Monday 31 December 2012

Ghana yapiga marufuku majokofu mitumba

Serikali ya Ghana imepiga marufuku uagizaji wa majokofu yaliyotumika au mitumba ili kupunguza matumizi ya nishati na uchafuzi wa mazingara.
Majokofu mengi kukuu yana kemikali inayoitwa Chlorofluorocarbons (CFCs) inayoharibu mazingiria.
Licha ya kuwa bidhaa hizo zimepigwa marufuku, na hazitengenezwi tena, majokofu hayo yanaaminika kutumika barani Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Nishati ya Ghana ameimbia BBC kuwa marufuku hiyo, imelifanya taifa lao kuwa kielelezo katika kanda ya Afrika Magharibi.
Sheria ya kupiga marufuku majokofu hayo iliidhinishwa mwaka wa 2008, lakini muda wake uliongezwa ili kuwa na wauzaji wa bidhaa hizo kufanya marekebisho.
Hata hivyo wafanyabiashara kadha nchini Ghana wameshutumu uamuzi huo wa serikali wakisema idadi kubwa ya watu watakosa kazi.
Afisa mkuu wa tume hiyo ya nishati Alfred Ofosu-Ahenkora amesema majokofu hayo ya mitumba yanaharibu taifa hilo kwa sababu hayakutengenezwa kutumika barani Afrika na pia yanatumia kiasi kikubwa cha umeme.

Sababu ya kuyapiga marufuku

Tume hiyo imesema zaidi ya majokofu milioni mbili zilizoagizwa kutoka ng'ambo hususan kutoka mataifa ya Ulaya.
Kemikali za CFCs zimepigwa marufuku kwa mujibu wa azimio lililotiwa saini mjini Montreal Canada, kuzuia kemikali zinazoharibu tabaka la hewa ya Ozone.
Ili kuhimiza raia wa nchi hiyo kutotumia majokofu hayo, serikali imetoa ruzuku kwa kuwapa majokofu mapya wanaorudisha ya zamani.
Mwandishi wa BBC mjini Accra anasema, sio raia wengi wa taifa hilo wanaweza kumudu gharama ya jokofu jipya, kwa hivyo mahitaji ya majokofu ya mitumba yamekuwa makubwa, katika maduka yanayouza bidhaa hiyo katika mji mkuu wa nchi hiyo.
'' Tutapoteza kazi yetu mwaka ujao, hii ndio biashara inayotupa sisi fedha za kulisha familia zetu'' alisema mmoja wa wafanyabiashara Albert Kwasi Breku.
Lakini Bwana Ofosu-Ahenkora amesema suluhisho la kudumu ni kuanzisha kiwanda cha kutengeneza majokofu nchini humo.
'' Suala la kufunga biashara za watu sio wazo zuri, ila serikali ingeliimarisha kwa kuanzisha viwanda zaidi na nadhani hilo litasaidia kubuni nafasi zaidi za kazi, badala ya kuagiza majokofu ya mitumba'' alisema Ahenkora.
Tangu kemikali ya CFCs, kupigwa marufuku, kampuni nyingi za kutengeneza majokofu zimekuwa zikitumia ina mpya inayoitwa Hydrofluorocarbons (HFCs).
Lakini mwaka uliopita ripoti ya Umoja wa Mataifa ilisema kuwa majokofu yanayotumia mfumo huo mpya wa HFCs yanatoa hewa ya sumu zaidi ambayo ni asilimia ishirini hatari zaidi kuliko hewa ya Carbon Monoxide au CO2, na hivyo matumizi ya teknolojia hiyo huenda yakaathiri mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Taifa la Ghana katika miaka ya hivi karibuni limekuwa kivutio cha mabaki ya viwanda vya kompyuta na televisheni kutoka mataifa ya Magharibi, na nyingi kati ya mabaki hayo yana sumu.
Chanzo: BBC

