Sunday 30 September 2012

Nahodha: Wanaobeza Muungano watimuliwe CCM

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Shamsi Vuai Nahodha amesema viongozi wanaokejeli na kubeza Muungano hawastahili kuendelea kubaki ndani ya chama tawala na serikali zake.
Nahodha alitamka hayo wakati akifungua mkutano wa uchaguzi wa viongozi wanaogombea nafasi mbalimbali ikiwemo ujumbe wa halmashuri Kuu ya Taifa ya CCM NEC wilaya Dimani mjini Unguja jana.
Alisema kimantiki viongozi wanaodiriki na kuthubutu kusimama hadharani bila aibu wakipinga Muungano uliopo amewafananisha na watu waliokosa utu na shukrani.
“Wanaopita na kusema Muungano haufai hata kufika kwao mahali walipo wakipata hadhi na heshima ni kutokana na nguvu za CCM na serikali zake,” alisema Nahodha.
Aliwafananisha watu hao na wasaliti wanaotoboa jahazi wanamosafiria huku wakiwa kwenye kina kikubwa cha bahari.
Nahodha ambaye ni Waziri Kiongozi mstaafu wa SMZ alisema yuko tayari kupoteza marafiki kwa na kubaki kuwa mtetezi na muumini wa Muunagno wa serikali mbili.
“Sitajutia kupoteza marafiki wanafiki katika mambo ya msingi yanayogusa umoja wa kitaifa, potelea mbali liwalo na liwe,” alisema Nahodha.
Akizungumza na kuufanya ukumbi kukaa kimya, Nahodha aliwataka viongozi wenye fikra mbadala kupitisha mawazo yao kwenye vikao vya kikatiba na wakishindwa watoke kama hawakubaliani na misimamo ya kisera ya chama hicho.
Alisema siri ya Muungano huo chini ya waasisi wake hayati Baba wa Taifa na Sheikh Abeid Karume ni dhahiri walizingatia na kuweka mbele maslahi ya umoja kwa kupinga utengano.
Akizungumzia umuhimu wa kuwachagua viongozi bora kwa miaka mingine mitano ijayo wanachama wenzake kuchagua wenye sifa za uadilifu, uaminifu na majasiri katika kutii sera za chama na kuheshimu katiba yao.
“Huu si wakati wa kuchagua viongozi kwa pupa na papara, chagueni kwa umakini, msichague viongozi mamluki wanaojibadili rangi zao kuliko kinyonga na kuhatarisha uhai wa chama chetu,” alisema Nahodha.
Kauli hiyo ya Nahodha imekuja huku baadhi ya makada na viongozi wa juu wa CCM Zanzibar wakipigania kuwepo kwa Muungano wa mkataba agenda ambayo pia inapigiwa upatu na Jumuiya ya kidini ya Uamsho visiwani humu.
Hata hiyo viongozi hao wamekumbana na upinzani mkali toka kwa waaasisi wa Mapindzi na Muungano ambao wanapinga vikali wazo la Muungano wa mkataba wakiamini mpango huo umebeba ajenda ya siri ya kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment