Friday 15 June 2012

Nyerere na fitna za Upemba na Uunguja


Ahmed Rajab
ALIPOFARIKI  dunia Mwalimu Julius Nyerere Oktoba 14 mwaka 1999, gazeti la Guardian la Uingereza liliniomba niandike makala maalumu ya kuyatathmini maisha yake.
Nilipokuwa naanza kuiandika tathmini hiyo iliyochapishwa siku ya pili yake, niliyakumbuka aliyowahi kuyasema Mwenyekiti Mao wa China kumhusu Josef Stalin, mtawala wa pili wa Muungano wa Sovieti baada ya Vladimir Lenin.
Nami nikayatumia maneno hayohayo kuanzia makala yangu  kwa kuandika: Julius Nyerere was "a great leader who made great mistakes," as one ruler once famously said of another.(“Julius Nyerere alikuwa “kiongozi mkubwa (adhimu) aliyefanya makosa makubwa,” chambilecho mtawala mmoja aliyewahi kumuelezea hivyo mtawala mwenzake.)
Nyerere alifanya makosa ya kinadharia, ya kifikra na ya kiutendaji katika utekelezaji wa sera zake. Sikulidhukuru jina la Stalin kwa sababu sikutaka wasomaji wangu wafanye kosa la kudhania namfananisha Nyerere na Stalin.  Siamini kama Nyerere alikuwa na uovu wa Stalin.  Na kama ilivyokuwa kwa Stalin si yote ya Nyerere yaliyokuwa maovu.  Alitenda mema yanayostahiki sifa.
Watu wa kale wasema: “Kheri ya mja ni ulimi wake na shari ya mja ni huohuo.”  Kwa ulimi wake Nyerere aliwahi kutamka maneno ya maana na mengine ya kibahaluli. Baadhi ya maneno yake yalikuwa kama lulu na baadhi yalikuwa kama utumbo kama pale, kwa mfano, aliposema kuwa hakuna watu waitwao Waswahili.  Nilimsikia akiyasema hayo alipotoa hotuba katika ukumbi wa London School of Economics alipokuwa ziarani London kabla ya kuuacha urais.
Yote hayo yaonyesha kwamba Nyerere alikuwa mja, mtu kama watu wengine.  Hakuwa Mungu, hakuwa malaika. Wala hakuwa mtume na hata hakuwa mpigaji ramli.  Na si kila alichokitamka kilikuwa sahihi.  Lakini binadamu yule alikuwa na ulimi uliowalaza wengi na kuwafanya waache kufikiri kwani alikuwa na kipaji cha kuwafanya waamini kwamba kila alilolisema lilikuwa la kweli kabisa na hivyo hapakuwa na haja ya kumfanya mtu mwengine alifikirie.  Ilikuwa nadra kumpata mtu aliyethubutu kumpinga au kumkosoa, hasa kadamnasi.   Walikuwapo waliochelea kukiona cha mtema kuni na wengine waliridhia kuwa vibarakalla vya kuitika tu ‘hewala bwana.’
Moja ya makosa makubwa aliyoyafanya Nyerere kwa kusudi au kwa sadfa, ni hilo la kuwafanya wananchi wenzake waache kufikiri na wawe wanayafuata tu aliyokuwa akiyasema bila ya kuyazingatia au kuyapima.
Miongoni mwa aliyowahi kuyasema Nyerere ni kuwa ati iwapo Zanzibar itaachana na Tanganyika basi Tanganyika kutakuwa shuwari lakini Wazanzibari wataanza kubaguana baina ya Wapemba na Waunguja na halafu wataendelea kutafutana asili zao. 
Tangu wiki iliyopita waandishi kadhaa wa Bara wamekuwa wakiyanukuu haya kana kwamba ni maneno yenye ukweli usiopingika.  Hii ni fitna tu; na inatumiwa kuwatisha na kuwagawa Wazanzibari.