Wednesday 26 December 2012

Jinsi watawala wanavyowatumia wasomi wetu

Barazani kwa Ahmed Rajab
TAKRIBAN nchi zote za Kiafrika zimeshuhudia jinsi baadhi ya raia wake walivyojilimbikizia utajiri mkubwa na fedha nyingi mno wakiwa katika vivuli vya utawala. Baadhi yao ni watawala wenyewe.
Wengine wanawatumia hao watawala au mfumo uliopo wa utawala kujipatia mali hizo. Mara zote njia wanazozitumia huwa si za halali.
Hali hiyo haikuanza leo wala jana barani Afrika. Ibn Khaldun aliyefariki dunia 1406 aliyaona hayo zama zake. Bwana huyo alizaliwa Tunis na mababu zake walitokea Hadhramaut, Yemen Kusini.
Miongoni mwa fani alizosomea utotoni mwake ni isimu ya lugha ya Kiarabu, hisabati, mantiki na falsafa. Aliandika kitabu chake cha mwanzo akiwa na umri wa miaka 19. Ibn Khaldun anatambuliwa kuwa ndiye baba wa uandishi wa historia, wa elimu-jamii (sosiolojia) na wa sayansi ya uchumi.
Baada ya kuipata taalimu yote aliyojaaliwa kuipata Ibn Khaldun alifanya kazi serikalini akishika nyadhifa kadhaa za kisiasa pamoja na uwaziri. Wakati mmoja alikorofishana na mtawala Ibn Amar Abdullah na akaamua kuhama Tunis na kwenda Granada, Hispania, ambako alishika nyadhifa kubwa kubwa chini ya Sultan Muhammed wa tano. Siku hizo Hispania ilikuwa dola ya Kiislamu. Baadaye Sultani alimrejesha kwao Ibn Khaldun baada ya kuzuka uhasama baina ya waziri wake mmoja na Ibn Khaldun.
Aliporudi Afrika Ibn Khaldun alikaribishwa kwa mikono miwili na mtawala na akateuliwa waziri mkuu. Kutokana na muda wake mrefu katika duru za watawala Ibn Khaldun aliona mengi. Moja aliloliona na kulitaja ni kwamba ufisadi na udikteta ni pacha.
Na si lazima pawepo ufisadi wa kupora mali. Wanachofanya madikteta wengine — na huo pia ni aina ya ufisadi — ni kuwatunukia akina ‘hewalla bwana’ vyeo vikubwa wasivyostahili na mishahara minene au manufaa na marupurupu mengine.
Wanapoonyesha dalili ya kwenda kinyume na mtawala au hata pale mtawala anapokuwa na shaka nao basi vibarakala akina ‘hewalla bwana’ hupokonywa ulwa waliotunukiwa.
Katika mfumo huo mtawala analazimika kila mara kuwa na kitu cha kuwapa vibarakala au hata kuwapokonya walicho nacho ili hao watawala waweze kuidhibiti dunia yao.
Ufisadi wa aina hiyo hutokea hata katika nchi za kidemokarasia. Hivyo, si ajabu kwamba ufisadi wa aina zote umekithiri katika nchi zetu tangu wimbi la demokrasia lianze kung’uruma barani Afrika. Hii leo takriban kila nchi inaiigiza kivyake dhana hiyo.
Juu ya hayo si nyingi ya nchi za Kiafrika zilizo na mfumo wa demokrasia iliyokomaa. Nchi nyingine zimekuwa zikijitia tu katika mkumbo wa demokrasia kwa vile zilikuwa hazina hila ila kujifanya kuukubali mfumo huo. Ziliukubali shingo upande mfumo huo kutokana na mashinikizo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Kuna wenye kuipima demokrasia kwa kigezo cha uchaguzi lakini hicho ni kigezo kimoja tu. Tena kina mushkili wake kwani hata hicho kinatakiwa kiwe na sifa fulani. Kati ya sifa hizo ni kwamba uchaguzi uwe huru, wa haki, uliofanywa kwa uwazi kabisa na uwe wa kuaminika na wenye matokeo yasiokanika.
Ikiwa tutakitumia kigezo hicho cha uchaguzi na sifa hizo tulizozitaja basi ni nchi chache za Kiafrika zinazostahiki kuitwa za demokrasia halisi.
Katika miaka toka ya 1960 hadi 1990 mtindo uliokuwapo ni kwa serikali za Kiafrika kubadilishwa kwa njia ya mapinduzi ambayo mara nyingi yaliwaua viongozi. Baada ya muda walioua nao pia wakiuawa kwani kulikuwa hakuna mfumo mbadala wa kubadilishana madaraka.
Mtindo huo wa kupinduana haukuwa ukiendeshwa na wanakwaya wa kanisani. Ulikuwa ni mfumo wa kikatili ulioendeshwa na makatili.
Mtindo huo uligeuka na kuwa kama mila ya Afrika. ‘Udikteta wa Kiafrika’ ukawa unatumia mantiki ya kikatili na ya umwagaji damu. Lakini kila pale demokrasia ilipotia mizizi medani huwa si tena uwanja wa kunyakua madaraka.
Siku hizi kwingi Afrika madaraka hupatikana kwa yaliyomo kwenye madebe au visanduku vya kura na si kwa mtutu wa bunduki. Na Afrika hatuna upungufu wa visanduku vya kura. Taksiri iliyopo ni kwamba visanduku hivyo huwa ama vimekwishajazwa kura kabla ya wapiga kura kutumbukiza kura zao au hujazwa baadaye kwa kura za bandia. Hapo ndipo penye tatizo. Hapo ndipo tunapoweza kutofautisha baina ya demokrasia halisi na ile ya shaghalabaghala.
Kwa hivyo haitoshi nchi kujinata kwamba inafuata demokrasia. Katiba za nchi nyingi za Kiafrika zinasema kwamba zinaufuata mfumo huo. Lakini katika nchi hizo kuna pengo kubwa baina ya nadharia na vitendo, baina ya kilichomo ndani ya katiba na kinachotendwa na serikali na wakubwa wake.
Katika nyingi ya nchi za Kiafrika demokrasia imegeuzwa na kuwa tamthilia. Na sisi raia tumekuwa waigizaji wa tamthilia ya kidemokrasi. Watawala wetu ni wasanii mahiri. Wametuwekea majukwaa na yote yanayohitajika katika majukwaa hayo pamoja na maneno yote ya Kimagharibi yanayohitajika katika tamthilia hiyo pamoja na wahka na hali ya mshawasha inayozuka wakati wa kuhisabiwa kura.
Sisi tumezoea kuhamaki magazeti ya nchi za Magharibi yanapozielezea chaguzi zetu kuwa kama soko linalofunguliwa katika vipindi maalumu aghalabu vya miaka mitano mitano.
Pengine magazeti hayo yanasema kweli kwani chaguzi katika baadhi ya nchi zetu ni mzaha na viongozi wetu ni machale. Wakati mwingine chaguzi zetu zinakuwa mithili ya dansi kubwa ya vinyago. Ngoma inapomalizika visanduku vya kura hujazwa kura ambazo hakuna aliyezipiga.
Katika nchi zinazofanya uchaguzi wa bandia serikali huwa na uwezo wa kuwakashifu wasomi kwa kuwafanya wayakubali matokeo ya uchaguzi na hata kuwafanya wayathibitishe hadharani matokeo hayo. Hivyo wasomi hao hulainishwa laisa kiasi. Makali yao ya kuusema ukweli yanazimuliwa, wanageuzwa vibarakala na inapohitajika huhongwa marupurupu ya utawala
Chanzo: Raia Mwema

Saturday 22 December 2012

Wazanzibari tunayajuwa haya???


The Partnership
Na Aboud Jumbe
"Njia haikuwa rahisi na siku zote iliibuka ile shaka ya Zanzibar kumezwa na Tanganyika kwa kupitia Muungano huo. Kama vile Mwalimu alivyoonesha katika hotuba yake ya Sherehe za miaka 10 ya Muungano kuwa watu walikuwa na wasiwasi na "nchi ndogo kama Zanzibar kumezwa na nchi kubwa kama Tanganyika". Khofu hii haikuwa kwa watu wa Zanzibar tu. Kwa wafuatiliaji wengi hali hii ya zimwi kushirikiana na kibushuti kumeifanya dunia siku zote ikae ikisubiri ni kipi kitatokea. Picha inayoonekana ukitizama kipindi cha miaka thelathini ya Muungano huu ni ya kutisha. Inatia mashaka na masuali juu ya yale madhumuni halisi ya Muungano huu huku kukiwa kuna dalili za wazi za kukimbia matakwa ya Mkataba wa Muungano.

Inaweza kuwa jambo jema iwapo tutajiuliza: Kwa nini hapo 1963 nchi za Afrika Mashariki zilikuwa zimejifunga kukubali kuunda Shirikisho zikashindwa kujiunga na Muungano wa Tanzania? Hakuna moja iliyofanya hivyo. Jee, hii ni kutokana na mtiririko wa matukio kuanzia Aprili, 1964 kushindwa mbali ya kudhihirisha khofu ya kumezwa.
Ingefaa hapa nitaje kuwa miezi minne tu baada ya Muungano, marehemu Jomo Kenyatta alinukuliwa na gazeti la Times of London hapo Agosti 3, 1964 akisema hayuko tayari kumpigia magoti Nyerere na Tanganyika. Kitu gani basi kilichomfanya Kenyatta akatae kabisa Muungano ikiwa ni mwaka mmoja tu tokea atoe tamko la kuwa tayari kushirikiana na Obote na Nyerere? Historia imekuwa shahidi upande wake. Jee, hilo ndilo lililokuwa tukilifanya wakati wote?"

Hayo si maneno yangu. Ni maneno ya Sheikh Aboud Jumbe, aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alikuwa pia Katibu Mipango wa ASP na baadaye Rais wa ASP. Huyu si HIZBU na sidhani kama anaweza kutuhumiwa kuwa mpinga Mapinduzi au anataka kurudisha Usultani Zanzibar. Hizo ndizo tafakuri zake.

Langu mimi ni moja tu ninalotaka kuongeza. Nalo ni kwamba aina pekee ya Muungano itakayoondoa khofu ya nchi moja kumezwa na nyingine ni ile ambayo kila nchi shiriki itabaki na mamlaka yake kamili kitaifa na kimataifa na kisha kushirikiana kupitia Muungano wa Mkataba (Treaty based Union). Hivyo ndivyo ulivyo Muungano wa Ulaya (European Union) ambao umeendelea kukua na kufikia kuwa na nchi shiriki 27 na ambao mwaka huu umepewa tuzo ya Nobel. Insha'Allah hiyo ndiyo njia ya kufuatwa katika kujenga mahusiano mapya kati ya Tanganyika na Zanzibar yatakayovutia na nchi nyingine kujiunga na kuondoa khofu kama zile za Jomo Kenyatta alizozitoa Agosti 3, 1964.

Friday 21 December 2012

‘Katiba inayoandaliwa ni ya watawala’

JUKWAA la Katiba limesisitiza kuwa Katiba mpya haiwezi kupatikana Aprili 26, 2014 na endapo itafanyika hivyo litazunguka nchi nzima kuhamasisha wananchi kuikataa rasimu ya Katiba hiyo kwa njia ya kura.
Jukwaa hilo limesema litafikia hatua hiyo kwa kuwa Katiba itakayopatikana itakuwa ni ya watawala kwa kuwa wananchi wengi hawajapata fursa ya kutoa maoni yao.
Kauli hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deus Kibamba, alipozungumza na waandishi wa habari alipokuwa akitoa tathmini ya mchakato wa Katiba kwa mzunguko kwa kwanza.
Alisema endapo nchi inahitaji Katiba ya demokrasia haiwezi kupatikana ndani ya kipindi hicho na kumuonya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji mstafuu, Joseph Warioba, na wenzake kulitilia maanani suala hilo.
“Dharura imewahi kuligharimu taifa letu na katika nchi nyingine kushindwa kufanya maandalizi kunaweza kusababisha machafuko kwa kutokamilika kwa Katiba mpya huku muafaka ukiwa umeshuka na jamii kutokubaliana kwa mambo mengi ya msingi.”
Pamoja na hayo, jukwaa hilo limetoa hati chafu kwa wakuu wa wilaya wawili, Rosemary Kirigini (Meatu) na Jokiwa Kasunga (Monduli), kwa madai kuwa ni maadui wa mchakato wa Katiba kwa mwaka 2012.
Alisema Kirigini alizuia kumfanyika mkutano wa Katiba ulioandaliwa na asasi ya kiraia ya Mongonet akitaka wasijadili masuala ya Katiba bali mambo mengine wakati Kasunga alizuia mikutano ya uhamasishaji uliokuwa ukifanywa na taasisi ya Pingo’s Forum ambayo ilikuwa na lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya mchakato wa Katiba mpya kwa madai ya kutaka taarifa zaidi za taasisi hiyo kabla ya kuruhusu kufaya kazi katika wilaya yake.
“Kutokana na ukubwa wa makosa yaliyofanywa na wakuu hawa wa wilaya na hatari yake katika kufifisha mchakato wa Katiba, Jukwaa la Katiba leo tunatoa hatia maalumu kwa viongozi hawa kama ishara ya kuwatangaza kuwa maadui wa Katiba mpya. Utaratibu huu utaendelea katika muda wote wa uundaji wa Katiba mpya hadi kukamilika,” alisema Kibamba na kuongeza nakala za hati hizo zitapelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete.
Alisema kwa mwaka ujao wanatarajiwa kuwapeleka watu wa aina hiyo mahakamani kwa kuwa wanavunja Katiba ibara ya 18.
Akielezea dosari zilizojitokeza katika mzunguko wanne na wa mwisho wa awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni ya Katiba ni fursa finyu ya utoaji maoni kwa wananachi.
“Jukwaa la Katiba Tanzania tulishuhudia watu wakijitokeza kwa wingi huku muda uliotengwa ukiendelea kuwa mdogo kwa idadi ya watu wengi waliojitokeza katika mzunguko huu.
“Watazamaji wetu walishuhudia wananchi wakishauriwa kutoa maoni yao kwa njia ya maandishi kwa kuwa wengi wao walikosa fursa ya kuzungumza katika mikutano ya tume,” alisema na kutoa mfano suala hilo limejitokeza eneo la Segerea na Temeke, kata ya Pemba Mnazi.
Alisema suala hilo liliwakatisha tamaa watu wasiojua kusoma na kuandika, ni kinyume na lengo kuwa Katiba itaandikwa na Watanzania wote hata kama hawawezi kusoma wala kuandika.
Aidha alisema wakati mwingine tume ilionekana kuwa na haraka ya kuondoka kutokana na muda waliopangiwa kuwa finyu na walikuwa wakiwahi mikutano mingine.
Alieleza kuwa dosari nyingine waliyoibaini ni kwa vyama kuendelea kuingilia mchakato wa Katiba, jambo linalosababisha kutokea kwa fujo kwa wafuasi kupigana na kutolea mfano vurugu zilizotokea Zanzibar.
Kutokana na hali hiyo, jukwaa hilo limeshauri kuwapo na majadiliano aina ya taifa tunalohitaji kulijenga ikiwa ni pamoja na kukubaliana mipaka ya Katiba tunayoiunda.
“Tujadiliane kwanza tunaunda Katiba ya Muungano? Kama ndiyo tunataka Muungano wa aina gani wa serikali mbili, tatu au wa mkataba,” alisema.
Aidha wanapendekeza mchakato wa Katiba mpya lazima utenganishwe na michakato ya uchaguzi ujao, kwani kuna hatari ya mchakato mmojawapo kuvurugwa.
“Hii itatoa fursa kwa mchakato wa Katiba mpya kuendelea taratibu na bila kuhitaji kukimbizwa hata kama utahitajika kuendelea mpaka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,” alisema.
Aidha alisema jukwaa hilo litaendelea na kampeni ya kugawa Katiba ya sasa kwa kila Mtanzania na kwamba mpaka sasa kwa kushirikiana na asasi mbalimbali wameshasambaza nakala zaidi ya 300,000 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nakala 10,000 za Katiba ya Zanzibar.
Alisema katika mwaka ujao, jukwaa limejipanga kuendelea na kampeni ya kuongeza nakala za Katiba nukta nundu kwa ajili ya watu wasioona
Chanzo: Tanzania Daima

Thursday 20 December 2012

Kama Chávez ameweza kwa nini wakwetu hawawezi?


