KWA mara nyingine watu wa Zanzibar wameshitushwa na habari za ubadhirifu
mkubwa wa fedha uliogunduliwa na Kamati ya Baraza la Wawakilishi katika
uchunguzi wake wa Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).
Kwangu mimi hili ni jambo la kawaida, ila ninashangaa kuwa kimepita kipindi
kirefu kidogo tokea mara ya mwisho kusikika habari za aina hii, za baadhi ya
watu kuchezea wanavyotaka fedha na mali za serikali na taasisi zake.
Nasema hivi kwa sababu bado haijaonekana kwa vitendo watu wanaofanya ufisadi
na kuitia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi kuwajibishwa kisheria.
Panapotokea vishindo vya kuwabana wanaodaiwa kuhusika na ufisadi basi
wanaokabwa ni dagaa na wale mapapa kubaki wakielea habarini.
Watu hawana wasiwasi kama vile fedha walizochezea ni zao au za familia zao.
Huku ndiko kutesa kwa zamu.
Machi mwaka jana, Kamati ya Kuchunguza Mahesabu ya Serikali na Mashirika ya
Umma (PAC) ya Zanzibar ilionya kuwa ingeliwapelekea mahakamani baadhi ya
watendaji wakuu wa serikali na wahasibu ifikapo Mei wale waliokiuka sheria za
matumizi ya fedha za serikali.
Sasa ni karibu mwaka mmoja na hakuna aliyefikishwa mahakamani kwa wizi au
ubadhirifu wa fedha za umma uliogunduliwa wakati ule.
Hii ilitokana na PAC kuona kwamba ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali
iligundua kuwa miradi mingi iliyokamilika ilikuwa hailingani na fedha
zilizotumika.
Ripoti ile ilieleza kuwa yapo magari ya serikali yaliodaiwa kuwa mabovu,
lakini ukweli ni kwamba huo ulikuwa mradi wa kuiba vipuri.
Katika mambo yaliyogunduliwa wakati ule ni kwamba katika kipindi cha mwaka wa
fedha wa 2008-09 fedha za masurufu zilizopotea zilikuwa sh mibilioni 5.1.
Mambo mengine yalikuwa na sura ya ufisadi uliokithiri na unaonuka
yaliyoelezwa katika ripoti ile ni pamoja na :
Malipo ya dola 94,000 za
Marekani yalifanywa bila ya kuwepo stakabadhi.
Fedha zilizopotea katika mikataba ni sh milioni 413.6, vifaa vingi
vilinunuliwa na baadhi ya ofisi za serikali bila kutumia zabuni.
Tulielezwa na baadhi ya watu kuamini (si mimi) kwamba PAC haitakuwa tena na
muhali au kumuonea huruma mtu yeyote aliyeiba au kutumia vibaya fedha za
serikali.
Hivi sasa tunapewa hadithi mpya ya ubadhirifu unaosemekana kufanyika ZECO,
lakini ukweli ni kwamba kilichofanyika ni kuendeleza utamaduni wa kuiba na
kuvuruga fedha za umma. Wapo wanaosema fedha za umma hazina mwenyewe na
ukizipata ni sawa na zile za kuokota! Hivyo ni haki kuzichota.
Tunaambiwa kuwa miongoni mwa madudu yaliyogunduliwa katika Shirika la Umeme
ni haya yafuatayo:
Kuwapo tofauti ya malipo kati ya kazi zinazofanana na baadhi ya malipo
yaliyopo kwenye risiti yanatofautiana na malipo halisi.
Wapo wateja wanaotumia umeme bure na hawamo kwenye orodha ya shirika. Ipo
tofauti kubwa ya ada za malipo zinazotozwa kwa wanaounganishiwa umeme na majina
ya watu wanaodaiwa kufaidika kutajwa.
Yupo mteja (ametajwa jina) anayedaiwa kuungiwa umeme wa njia tatu na kuonesha
kuwa amelipa sh milioni nane wakati mtu huyo anadai amelipa sh milioni 37,
lakini kwenye akaunti ya mtu binafsi.
