Monday 25 February 2013

TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR KULAANI MASHAMBULIZI NA MAUAJI YA VIONGOZI WA DINI PAMOJA NA KUPINGA KAULI ZA UCHOCHEZI DHIDI YA ZANZIBAR

Masheikh wa Jumuia na Taasisi za kiislamu Zanzibar, kutoka kushoto ni Sheikh farid, Sheikh Mselem na sheikh Azzan

TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR KULAANI MASHAMBULIZI NA MAUAJI YA VIONGOZI WA DINI PAMOJA NA KUPINGA KAULI ZA UCHOCHEZI DHIDI YA ZANZIBAR
Kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu Mlezi wa Viumbe. Sala na salamu zimfikie Mtume wetu Mtukufu Muhammad (S.A.W), jamaa zake, maswahaba zake waongofu na wote wanaowafuata kwa wema hadi Siku ya Malipo.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar lililokaa Jumapili tarehe 23/2/2013 katika kikao cha kutathmini matukio ya kushambuliwa na kuuliwa viongozi wa Dini yakiwemo ya karibuni ya kupigwa risasi na kuuliwa Padri Mushi pamoja na kupigwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje na kuendelea kutolewa kwa kauli za uchochezi dhidi ya Zanzibar linatamka ifuatavyo:
1. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani vikali na kwa nguvu zote matukio ya kushambuliwa na kuuliwa viongozi wa Dini likiwemo tukio la karibuni la kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi kulikofanywa na wahalifu wasioitakia mema Zanzibar.
2. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linapenda kuweka wazi kuwa uhai ni tunu kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyotunukiwa binaadamu hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuiondoa haki hiyo isipokuwa yeye mweyewe Mwenyezi Mungu. Kutokana na ukweli huu ndio maana Sheria za Kiislamu zimeweka wazi mtu mwenye kumuuwa mwenziwe naye auliwe kama inavyoelezwa katika Kitabu kitufu cha Quran kama ifuatavyo:
“Na humo (katika Taurati) tuliwaandikia ya kwamba mtu (huuwawa kwa sababu ya kuuwa mtu) kwa mtu, ……….” (5:44)
Hivyo, vitendo vya kiharamia vya kushambuliwa viongozi wa Dini kulikoanzia kwa kumwagiwa tindi kali Sheikh Soraga, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda, kuuliwa Padri huko Musoma, kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi na kushambuliwa kwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje kwa dhulma kulikofanywa na wahalifu ni jambo lisilokubalika na Uislamu na Waislamu wenyewe. Aidha wahusika wa matendo haya wawe wafuasi wa Dini yoyote ile bado watahesabika ni wahalifu kwani vitendo vya kihalifu na kiharamia kamwe haviwezi kunasibishwa na Dini fulani.
3. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaviomba vyombo husika kufanya upelelezi wa kina kuhusu matukio haya kwa kuzingatia uadilifu na misingi ya kazi zao ili kuwabaini wahalifu na kufikishwa katika vyombo vya kisheria. Aidha Baraza linavitahadharisha vyombo hivyo kuepuka kufanya kazi yao kwa kusukumwa na matashi binafsi, jazba, chuki, matashi ya baadhi ya wanasiasa na viongozi wa Dini pamoja na shindikizo la baadhi ya vyombo vya habari.
4. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani na kupinga kwa nguvu zake zote kauli aliyoitoa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania na baadhi ya vyombo vya habari kuihusisha Zanzibar na ugaidi kutokana na tukio la kuuliwa Padri Mushi. Kauli hii inaonesha kuwa Mheshimiwa Waziri anaibagua Zanzibar katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwasababu tunavyoelewa sisi suala la usalama wa nchi ni suala la Muungano hivyo huwezi kuihusisha Zanzibar pekee na suala la ugaidi. Hivyo, Baraza linaona kuwa kauli hizi zinazotolewa ni mbinu za makusudi za kuichafua Zanzibar katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na chuki binafsi dhidi ya Zanzibar na watu wake.
5. Aidha Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linamtaka Mheshimiwa Waziri kwa kulinda heshima yake kuwajibika kwa Watanzania kwa kujiuzulu kutokana na kushindwa kulinda usalama wa wananchi wakiwemo viongozi wa Dini ambao ndio walezi wa jamii.
6. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani kauli za uchochezi zinazoendelea kutolewa na baadhi ya vyombo vya habari zinazochochea chuki, uadui, hasama na mtafaruku kati ya Waislamu na Wakristo na kusahau kuwa Waislamu wameishi na Wakristo kwa amani, mapenzi na mashirikiano hapa Zanzibar karne na karne. Baraza linaona kuwa vyombo hivyo vya habari vinatekeleza ajenda ya kuivuruga Zanzibar kwa kuchochea vita vya kidini ili kufikia malengo yao wanayoyajua wenyewe. Hivyo, Baraza linaiomba Serikali kuvidhibiti kwa kuvichukulia hatua vyombo vyote vinavyotumia matukio haya kuchochea uadui na chuki kati ya Waislamu na Wakristo.
7. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaviomba vyombo vya habari vya Zanzibar kuwajibika kwa Wazanzibari wanaolipa kodi kwa kuwapasha taarifa sahihi juu ya matukio muhimu yanayotokea katika jamii yao badala ya wananchi kutegemea kupokea taarifa za upotoshaji na uchochezi kutoka katika vyombo vya habari visivyotutakia mema.
8. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaziomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kuwasilisha kwa Watanzania taarifa ya wazi ya matokeo ya uchunguzi wa matukio haya kwa kuanzia na lile la kumwagiwa tindi kali Sheikh Soraga, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda, kuuliwa Padri huko Musoma, kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi na kushambuliwa kwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje.
9. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linawaomba Wazanzibari wote kuwa watulivu katika kipindi hichi ambapo upelelezi wa matukio haya ukiendelea. Aidha Baraza linawasihi Wazanzibari wote bila ya kujali tofauti zao za kidini kulinda umoja wao na kudumisha amani pamoja na kukataa kugawanywa ili kuwatoa katika ajenda yao ya msingi ya kudai Mamlaka Kamili ya Zanzibar katika Muungano.
MOLA WETU MTUKUFU TUNAKUOMBA UINUSURU ZANZIBAR NA WATU WAKE DHIDI YA MAADUI WA NDANI NA NJE WASIOITAKIA MEMA NCHI YETU
Imesainiwa na:
Sheikh Ali Abdalla Shamte
Amir wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar

Saturday 23 February 2013

TUSIPOTUMIA AKILI ZETU VIZURI, WAZANZIBAR TUTAPIGANISHWA KAMA MAKUCHI

Matukio ya kusikitisha, kufedhehesha na yakushangza yamekuwa yakitokea Zanzibar tangu mwaka jana baada ya wazinzabar kuanzisha harakati za kurudisha Zanzibar yenye mamlaka kamili (Zanzibar huru), harakati zilizoanzia kwenye baraza la wawakilishi mwaka 2010, kwa kubadili katiba ya Zanzibar na kuitaja Zanzibar kuwa ni nchi kamili! Vugu vugu lililochagizwa zaidi na jumuia ya mihadhara na ya kiislam ( al maarufu kama UAMSHO)!
Vugu vugu hilo lilipelekea mvutano kati ya jeshi la polisi na wafuasi wa masheikh wanaoongoza jumuia ya UAMSHO. Chakushangaza mvutano au mapambano yalikuwa ni kati ya polisi na wafuasi wa UAMSHO, lakini tukaamka asubuhi nakusikia MAKANISA kadhaa yamechomwa moto! Eti waZanzibar hao (UAMSHO) ambao wamekuwa wakiishi kwa amani na upendo na wakristo kwa karne tele zilizopita, leo hii wameacha nyumba zote za askari wanaopigana nao, wanaCCM, viongozi wa SMZ, na masheha badala yake wameenda kuchoma moto makanisa! Hapa tukaambiwa uchunguzi utafanyika na wahusika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria….watu wakakamatwa kwa nzo, wakatafutwa kila mwenye ndevu akanyolewa, wakahilikishwa, na kwa kutumia technologia (kama alivyosema Kamishna Mussa), wakaangalia kanda za video kubaini walokuwepo kwenye vurugu zile na kuwakamata! Tukasubri majibu , tuambiwe ni nani hasa alochoma makanisa? Ikabaki kuwa “watu wasiojulikana” Jibu mpaka leo hakuna!
Tutakaa tena kidogo, tukasikia Sheikh Farid katekwa, jeshi la polisi likasema hajui alipo, itakuwa kajiteka! Vurugu zikazuka tena, makanisa yakachomwa tena, lakini mara hii wakaongeza na kuchoma maskani za CCM, na polisi mmoja akauliwa kwa kukatwa katwa kwa mapanga! Mkuu wa jeshi la polisi nchini Said Mwema, akasema ametuma makachero wenye ujuzi wa hali ya juu (walobobea) kutoka makao makuu Dar es salaam, kuja Zanzibar kuwatafuta wahusika wote walouwa na kuchoma makanisa ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria…tukasubiri na tunaendelea kusubiri, bila kupata majibu mpaka leo!
Hatujakaa vizuri, tukasikia Sheikh Soraga, kamwagiwa tindi kali usoni, na “mtu asiejulikana”! Kama kawaida tukaambiwa tena, jeshi la polisi linafanya uchunguzi kuwatia nguvuni wahusika….mpaka naandika habari hii hakuna jibu la nani alommwagia Sheikh Soraga tindi kali! Jeshi la polisi bado lafanya uchunguzi tu!
Tukiwa bado tunatafakari hayo, tunasikia tena Padri Ambrose kashambuliwa kwa risasi, na “watu wasiojulikana”! Lengo ilikuwa ni kumuuwa, lakini bahati nzuri yupo hai! Hili likaendelea kutushangaza wengi, eti mara hii wazanzibar wamekuwa wanamiliki silaha za moto, na ni wajuzi wakuzitumia?!! Hapa sasa tukasikia kauli kali zaidi, tena kutoka kwa viongozi wajuu zaidi kisiasa katika nchi yetu, akiwemo Rais wa Tanzania, Kanali, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa serkali ya Zanzibar Biochemist, Dr. Ali Shein, wakilaani nakuvitaka vyombo vyote vya jeshi la polisi, wakiwemo usalama wa taifa kufanya uchunguzi kwa weledi wajuu kabisa ili kubaini na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wahusika! Tukasubiri na tunaendelea kusubiri kuwajuwa wahusika, lakini mpaka sasa hakuna jibu!
Eeeh juzi tena tunasikia Pandri Mushi, ameuliwa kwa risasi na “watu wasojulikana”! Mauaji hayo yanatokea tena ndani ya Zanzibar hiyo hiyo! Mara hii Tanzania zima ikatikisika, kauli nzito nzito, kutoka kila kiongozi wanchi hii, kuanzia rais wa Tanzania, rais wa SMZ, waziri wa mambo ya ndani, n.k…karibu kila mwenye mdomo (access ya vyombo vya habari) alisema na kulaani. Tukaambiwa FBI, CIA, Mossad wote hao wakishirikiana na TISS watakuja kuchunguza na kuwatia nguvuni walomuuwa na walo ratibu mauwaji hayo….tukasubiri nab ado twasubiri!
Tukiwa bado tumehamanika na matukio hayo, tukiwa bado tunanyoosheana vidole, na kutupiana lawama, tukiwa tunazidi kuandamwa na wingo zito…leo tunasikia imamu sheikh Ali Khamis huko kitope (kaskazini Unguja), ameuliwa kwa kukatwa katwa mapanga na “ watu wasiojulikana”! Nategemea kauli zitakuwa hizo hizo “Uchunguzi utafanyika…” Na sisi ni kama vifaranga vya kuku…tutanyonya kesho, nabado twasubiri kunyonya!
Kwa kweli ukiangalia ukubwa wa visiwa vyetu (Zanzibar) na population yake na ukilinganisha na matukio haya, utaona kwamba ni matukio mengi sana na yametokea katika kipindi kifupi sana, matukio yakusikitisha na kulaaniwa na kila muungwana! Matukio yasiyopaswa kutokea katika jamii ya watu walostaarabika kama Zanzibar.
Chakusikitisha na kutisha ambacho ndicho kilichonisukuma kuandika haya, ni kuwa matukio yote haya, yamekuwa yakiishia kuhukumiwa na jamii kwa hisia tu, huku serkali ikiishia na jibu la “watu wasojulikana upelelezi unaendelea”, lakini jamii, na hata viongozi wa serkali na dini wamekuwa wakitumia hisia zao, utashi na mihemko yao kushutumu na hata kuhukumu baadhi ya kikundi au kundi katika jamii.
Mwanzaoni wapo walojaribu kuhusisha matukio hayo na CUF, lakini walipoona wazanzibar wa hivi sasa hawatopigana wala kuuwana kwa sababu ya vyama vya siasa, wakakosa nguvu! Lakini mara zote kundi la UAMSHO, likawa ndio kitambaa chao (leso) cha kufutia mafua, jasho, mate, n.k., kila tukio likitokea, basi utaskia UAMSHO hao, kauliwa padre “UAMSHO” , Kamwagiwa tindi kali sheikh -“UAMSHO”, limechomwa kanisa-“UAMSHO”! Khaa, mengine enhe, lakini mengine nkinehe!