Wakoloni walipowaona wanaowatawala wanaungana kuwapinga, basi walitumia mbinu ya kuwagawa wazidhoofishe nguvu zao ili waendelee kuwatawala. 
Mbinu kama hiyo inatumiwa siku hizi na baadhi ya viongozi wa CCM wa Bara pamoja na baadhi ya waandishi wa huko huko Bara ‘walioshtushwa’ na mwamko wa kisiasa uliowafanya Wazanzibari wawe na ujasiri wa kuujadili kwa mapana na marefu Muungano wa Tanzania. 
Ujasiri huo umewafanya wengi wao waseme kwamba ama wanaupinga muundo wa sasa wa Muungano au hawautaki kabisa na wanataka Zanzibar iwe dola huru yenye mamlaka yake kamili.
Huo si mwamko wa leo au wa jana; tumekuwa tukiugusia miaka nenda miaka rudi lakini tukionekana kuwa ni wazushi na wazandiki.  Sasa mambo yanajidhihiri yenyewe.  Matokeo yake ni kwamba waliokuwa wakijidanganya sasa wamegutuka na hawajui jinsi ya kulizuia hilo wimbi la uzalendo Wakizanzibari minghairi ya kutumia hoja finyu za kikabila na udini.
Mmoja amefika hadi ya kuandika kuhusu ‘Waarabu’ na ‘watu Weusi’ kana kwamba hao wanaonasibishwa na uarabu ni wa rangi aina ya pekee iliyo tofauti kabisa na ya Wazanzibari wasio na asili ya Kiarabu.  Mwandishi huyohuyo alitishwa na sura rahimu ya Sheikh Farid Hadi Ahmed, mmoja wa viongozi wakuu wa Uamsho. 
Aliandika kwamba baada ya kuiona picha ya Sheikh Farid yalimjia mawazo kwamba Uamsho si jumuiya ya kidini na wala si ya Wazanzibari na kwamba Sheikh Farid ametumwa (hakusema na nani) kuwafitinisha Wazanzibari.  Alichotaka kusema mwandishi huyo ni kwamba kwa vile Sheikh Farid ana asili ya Kiarabu basi Uamsho inataka kuurejesha usultani.
Ni uchambuzi uchwara, tena wenye kutumia lugha ya kibri. Unashtua kwa vile ni ‘uchambuzi’ wa hatari unaofanana na simulizi za  Wahutu wa Rwanda kabla ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini humo. 
Hizi fitna za ‘Upemba’ na ‘Uunguja’, za ‘ubwana’ na ‘utwana’ na za ‘ugaidi’ wa Uamsho ni fitna zinazotiwa na watu walio maluuni.  Lengo lao kubwa ni kuwapotosha Wazanzibari wauzime mjadala wa Muungano.  Hawajali iwapo watalitimiza lengo hilo kwa kuyakiuka maadili ya uongozi au ya uandishi. 
Hila wanazotumia ni kwanza, kuwafitinisha Wazanzibari kwa kutia fitna za kikabila na za kidini.  Kwa mfano, wanawatisha wahafidhina wa CCM/Zanzibar, wale wenye kusherehekea kaulimbiu ya ‘Mapinduzi Daima’, kwa kuwaonya ya kuwa Uamsho ina “msukumo wa kiarabu”  na kwamba kusudio lake ni hatimaye kuyapinga Mapinduzi na kuirejesha Zanzibar katika ‘utumwa’. Maneno ya kijinga kabisa.
Hila yao ya pili ni kuwagonganisha vichwa Waunguja na Wapemba kwa kutumia hoja zisizo na mshiko wowote wa kimantiki.  Wanasema wamewapata Wapemba wengi wenye kutaka Muungano uendelee kama ulivyo. Wamewahoji na matamshi yao kusambazwa na magazeti fulani nchini.  Huu ni mfano mzuri wa propaganda ya kitoto.