Benki moja inasemekana kuwa ilitozwa sh 3,718,000 kuungiwa umeme, lakini
vifaa hasa vilivyotumika kwa kazi hiyo vina thamani ya sh milioni 14.
Baadhi ya wateja, zikiwamo hoteli za kitalii, hawamo kwenye orodha ya malipo
ya shirika, nguzo feki zimetumika kuunga umeme, mafaili ya wateja wakubwa 147
yamekosekana.
Ipo kampuni iliyokodishwa mnara na haijawahi kulipa tangu ilipokodishwa.
Hakuna maelezo yanayoeleweka juu ya ununuzi wa jenereta 32 ya akiba ya shirika
yaliyopo hapo Mtoni. Hapakuwepo na zabuni za ununuzi wa majenereta haya.
Kwa kweli yapo madudu mengi katika ripoti hii na tuhuma zilizoambatanishwa na
madai haya ya ufisadi ni nzito na zinaunguza kuliko huo umeme wenyewe.
Ni mahakama tu, kama ipo huru na inaachiwa kufanya kazi yake inayotarajiwa
kufanya, ndiyo inayoweza kutoa uamuzi wa haki na ukweli kujulikana. Inawezekana
pia tuhuma hizo ni majungu, lakini mahakama ndiyo itakayosema kama ni jungu au
sufuria.
Lakini kwa Zanzibar ninayoijua, labda ibadilike kama ilivyo kwa usiku na
mchana, hili suala litamalizikia hewani kama lile la kugunduliwa zaidi ya
wafanyakazi hewa 3,500 katika serikali miaka mitatu iliyopita.
Kikwazo kikubwa kilichopo ni utamaduni wa kulindanana na kuwaonea muhali watu
wanaosemekana wamewiba fedha za umma na kuharibu mali za serikali.
Mafisadi huonewa huruma kama vile wameiba kwa bahati mbaya na rungu la dola
siku zote huwaaangukia wanaoiba embe, ndizi, chapati na mandazi au kutoa kauli
za kisiasa, kama juu ya Muungano, zisiowafurahisha wakubwa.
Tuliwahi kuambiwa katika miezi ya mwisho ya utawala wa Rais Amani Abeid
Karume kuwa Zanzibar haina mafisadi na kwamba viongozi wake ni wasafi na sasa
tunaendelea kuuona usafi huo wa viongozi!
Ukweli ni kuwa ufisadi unanuka Visiwani na kama maelezo yaliyotolewa na
Kamati ya Baraza la Wawakilishi yana ukweli basi ufisadi uliopo unatisha.
Tusijidanganye na kutaka kuwafanya malaika viongozi wetu na watumishi wa
ngazi za juu wa serikali. Wapo miongoni mwao ambao ni wezi wakubwa na
wabadhirifu na haifai kuwafumbia macho wala kuwazibia masikio.
Tuache kulindana kwa mambo maovu kwani watu wazuri ni wale wanaolindana kwa
mema na si uchafu. Mwenendo huu wa kuwalinda mafisadi utaiponza Zanzibar.
Ukiangalia matokeo kama ya wakubwa kudaiwa kupora mali, ardhi na mashamba ya
watu na hata kuua, japokuwa si kwa makusudi, utaona wanakingiwa kifua na
kulindwa.
Kwa bahati mbaya waandishi wa habari wanaofichua haya kwa kuwapa nafasi ya
kusikika wale wanaodai kudhulumiwa huandamwa kama wao ni wahalifu na hata
kuhatarishiwa maisha yao.
Sasa waandishi wa habari wamekaa pembeni na kupumua huku wakiiangalia kwa
masikitiko Zanzibar inakwenda mrama na badala yake wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi wapo mbele kufichua ufisadi.
Sijui kwa uoza huu ulioanikwa katika Baraza la Wawakilishi serikali itasemaje
au itachukua hatua gani kwa wanaotuhumiwa au vyama vyao vitaambiwa
wawashughulikie wawakilishi wao walioweka mambo hadharani.
Tunasubiri kitakachotokea na wakati ndio utatupa jawabu. Maskini Zanzibar. Au
sasa ndiyo tuseme Zanzibar ni njema, atakaye aibe?
Chanzo: Tanzania Daima