Barazani kwa Ahmed Rajab
SIMON Bolivar alikuwa mwanamapinduzi wa Venezuela aliyeiaga dunia Desemba 17, mwaka 1830 akiwa na umri wa miaka 47. Kuna wanaoamini kwamba alikufa kwa kulishwa sumu. Miongoni mwao ni Hugo Chávez, Rais wa Venezuela, ambaye kwa sasa anatibiwa Cuba baada ya kupasuliwa kwa ugonjwa wa saratani.
Oktoba 7, mwaka huu, Chávez kwa mara ya nne alishinda uchaguzi wa urais. Alishinda licha ya ule msaada wa dola zisizopungua milioni 50 ambazo inasemekana Marekani mwaka huu iliwapa wapinzani wake wamshinde.
Lakini yeye ndiye aliyewatwanga na katika uchaguzi wa magavana uliofanywa Jumapili iliyopita chama chake cha Kisoshalisti kiliongeza idadi ya viti vya magavana ilivyoshinda.
Januari, kama atakuwa mzima, Chávez ataapishwa kwa muhula mwingine wa urais wa miaka sita.Chávez anaona fahari kujinasibisha kuwa ni mrithi wa dhati wa Bolivar.Tangu ashike madaraka miaka 13 iliyopita hachoki kukumbusha kwamba siasa zake za ‘Chavismo’ zinalenga kuyatekeleza mapinduzi ya kibolivar.
Vyombo vya habari vya Marekani na vya vibaraka wake vimezoea kumfanyia tashtishi na kumcheza shere Chávez vikimfananisha na bahaluli au Juha Kalulu.Hayo si ya ajabu kwani ni kawaida yao kumkebehi kila kiongozi wa wanyonge anayethubutu kusimama kidete na kwenda kinyume cha ubepari wa utandawazi.
Kwa hakika, Chávez alianza kufanyiwa vitimbwi alipotangaza mara ya mwanzo kwamba atawania urais 1998. Alisema anataka kuijenga upya nchi yake kwa misingi mipya. Wengi walimcheka.
Kwa mtizamo wao katika mwanzo wa karne ya 21 Chávez alikuwa mtu mwenye fikra za kizamani zilizopitwa na wakati. Alikuwa mwanamapinduzi wa mrengo wa kushoto aliyekuwa akiungwa mkono na Wakomunisti wachache waliobaki nchini mwake na makundi kama sita ya mielekeo mbalimbali ya kisoshalisti.
Nadhani Tanzania hii leo akisimama mtu na kusema anataka kuurejesha ujamaa ataonekana mwehu — hata akisema kama ujamaa anaoutaka ni wa aina mpya. Itakuwa hivyo kwa sababu wengi wetu tuna fikra finyu na tumezoea kuyumbishwa na wimbi litokalo nchi za kimagharibi.
Cháveza na mbwembwe za aina yake.Pia ana mtindo wa aina yake wa uongozi ulio na dosari zake lakini wenye kumpa haiba kubwa. Si watu wote wenye kumpenda. Maadui zake wanasema ulimi wake hauna akili. Hauna ubongo.
La muhimu ni kwamba yeye ni miongoni mwa viongozi wachache wa dunia hii wenye kuwajali watu wao. Ni kiongozi ambaye Bara la Afrika halikujaaliwa kumpata. Inasemekana kwamba nchi yake ni ya tano, ikiwa pamoja na Finland, yenye wakaazi wenye furaha mno duniani. Hayo si mafanikio madogo.
Chávez ameweza kuupunguza ufukara kwa hatua mbili muhimu: ya kwanza ni kulitaifisha Shirika la Taifa la Mafuta la Petróleos de Venezuela (PDVSA) na ya pili ni kuugawa kwa haki utajiri wataifa na sio kuwanufaisha wachache tu katika jamii. Umasikini umeporomoka kutoka asilimia 70.8 katika 1996 na sasa ni chini ya asimilia 21.
Ufukara wakutupwa umepungua kutoka asilimia 40 katika 1996 na kufikia sasa kasoro ya asilimia saba. Mwaka 1990 asilimia 7.7 ya watoto walikuwa wakifa kutoka na utapiamlo lakini sasa takwimu hiyo imeshuka na kuwa asilimia 2.9.
Tangu Chávez awe rais idadi ya wasio na ajira imepungua kutoka asilimia 11.3 na kuwa asilimia 7.7. Katika kipindi cha miaka 10 uchumi wa Venezuela umetanuka kwa asilimia 47.7 na leo uchumi huo ni madhubuti kushinda uchumi wa Marekani na nchi kadhaa za Ulaya.
Kuna mafanikio mengine ambayo Venezuela imeyapata ikiongozwa na Chávez. Wazee zaidi ya milioni mbili na laki moja wanalipwa malipo ya uzeeni na idadi hiyo inazidi kuongezeka. Kabla ya Chavez watu 387,000 tu ndio waliokuwa wakilipwa malipo hayo.
Elimu ni bure kutoka ya chekechea hadi ya chuo kikuu. Wananchi milioni tano wanalishwa bure na serikali. Venezuela haina watoto masikini wa mitaani au chokora kama wanavyoitwa Kenya. Dawa zinapatikana kwa bei rahisi. Venezuela pia ina maduka mahsusi yenye kuwauzia watu wa chini vyakula na vitu vingine kwa bei za chini.
Swali la kujiuliza ni: Ilikuwaje Venezuela chini ya Chávez ikaweza kupiga hatua kubwa hivyo katika muda mfupi?
Huenda ukajibu kwamba nchi hiyo inachimba na kusafirisha mafuta na hivyo inajipatia mapato makubwa. Lakini Afrika ya Kusini, Algeria, Angola, Chad, Cameroon, Congo-Brazzaville, Congo-Kinshasa, Cote d’ Ivoire, Equatorial Guinea, Gabon, Ghana, Misri, Morocco, Nigeria, Tunisia, Sudan na Sudan ya Kusini zote hizo zinachimba au zinachimba na kuuza mafuta lakini wengi wa watu wa nchi hizo wanaishi maisha ya dhiki na usumbufu mkubwa.
Alipoingia Ikulu mara ya kwanza 1998, Chávez aliingia akiwa na kikapu cha ahadi akilini mwake. Aliahidi kwamba ataufyeka ufisadi uliokuwa ukiila nchi yake kama unavyoila Tanzania.
Aliahidi kwamba atakuwa na sera mbadala kwa nchi yake, sera ambayo itajitenga kabisa na ile ya uchumi wa kiliberali mamboleo iliyokuwa ikifuatwa nchini humo na ambayo sisi Tanzania na kwingineko Afrika tumeing’ang’ania.
Badala ya kutegemea zile ziitwazo ‘nguvu za soko’ na utandawazi serikali yake ikaanza kupanga maendeleo ya nchi kwa kutumia rasilimali zake na sio kwa kuwategemea wawekezaji. Kadhalika, Chávez alizivunja nguvu Shirika la Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na Benki Kuu ya Dunia katika uendeshaji wa uchumi wa nchi yake.
Alichofanya ni kuthibitisha kwamba kuna sera mbadala za kiuchumi zinazoweza kufuatwa na nchi kama zetu badala ya hizi tunazozikumbatia.
Jengine alilolifanya Chávez ni kuwa macho na kutoipa Marekani nafasi ya kuichezea nchi yake kinyume cha wafanyavyo viongozi wetu. Kwa mfano, amekataa kuziruhusu ndege za Marekani kuingia katika anga ya Venezuela kwa kisingizio cha kuwafukuzia wenye kufanya biashara haramu ya mihadarati. Viongozi wetu wanaipa Marekani fursa hiyo kwa kisingizio cha kuwafukuzia magaidi
Chanzo: raia Mwema

Thursday 13 December 2012

Jinsi Nyerere alivyotawala kimabavu

Barazani kwa Ahmed Rajab
KITU kimoja mataifa ya Magharibi yanachojivunia ni Sheria ya Haki za Binadamu (Bill of Rights). Mataifa hayo na mengine yenye kujigamba kwamba ni ya kidemokrasia halisi yameiingiza sheria hiyo katika katiba zao.
Walimwengu kwa jumla huipigania na kuitetea sheria hiyo kwa sababu wengi wao wanataka tuwe na dunia yenye kuwahakikishia binadamu wote kwamba wataishi maisha ya heshima, ya utu, yenye kuwafanya binadamu wote wawe sawa mbele ya sheria na yenye kuwapa wote uhuru.
Sheria ya Haki za Binadamu ni msingi muhimu wa mfumo wa kidemokrasia na utawala bora. Ndiyo maana tunawaona wanasiasa wengi, walio wema na hata wasio wema, wakiipigia debe sheria hiyo.
Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar zote zinaielezea kwa makini Sheria ya Haki za Binadamu. Katiba zote mbili zilifanyiwa marekebisho mwaka 1984 ili iingizwe hiyo Sheria ya Haki za Binadamu katika kila moja ya katiba hizo.
Wakati wa uhuru mwaka 1961 Tanganyika haikuwa na Sheria ya Haki za Binadamu katika katiba yake. Zanzibar, kwa upande mwingine, iliwahi kuwa na mlango mzima wa Sheria ya Haki za Binadamu katika katiba yake ya uhuru ya mwaka 1963. Katiba hiyo ilifutwa baada ya Mapinduzi ya 1964 na Zanzibar ilipoungana na Tanganyika ikawa inaitumia katiba ya Muungano ambayo kama nilivyogusia haikuwa na Sheria ya Haki za Binadamu.
Tanzania iliiingiza Sheria ya Haki za Binadamu katika katiba yake miaka miwili baada ya viongozi wa nchi za Kiafrika kukutana jijini Nairobi na kuuidhinisha Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu (ACHPR) na pia kuunda Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu yenye makao yake makuu mjini Banjul, Gambia.
Kuna sababu ya kwa nini Tanganyika (na baadaye Tanzania) haikuwa na Sheria ya Haki za Binadamu katika katiba yake. Kwa hakika, Mwalimu Julius Nyerere na wenzake waliokuwa wakipigania uhuru wa Tanganyika hawakutaka kwa makusudi kuliingiza suala hilo katika katiba ya Tanganyika huru.
Kisingizio walichotoa akina Nyerere ni kuwa wakichelea majaji wa kikoloni ambao ndio siku hizo wakisimamia mahakama kwamba huenda wakavitumia vifungu vya Sheria ya Haki za Binadamu ili kuzisambaratisha jitihada za serikali mpya ya wazalendo za kuupatia umma maendeleo ya haraka ya kiuchumi.
Nyerere alikataa katukatu kwamba katiba ya Tanganyika ya wakati wa uhuru iwe na Sheria ya Haki za Binadamu. Alifanya ukaidi huohuo wakati katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ilipokuwa inaandaliwa mwaka 1962. Hivyo, katiba zote hizo mbili zilimwezesha Nyerere aitawale nchi kwa mabavu kama walivyofanya wakoloni wa Kiingereza kabla yake.
Taifa jipya la Tanganyika lilifungua macho likijikuta limezirithi sheria za kimabavu. La kusikitisha ni kwamba Nyerere hakufanya jitihada yoyote ya kuzifuta sheria hizo na kuweka sheria zenye kuheshimu haki za binadamu.
Kwa hili Nyerere na Tanganyika hawakuwa peke yao barani Afrika. Nchi nyingi nyingine za Kiafrika zilikuwa na utawala uliojengeka juu ya misingi ya kimabavu na isiyoheshimu haki za binadamu.
Sheria ya Haki za Binadamu iliyoingizwa kwenye Katiba ya Muungano mwaka 1984 ilikuwa isitumike katika mahakama ya kisheria kwa muda wa miaka mitatu ili kuipa Serikali ya Muungano muda wa kutosha wa kuzifuta au kuzibadili sheria zake zote zenye kwenda kinyume na Haki za Binadamu. Hata hivyo, hatua hiyo haikuisaidia Serikali ya Muungano kuzibatilisha sheria zake zote za kimabavu.
Sidhani kama ninakosea nikisema kwamba Tanzania ilikubali kichwa upande kuiingiza Sheria ya Haki za Binadamu katika katiba yake. Nasema hivi kwa sababu ingawa Sheria ya Haki za Binadamu imo ndani ya katiba za Muungano na Zanzibar bado kuna mushkili mkubwa katika utakelezwaji wake. Inavyoonyesha ni kwamba serikali imefanya kusudi iwe ngumu kwa watu binafsi kuzitetea haki zao za kimsingi katika mahakama.
Jingine ni kwamba ingawa katiba zote hizo mbili zinazitambua takriban haki zote za kiraia na za kisiasa hata hivyo kuna nyakati ambapo wananchi wanapata taabu kuzipata au wanazuiwa wasizipate haki zao. Mfano mzuri ni haki ya wananchi ya kuwa na uhuru wa kukusanyika au wa kuandamana wakati wanapotaka. Hizi ni haki za kimsingi za binadamu na uhalali wake si lazima upatikane kwa haki hizo kutajwa ndani ya katiba.
Kwa hali ilivyo Bara na Visiwani haki hizo za kukusanyika na kuandamana zinautegemea sana ukarimu wa Polisi. Wao ndio wenye kutoa kibali cha kufanyika mkutano wa hadhara au maandamano. Wakati wa maandamano Polisi wanatakiwa wawe wanasimamia usalama na amani na si wao kuanza kuichafua amani.
Kesi inayoendelea sasa Zanzibar ya washukiwa wa Uamsho imezidi kufichua jinsi serikali ya huko inavyoikiuka Sheria ya Haki za Binadamu licha ya kuwa imo ndani ya katiba zote mbili, ya Muungano na ya Zanzibar.
Sheria ya Haki za Binadamu inasema kesi ziwe zinaendeshwa kwa haraka. Lakini tukiiangalia hii kesi ya Uamsho tunaona kwamba mahakama yanasotasota katika kuiendesha.
Zaidi ni kwamba washtakiwa ingawa ni watuhumiwa na hawajapatikana na hatia hadi sasa wanatendewa mambo kana kwamba wamekwishapatikana na hatia. Wananyimwa haki zao za kimsingi wakiwa korokoroni na wanafanyiwa mambo ya kuudhalilisha utu wao. Na Bara kuna kesi chungu nzima ambazo kwa miaka mingi baada ya kufunguliwa bado hazijasikilizwa.
Swali la kujiuliza ni: Nani wa kulaumiwa pale wakubwa wa serikali wanapoukiuka huo msingi wa demokrasia halisi? Tumezoea kuwatupia lawama wakubwa wa serikali. Lakini wapo wengine ambao pia wanastahiki kuibeba. Nao ni umma, tukiwemo mimi na wewe.
Umma usiojali serikali inafanya nini au nini haifanyi inachopaswa kufanya ni umma uliopotoka na unaoweza kutiwa shemere na kubururwa kama kondoo na hao wakubwa wa serikali.
Tusitarajie kupewa haki zetu. Lazima wananchi sote tuzipiganie haki zetu zote zikiwa pamoja na zile za kutaka elimu, afya na ajira. Na hatutoweza kufanya hivyo mpaka tujipange. Tuunde jumuiya za kupigania haki zetu, tushurutishe somo la Sheria ya Haki za Binadamu lifundishwe katika maskuli hadi vyuo vikuu. Lengo liwe kuhakikisha kwamba wananchi tusiwe na uwezo wa kusema tu bali pia tuwe na uwezo wa kuamua. Hiyo ndiyo nguvu ya Umma.
Chanzo: Raia Mwema

Tuesday 11 December 2012

Mkutano wa katiba Z’bar vurugu tupu

MIKUTANO ya kukusanya maoni ya upatikanaji wa Katiba Mpya Visiwani Zanzibar, imeingia dosari baada kuzuka ghasia na baadhi ya watu kujeruhiwa kwa kuchomwa visu.

Vurugu hizo ambazo chanzo chake ni siasa, zilitokana na wafuasi wa baadhi ya vyama vya siasa, kuvamia mikutano iliyokuwa ikifanyika Unguja na kusababisha hofu za kiusalama.

Baadhi ya maeneo ambayo wanasiasa hao walivamia mikutano ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kusababisha ivunjike ni Shehia za Magomeni na Mpendae Mkoa wa Mjini Magharibi.Hii ni mara ya kwanza ghasia kuzuka katika mikutano ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya visiwani humo.