Serkali imeacha kufanya kazi yake (Jeshi la polisi) kama walivyoafanya kule mwanza alipouliwa RCO , badala yake imeachia jamii ihukumu kwa hisia, ni hatari! Maana sasa viongozi wa UAMSHO wako ndani, UAMSHO hajulikani ni nani, lakini mauwaji yanaendelea! Sasa akiuliwa padri au kuchomwa kanisa utaskia ni waislam hao, naam hisia hisia, waislam hao wa Zanzibar sasa washakuwa magaidi! Si ndo alivyosema Nchimbi! Na sasa akiuliwa sheikh au ikichomwa misikiti, kwa hisia tu watasema “ WAKRISTO hao” na wakristo nao washakuwa magaidi! Tunako kwenda siko!
Siamini na kamwe sitoamini kwamba eti matukio haya yanafanywa na mzanzibar wakawaida, awe mkiristo au muislam, kamwe siamini kama mzanzibar wakawaida anamiliki silaha ya moto, na amekuwa mjuzi wakuitumia kiasi kwamba anaweza kulenga shabaha kwa ustadi mkubwa huku akiwa kwenye vespa na kumuuwa padri! Siamini kabisa, kama kweli mzanzibar anaweza kumvamia sheikh na kumkata kata mapanga! Nani basi anae fanya haya? Na anafanya haya kwa nini? Na Kwanini mapaka leo Kamishna Mussa hajatoa majibu ya walofanya matukio haya?
Inasikitisha na kushangaza sana, waziri mwenye dhamana na ulinzi wa taifa hili, anaibuka akiwa na maruwe ruwe (hangover) ya mapombe yake alokunywa “Rose garden” anasema eti wanaofanya matukio hayo ni MAGAIDI, huyu ni msomi wa PhD, eti daktari wa falsafa! Kwa falsafa ya aliepata Div 0 matokeo ya mwaka huu ya form 4, basi inatosha kumwambia waziri wakati unatanganza hayo, hukupaswa kuendelea kuwa waziri wa wazara hiyo tena! Ikiwa umeshindwa kudhibiti magaidi mpaka wameweza kuingia ndani ya nchi yako, lakini kama haitoshi, wakaweza kumiliki silaha, wakaweza kupanga na kutekeleza mauwaji na uharibifu wa nyumba za ibada wakati wewe ndie mwenye dhamana ya kulinda hayo yasitokee, sijui alikuwa au bado anangoja nini kwenye ofisi yake? Lakini pia angetwambia hawa magaidi wana demand (madai) nini?
Maana ya neno gaidi (terrorist), ni mtu anaeletea madhara katika jamii au anaefanya mashambulizi au utekaji kwa lengo la kugofya mamlaka au mtu husika ili atekelezewe madai yake! Kwa misingi hiyo gaidi huwa akishatenda huwa hutokeza wazi wazi na kusmema, mimi ndio niliofanya jambo kadhaa, ili unipe, au utekeleze masharti kadhaa, usipotekeleza ntafanya tena jambo kadhaaa…! Sasa matukio yote haya hakuna kikundi, wala mtu alojitokeza kukiri kufanya na kusema amefanya ili apewe nini au anadai nini. Sasa Dr. Nchimbi atwambie magaidi wake hawa wana mdai nini? Atwambie, wanauwa mapadri ili wapewe nini na kanisa katoliki? Wanauwa masheikh ili wapewe nini na waislam?
Nakumbuka, nilipokuwa na miaka 12, ilikuwa tukifunga skuli (nilikuwa skuli ya Jadida, Wete), nikienda kwa bibi yangu Pandani kwa mwewe, kuna mengi niliyapenda huko pandani ikiwemo kuchota maji kwenye kisima cha ndoo kwa kutumia “roda”, lakini jambo jengine ilikuwa lilonifanya niamke mapema sana ni “mchezo wa kupiganisha kuku” ! Niliupenda sana mchezo huu! Walipiganishwa majongoo wakila aina kuanzia makuchi, majogoo upanga n.k. Lakini ugomvi wa makuchi ulikuwa mtamu sana, hawachoki haraka, wajuzi wakupigana, hawakubali kushindwa, si woga na wepesi wakupiganishwa!
Walipiganishwa makuchi wale bila wenyewe kuwa na sababu ya msingi yakupigana! Walipiganishwa bila kujuwa kwanini wanapigana? Walipigana sababu tu wametumwa kupigana! Kupigana kwao makuchi hawa ndo furaha ya wapiganishaji, pengine wapiganaishaji hucheza kamari, na mwenye kuchi alieshinda akapata malipo!
Historia ni mwalimu nzuri, tunasoma kwamba kule India wakati wa harakati za kudai Uhuru zilizokuwa zikiongozwa na Mahtma Gandhi, wakati huo India ikiwa koloni la British, wakoloni hawa walikuwa wakiwapiganisha waislam na wahindu, ili kujenga hoja ya kutowapa uhuru! Walikuwa wakichinja nguruwe kasha wakiwatupa kwenye misikiti ya waislam…kwa hisia waislam wakiwashutumu wahindu kwa kuwatupia nyama haramu, najisi kenye nyumba zao tukufu za ibada, kisha wakoloni hawa wakichnja ng’ombe na kuwatupa kwenye mahekalu ya wahindu, wahindu nao kwa hisia tu, wakawashutumu waislam, kwamba ndio wanaowauwa miungu yao (wahindu wanaabudu ng’ombe kama mungu wao), kisha wanawatupa kwenye nyumba zao za ibada! Kwa hisia wakaishia kupigana na kuuwana….mkoloni akazidi kutawala!
Hali hii ndio nnayo iona Zanzibar, matukio ya kumwagia mavi visima vya maji, kuchomwa moto nyumba za masheha, kulipuliwa mabomu ofisi za CCM, tuliyaona mageni yalipoanza miaka 90 kule kisiwani Pemba, tukawa twaambiwa ni wapinzani, wafukuwa hadi barabara na kuvunja mabomba ya maji! Lakini kisha tukayazoea, na jamiii ikamjuwa hasa anaefanya hayo ni nani! Sasa kuna kumezuka jipya, lakini safari hii si Pemba, ni kwa dada yake, Unguja, kumezuka fasheni ya sampuli yake ya kuwauwa viongozi wa dini, wanauliwa mapadri leo, na kesho wanauliwa masheikh, kwa zamu!
Ni lazima tutumie akili zetu vizuri katika kutafakari mambo haya! Tuweke hisia zetu na misukumo ya kiimani pembeni! Tumuombe Mungu wetu atupe hekima ya kuangalia matukio haya kwa jicho la 3, atupe hekma ya kuwa waadilifu katika kuchambuwa matukio haya! La sivyo, basi, leo atauliwa Padri John, kwa hisia upande mmoja utasema –“WAISLAM hao”, kesho atauliwa Sheikh Abdalllah, kwa hisia upande mwengine utasema – “WAKRISTO hao”, kitakachofuata sihitaji kukieleza hapa, maana wote tunajuwa! Mungu atunusuru!
Wapiganishaji watakuwa wamekaa pembeni wakitutazama tunavyouwana kwa ujinga wetu! Watakuwa wanasubiri kuleta misaada ya kibinaadam” (kama wanavyoita wenyewe), watasubiri kuleta majeshi yao kusimamia amani, watapa habari za kutanganza kwenye vyombo vyao vya habari kama vile CNN, BBC, Al jazeera n.k Zanzibar itakuwa maarufu kama ilivyo afghanstan, Iraq, Syria, n.k! Watapata sababu za kutosha za kuifanya Zanzibar kuwa mkoa wa Tanzania! Utamaduni na asili ya Zanzibar sasa ndo itapotea kabisa!
Tusikubali kufanywa makuchi tukapiganishwa sie kwa sie….!
Chanzo: Mzalendo