Hila yao ya tatu ni kutumia lugha kuparaganya mambo.  Ingawa Uamsho ni jumuiya kamili wao badala yake wanasema kuwa hiki ni kikundi. Sio kundi bali ‘kikundi.’  Na wanaishtumu jumuiya hiyo kuwa ‘inawatumia’ baadhi ya vijana kufanya vitendo vya kihuni vya kuchoma moto makanisa. Hakuna ushahidi wa hili.
Nne, wanajaribu kuwatisha Watanzania na hasa wakuu wa dunia hii kwa kuifananisha Jumuiya ya Uamsho na mitandao ya kigaidi ya Al-Qa’eda, Boko Haram na Al-Shabab.  Bila ya shaka wenye kueneza fitna hii hawajui walisemalo na wanajikashifu si mbele ya Watanzania wenzao tu bali hata machoni mwa balozi za nchi za Magharibi. 
Sijui kama wanaelewa ya kuwa maofisa wa baadhi ya balozi za Magharibi wameshakutana na viongozi wa Uamsho katika juhudi zao za kuitathmini Jumuiya hiyo na wanayaelewa makusudio halisi ya Uamsho.
Kwa hakika, kinyume na wanavyoandika baadhi ya waandishi wa Bara, Jumuiya ya Uamsho haikuzuka juzi. Imekuwako kwa muda wa takriban miaka 10 sasa.  Jumuiya hii ni kama mwavuli ambao chini yake kuna jumuiya mbalimbali za Kiislamu, pamoja na ile ya maimamu. 
Uamsho imekuwa ikiendesha harakati zake kwa msaada wa taasisi za nchi za Magharibi.  Ilikuwa miongoni mwa  waangalizi rasmi wa Uchaguzi Mkuu uliopita na ripoti yake kuhusu uchaguzi huo ni ya kupigiwa mfano kwa maelezo yake ya kina. 
Kati ya wafadhili wa Jumuiya hiyo katika harakati hizo za kuangalia uchaguzi lilikuwa shirika la USAID la Marekani.  Hata vizibao wanavovaa baadhi ya viongozi wa Uamsho na vikuza sauti vyao walipewa na Wamarekani wakati huo wa uchaguzi uliopita.
Wenye kujuwa mambo watakwambia kwamba kuna tofauti kubwa kama ya mbingu na ardhi kati ya jumuiya ya Uamsho na mtandao wa Al-Qa’eda au kundi la al-Shabab.  Huwezi kabisa kuzifananisha falsafa zao au makusidio yao.  Hata Boko Haram nayo licha ya mbinu inazozitumia inatofautiana sana na al-Qa’eda.
Huko Zanzibar mafatani hawa wana washirika wanaojulikana.  Nao ni wale wanaochomwa na kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).  Ndiyo maana wakaruka harakaharaka kuwatupia lawama za machafuko ya hivi karibuni viongozi wa CUF waliomo kwenye SUK na kutaka watimuliwe kutoka serikalini.  Na ni wao waliohusika na vipeperushi vilivyotolewa wiki iliyopita kuwafitinisha Wapemba na Waunguja.
Na ni haohao wenye kujaribu kuwachimba waasisi wakuu wa Maridhiano yaani Rais mstaafu Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad.
Inasikitisha kuwaona baadhi ya Wabara wenye kujigamba kuwa ni wasomi wakitaka mijadala ya kisiasa ipigwe marufuku katika majukwaa ya kidini. Hawaelewi kwamba ni dhima ya dini za Ukristo na Uislamu kuzungumzia na kuyatafutia ufumbuzi mambo yanayoyagusa maisha ya kila siku ya waumini wa dini hizo. Na mambo hayo yawe yepi kama si ya kisiasa?
La kutisha ni kuwa  ‘wasomi’ hao wanamtaka Rais Jakaya Kikwete awachukulie hatua za kimabavu wakuu wenzake walio serikalini kwa kisingizio kuwa ati wanaunga mkono harakati za Uamsho. 
Ulimwengu haukufunga macho wala haukuziba masikio.  Unawaona na kuwasikia.  La ajabu ni kwamba wanasiasa na waandishi wenye kuchochea hisia kama hizo wamesahau ni nyakati gani tulizo nazo na ni ulimwengu gani tulio nao.  Katika ulimwengu wao wa leo Wazanzibari wanasema hawakubali tena kugawanywa kwa propaganda za kikabila au za kidini. 
Inatisha kwamba kuna wanasiasa na waandishi waliosahau kwamba siku hizi kuna Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) na mahakama nyingine mahsusi za kimataifa, mithili ya ile Mahakama Maalumu ya Sierra Leone. Mahakama kama ile ya Sierra Leone inaweza kuundwa mara moja na Umoja wa Mataifa kuwatia adabu wenye kupalilia fitna zinazoweza kuzusha mauaji ya kimbari. 
Ni hiyo Mahakama Maalumu ya Sierra Leone iliyomhukumu Charles Taylor, rais wa zamani wa Liberia, kifungo cha miaka 80 baada ya kupatikana na hatia ya  kuishushia nakama Sierra Leone.
Dhana waliyonayo baadhi ya wasomi na waandishi wa Bara ni kwamba viongozi wa Uamsho ni mijitu isiyosoma.  Kuna mmoja aliyepandwa na jeuri na kuandika kwamba mbali na kujua kusoma Qur’an viongozi hao ni watu wasiojuwa kuandika wala kusoma.
Ukweli ni kwamba viongozi wa Uamsho ni wasomi waliohitimu masomo ya chuo kikuu na wana shahada za juu za uzamili katika fani mbalimbali kama vile za uhandisi, sayansi na jiografia.  Ni wasomi wa nyanja zote — za dini na dunia.
Mfano mzuri ni Sheikh Msellem ambaye mbali na kuwa gwiji wa tafsiri ya Qur’an pia alisomea taaluma ya hali ya hewa. 
Baadhi yao walisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako walivutiwa na hotuba za kidini za Professor Malik, mtaalamu wa fani ya hesabati, ambazo ziliwashajiisha na kuwafanya wawe na mwamko wa Kiislamu.  Wengine walisoma kwenye vyuo vikuu vya nje vikiwemo vile vya Sudan, Saudi Arabia na Qatar.
Ni wazi kutokana na ripoti na taarifa zao kwamba baadhi ya wasomi na waandishi wetu wa Bara wanawadharau Wazanzibari. Nadhani hizo dharau zao ndizo zinazowafumba macho wasiweze kuona nani hasa aliyechochea fukuto hili la upinzani dhidi ya makandamizo ya walioshika hatamu za utawala wa Muungano.
Maandishi yao yamebainisha wazi kwamba hawaamini ya kuwa Unguja na Pemba si majimbo wala koloni za Bara.  Inakirihisha kuona namna wengi wao wanavyozitapika hadharani chuki zao (na udini uliowapamba) bila ya hata staha na uvumilivu wa kimaadili.

Wednesday 6 June 2012

Kuvunja Makanisa Si Kuvunja Muungano

Ahmed Rajab
UKILALA unaamka.  Kama huamki na bado una uhai basi unaamshwa.  Jumuiya ya Uamsho  na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiko) ya huko Zanzibar inasema kwamba imejitweka jukumu la kuwaamsha Wazanzibari kuhusu mengi — ya dini na dunia.  
Miongoni mwa hayo ni Muungano wa Tanzania ulioziunganisha nchi za Tanganyika na Zanzibar tarehe 26 Aprili mwaka 1964.  Kwa ufupi,  Jumuiya ya Uamsho inaupinga Muungano.  Hamna shaka yoyote kwamba kwa hilo ina wafuasi wengi sana Visiwani.
Jumuiya hiyo imekuwa ikiandaa mihadhara ya kuwapa elimu ya kiraia waumini wa dini ya Kiislamu kuhusu masuala ya katiba likiwamo suala la Muungano na uhalali wake.
Tukumbuke kwamba wanao uhuru wa kufanya hivyo na wakati huohuo tusiyasahau maneno ambayo Mwalimu Julius Nyerere alimwambia mwandishi Colin Legum wa gazeti la Obsever la Uingereza mwaka 1965 kwamba hatowapiga mabomu Wazanzibari wamridhie endapo watakataa kuendelea na Muungano.
Mihadhara hiyo ya Uamsho inapendwa na huhudhuriwa na watu mia kadhaa kama si elfu kadhaa kila inapofanywa.  Japokuwa inapendwa hivyo imekuwa ikiwakera baadhi ya walio na madaraka Zanzibar na wasiofurahishwa na Maridhiano yaliyopo Visiwani.  Wanachokitaka waheshimiwa hao ni kuzuka kwa fujo zitazoweza kuisambaratisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hata kuzusha hali zitazopelekea kusimamishwa kwa mchakato wa katiba.
Mkakati wao ni rahisi kuuelewa:  chochea fujo kwa kuwatumia vijana, watomeze wenye jazba washambulie makanisa, wahusishe viongozi wa Uamsho na mtandao wa kigaidi wa al-Qa’eda, wahusishe viongozi wa CUF na Uamsho na harakati zao.
Wanatumai kwamba kwa kufanya hivyo wataweza kuwafanya wakuu wa serikali ya Tanzania na wakubwa wa dunia hii waiangalie Zanzibar kwa jicho jingine.  Wanachotaka hasa, na kwa hili wana wenzao Bara,  ni kuzizima harakati za kuujadli Muungano.
Fujo zilizoanzia Jumamosi ya tarehe 26 Mei zilichochewa na polisi kwa kutotumia hekima walipomtia nguvuni Sheikh Mussa Issa.  Wafuasi wake wakamiminika, wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo mbele ya kituo cha polisi alikoshikwa na wakadai aachiwe huru.
Polisi nao wakapambana na umati huo kwa kuwarushia mabomu ya kutoa machozi. Ndipo palipozuka kikundi cha watu na kwenda kutia moto kanisa na kuvunja mabaa.  Baadhi ya waliovunja hizo baa wakipiga takbir (Allahu Akbar) na huku wakinywa pombe. Haiyumkiniki kwamba hawa walikuwa wafuasi wa dhati wa Uamsho.
Inafaa tuangalie jinsi matukio hayo yalivyokuzwa kupita kiasi na vyombo vya habari na kuwapelekea watu waamini kwamba ‘Zanzibar yateketea’ na si pahala pa watalii, Wakristo au Wabara.
Bahati nzuri hakuna ubalozi wowote wa kigeni uliotoa taarifa kuwaonya wananchi wao wasiizuru Zanzibar;  na wala hakuna mtalii yoyote au Mkristo kutoka Bara aliyedhuriwa.  Kwa hakika tunapaswa kuwapongeza waandamanaji pamoja na majeshi ya usalama kwa kutofanya mambo ambayo yangelizidi kuifanya hali iwe mbaya.
Zamani polisi wakizoea kutumia nguvu kupita kiasi na waliwahi kuwaua waandamanaji wasiokuwa na silaha kama ilivyotokea Pemba mapema mwa mwaka 2001 pale watu kadhaa wasio na silaha walipouawa na vikosi vya usalama walipokuwa wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010.  Wao wakishikilia kwamba chama cha CUF ndicho kilichoshinda kwenye uchaguzi huo.  Hayo yamepita.
Tukiyaangazia ya leo inasikitisha kwamba miongoni mwa waathirika wa matukio ya siku ile ya machafuko ni kanisa moja lililotiwa moto.  Hiki ni kitendo kiovu, cha kishenzi na chenye kwenda kinyume na mafundisho ya Kiislamu.
Ni kosa la jinai kuchoma moto mahala popote pa ibada.  Pia ni kosa kubwa kujaribu kukilaumu chama chochote au jumuiya yoyote kuwa ndio iliyohusika na uchomaji moto huo.
Zanzibar ina umaarufu kwa mchanganyiko wake wa watu wa makabila, rangi na dini tofauti.  Pia inasifika kwa jinsi Waislamu wake — ambao ndio wengi nchini humo — wanavyoingiliana na Wakristo wake ambao ni wachache sana.  Kwa muda wa zaidi ya karne Wakristo hao wamekuwa na uhuru kamili wa kuabudu na wamekuwa wakipata hifadhi.
Juu ya kuwa Zanzibar inatafahari kuwa ni nchi ya Kiislamu, hatukuwahi kusikia katika historia au kushuhudia kwamba Wakristo wa Zanzibar wanabughudhiwa kwa sababu ya imani yao.
Kwa hakika, katikati mwa karne ya 19 na baadaye pale wamisionari Wakikristo wa kizungu walipokuwa wakitafuta njia za usalama za kupenya na kuingia katika eneo la Maziwa Makuu na sehemu za bara za Afrika ya Mashariki misafara yao yote ilianzia Zanzibar.
Masultani wa wakati huo waliwapa hao mamisionari wakizungu risala za kuwajulisha na machifu wa bara.  Isitoshe masultani  waliwapa hifadhi wamisionari huko Zanzibar.  Hakuna mtu yoyote aliyethubutu kuwagusa hao wamisionari.
Kadhalika masultani walikuwa wakiwapa wamisionari watu wa kuwaongoza katika misafara yao ya kueneza Ukristo katika kanda ya Afrika ya Mashariki.  Kama ilivyokuwa kwa mengi katika zama zile Ukristo nao pia ulianzia Zanzibar.  Ndio maana makanisa makongwe kabisa katika Afrika ya Mashariki yako Zanzibar.   Hata ile ardhi iliyojengewa makanisa ya Kianglikana na Kikatoliki katika Mji Mkongwe huko Unguja ilitolewa bure na sultani wa Zanzibar na kugaiwa madhehebu hayo mawili ya Kikristo.
Haielekei kwamba uvumilivu huo utatoweka.  Hautotoweka kwa sababu uvumilivu huo umejengeka katika utamaduni Wakizanzibari na utamaduni huo ni wenye kuufuata Uislamu kama unavyotakiwa kufuatwa bila ya kuufanya uwe mgumu.
Utamaduni huo si tu kwamba unavumilia dini nyingine bali pia unaheshimu tofauti za kidini na za kitamaduni zilizo katika jamii.   Na wala tofauti hizo hazitumiwi vibaya kwa minajili ya kisiasa.
Ndipo tunapokuwa hatuna budi ila kukubaliana na Rais Jakaya Kikwete aliposema kwamba kuuvunja Muungano hakuwezi kupatikana kwa kuchoma moto makanisa.
Kwa sasa jambo la busara ni kusubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi kuhusu kadhia ya uchomaji moto kanisa.  Tunatumai kwamba wahalifu waliochukua hatua hiyo watafikishwa mahakamani.  Hatua yao si ya  kijinga tu bali inaweza kuleta hasara kwa mengi.
Tusighafilike tukasahau kwamba hii leo wananchi wa Zanzibar wana uhuru wa kusema na wa kukusanyika kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na sheria za nchi hiyo pamoja na zile za serikali ya Muungano zinazosema kwamba Tanzania — na hivyo Zanzibar — ni nchi za kidemokrasia.
Kadhalika, ni muhimu kukumbuka kwamba suala la Muungano ni suala lenye kuzusha hamasa na jazba kubwa kila linapojadiliwa na huvutia makundi ya watu bila ya kujali nani au jumuiya gani inalijadili suala hilo.
Jambo moja linalojitokeza katika mijadala yote hiyo na bahati nzuri hili si siri tena kwani Wazanzibari wamekwishauvua woga wao ni kwamba wengi wao, ingawa hawataki Muungano uvunjike, hawaitaki hali iliyopo sasa ya Muungano wa Katiba wenye kuifanya serikali yake iwe na nguvu na madaraka makubwa mno. 