Tukio la kuchomana visu, lilitokea katika Shehia ya Mpendae baada ya vurugu zilizosababishwa na vijana kuvamia mkutano uliokuwa ufanyike jana mchana.
Vijana hao walianzisha ghasia hizo baada ya kutaka kuvunja utaratibu uliokuwa umewekwa. Walitaka wakae mbele ya wengine waliokuwa wametangulia katika mkutano huo.

Hatua hiyo ilipingwa na kuibua ghasia ziliozababisha watu kadhaa kujeruhiwa kwa visu.

Tukio jingine lililovuruga mkutano huo ni lile lililotokea katika Shehia ya Magomeni, Jumatatu wiki hii baada ya kuibuka kwa mvutano baina ya makundi mawili yenye misimamo tofauti juu ya mfumo wa Muungano; kuna wanaopinga na wanaoukubali.
Misimamo hiyo imeelezwa kujikita katika misingi na sera za vyama vyao vya kisiasa.
Katika misimamo hiyo, CUF kinaamini katika Serikali ya Zanzibar na Tanganyika kila moja kuwa na mamlaka kamili na Muungano uwe wa mkataba wakati, CCM kinasimamia kwenye Serikali mbili; Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Shehia ya Magomeni
Saa mbili kabla mkutano kuanza, watu wengi walifika Uwanja wa Mzalendo ambako mkutano ulitakiwa kufanyika. Walijipanga kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Tume ambao ni aliyewahi kufika ndiye anayetangulia kutoa maoni.

Hali hiyo ilisababisha wakazi wa Shehia hiyo waliokuwa wenyeji wa mkutano, kukosa nafasi ambayo ingewawezesha kutoa maoni kwa mazungumzo ya ana kwa ana.
Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin, alisema hawakuwa tayari kuwa wenyeji wa mkutano ambao hawatashiriki akisema waliokuwa wamejipanga wote walifikishwa kituoni hapo kwa magari kwa lengo maalumu la kuwakosesha wenyeji kutoa maoni yao, kwa kuwa inafahamika kuwa wengi wao ni wana CCM.

Hoja hizo alizitoa kwa wajumbe wa Tume ambao pia hawakuridhishwa na hali ya usalama katika eneo hilo kutokana na vurugu zilizokuwa zikifanywa na wafuasi wa CCM na CUF.

“Kwa hali ilivyo, hatuwezi kupata utulivu utakaowezesha tufanye kazi kwa ufanisi na kumaliza mkutano kwa amani bila fujo. Natangaza rasmi kuwa leo hakuna mkutano,” Mwenyekiti wa Timu ya Tume hiyo inayokusanya maoni visiwani hapa, Profesa Mwesiga Baregu.

Akizungumza baada ya kuvunjika kwa mkutano huo, Salmin alisema waliokuwa wamefika kutoa maoni walikuwa wakitaka kunadi misimamo ya vyama vyao akisema hiyo ni hali ya kihistoria inayowakabili wakazi visiwani humo.
“Hata katika kupata huduma za kijamii, siasa inapewa kupaumbele na hili ndilo chimbuko la matatizo yote haya, ndiyo maana hata maoni yanayotolewa ni ya aina mbili, Muungano udumu au uwe wa mkataba na serikali mbili.

Dalili za vurugu
Dalili za kuwapo kwa vurugu zilianzia kwenye mkutano uliofanyika Jumatatu asubuhi kwenye Viwanja vya Kibanda Maiti katika Shehiya ya Kwa-Alamsha, ambako watu waliotaka Muungano ubaki, walizomewa huku waliotaka Serikali ya Zanzibar na Tanganyika kila moja ikiwa na mamlaka kamili, muungano uwe wa mkataba walishangiliwa.

Hali hiyo ilitawala mkutano huo bila kujali jitihada za Profesa Baregu kukemea mara kwa mara hali hiyo. Pamoja na kwamba maoni yatafanyiwa mchujo, Wananchi hao wanaamini kuwa upande utakaotoa maoni kwa wingi ndiyo utakaoshinda kwa matakwa yao kuingizwa kwenye Katiba Mpya.

Mbunge amshambulia Mratibu
Katika mkutano uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Wandarasi, Shehia ya Meya, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Faharia Shomari alimshambulia Mratibu wa shughuli za Tume visiwani humo, Ahmed Haji Saadat kwa maneno akiwambia:
“Mimi ni Mjumbe wa Tume ya Bunge ya Sheria na Katiba. Nilihusika kutunga sheria inayowaongoza kufanya kazi hii, inatakiwa wakazi wa shehia mnayofanyia mkutano watoe maoni kwa kuzungumza, wengine wapewe fomu; tatizo wewe unajidai mkubwa kuliko hata tume yenyewe. Mikutano yote umeivuruga wewe, tangu mwanzo nilikwambia, kiko wapi sasa,” alisema mbunge kwa hasira.

baada ya mashambulizi hayo, Saadat naye alijibu: “Mheshimiwa, ninakuheshimu sana, ikiwa tatizo unaliona ndani ya sheria na unakiri ulihusika kutunga sheria hiyo bila kueleza uzoefu ulionao kwa mazingira ya Zanzibar, wewe ni sehemu ya tatizo. Tangu nilipokuwa Mji Mkongwe umekuwa ukinifuata kwa maneno, tatizo lako hasa nini?”
Zogo hilo lilikuwa kubwa na kusababisha askari kumwondoa mbunge huyo kumpeleka pembeni. Lakini baada ya muda, mbunge huyo alijivuta mpaka alikokuwa Saadat na kuanza tena kumwandama kwa maneno akisema: “Kiko wapi? Jana hamkufanya mkutano kwa kujidai kwako, leo pia zogo hilo, huenda msiufanye kwa kujidai mkubwa lol, unajidai una nguvu kuliko hata wajumbe wa tume? Kiko wapi sasa?”
Maneno hayo yalimkera Mratibu huyo ambaye alimtaka athibitishe anayomtuhumu kwa maandishi.

Iliwalazimu askari polisi kuingilia kati tena kati na kumshauri Saadati kumfungulia mashtaka mbunge huyo.

Mbunge huyo alitoa maoni yake kwenye Jimbo la Mji Mkongwe, Vuga na kuhudhuria mkutano wa maoni uliyofanyika siku hiyo hiyo kwenye Hoteli ya Bwawani ambako inadaiwa kuwa ndiko alikoanza kuzozana na Saadat; akimtuhumu kupendelea wanaotaka muungano uwe wa mkataba na Serikali ya Zanzibar yenye mamlaka yake kamili.

Tuhuma hizo zilitokana na Saadat kukataa kuruhusu kundi la wanawake ambao Shomari alitaka wakatoe maoni tofauti na utaratibu uliowekwa ambao unampa nafasi aliyewahi kufika na kujipanga kwenye foleni kutoa maoni kwanza.