Friday 22 February 2013

Viongozi wetu na urongo wausemao

MWANDISHI George Orwell aliwahi kuandika kwamba kutamka ukweli huwa ni kitendo cha kimapinduzi pale udanganyifu unapozagaa na kuenea pote kwa watu wote.
Nadhani alikusudia kusema kwamba katika nyakati za uongo, kama hizi tunazoziishi sasa, kutamka ukweli huwa ni kitendo cha kishujaa kinachoweza hatimaye kusababisha mapinduzi.
Huenda pia ikawa alikusudia ya kuwa katika nyakati za uongo panahitajika shujaa kusema kweli kwa sababu jamii huwa imekwishazoea kudanganywa na hufuata tu inachoambiwa na wakubwa wake.
Jamii inakuwa kama ng’ombe aliyetiwa shemere. Na hao wakubwa hujifanya kuwa wao ndio wenye kujua kila kitu na kwamba walisemalo ndo ndilo. Ndio ukweli usiopingika.
Siku hizi uongo umeenea kote hasa katika ngazi za utawala na unahatarisha mfumo wa utawala bora tunaouengaenga. Uongo ni hatari kwa utawala bora kwa sababu unatumiwa kuwa visingizio pale haki za binadamu zinapokiukwa au viongozi wanapojiingiza katika ufisadi.
Uongo huo unaanzia juu kwa wanasiasa na viongozi wetu na kutiririka kwa maofisa wa ngazi za chini. Viongozi wetu, na wanasiasa wetu kwa jumla, wameugeuza ulaghai na kuufanya uwe sanaa pendwa. Wao wenyewe wamebobea katika kudanganya danganya na wamekuwa mafanani wa uongo. Na wala hawana haya.
Hii ndiyo sababu kwa nini viongozi wetu wanathubutu kutueleza chochote watakacho hata ikiwa wanajua kwamba sisi tunajua ya kuwa hicho wanachokieleza ni cha kubuni, ni ghiliba tupu.
Iko mifano mingi. Wa karibuni ni ule wa kiongozi mmoja wa taifa aliyesema kwamba nakala halisi ya Hati ya Muungano ipo ilhali ulimwengu mzima unajua kwamba hakuna kitu kama hicho. Haipo nchini wala haipo makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York.
Mfano mwingine ni wakati wa tukio la mauaji ya 2001 huko Pemba. Rais wa wakati huo Benjamin Mkapa alidanganya kuhusu idadi ya waliouawa na pia alidanganya kuhusu waandamanaji akisema walikuwa ‘magaidi’ waliotaka kuipindua serikali.
Baadaye tume aliyoiteua yeye mwenyewe kuchunguza tukio hilo ikiwa chini ya Kanali Hashim Mbita ilitoa ripoti iliyokuwa tofauti na aliyoyasema Mkapa.
Mfano mwingine ni hotuba aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete kwa Bunge Desemba 30, 2005 kulifungua baada ya uchaguzi wa mwaka huo. Alisema anashangazwa na Wazanzibari hao hao wanaofaidika na fursa za Muungano kuwa ndio haohao wanaoonyesha hisia za kujitenga.
Ni wazi kwamba aliwakusudia wapigaji kura wa Pemba waliokibwaga chama cha CCM. Lakini kusema kwamba wasiokitaka chama cha CCM hawautaki Muungano si kweli kwa sababu wakati wa uchaguzi huohuo takriban Kilimanjaro nzima ilipiga kura dhidi ya CCM.
Ukweli ni kwamba wapo wasiokitaka chama cha CCM na wasioutaka Muungano lakini pia wapo wanaoutaka Muungano na wasiokitaka chama cha CCM. Ukweli lazima usemwe.
Viongozi wetu wanasahau kwamba kusema kweli ni jambo lililo adhimu katika siasa. Ni jambo la uadilifu. Linampambanua kiongozi anayestahili kuheshimiwa na yule anayedharauliwa anayeonekana kuwa ana sifa za kihuni, za kijambazi, ili ajipatie muradi wake. Lengo lake huwa ni kujipatia alitakalo potelea mbali ikiwa ukweli atautupa jaani.
Inanijia hapa kuutaja ushairi na kuuhusisha na siasa kwani kuna wenye kuiona fani ya ushairi kuwa ni fani ya kisiasa. Wenye kuuangalia ushairi kwa mtazamo huo na kuufananisha na siasa hufanya hivyo kwa sababu wanasema ushairi humfanya mshairi aseme kweli.
Viongozi wetu pia wanasahau kwamba wananchi wengi hawataki kujiingiza katika mambo ya siasa kwa sababu wanaziona siasa kuwa ni chafu na kwamba chanzo cha uchafu huo ni uongo.
Ipo sababu inayowafanya viongozi wetu wazoee kusema uongo na kuifanya hali hiyo iwe hulka yao. Sababu yenyewe ni kwamba mara nyingi uongo huwafaa ingawa manufaa wayapatayo huwa ni ya muda mfupi tu. Hatimaye huo uongo huja kuwasuta.
Historia ina mifano mingi yenye kuonyesha jinsi uongo unavyokuwa hauna mwisho mwema kwa viongozi wausemao.
Athari zake ni nyingi. Moja na labda ni athari iliyo ndogo ni ile inayoathiri afya yake kiongozi mwenye kusema uongo.
Nakumbuka mwaka jana kulifanywa utafiti wa kitaalamu kuhusu athari ya uongo kwa afya ya waongo. Waliofanya utafiti huo walikuwa wataalamu wa Chuo Kikuu cha Notre Dame waliogundua kwamba kusema uongo kuna athari mbaya sana kwa afya ya wasemaji uongo kiasi cha kuwafanya waingiwe na wahaka, fadhaa ama huzuni. Wengine huingia kichaa na kuwa majnuni kwa uongo wasiokwisha kusema.
Hizo ni athari zinazowapata watu wa kawaida tu. Zinazidi kuwa mbaya kwa kiongozi mwenye majukumu makubwa na hasa wa nchi kama za kwetu. Hawa ni viongozi ambao aghalabu hutaka waonekane kuwa wao ni wababe wanaopaa angani wakiitia dunia katika kwapa zao.
Nadhani Orwell alipofananisha kusema kweli na ‘kitendo cha kimapinduzi’ alikusudia mapinduzi ya kifikra au ya hali halisi ya mambo ilivyo. Mapinduzi ya kifikra ni yale yanayoubiruwa mfumo wa jinsi jamii ilivyozoea kufikiri.
Mapinduzi ya aina hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya jamii. Kuselelea kuitakidi fikra au dhana zilizojaa kutu zisizopigwa msasa ili ziyasibu mazingira yaliyobadilika ni kujitakia balaa. Ni kuutia pingu uwezo wetu wa kufikiri na kutufanya tufanye mambo yasiyoelekea katika wakati ambapo dunia, kwa jumla, huwa imepiga hatua mbele.
Fikra zetu hazitoweza kuchanua ikiwa sisi na wale tuliowachagua watuongoze tutakuwa na tabia ya kudanganyana.
Hapa ninawakumbuka watu wawili wasiojulikana ni nani (pengine alikuwa ni mtu huyohuyo mmoja) lakini waliotoa wasia ambao tunafaa tuuzingatie kwa makini.
Mmoja alisema: Siku zote sema kweli, hata kama itakubidi uubuni (huo ukweli).
Mwengine alisema: Sikuzote sema kweli. Na kama huwezi kusema kweli sikuzote, basi usiseme uongo.
chanzo: Raia mwema