Wengi wao wangependelea badala yake pawepo na Muungano kama ule Muungano wa Ulaya.  Kwa ufupi, wanataka Muungano wa nchi mbili zilizo huru zenye kutendeana wema na kushirikiana.
Kwa sasa Wazanzibari wanavuta subra wakingojea fursa ya kutoa maoni yao katika shehia zao juu ya mustakbali wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. 
Kadhalika wanatambua kwamba  baada ya hapo watapata fursa nyingine ya kutoa maoni  yao kwenye kura ya maoni watapoulizwa iwapo wanaikubali au hawaikubali katiba mpya itayotungwa baada ya mchakato wa kutoa maoni.
Hiyo itakuwa ni fursa wasiowahi kuipata na itawawezesha kuigeuza hiyo kura ya maoni kuhusu katiba iwe kura juu ya Muungano.
Uamsho una msimamo wenye kuupinga Muungano.  Sasa tujiulize iwapo Uamsho unaweza kuupata muradi wake wakati huu wa sasa katika mchakato wa kuipitia tena katiba.
Tusisahau kuwa jumuiya za kidini na zisizo za kidini zote zinaruhusiwa kutoa maoni yao juu ya suala la Muungano na hatima yake.  Ruhusa hiyo ipo ilimradi pasiwe na sera ya kupambana na vyombo vya dola.
Kwa  Zanzibar mpambano huo hauhitajiki kwa vile viongozi wa kisiasa wa itikadi tofauti mara nyingi wametoa matamshi wakieleza wazi msimamo wao kuhusu Muungano.  Hata Rais Dk.  Ali Mohamed Shein alinukuliwa hivi karibuni akisema kwamba anashiriki kikamilifu katika zoezi la kuipitia katiba akishirikiana na Rais Kikwete.
Tena kuna wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar  ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakieleza jinsi wasivyoridhishwa na Muungano.  Hata kabla ya Uamsho kuanza harakati zake wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekuwa wakiyatetea maslahi ya Zanzibar kama  pale masuala ya mafuta na gesi asilia yalipofikishwa mbele ya Baraza.
Ingawa Uamsho bado haujatoa taarifa rasmi kuhusu sera zake, na ukifanya hivyo utajigeuza na kuwa chama cha kisiasa, viongozi wake hata hivyo, wamekuwa wakitoa mwito kutaka irejeshwe ile iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kwa kupitia kura ya maoni itayowauliza wananchi iwapo wanautaka au hawautaki Muungano.
Ni wazi kuwa viongozi wa Uamsho wanauona huu mchakato wa sasa kuhusu katiba kuwa usio na maana.
Juu ya hayo bado viongozi hao hawakuonyesha njia inayoweza kutumiwa kutimiza lengo la kuirejeshea Zanzibar uhuru wake.  Wala hawakuonyesha vipi hiyo kura ya maoni itapigwa na iwapo wataweza kutimiza lengo lao kwa kutumia njia za kidini na mikusanyiko ya kidini bila ya kuwahusisha viongozi wa Zanzibar na wa Muungano.

Saturday 2 June 2012

Rais Banda auza ndege ya rais


Rais wa Malawi, Joyce Banda, ameamua kuuza ndege ya rais pamoja na magari 60 ya fakhari.
Rais Banda amenukuliwa kusema kwamba anatosheka kusafiri kwenye ndege za abiria kama watu wengine, kwa sababu ameshazowea kutembea kwa miguu na kusaidiwa na wasafiri njiani.Ndege hiyo ilinunuliwa kwa dola milioni-13 na rais aliyemtangulia, Bingu wa Mutharika, aliyefariki mwezi wa Aprili.
Fedha zitazopatikana katika mauzo ya ndege na magari hayo, zitatumiwa kuwasaidia maskini wa Malawi.
Serikali ya Uingereza, ambayo ndio mfadhili mkubwa wa koloni yake hiyo ya zamani, imepokea vema uamuzi huo kuwa ni ishara inayotia moyo