“Nimeishakuona unapendelea watu wa mkataba, subiri nitakuripoti kwa (mmoja wa wajumbe ambaye pia ni kada wa CCM),” Shomari alisikika akimweleza Saadat ambaye alimjibu kuwa kinachoangaliwa si nani wala itikadi gani, bali utaratibu uliowekwa tu
Chanzo: Mwananchi

Sunday 9 December 2012

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni sawa na ndoa ya mkeka’

MCHAKATO wa utoaji wa maoni ya Katiba Mpya unaendelea kwenye mikoa sita katika awamu hii ya nne. Mikoa ambayo Tume iko katika kuchukua maoni ya wananchi ni Arusha, Dar es Salaam, Mara, Simiyu, Geita pamoja na Zanzibar Mjini Magharibi. Katika mikutano hiyo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wananchi wamekuwa wakitoa maoni mengi yenye hoja tofauti.
Katika mikutano hiyo, wajumbe wa Tume wamekuwa wakiwahimiza wananchi kushiriki kwa uhuru katika kutoa maoni yao bila hofu. Wito huo wa Tume umekuwa ni jambo la msingi ikizingatiwa kwamba Watanzania wengi wamekuwa na tabia ya kuogopa na hata kukosa ujasiri wa kuzungumza hadharani kwa kuikosoa ama Serikali au viongozi wake kwa hofu ya kuogopa kukamatwa au kufuatiliwa na vyombo vya usalama.
Katika mchakato unaoendelea wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi, imeshuhudiwa wananchi hao wakijieleza kwa uhuru bila hofu kwenye mikutano mbalimbali ya Tume.
Hii ni haki yao ya kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kitu ambacho wananchi kwenye kila mkutano wa Tume wamekizungumzia ni suala la Muungano wa Serikali tatu.
Wananchi wengi wamekuwa wakisisitiza kuwa Katiba Mpya haina budi kuitambua na kuirejesha Serikali ya Tanganyika. Wananchi hao wamesema kuwa Serikali ya Tanganyika ni haki ya Watanganyika kama ilivyo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Watanganyika tumekosa fursa ya kuwa na Serikali tofauti na wenzetu Wazinzibari ambao wao wanayo Serikali. Kwa hiyo nataka kuona kuwa Katiba Mpya inairejesha Serikali ya Tanganyika ili kuleta uwiano sawa kati ya pande mbili za Muungano,” anasema Haji Juma mkazi wa Kata ya Jangwani Jijini Dar es Salaam.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Thadeus Mangia mkazi wa Tabata Kimanga ambaye ameufananisha muundo wa Muungano uliopo kuwa sawa na ndoa ya mkeka. Anasema kuwa Katiba Mpya inapaswa kuheshimu uamuzi wa wananchi juu ya aina gani ya Muungano wanaoutaka na siyo kulazimishwa waishi kwenye Muungano wasioutaka. Mangia anasema kuwa muundo unaowafaa Watanzania kwa sasa ni Muungano wa Serikali tatu.
Mangia anasema kuwa Muungano wa Serikali tatu utaondoa manung’uniko yaliyopo miongoni mwa wananchi kuwa upande fulani unaonewa na upande fulani wa Muungano ndiyo unaofaidika.
Anasema suluhu ya matatizo ya Muungano ni kuirejesha Serikali ya Tanganyika kama ilivyo kwa Serikali ya Zanzibar kisha iundwe Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Wananchi hao wanasisitiza kuwa katika Muungano huo walioathirika ni Watanganyika kwa kupoteza Serikali yao. Wanasema Wazanzibari wana Rais na Serikali tangu mwanzo wa Muungano, lakini Watanganyika wamepoteza vyote, yaani Rais na Serikali. Kutokana na hali hiyo, Mwalimu Florah Ishengoma (50) kutoka Tabata Kimanga anasema kuwa Muungano uwe wa Serikali moja na hilo likishindikana basi Serikali ziwe tatu ili na Watanganyika nao wapate haki yao.
“Kila siku wenzetu Wazanzibari wanalalamika kuwa wao wamemezwa na muundo wa Muungano huu. Sasa ili kuondoa malalamiko, napendekeza kuwapo Serikali tatu, yaani ya Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Kama hilo haliwezekani napendekeza tuwe na Serikali moja, Rais mmoja na mawaziri wakuu wawili, mmoja wa Zanzibar na mwingine wa Tanganyika, na hao mawaziri wakuu wachaguliwe na Bunge,” anasema Hamad Tao mkazi wa Kata ya Ilala.
Wananchi hao wamezidi kusisitiza kuwa Katiba iliyopo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inapotosha historia kuhusu suala la Muungano kwa kuwa imeiua Tanganyika na badala yake imeanzisha kitu kinachoitwa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Wanasema kuwa hakuna nchi inayoitwa Tanzania Bara iliyoungana na Tanzania Visiwani ikatokea Tanzania.
“Hakujawahi kuwepo kwa nchi inayoitwa Tanzania Bara wala Tanzania Visiwani. Haya ni mapungufu ambayo Katiba Mpya inatakiwa kuyarekebisha ili historia ibaki kama ilivyokuwa. Tanganyika itambulike kwa kuwa Muungano uliopo ni kati ya nchi ya Tanganyika na nchi ya Zanzibar,” anasema Adventina Ndibalema mkazi wa Kimara Korogwe.
Katika Sura ya Kwanza, Ibara ya (1) na Ibara ya 2(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 zinaeleza maana ya Muungano. Ibara hizo kwa pamoja zinasema kuwa Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano. Inaendelea kufafanua kuwa eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.
Ibara hizi hazisemi chochote kuhusu nchi za Tanganyika na Zanzibar, bali zimebadilishwa jina na kuitwa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Hapa ndipo wananchi wengi kwenye mikutano ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba wanapotaka Serikali ya Tanganyika irejeshwe kama ilivyokuwa kwa Serikali ya Zanzibar ambayo ipo tangu Muungano uanzishwe, Aprili 26, 1964.
Mwenyekiti wa Chama cha NLD (National League for Democracy) Dk Emmanuel Makaidi ameiambia Tume kuwa Serikali ya Tanganyika iliyouawa wakati wa Muungano inatakiwa kurejeshwa kupitia Katiba ijayo. Dk Makaidi anasema kuwa Wazanzibari katika Katiba yao, wanaitambua nchi yao, lakini Tanganyika haitambuliki mahali popote.
Kutokana na sintofahamu iliyopo kuhusu Tanganyika, Dk Makaidi kama ilivyo kwa wananchi wengine anaona kuwa Serikali ya Tanganyika ni haki ya Watanganyika ambayo hainabudi kurejeshwa kupitia mchakato huu wa kurekebisha Katiba ya nchi. Anasema kuwa kuuawa kwa Serikali ya Tanganyika ni kesi ambayo kwa muda mrefu haikupata majibu, lakini sasa majibu yake yapatikane kupitia Katiba ijayo.
“Haiwezekani tuwe kwenye Muungano ambao unaruhusu upande mmoja wa Muungano kuwa na Serikali yake, Bunge lake na kila kitu, halafu upande mwingine uwe umepoteza Serikali na mambo yake yote. Wenzetu wa Zanzibar wanayo Serikali lakini Tanganyika haijulikani iko wapi, ni bora tuungane na Burundi kuliko kuendelea kuwa kwenye Muungano huu,” anasema Abeid Rutozi ambaye kitaaluma ni mkalimani kutoka Kata ya Saranga jijini Dar es Salaam.

Chanzo: Mwananchi

Ukweli kuhusu Uhuru wa Tanzania

SHEREHE ZA UHURU ‘FEKI’ WA TANZANIA…!
• Msimu wa Tanganyika kuizuga dunia wawadia!
• Hufanya sherehe za mamilioni ya walipa kodi dunia nzima!
Tarehe 09 Disemba mwaka huu, yatajwa kitaifa na kimataifa kuwa ndio siku ya Uhuru wa Tanzania ambao hadi siku hio, Taifa hilo la ‘kufikirika’ la Riwaya za Shaaban Robert litatimiza miaka 51, tangu lipate uhuru kutoka kwa Wakoloni wa nchi jirani ya ‘Kusadikika’ pia ya Shaaban Robert.
Kwa wasiokuwa wasomaji wa Riwaya za Mwandishi mahiri, na baba wa fasihi ya Kiswahili hayati Shaabani Bin Ufukwe (Shaaban Robert), nataka niwakumbushe tu kuwa katika Riwaya zake mbili za Kusadikika na Kufikirika, alijaribu kusawili mazingira ya nchi zisizokuwepo kiuhalisia bali kivitendo na muonekano wa kitaswira nchi hizo hufanywa zionekane zipo au huwepo kimawazo. Lakini kiuhakiki nchi hizo zaweza kuwa sawa na nchi yoyote ile yenye sifa zilizotajwa na mwandishi huyo.
Nalazimika kujenga hoja kuwa uhuru wa Tanzania ni wa nchi za Kusadikika na kufikirika kwa sababu dhana nzima ya uhuru na nchi yenyewe haipo kiuhalisia na kimantiki. Kwanza hakuna nchi ambayo inaitwa Tanzania kiukweli hasa na kama ni jina tu, ‘Tanzania’ ni sawa na jina lilibuniwa na watu la Dar es Salaam kuiita ‘Bongo’ na si vyenginevyo. Pili, hata kama nchi hiyo tunalazimishwa kuamini kuwa ipo, basi haihusiani kabisa na dhana ya uhuru na Ukombozi wan chi za Afrika na ndio hata ukifuatilia harakati za uhuru na ukombozi wa bara la Afrika utakutia nchi iitwayo Tanzania haimo kabisa.
Dhana ya uhuru wa nchi haihitaji mtu aliesoma sana kuijua fasili yake. Kwani kimsingi Uhuru ni hatua ya nchi kujipatia nafasi ya kujitawala yenyewe na uwezo wa kujifanyia maamuzi ambapo kabla ilikuwa mamlaka hayo hayakuwa mikononi mwa Wazalendo au wananchi wenyewe, bali yalikuwa chini ya mikono ya wageni waitwao Wakoloni.
Kwa mantiki hii tunarudia kusema kuwa, Tanzania haikuwepo kabla na hata muda mfupi baada ya Uhuru wa bara na Visiwani, itakuwaje iwe nchi huru? Unaposema Uhuru wa Tanzania, kwa wenye akili za kidadisi watakuuliza nchi hio ilitawaliwa na nani? Labda tujikumbushe historia kidogo ya Afrika Mashariki. Zanzibar ilitawaliwa na Muarabu, Kenya Muingereza, Uganda Muingereza, na Tanganyika au German East Africa, ilitawaliwa na Mjerumani.
Hili ni somo la Hitoria ya darasa la sita na la saba hapa kwetu.
Pia tujikumbushe tarehe muhimu za Uhuru wa nchi hizo. Kenya ilipata Uhuru tarehe 10 Disemba 1963, Uganda tarehe 09 Oktoba 1962, Zanzibar 12 Disemba, 1963, na Tanganyika Tarehe 09 Disemba, 1961. Kwa hivyo, hapa hapana cha kuwazuga watu, kwani kwa hakika katika nchi hizi kuu nne za Afrika Mashariki utaona kuwa Tanzania haimo.
Juu ya hayo, hivi sasa kuna mabango kila pahala duniani na katika mitandao ya jamii inayosema na kunadi Sherehe za kufa mtu za Uhuru wa Tanzania kutimiza miaka 51. Wenzetu wa bara wamezoea kuwazuga Wazanzibari kwa sababu ndio ‘mazuzu’ labda au ‘mayakhe’ au ‘mdebwedo’ kama walivyozoea kutuita, na wanafikiria kuwa Wazanzibari waliokuwa ‘mazuzu’ wakati huo watakuwa mazuzu na vizazi vyao vijavyo kiasi ya kutoweza kujua hata hesabu ya kutoa na kujumlisha.
Kwa vile wanaaamini waliweza kuitawala Zanzibar kwa hadaa, ujanja, na kuwazuga wazanzibari kwa kuwapa vyeo na kuwatisha wengine kwa adhabu na mambo mbali mbali, wenzetu hawa bado wanaamini kuwa dunia nzima ina mazuzu kama hivi wanvyowaona Wazanzibari walioshindwa kujuwa hesabu ya Mwalimu ya 1+ 1 = 2 ( Wazanzibari walisema 1+1=3).
Baada ya kuona kuwa hatujui hesabu ndio hapo ukaona kuwa Uhuru wa Tanganyika unatimiza miaka 51 yaani ni sawa na 2012-1961, wao wakidhani na hesabu hii itaushinda pia.Cha kushangaza, hesabu ya darasa la kwanza hadi la tatu tu hii na bado dunia nzima inazugwa ik iamini kuwa Tanzania leo inatimiza miaka 51 ya uhuru wakati nchi yenyewe hata haipo, imeundwa tu kutokana na Riwaya za Shaaban Robert za kusadikika na kufikirika.
Mpaka hapa naamini umeweza kuona kuwa wenzetu wa bara wanatumia hila na mbinu kuudanganya Ulimwengu na huku wakitumia pesa zisikuwa kidogo za walipa kodi ndani na nje ya nchi kwa kusherehekea Uhuru wa nchi isiyokuwepo katika nchi zilizotawaliwa. Huu ni upotoshaji mkubwa wa dunia na kusema kweli unaiondolea hadhi nchi yetu kwa kusema Uongo ulio dhahiri mbele ya kadamnasi ya kimataifa.
Leo hii kuna Sherehe kila pahali: London, Canada, Italia, China, Ufaransa, Ujerumani, Marekani na nchi zote; eti ‘Miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania’. Hii haileti maana wala haina mvuto wowote zaidi ya kuuonesha Umma ufinyu wetu wa mawazo na fikira za kutojua maana ya neno Uhuru na baya zaidi hata kutojua historia yetu na hesabu ya kujumlisha na kutoa tu ambayo kila mtoto wetu wa darasa la kwanza na la pili anaijua.
Nionavyo, Ipo haja tubadilike. Hakuna ubaya kusema ukweli hata kama unauma. Wala haitaibabua sura haiba ya bara kwa kuandika na kujitangazia ‘Miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika’. Si vibaya kwani huu ndio ukweli. Ni afadhali tuseme ukweli tuepuke kuchekwa na kuadhirishwa.
Nakumbuka mwaka jana pale London, kuna Mzanzibari mmoja alifanikiwa kupenya na kuingia katika Sherehe za Miaka 50 ya uhuru wa ‘Tanzania’. Alipofika alimuuliza balozi ‘Hivi Tanzania ilipata uhuru kutoka kwa nani?’. Balozi hakuwa na Jibu. Baada ya hili, tulifikiri watajirekebisha, lakini ndio kwanza wanazidi kujitangaza hivyo ilhali dunia inajuwa kuwa huu wanaoufanya ni Uongo wa mchana, kuzimu hakuna nyota.
Kwa muungwana ni wajibu ukweli usemwe, hakuna uhuru wa Tanzania. Tusidanganyane na kudanganya watu kwani mwisho tutashindwa kwani ukisema uongo, Ukweli haujifichi,na ukiibuka ukweli kinachofata ni kuona aibu tu. Kwani wazungu husema ‘Unaweza kuwadanganya baadhi ya watu, baadhi wa wakati, lakini huwezi kuwadanganya watu wote, siku zote’.