Thursday 14 February 2013

Uchama usiruhusiwe kuyapiku maslahi ya Zanzibar

AGHALABU umma unapoachiwa na kupewa uhuru kamili wa kujiamulia wenyewe mambo yao hujiamulia mambo yenye kheri nao.
Tuliyashuhudia hayo Zanzibar, Julai 31, 2010 pale wananchi wa huko walipopiga kura ya maoni wakipendelea nchi yao iwe inaendeshwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Ulikuwa ni uamuzi wa busara, wa kujiepusha na shari.
Ulikuwa pia uamuzi uliozusha matumaini mengi na makubwa hasa baada ya Serikali hiyo kuundwa Novemba 1, 2010 baada ya uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka huo. Wazanzibari wakitaraji kwamba angalau watumishi wakuu wa serikali watateuliwa kwa kuzingatia sifa zao za utendaji wa kazi na si mengine.
Watu wakidhani kwamba mambo ya zamani yatatupiliwa mbali, kwamba wakuu serikalini watateuliwa kwa mujibu wa ustahili wao na si kwa mapendeleo — yawe ya kisiasa, ya kikabila au ya kujuana.
Kadhalika, wengi wakitumai kwamba hatimaye Zanzibar inaelekea ndiko — kwenye maendeleo. Wengine wakihisi kwamba angalau kutawekwa msingi madhubuti wa kuzitengeneza huduma zilizo muhimu sana na miundombinu imara pamoja na kuufanya uchumi ustawi. Alhasili wakiamini kwamba mambo yataanza kutengemaa.
Walikosea. Tunaelekea mwaka wa tatu tangu iundwe hiyo Serikali ya ubia na wengi wa Wazanzibari wanaona kuwa hali zao za maisha zimezidi kuwa ngumu. Siku hizi, kwa mfano, wakitaka kununua chakula inawabidi wanunue kwa bei za kuruka juu sana kushinda zile walizokuwa wakilipa katika 2010. Ukizilinganisha bei za vyakula zilivyokuwa miaka miwili iliyopita na zilivyo sasa hutoshangaa ukiwaona wanalia.
Isitoshe zile idara au wizara zilizo chini ya udhibiti wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama vile za afya na elimu hazikufanya mengi ya kutia moyo.
Ni muhimu Wazanzibari wote wawe wanaitafakari hali hii hasa wakiwa katika mchakato wa kuandikwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni muhimu pia wajiulize wamefanikiwa kwa kiasi gani hadi sasa, na wajiwekee mkakati wa kuuhitimisha mchakato huu wakiwa wameungana, wakiwa na msimamo mmoja kuhusu Katiba mpya waitakayo.
Tunavyoambiwa ni kwamba Katiba hiyo mpya itakuwa tayari Aprili 2014 wakati ambapo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utatimia miaka 50.
Mswada wa Katiba hiyo mpya utapigiwa kura ya maamuzi Tanganyika na Zanzibar chini ya usimamizi wa tume za uchaguzi za sehemu hizo mbili za Jamhuri ya Muungano.
Ili waweze kuupata muradi wao Wazanzibari hawana hila ila waungane; wawe na msimamo mmoja wakati wa kupiga kura ya maamuzi wakitambua kwamba uchama au itikadi za kisiasa haziwezi kuyapiku maslahi ya Zanzibar.
Ninaamini kwamba wamekwishajifunza vya kutosha kutokana na makosa ya zamani ya viongozi wao wa kisiasa, ambao badala ya ushirikiano wakipingana, wakizozana na wakizusha mgawanyiko katika jamii.
Viongozi wenyewe waligawanyika na waliwagawanya wafuasi wao kiasi cha kuwafanya baadhi yao wayaone maslahi ya nchi yao kuwa ni duni yakilinganishwa na maslahi ya vyama vyao vya kisiasa.
Wazanzibari waligawika vibaya sana tangu miaka ya 1950 Waingereza walipoanzisha siasa za ushindani wa vyama na chaguzi hadi 2010 palipopatikana Maridhiano na baadaye Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Wazanzibari waligawika hata walipokuwa chini ya mfumo uliohalalisha chama kimoja tu cha kisiasa kutoka 1964 hadi 1995 kwani takriban nusu yao hawakuwa na imani na Serikali ya Mapinduzi.
Si tabu kung’amua kwa nini hawakuwa na imani na serikali hiyo. Sababu kubwa ni kwamba awamu zote za Serikali ya Mapinduzi zilikuwa zikihubiri na zikifuata siasa za kibaguzi. Kwa hizo siasa zao chafu awamu zote hizo ziliwatenga na kuwafanya si kitu Wazanzibari wasiovaa mashati ya kijani na kuimba nyimbo za CCM.
Ndiyo maana kuna haja ya kuwa tangu sasa Wazanzibari wawe na mtazamo mmoja kuhusu jinsi nchi yao itavyotawaliwa baada ya kupatikana Katiba mpya. Mtazamano huo lazima uhakikishe kwamba jamii itayoibuka itakuwa ya haki na usawa, itayowapa Wazanzibari wote fursa sawa bila ya ubaguzi au upendeleo wa aina yoyote.
Ili waweze kuijenga jamii waitakayo yenye kuwapa wote haki sawa, Wazanzibari wanapaswa wawe na mdahalo juu ya mapendekezo yote yaliyotolewa wakati Tume ya Katiba ilipokuwa ikikusanya mawazo ya wananchi kuhusu Katiba waitakayo kazi ambayo ilimalizika karibuni tu Visiwani.
Sasa tukiwa tunazisubiri hatua za mchakato huo zitazotufikisha Aprili 2014 ni muhimu Wazanzibari wote waungane na wautetee mfumo wa Muungano utaojengwa juu ya msingi wa Mkataba.
Huo ndio mfumo pekee utaoirejeshea Zanzibar mamlaka yanayoiwezesha iendeshe shughuli zake za ndani na nje ya nchi bila ya kuomba ruhusa Bara au kutoka nchi yoyote ya kigeni.
Ni muhali hii leo kumpata mzalendo wa Kizanzibari asiyetaka Rais wa Zanzibar na Serikali ya Umoja wa Kitaifa warejeshewe mamlaka yao kamili pamoja na Baraza la Wawakilishi kuwa na uwezo wa kutunga sheria kuhusu mambo yote na si yale yasiyo ya Muungano tu.
Wapo, bila ya shaka, wenye kutaka mfumo wa sasa uendelee. Lakini Wazanzibari aina hiyo, ambao wenzao wanawaita vibaraka, si wengi na hata hao nao wanataka Zanzibar irejeshewe ‘mamlaka’ yake ingawa hawaelezi jinsi mamlaka hayo yanavyoweza kurejeshwa chini ya mfumo uliopo wa serikali mbili.
Wengi wanaiunga mkono kauli iliyotolewa Jumamosi iliyopita huko Nungwi, Unguja, na Ismail Jussa ambaye ni mwakilishi wa Mji Mkongwe. Jussa alisema kwamba Wazanzibari hawana sababu ya kuendelea na mfumo uliopo wa Muungano kwa kuwa ‘unaididimiza Zanzibar, kiuchumi na kijamii’. Kwa mujibu wa Jussa mfumo pekee utakaoipa Zanzibar fursa ya kusonga mbele ni mfumo wa Muungano wa Mkataba.
Hayo ndiyo maoni ya baadhi ya Wazanzibari na Serikali ya Muungano inawajibika kuyaheshimu maoni hayo. Kwa kufanya hivyo tu ndipo tatizo hili tata la Muungano litavyoweza kutanzuliwa ili nchi hizo mbili ziweze kusonga mbele bila ya kubughudhiana.
Chanzo: Raia Mwema

Friday 8 February 2013

Mohamed Ali Foum: Mzalendo wa Kizanzibari na msiri wa Nyerere

MOHAMMED Ali Foum aliyefariki dunia jijini Cairo Ijumaa usiku, atakumbukwa kama mwanamapinduzi na shujaa aliyepigania uhuru wa Zanzibar na kuchangia mengi katika juhudi za kulikomboa Bara la Afrika.
Wengi waliokuwa wakimfahamu juu juu, hawakuutambua mchango wake uliokuwa adhimu katika harakati za ukombozi wa Afrika.
Hayo si ya ajabu kwa kuwa Foum hakuwa mtu wa kujionyesha na akipendelea kuuficha umahiri wake hasa katika nyanja ya diplomasia.
Nikimfahamu tangu kufungua kwangu macho kwani sote tulizaliwa Vuga, Mji Mkongwe, Unguja.
Alikuwa ni mmoja miongoni mwa kaka zetu wa Vuga waliowashajiisha wadogo zao mtaani wawe na moyo wa kuwa pamoja.
Mwenzake mmoja katika hili, alikuwa Salim Hakim, ambaye sasa ni mmoja wa mabalozi wanaosifika wa Omani. Baadaye wote wawili walikuwa mabalozi katika Umoja wa Matifa, Foum akiiwakilisha Tanzania na Hakim akiiwakilisha Omani.
Katika miaka ya hivi karihuni wakawa tena pamoja wakiishughulikia Somalia. Foum alikuwa Mwakilishi wa Muungano wa Afrika, na Hakim alikuwa Mwakilishi wa Umoja wa Kiarabu (Arab League).
Lakini huko utotoni waliwatia ari watoto wa Vuga waunde timu ya soka ya Young Brothers. Nakumbuka hao wawili na wenzao wa rika lao, walikuwa na tabia ya kuitana kwa kupiga mbinja au mluzi, kama wasemavyo Bara.
Tangu utotoni, Foum alikuwa si mtu wa kukaa nyuma. Daima akipenda kushirikiana na wenzake mtaani na pia skuli. Ingawa hakuwa pocho Foum aliamua kukatiza masomo yake ya sekondari na kuanza kufanya kazi katika Ofisi ya Leba ambako pia akifanya kazi Ahmed Diria Hassan. Baadaye Diria naye atakuja kuwa mmoja wa mabalozi madhubuti wa Tanzania.
Foum alianza kuzivaa siasa alipojiunga na chama cha Hizbu, yaani Zanzibar Nationalist Party (ZNP). Chama hicho kilimpeleka Cuba kwenda kufungua ile iliyokuwa ikiitwa Ofisi ya Zanzibar. Huko alikuwa pamoja na Ali Mahfoudh. Salim Ahmed Salim alijiunga nao kwa muda mfupi.
Nyumba yao mjini Havana, ambayo pia ilikuwa ni ofisi yao, ilikuwa katika eneo la Vedado ambako wakiishi Wacuba wa tabaka la kati. Sehemu moja ya nyumba hiyo ilikuwa ofisi ya chama cha ANC cha Afrika ya Kusini.
Foum na wenzake waliwasili Havana si muda mrefu baada ya Fidel Castro na Che Guevara kuuteka mji huo katika Mapinduzi yaliyomwondoa Fulgencio Batista madarakani. Tayari wakati huo Foum alikuwa amekwishaanza kuzikumbatia siasa za mrengo wa kushoto.
Huko Cuba pia alikuwa akihudhuria mafunzo ya kijeshi yaliyokuwa yameandaliwa mahsusi kwa vijana Wakikomred kutoka Zanzibar, waliokuwa wakifunzwa namna ya kupindua Serikali.
Baadaye vijana hao pamoja na kina Foum, Ali Mahfoudh na Salim Ahmed walijiunga na chama cha Umma Party cha Abdulrahman Babu na kushiriki katika Mapinduzi ya 1964.
Waandishi wa habari kutoka nje waliofika Zanzibar baada ya Mapinduzi na kuandika kwamba walikuwako Wacuba huko, walikuwa kwa hakika wakiwazungumza kina Foum na makomred wenzake waliorejea kutoka Cuba na waliokuwa wakizungumza Kispanyola.
Mwaka 1963 walipokuwa bado Havana, Foum na Ali Mahfoudh waliandika kijitabu kilichoitwa: ‘Forge Ahead To Emancipation’ (Songelea Ukombozi) kilichozungumzia vuguvugu la Zanzibar la kuupinga ubeberu.
Historia ya Umma Party, inaonyesha kwamba Ali Sultan Issa, Foum, Mahfoudh na Salim Rashid ndio waliokuwa wakimshadidia zaidi Babu wakiache mkono chama cha ZNP.
Katika miezi ya mwanzo ya Mapinduzi, Foum alikuwa pamoja na Mahfoudh kwenye kambi ya kijeshi na baada ya kuundwa Muungano, akateuliwa awe mshauri (counselor) katika Ubalozi wa Tanzania, New York.
Hapo ndipo Foum alipoanza kazi zake za kidiplomasia na kuanza kung’ara katika shughuli hizo. Rais Julius Nyerere alimteua awe Balozi wa Tanzania India, Italia na pia katika Umoja wa Mataifa. Foum aliwahi pia kuwa waziri mdogo wa mambo ya nje.
Nyerere akimuamini sana, na Foum alikuwa ni msiri wake mkubwa, na hasa kuhusu shughuli za kimataifa. Mara nyingi Mwalimu Nyerere alikuwa akimtuma kuonana na viongozi wa nchi nyingine alipokuwa ana mambo nyeti yaliomfanya awasiliane na viongozi hao.
Yeye mwenyewe Foum, alikuwa na uhusiano na wanaharakati mbalimbali wa kimataifa.
Miaka michache iliyopita nilimpelekea baruapepe Amiri Baraka, Mshairi, Mwandishi na Mwanaharakati wa Kimarekani mwenye asili ya Kiafrika na nikamuuliza lini alikutana mwanzo na Babu.
Baraka (ambaye zamani akijulikana kwa jina la LeRoi Jones) alinijibu: “Nilikutana naye Astoria Hotel, New York, mwaka 1964 wakati uleule nilipokutana mwanzo na Malcolm X.”
Wakati huo, Foum tayari alikuwa New York na alikuwa Mtanzania wa mwanzo kujuana na Malcom X na halafu akamjulisha kwa Babu aliyekuwa akidhuhuria kikao cha Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Gamba la albamu moja ya hotuba za Malcolm X lina picha ya Foum na Babu wakiwa pamoja naye Malcolm X. Ninajua kwamba Babu aliwahi kuiona albamu hiyo na gamba lake, lakini Foum hakuwahi kuiona.
Miaka miwili iliyopita tukiwa pamoja Nairobi alinishikiia nimtafutie gamba la albamu hilo. Moja ya masikitiko yangu ni kwamba sikujaaliwa kumtimizia haja yake.
Usuhuba wa Foum na Malcolm X ulikuwa mkubwa kiasi cha kuwafanya wawe wanatembeleana majumbani mwao. Mwengine aliyekuwa akimtembelea Foum nyumbani kwake New York alikuwa mwanamapinduzi wa Cuba Che Guevara.
Kwa ujasiri wake na licha ya kujuwa kwamba akiandamwa na majasusi wa CIA wa Marekani Foum alikuwa akifuatana bila ya kificho na Malcolm X pamoja na Che.
Kwa hilo na pia kwa harakati zake za kupinga ukoloni na ubeberu Foum alikuwa heshi kuwakera Wamarekani. Aliwakera sana kwa msimamo wake imara wakati mijadala ya vikao vya Kamati ya 24 ya kuufyeka ukoloni duniani. Foum aliteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika kamati hiyo.
Mfano wa jinsi Wamarekani walivyokuwa wakimuona kuwa ni mkorofi ni telegramu moja kutoka ujumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa iliyopelekwa kwenye wizara ya mambo ya nje ya Marekani.
Telegramu hiyo iliandikwa Novemba 26, 1968, wakati Marekani ilipokuwa ikizingatia kujitoa kutoka kwenye Kamati ya 24.
Ilisema hivi: “Maazimio kama hayo yanatungwa hasa na Waafrika wenye siasa kali — kama Foum (Tanzania) wakisaidiwa na Masovieti na Waarabu wenye siasa kali kama Syria na Iraq.”
Diplomasia kama ilikuwa katika damu yake na inaonyesha alimrithisha mdogo Abdillahi ambaye mwaka jana tu alistaafu akiwa balozi mdogo wa Sweden mjini Addis Ababa.
Yeye mwenyewe Foum aliendelea na shughuli za kidiplomasia hata baada ya kustaafu serikalini. Novemba 22, 2002, Amara Essy, Mwenyekiti wa muda wa wakati huo wa Muungano wa Afrika, alimteua awe mjumbe wake maalum nchini Somalia.
Foum alijipatia sifa kwa uchapaji kazi wake na kwa jitihada zake wakati wa Mkutano wa Somalia wa Kuleta Suluhu ya Kitaifa uliofanywa nchini Kenya toka Oktoba 2002 hadi Oktoba 2004.
Alikuwa mbioni pia wakati wa jitihada nyingine zilizochukuliwa baadaye na jumuiya ya kimataifa kujaribu kustawisha amani na kuleta suluhu nchini Somalia.
Aliuacha wadhifa wa kuwa Mwakilishi Maalum wa Muungano wa Afrika kwa Somalia mnamo 2007 na mahala pake pakashikwa na Nicolas Bwakira kutoka Burundi.
Baadaye kama miaka miwili hivi iliyopita alichukuliwa kwa muda na Augustine Mahiga, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Somalia, awe mshauri wake. Aliiacha kazi hiyo mwaka jana akishughulika na biashara.
Ujuzi wake wa siasa za Somalia na majungu ya wanasiasa Wakisomali ulikuwa wa kupigiwa mfano. Binafsi nilifaidika nao nilipokuja kuishi Nairobi na kusimamia mradi mmoja wa shirika la UNDP la Umoja wa Mataifa kuhusu kielelezo cha katiba mpya ya Somalia.
Alinishauri na kunielekeza wapi pa kupiga hodi ili kazi zangu kuhusu Somalia zifanikiwe. Wakati mwingine akinishauri hata bila kuomba ushauri wake. Huo ni mfano wa sifa nyingine aliyokuwa nayo — ya ukarimu na kutokuwa na uchoyo.
Hizo ni sifa za mcha Mungu na Foum alikuwa mtu wa aina hiyo kama marehemu baba yake, Inspekta Ali Foum.
Safari moja nikiwa Jeddah, Saudi Arabia, mfanyakazi mmoja katika Ubalozi mdogo wa Tanzania aliniambia kwa masikitiko: “Sijui Foum mzima kwa sababu haipiti mwezi hutokea hapa kuja kufanya umra Makkah. Mwezi huu sijamuona.”
Ama mimi sitomuona tena siku za Ijumaa katika Msikiti wa Hurlingham hapa Nairobi.
Chanzo: Raia Mwema

Sunday 3 February 2013

Uwanja wa ndege Z`bar kuwa wa Kimataifa mwakani

Chapa
Uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume Zanzibar utafikia vigezo vya Kimataifa baada ya kukamilika mradi wa miezi 18 wa kuzungusha ukuta na kutanua sehemu ya maegesho ya ndege mwakani.
Tamko hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Viwanja vya ndege Zanzibar , Kapteni Said Ndumbugani, katika ziara ya Naibu Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano Zanzibar, Issa Haji Gavu ya kukagua mradi huo.
Ndumbugani, alisema mradi huo unatarajia kutumia dola za Marekani Milioni 50 ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya dunia na ujenzi wake unafanywa na Kampuni ya Sogea Satom ya Ufaransa.
Alisema kuanzia Febuari 4 mwaka huu kilomita 2.2 za eneo la kuegesha ndege katika uwanja huo litafungwa kupisha ujenzi wa mradi huo.
Hata hivyo alisema huduma za ndege zitaendelea kama kawaida katika uwanja huo wakati wote wa ujenzi.
Alisema eneo la ukuta unaojengwa utakuwa na mzunguko wa kilomita 12 hadi baada ya kukamilika na tayari kilomita saba zimekamilika tangu kuanza kwa ujenzi wa mradi huo Novemaba mwaka jana.
Aidha alisema kiasia cha Shilingi Bilioni 3 kimetumika kulipa fidia wananchi pamoja na kufanikisha kazi ya kujenga ukuta unaozunguka uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.
Mkurugenzi huyo alisema baada ya kukamilika mategenezo yote uwanja huo utakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa ndege nane kwa wakati zikiwemo aina ya Boeing badala ya ndege tatu.
Alisema uwanja wa ndege Zanzibar baada ya njia ya kutua na kuondokea kukamilika ujenzi wake sasa umekuwa na urefu wa kilomita 3.22 na hupana mita 45.
Naibu Waziri Gavu alisema ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kutaka uongozi kuhakikisha ujenzi unakamilika muda muafaka.
Gavu, alisema kukamilika kwa mradi wa kuzungusha ukuta kutaondoa tatizo la mifugo kukatisha uwanjani pamoja na maeneo ya makaazi ya wananchi kuvamiwa.
“Lengo kubwa la serikali kuona uwanja wa ndege Pemba unatoa huduma kwa muda wa saa 24 tayari tumepanga kutumia dola za Marekani milioni 1.5 kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo makubwa mwaka huu,”alisema Gavu.
Alisema kwamba kuimarishwa kwa viwanja vya ndege kutaongeza pato la Taifa kutokana na idadi ya watu wanaotumia huduma za ndege kufikia milioni moja kwa mwaka Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Friday 1 February 2013

Ukivunjika muungano nini Kitatokea?


Hoja za Watetezi wa Muungano
1. Muungano ukivunjika Wapemba walio na maduka dar watarudi kwao
  Huu ni upotoshaji kwani kuna wachina wanauza hadi karanga, jee kuna muungano wa china na Tanganyika?
2. Wazanzibari na Watanganyika wameowana
  Hii ni hoja ya pili ambayo pia haina mashiko, Wazanzibari na Watanganyika wameowa wazungu na wachina jee kuna muungano na nchi hizo, Mzee wetu (Mpigania haki Maarufu za wazanzibari) Nassoro Moyo aliowa mtanganyika mwaka 1951, jee kulikuwa na muungano wakati huo.
3. Wazanzibari tukivunja muungano tutakosa kununuwa vitunguu na mbatata tanganyika,
  Tunafanya biashana na nchi mbali mbali Africa na ulaya na Asia jee kuna muungano na nchi hizo.
4. Wanaodai muungano wa mkataba au uvunjike wanataka kumleta muarabu
  Huu ndio kabisa sio akili bali matope, nimezaliwa miaka ya sabiini, sijui habari za mfalme wala upumbavu gani nahitaji Zanzibar yangu yenye mamlaka kamili.
5. Wazanzibari tutagawanyika uunguja na Upemba
    Zanzibar ilikuwepo kabla ya Muungano, jee kuna muungano wa Unguja na Pemba?
6. Tunaihitaji Tanganyika kwa ajili ya ulinzi
     hii ni kututia woga ila kuna nchi ndogo kuliko Znz na zina ulinzi imara, jeshi letu la Zanzibar lilikuwa strong kabla ya muungano, baada ya muungano ndio tumefika tulipo.

Next time nitaeleza faida kwa nini tunahitaji Zanzibar mamlaka kamili