Sunday 3 March 2013

Tukiri Muungano Unazidi Kudhoofika

KWA muda mrefu sasa watu wengi wa Zanzibar wamekuwa wakilalamika kimya kimya kwamba pamekuwa pakifanyika kile wanachokiona kama mizengwe ya kuwalazimisha kukubali kuongozwa na watu ambao ndugu zao wa Tanzania Bara wanawaona wanaofaa kushika hatamu za uongozi visiwani.
Tafsiri iliyokuwa inapatikana miongoni mwa watu hawa ni kuwa watu wa visiwani hawajui kutenganisha kizuri na kibaya, kile chenye manufaa na maslahi na wao na kile ambacho hakina faida kwao na nchi.
Kwa kiwango kikubwa unaweza kusema watu hawa wamekuwa wanahisi wanaonekana kuwa hawajui tofauti iliyopo ya mbichi na mbivu.
Kwahivyo, njia nzuri ya kuwasaidia ni kuwafanyia uamuzi badala ya wao wenyewe kujiamulia wanataka nini.
Kwa bahati mbaya sana, wale ambao wamekuwa wakilalamikia mwenendo huu, wamekuwa wakipachikwa kila aina ya majina ambayo ni ya kejeli na kumfanya mtu aonekane si mzalendo na hata kupachikwa majina kama vile; “Huyo sio mwenzetu’, ‘Ametumwa’, ‘Hana nia njema’, ‘Anakwenda kinyume na utaratibu tuliojiwekea’ na kadhalika.
Lakini hivi sasa hali inaonekana kubadika, kwani hata baadhi ya wale walioweka chama chao cha siasa mbele kuliko nchi na kudharau uamuzi wa wengi, wameanza kuamka kutoka katika usingizi mzito waliokuwa nao.
Usingizi huu ulijengwa na utamaduni wa kuitikia ‘hewalla bwana’ au ‘hewalla bibi’ na kupiga makofi, hata pakiwa hapana sababu ya kufanya hivyo.
Yote haya yametokana na kutokuwa na ubavu wa kutamka “hapana” au kutoa maoni ya kupinga baadhi ya mwenendo unaotumika katika chama chao kwa kisingizio cha kile walichokuwa wanakiita “jeuri ya chama”. Sijui jeuri hii ni ya maana au vinginevyo.
Lakini sasa wingu la kiza linaonekana kutoweka na mwanga umeanza kuonekana.
Hivi karibuni pameanza kusikika sauti za baadhi ya hao wanaotaka mambo ya chama chao yasiingiliwe, wakielezea hadharani kutaka mabadiliko ili watu wa Zanzibar waachiwe kuchagua wale wanaowaona wao ndio wanaofaa kuwaongoza.
Miongoni mwa sauti zilizosikika zikitaka mabadiliko ya kutaka Zanzibar kuachiwa mamlaka ya kumchagua mgombea urais wa CCM wa visiwa vya Unguja na Pemba, badala ya utaratibu wa sasa unaoshirikisha wenzao wa Tanzania Bara ni ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Vuai anasema suala hilo linajadiliwa, na kwamba ana matumaini kuwa litapatiwa ufumbuzi muafaka.
Anasema ndani ya CCM upo utaratibu ambao chama hicho umejiwekea wa kupata viongozi, lakini suala la kuchaguliwa mgombea urais wa Zanzibar kutoka kwenye vikao vya Dodoma linawagusa, na sasa wapo kwenye mchakato wa kulijadili ili upatikane ufumbuzi.
Hakuelezea mchakato huo umefikia wapi. Hata hivyo, Vuai alikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa hata suala la kupokezana urais kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano na jinsi ya kupata viongozi wengine kama wabunge na wawakilishi, linajadiliwa ndani ya CCM (hakueleza wapi) kwa kina.
Ama kweli zama zimebadilika kwa sababu kwa muda mrefu yeyote yule aliyeweza kujitokeza hadharani kutoa kauli kama hiyo, angelisakamwa na viongozi wenzake wa CCM na angelielezwa kuwa “sio mwenzetu” na “amekwenda kinyume na utaratibu tuliojiwekea”.
Hapa tunachojifunza ni kwamba, kero (au malalamiko) juu ya Muungano hayapo tu katika mfumo na uendeshaji wa shughuli za Serikali ya Muungano, bali hata ndani ya chama tawala cha CCM.
Kutokana na hali hii, tunajifunza kwamba upo umuhimu mkubwa kwa mfumo wa Muungano ukaangaliwa upya na kwa upana na urefu kwa sababu kila kukicha malalamiko yanazidi na kuyafumbia macho sio suluhu.
Ukweli ni kwamba kuyafumbia macho kunaudhoofisha Muungano ijapokuwa tunajaribu kujidanganya kwamba kila siku zikienda mbele unazidi kuimarika, badala ya kukiri kwamba unadhoofika.
Hivi sasa mchakato wa kupata katiba mpya umepamba moto nchini kwetu, na kwa upande wa Zanzibar
suala lililochukua nafasi kubwa ya mjadala na watu wengi hata kuonekana kutojali mengine yote yanayohusu katiba ni hili la Muungano.
Mmoja wa wajumbe wa tume anakiri kwamba Wazanzibari wanatofautiana kwa mengi kisiasa, lakini linapokuja suala la Muungano sauti yao ni moja na unakuwa hujui ni nani CCM , CUF au chama kingine.
Kwa bahati mbaya wapo watu waliotaka Watanzania wanapojadili na kutoa maoni juu ya katiba mpya wasiuguse Muungano kama vile suala hilo limejaa utukufu kama maneno yaliyokuwemo kwenye Kuran au Biblia, na kwahivyo halipaswi kuguswa kwa lengo la kufanya mabadiliko yoyote.
Huu sio mwendo sahihi, na kulipuuza suala la Muungano katika kutenegeneza katiba mpya hakutawasaidia Watanzania waliopo Bara wala Visiwani.
Tunawajibika kuwa wakweli na kuukubali ukweli kwa maslahi yetu binafsi na nchi yetu, hata huo ukweli ukiwa na ladha ya uchungu au maumivu.
Suala la Muungano kwa watu wengi wa Zanzibar, sasa linaonesha kuwa hata ndani ya nyoyo za makada na viongozi wa juu wa CCM, lina matatizo yanayohitaji kushughulikiwa kitaifa na sio kichama.
Kama CCM wanahisi chama chao kinayo haki ya kuendelea kuwachagulia wagombea wa uchaguzi Dodoma, hilo ni suala la wanachama wenyewe kuamua, na wanaweza kuendelea kufanya hivyo kama katiba yao inawaruhusu.
Lakini ni vema ieleweke wazi kwamba hao wanaochaguliwa na baadaye kuitumikia Zanzibar, huwa watumishi wa umma sio wa CCM peke yake.
Suala la kuwepo zamu ya urais kati ya Bara na Visiwani (hizi ni nchi mbili zilizoungana kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) nalo lisipuuzwe kwa kisingizio cha kwamba Zanzibar ni ndogo kama baadhi ya watu Bara, wakiwemo wabunge walivyojaribu kueleza katika kutaka malalamiko ya watu wa Visiwani yasitiliwe maanani.
Hili ni suala nyeti, na ni lazima hekima na busara itumike na ukweli wa kwamba Zanzibar na Tanganyika ni washirika sawa katika Muungano ionekane kwa vitendo.
Sio vibaya, kama kiongozi wa awamu mbili au tatu akatoka upande mmoja wa Muungano, lakini hii ifanyike kwa ridhaa, na pande zote mbili za Muungano kuwa hazina kinyongo.
Katika miaka ya nyuma mwenendo huu wa uamuzi wa watu wa Zanzibar kuwekwa pembeni na yale ya Dodoma kutawala umezusha hisia mbaya Visiwani.
Wapo watu ambao hadi leo wanahisi wenzao wa Bara hawawatendei haki na kwamba Muungano wa vyama vya ASP na TANU na kuunda CCM na wa serikali mbili (Zanzibar na Tanganyika) umekuwa ukisababisha watu wa Visiwani kuburuzwa na kulazimishwa mbichi kuiita mbivu.
Kwa upande mwingine wapo wanaofanya jeuri ya kuwaambia wenzao wa Visiwani kama hawatamchagua yeye hashituki kwa sababu atapigwa jeki na kura za watu kutoka Bara wanapokutana Dodoma.
Katika mchakato wa katiba mpya, sauti za Wazanzibari juu ya mfumo wa Muungano zimesikika na itakuwa vizuri kama Tume ya Jaji Warioba itaziheshimu na kutozibana katika majumuisho yake kabla ya kuandikwa katiba mpya.
Kinachotakiwa hapa ni nini wananchi wanataka na sio wanasiasa.
Vinginevyo malalamiko juu ya Muungano yataendelea kusikika kila upande na kuwalaumu hao wanaopiga kelele bila ya hoja za msingi.
Hatimaye kitachotokea ni kuzidi kuudhoofisha Muungano ambao Watanzania wengi wanautaka na kuuthamini, lakini wanaonekana kutofautiana juu ya mfumo wake na namna ambavyo baadhi ya shughuli za Serikali ya Muungano zinavyoendeshwa.
Si ajabu watu hao watakaotoa maoni tofauti wakaitwa “Uamsho” kwani huu ndiyo mwenendo wa siasa za hapa nchini.
Hali hii ya kupuuza sauti za wananchi ndiyo iliyosababisha kuonekana baadhi ya watu kuona Bara inaionea na kuisakama Zanzibar, hasa kiuchumi, na wapo wanaohisi na kuamini kuwa Zanzibar inadekezwa ndani ya Muungano, na kwa kweli inafaidika zaidi kuliko upande wa pili wa Muungano.
Yote haya yatakwisha kama dosari za Muungano zilizopo zitashughulikiwa vyema kwa manufaa ya watu wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment