini hakuna kilichobadilika kimsingi kwa sababu kila mara juhudi zilizofanyika zimekuwa ni za kupoza jazba, kutuliza hisia, “kufunika kombe”, kama wasemavyo Waswahili, ili “mwanaharamu apite”.
Kama kawaida yetu, tumekataa kufanya kazi ya kina, kazi ya kudumu, kazi ya mtazamo wa masafa marefu. Tuna haraka kama vile tuko katika mpito tukielekea kwingine, sijui wapi?
Hakuna sababu ya kukumbushana kwamba huu ni muungano wa nchi mbili zilizokuwa huru kabla ya kuungana. Ingawaje ni kweli kwamba walio wengi katika nchi yetu wamezaliwa chini ya Muungano, bado ni kweli pia kwamba hisia za u-Tanganyika na u-Zanzibari hazijatoweka moja kwa moja.
Zimekuwa zikichomoza mara kwa mara, na kila mara zikizimwa kwa njia ambazo hazikushughulikia masuala ya msingi yaliyojitokeza wakati huo. Tusipoujadili Muungano kwa kina, upana na urefu, kwikwi hizi zitaendelea kujitokeza kama kielelezo cha matatizo yanayofunikwa funikwa kila mara.
Chanzo: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment