Thursday 24 May 2012

Hata tuyazime, maswali yale yale kuhusu Muungano yanaturejea

HUKO nyuma nimeeleza kwamba haiwezekani kuijadili Tanzania pasipo kuujadili Muungano, na kwamba dalili za makundi ya watu kuhoji Muungano wetu kama ulivyo leo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Fursa tuliyo nayo hivi sasa ya kujadili na kuandika katiba mpya ni fursa adhimu tunayoipata kuujadili Muungano kwa kina na kuupatia ufumbuzi utakaotupeleka masafa marefu kidogo.
Ye yote anayetaka kujua jinsi masuala ya Muungano yalivyotusumbua katika historia yetu ya takriban nusu karne atakumbuka mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na tume na kamati mbalimbali zilizoundwa katika jitihada za kujaribu kurekebisha baadhi ya masuala yaliyoonekana kukera makundi ndani ya nchi, na jinsi ambavyo jitihada hizo zote na kamati na tume hizo hazikufanikiwa kuondoa malalamiko kuhusu Muungano.
Sasa itakuwa ni jambo la ajabu iwapo, wakati tunasema tunataka kuandika katiba mpya, tutajinyima wasaa wa kuujadili Muungano kwa kuwauliza wananchi wa pande mbili (Tanganyika na Zanzibar) ni nini wanachotaka, iwapo wanataka Muungano au hawautaki.
Swali hilo la msingi likiiisha kupatikana, na jibu likawa kwamba wanautaka Muungano, ndipo sasa itawezekana kuangalia kwa undani ni mambo gani ndani ya mfumo na taratibu za Muungano yafanyiwe marekebisho ili kuyaweka sawa na kukidhi matarajio ya pande mbili zilizoungana.
Binafsi nakataa dhana ya kuwaambia watu kwamba kuujadili Muungano ni sharti tujadili namna ya kuuboresha. Mtu huboresha jambo analotaka kuendelea nalo, na kama hataki kundelea nalo ni upuuzi kuanza kuliboresha. Haina maana hata kidogo. Na si kweli kwamba hatujasikia sauti za watu wanosema kwamba hawautaki Muungano, na wala pia si kweli kwamba hawana haki ya kuwa na mawazo kama hayo.
Njia pekee kwa wale wanaopenda Muungano uendelee kuwapo (pamoja na marekebisho yatakayokubaliwa) ni kuwaacha wana-Muungano wenyewe waseme kwamba wanataka kuuendeleza kwa kuuboresha. Iwapo watasema kwamba hawautaki, na tujue kwamba hiyo ndiyo kauli yao, huo ndio utashi wao. Kujidai kwamba tutauendeleza Muungano bila ridhaa ya Watanganyika na Wazanzibari ni ndoto za Alinacha.
Katika historia yetu tumekuwa na matukio kadhaa yaliyoutikisha Muungano lakini ikawezekana kuyazima kwa njia moja au nyingine. Tutakumbuka sakata la “kuchafuka kwa hali ya hewa” Visiwani mwaka 1983-84, iliyosababisha kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi.
Kimsingi alichokuwa akisema Jumbe ni kwamba Muungano ulihitaji marekebisho katika muundo wake ili uweze kukidhi mahitaji ya Wazanzibari.
Tukumbuke pia kwamba wakati Jumbe akichukua hatua za kufanya mapendekezo ya kuuboresha Muungano kadri alivyoona inafaa, alikuwa ni kipenzi cha Mwalimu Nyerere, ambaye alijiona raha kufanya kazi na ‘msomi’ mwenzake baada ya kusumbuana sana na Abeid Karume, muasisi mwenzake wa Muungano, Karume akiwa ni mtu asiyetabirika, na mwenye maamuzi yaliyotatanisha.
Inawezekana kwamba usiri wa hatua alizokuwa akitaka kuzichukua Jumbe ndio uliomuudhi Nyerere hata akaamua kumwadhibu Jumbe. Hata hivyo, haijulikani msimmao wa Mwalimu ungekuwa upi iwapo Jumbe angepeleka mapendekezo yake mbele ya kikao rasmi cha CCM au serikali na kuomba ridhaa juu ya mawazo yake ya kuboresha Muungano.
Tofauti na hii leo, ambapo majadiliano ndani ya NEC ya chama-tawala yanajulikana Kariakoo na Manzese kabla kikao hakijafungwa, wakati ule wa sakata la Jumbe kikao cha siri maana yake ilikuwa ni kikao cha siri. Kikao hicho hakina hata ‘hansard’. Ndiyo maana itakuwa vigumu kujadili kwa undani maudhui ya mjadala uliofanyika ndani ya kikao kilichohitimishwa kwa kumvua Jumbe nyadhifa zake zote na kumpeleka ‘uhamishoni’ Mji Mwema.
Muongo mmoja baadaye kundi la wabunge wa CCM lililojulikana kama G-55 (jina lilinuniwa na Issa Shivji) likaibuka na kudai marekebisho katika muundo wa Muungano kwa kuasisi serikali ya Tangayika na kuwa na muundo wa Shirikisho.
Hoja iliyopelekwa bungeni na kundi hili iliungwa mkono kwa nguvu kubwa na watu wengi na hatimaye serikai ikaridhia hoja hiyo na kukubali marekebisho hayo yafanyike.
Kwa mara nyingine tena ilikuwa ni Mwalimu Nyerere aliyesimama na kuipinga hoja hiyo, ikiwa tayari imekwisha kupitishwa na Bunge, na hatimaye juhudi zake zikafanikiwa kuitengua hoja hiyo.
Ikumbukwe kwamba Mwalimu wakati huo hakuwa rais wala mwenyekiti wa chama chake, lakini kwa ushawishi aliokuwa nao aliweza kufanya alivyofanya.
Nakumbuka, nikiwa mmoja wa kundi la G-55, tulikuwa na mabishano mengi na Mwalimu nyumbani kwake Msasani katika kipindi hicho, na nakumbuka kwamba Mwalimu alishikilia msimamo wake bila kutetereka, ingawaje baadhi yetu hatukuona mantiki ya kile alichokuwa akikitetea.
Kimsingi, msimamo wake ulikuwa kwamba muundo wa serikali tatu ungevunja Muungano. Sisi tulikuwa na mawazo tofauti, kimsingi, kwa sababu tulikuwa hatuoni matiki ya kuwa na serikali mbili, moja ikiwa ni ya Zanzibar na ya pili ikiwa ni ya Zanzibar na Tanganyika.
Hiyo ni historia. Lakini sasa zimejitokeza sauti zinazotoa mwangwi wa haya ninayoyasimulia, kwa mara nyingine zikidai muundo wa serikali tatu. Hizi ziko pande mbili za Muungano, nazo zinadhihirisha ukweli kwamba jambo hili halijaondoka; lipo na linahitaji mjadala wa kina ndipo lipatiwe ufumbuzi. Kulizimazima hakutasaidia sana.
Nimekuwa nikikagua kumbukumbu ili kujua kama Mwalimu Nyerere aliwahi kupiga marufuku mjadala kuhusu Muungano. Sikumbuki. Alimtoa Jumbe madarakani. Aliizima hoja ya G-55. Lakini sikumbuki hata mara moja akisema kwamba ni marufuku kuujadili Muunagno. Aliwaachia waliomzunguka waelewe kwamba kwake Muungano ulikuwa kitu azizi kwake na hapendi kichezewe, lakini hakusema kinagaubaga kwamba ni marufuku kuujadili.
Ninaweza kwenda mbali zaidi na kusema kwamba, hata kama Mwalimu angekuwa amesema waziwazi kwamba ni marufuku kuujadili Muungano, bado tungeweza, katika mazingira ya leo, tukasema kwamba pamoja na heshima yetu kubwa kwake, lakini Muungano unajadilika. Mambo yamebadilika, na dunia inasonga mbele, na alichokiamini baba yako sicho unachotakiwa lazima ukiamini leo.
Kama hivyo ndivyo, hakuna sababu yo yote ya kuweka makatazo katika majadala kuhusu Muungano. Acheni ujadiliwe kwa uwazi mkubwa kiasi kinachowezekana, mawazo yanayokinzana yashindanishwe na mumo tupate elimu ya kuuboresha Muungano.
Mimi binafsi ni muumini mkubwa wa mamlaka ya watu ndani ya sehemu wanamoishi, kwa sababu mamlaka hayo ndicho kielelezo thabiti cha dhana ya kujitawala.
Hatua yo yote inayopunguza uwezo wa wananchi wa sehemu fulani kujiendeshea shughuli zao kwa uhuru mpana kiasi kinachowezekana ndani ya umoja wa jumla, ni kitendo kinachokinzana na maendeleo.
Wako Wazanzibari wanaosema uhuru wao wa kuendesha mambo yao umebinywa mno; wako Watanganyika wanaodhani kwamba katika Muunago huu Wazanzibari wanapewa nafasi ambazo si zao, na kwa hiyo wanawanyima nafasi Watanganyika. Hususan, dhana ya u-Zanzibari imekuzwa mno hadi inaamsha jawabu la u-Tanganyika.
Shetani naye amejiingiza. Waziri wa zamani wa mafuta nchini Venezuela aliwahi kusema kwamba mafuta ya peteroli ni kinyesi cha Shetani nasi sote tunaogelea ndani yake.
Inaelekea Shetani ametutembelea hivi karibuni, na tunasikia kelele za “Yangu! Yangu!” Baadhi ya Wazanzibari wameanza kuogelea mumo kabla hata Shetani hajaenda msalani.
Bila shaka viyu kama hivyo (mafuta, gesi asilia, ardhi, misitu, rasilimali-bahari na kadhalika) vitakuja kutusumbua huko tuendako. Na tutakumbana na ile dhana ya mzandiki anayesema, “Chako chetu, changu changu.” Njia pekee ya kuondokana na uzandiki huo ni kuwa na mjadala mpana, wa wazi, na wa kituo.
Chanzo: Raia Mwema

Zanzibar ingekuwa nyingine wangepatanishwa Abeid Karume na Ali Muhsin

HALI za maisha Zanzibar ni ngumu. Watu wanaishi lakini wengi wao wanaishi maisha ya taabu. Imekuwa kana kwamba Wazanzibari wa leo ni mahuluki taabu.
Asilimia kubwa ya vijana hawana ajira, wenye ajira wanalipwa mishahara ya chini kabisa kulinganishwa na wanavyolipwa wafanya kazi wenzao katika nchi jirani za Afrika ya Mashariki.
Wazanzibari wanayapata maji kwa taabu. Umeme vivyo hivyo. Ukija upande wa huduma nyingine zinazotolewa na Serikali ya Zanzibar mambo ni hayohayo.
Matatizo huzidi kuzuka pale serikali inapolazimika kutumia fedha nyingi isizoweza kuzimudu. Serikali hulazimika kufanya hivyo ama kutokana na shinikizo za kisiasa au uendeshaji na usimamizi mbovu wa wakuu wa idara.
Kati ya matatizo ya Zanzibar ni kwamba serikalini hakuna udhibiti wa kutosha wa madeni ya serikali na dhamana au rahani za madeni hayo.
Wizara ya Fedha ina mfumo maalumu wa matumizi ya kipindi cha wastani. Lengo la mfumo huo ni kuhakikisha kwamba fedha zinagawanywa kwa kipindi cha miaka mitatu kwa mujibu wa vipaumbele vya kitaifa na vya sekta maalumu.
Hadi sasa lakini utaratibu huo haufanyi kazi sawasawa. Bado masuala ya matumizi ya fedha za serikali yanapangwa kwa kipindi cha mwaka mmoja mmoja na hakuna mahusiano baina ya makadirio ya matumizi ya mwaka mmoja na viwango vya juu vya bajeti vya mwaka unaofuatia.
Japokuwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita kumepatikana maendeleo katika utoaji wa huduma za kimsingi za afya na elimu, kiwango cha vifo vya watoto wachanga ni 61 kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa hai. Na inakisiwa kwamba utapiamlo unawaathiri kama thuluthi moja ya wakaazi wa Zanzibar.
Inakisiwa pia kwamba sasa Visiwa vya Zanzibar vina wakaazi wapatao milioni moja na robo — ikiwa asilimia 2.7 ya wakaazi wote wa Tanzania. Na idadi ya wakaazi wa Zanzibar inaongezeka kwa kima cha takriban asilimia 3.1.
Kama nusu ya idadi ya wakaazi wa Zanzibar wanaishi chini ya mstari wa umasikini. Hivyo, uwezo wao wa kuyakidhi mahitaji yao ya kimsingi ya maisha ya kila leo ni mdogo mno.
Tukiziangalia hali za maisha ya Wazanzibari kwa kile kipimo ambacho wataalamu wa kiuchumi wanakiita kizigeu wiano cha Gini cha tofauti kati ya tajiri na maskini (the Gini coefficient of inequality) tutaona kwamba kuna usawa zaidi wa hali za maisha huko Zanzibar kuliko ilivyo Tanzania Bara au hata katika nchi nyingine za Afrika ya Mashariki. Bahati mbaya huo ni usawa wa ufukara. Hali za wengi wao ni za umasikini.
Moja ya athari za umasikini huo uliozagaa katika jamii ni kuongezeka kwa ufisadi pamoja na vitendo vingine vya ulaji rushwa na vya matumizi mabaya ya mali za umma. Ufisadi huo unazidi kwenda arijojo kwa vile mashirika au taasisi zinazowajibika kuuzuia hazina uwezo wa kuuchukulia hatua madhubuti.
Taasisi hizo pia huvunjwa nguvu kwa tashwishi za kisiasa za viongozi waliopanda vichwa na kujiona kuwa wao ndio wao, wenye nchi na vyote vilivyomo nchini.
Huo uroho wao wa mali na matumizi mabaya ya madaraka yao ya kiserikali ndio unaowafanya wakawa watovu wa nidhamu na wakathubutu kukiuka sheria na kujichukulia mali za umma, toka ardhi, majumba au kuzikodisha, tena kwa ujeuri, rasilimali za umma kwa bei za kutupwa ilimradi wao binafsi wanufaike. Potelea mbali ikiwa nchi inaingia hasara.
Hata hivyo, na juu ya shida zao zote hizo za kiuchumi, Wazanzibari wako makini na wanaonyesha kuwa wana subira na uvumilivu mkubwa. Wanaendelea kuwa na matumaini, pengine yaliyo makubwa kuliko pale yalipopatikana maridhiano na suluhu kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi — Civic United Front (CUF) — na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Ilipoundwa serikali hiyo, Novemba 2010, Wazanzibari wengi waliamini kwamba yale matatizo ya kiuchumi na ya kijamii waliokuwa wakiyakabili kwa muda mrefu yatatoweka.
Miongoni mwa matatizo hayo ni kuruka kwa haraka kwa bei za vyakula na za bidhaa nyingine zilizo muhimu kwa maisha, ufisadi na uzorotaji wa kazi serikalini, huduma zisizoaminika au kutabirika za umeme na maji na uchumi ambao kwa jumla umekuwa ukirudi nyuma ijapokuwa takwimu za serikali zinaonyesha vingine.
Ukweli wa mambo ulivyo hii leo Zanzibar ni kwamba jambo linalowashughulisha wengi ni namna ya kujipatia ajira ya halali itayowawezesha kupata pato. Hivyo changamoto yao kubwa ni namna ya kujipatia rizki na kujilisha wao na walio wao. Wengi wao wameshindwa.
Hata hivyo, bado wangali wakiamini kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa itachukuwa hatua za haraka za kuiondosha hiyo njaa iliyozagaa nchini.
Hapana shaka yoyote kwamba juu ya shida na mashakil ya kimaisha yaliyopo Zanzibar, maridhiano yamefanikiwa kuuzika ule uhasama wa kisiasa ulioibuka tangu mwaka 1957 pale wakoloni Wakiingereza walipoanzisha mfumo wa uchaguzi Visiwani humo.
Mfumo huo haukutumika toka 1964 hadi 1995 wakati ambapo kulikuwa na mfumo mbadala wa utawala wa chama kimoja, mfumo ambao tumeona jinsi ulivyowawezesha watawala kutumia vibaya madaraka yao.
Inatupasa tushukuru kwamba hii leo watu hawaonekani kuwa ni maadui wa taifa au makhaini wanapochukua msimamo wa kijasiri wa kuikosoa serikali yao, kama kwa mfano kuhusu suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Msimamo huo, niliokuwa nikiuashiria kwa muda mrefu katika makala mbalimbali, sasa umedhihirika bayana katika vikao na mihadhara inayofanywa Visiwani kuhusu Katiba mpya ya Tanzania.
Kikichojitokeza wazi ni jinsi Wazanzibari wanavyoupinga Muungano wa miaka 48 kati ya nchi yao na Tanganyika. Kwa kawaida, Wazanzibari ni watu walio wavumilivu, walio wataratibu na wa pole na wanajivunia ukarimu wao wa kuwapokea wageni wanaozuru Visiwa vyao. Hata hivyo, wana sifa ya kuwa wakali wanapohisi kuwa wanaingiliwa na wageni katika mambo yao ya ndani.
Historia imetuonyesha athari mbaya za wageni kuingilia siasa za Zanzibar kama kwa mfano pale Tanganyika ilipokiunga mkono chama cha Afro-Shirazi Party na Misri ilipokiunga mkono chama cha Zanzibar Nationalist Party (Hizbu).
Labda mambo yasingeliharibika lau nchi jirani zingewapatanisha Sheikh Abeid Karume na Sheikh Ali Muhsin waliokuwa viongozi wa vyama hivyo viwili vya huko Zanzibar. Uhasama kati ya vyama hivyo ndio uliopelekea Mapinduzi ya Zanzibar, kuundwa kwa Muungano na kutoweka kwa Zanzibar katika ramani ya dunia.
Wazanzibari wameshuhudia jinsi hali zao za kiuchumi, za kijamii na za kimazingira zilivyodidimia katika kipindi ambacho serikali yao ilipoteza mamlaka yake makuu ya kuendesha nchi. Mamlaka hayo yakaingizwa katika ‘mambo ya Muungano’ na kwa bahati mbaya hakuna ushahidi wenye kuonyesha kwamba Serikali ya Muungano ilifanya chochote cha kuisaidia Zanzibar ipate maendeleo.
Ndiyo maana Wazanzibari, hasa wa kizazi cha baada ya Mapinduzi, wanashikilia kwamba mfumo wa Muungano ubadilishwe na uwe juu ya msingi wa Mkataba na si Katiba.
Matokeo yake yataifanya kila moja ya nchi hizo mbili za kindugu — yaani Tanganyika na Zanzibar — iwe sawa na mwenzake bila ya mmojawao kujifanya kaka wa mwenzake. Wanachodai ni kila moja ya nchi hizo mbili iwe na uhuru wake na isiwe na haja ya kutaka ridhaa ya mwenzake inapochukuwa hatua kuhusu mustakbali wake.
Bila ya shaka nchi hizo zinaweza zikashauriana lakini ziwe zinashauriana zikiwa nchi sawa ndani ya Muungano unaotambua haki ya kila nchi kuwa na kura ya turufu na haki ya kujitoa katika jambo lolote kati ya mambo yatayokubaliwa kuwa ni mambo ya kushirikiana kati ya nchi hizo mbili.
Mchakato huu wa sasa wa Katiba umezipa nchi zote mbili za Tanganyika na Zanzibar fursa nzuri ya kujiandalia mwanzo mpya wa kujenga mahusiano ya karibu zaidi, yaliyo mema zaidi na yenye manufaa kwao. Nchi hizo zimekwishaamuliwa na historia pamoja na jiografia kwamba lazima ziwe zinafuata sera za ujirani mwema na zisiwe na uhasama wa nchi moja kutaka kuyachimba maslahi ya nchi nyingine.
Hizi ni nchi zenye historia moja na mustakbali mmoja na lazima zishirikiane kunyanyua hali za maisha ya Watanganyika na ya Wazanzibari — na hasa za Wazanzibari kwa sababu ingawa Tanganyika imepata maendeleo kwa kiasi fulani Zanzibar imerudi nyuma.
Viwango vyake vya maendeleo vinaaibisha na yote hayo yanatokana na miongo minne ya utawala mbovu huko Visiwani pamoja na sera ya ubaguzi iliyokuwa ikifuatwa kujaza nafasi za kazi serikalini.
Chanzo: Raia Mwema

Monday 21 May 2012

Jengo la Wizara Pemba labomoka

Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Uchumi Zanzibar, imekubwa na kashfa ya kutoa zabuni ya mradi wa Ujenzi kwa Kampuni isiyokua na sifa na kusababisha jengo la ghorofa kubomoka kabla ya kukamilika huko kisiwani Pemba.
Kwa mujibu wa ripoti ya kuchunguza ubadhirifu wa mali za Serikali ya Baraza la Wawakilishi (BLW), imesema wizara hiyo ilifunga mkataba na Kampuni ya Ujenzi Jonsons Costruction Limited kutoka nchini Kenya Mei 13, 2009.
Ripoti hiyo imesema kwamba wizara hiyo ilitoa zabuni ya ujenzi wa makao makuu ya wizara hiyo Pemba mradi ambao ulikuwa na thamani ya Sh 1,460,000,000, kinyume na sheria namba 6 ya usajili wa wakadarasi ya mwaka 2008.
Akihojiwa na kamati hiyo mhandisi kutoka Idara ya Ujenzi ya SMZ, Sabra Ameir Issa, alisema kwamba serikali iliwataka kufanya uchunguzi baada ya jengo kuanza kutitia kabla ya kukamilika.
Akifafanua mbele ya kamati hiyo, mhandisi Sabra, alisema tatizo kubwa waligundua mjenzi wa mradi huo, hakuwa na utaalamu unaohitajika katika kazi kama hiyo.
Mhandisi huyo alisema kwamba kampuni hiyo haina sifa ya kufanyakzi Zanzibar hata kupewa kwake zabuni na Wizara hiyo ilikuwa ni kwenda kinyume na sheria kwa sababu haikusajiliwa katika bodi ya wakandarasi Tanzania bara wala Zanzibar.
Alitaja sababu nyingine za jengo hilo kutitia kuwa ni ubunifu mbaya ya jengo, usimamizi mbovu, ujenzi uliokosa utaalamu, na uwezo mdogo wa mjenzi huyo.
Mhandisi Sabra, alisema katika uchunguzi wao walibaini hakuna Mhandisi hata mmoja wa ujenzi katika kampuni hiyo aliyesajiliwa na Bodi ya Wakandarasi Tanzania bara au Zanzibar.
Hata hivyo, mshauri mwelekezi wa mradi huo mhandisi Arch Yared Dondo, kutoka kampuni ya K&M Archplans Tanzania LTD, alieleza Kamati ya uchunguzi kwamba katika mchakato kumtafuta mkandarasi wa ujenzi huo Kampuni yake hakushirikishwa na Wizara huyo.
Alisema kwamba kwa upande wake hakuona kama ni tatizo kwa kuwa katika mkataba wao haikuonyeshwa kuwa anatakiwa kushiriki katika mchakato wa kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa jengo hilo.
Aidha Dondo, alisema kwamba mmiliki wa kampuni hiyo bahati mbaya sio mtaalamu wa ujenzi (Civil Enginer) bali ni fundi Bomba na kampuni yake haikuajili Muhandisi wa ujenzi hata mmoja kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo.
Mshauri mwelekezi pia alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza kufanyika bila ya kuwepo ‘Local Engineer’ hadi jengo linafikia hatua ya uwekaji msingi.
Hata hivyo alisema kabla ya kuanza kwa ujenzi huo walielekeza kila kitako cha nguzo kiwe na ukubwa wa Milimita 250 badala yake waliweka ukubwa wa Milimita 200 na kuna baadhi ya nguzo hazikuwekewa vitako na kutitia ardhini. “Msingi ulipokuja kubeba mzigo nguzo zikatitia kwenye matope.” Mshauri mwelekezi alisema katika mahojiano na kamati hiyo.
Ripoti ya kamati hiyo ambayo imeibua mjadala mkubwa Zanzibar, imesema Wizara hiyo pia haikuwa makini katika matumizi ya fedha za umma kwa vile mshauri mwelekezi alitakiwa kulipwa kwa kazi ya uchoraji na ushauri mil. 81,552,200/- lakini hadi kazi inafikia hatua ya awali tayali amelipwa Mil 65,344,470/- kabla ya maendeleo ya mradi kuonekana.
Upande wake Mkandarasi wa Ujenzi huo ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Jansons Construction LTD,LTDrvinder Singu Jandu, amekiri kuwa Kampuni yake imesajiliwa na Msajili wa Makampuni na sio Bodi ya Wakandarasi Tanzania Bara au Zanzibar.
Akihojiwa na Kamati ya Uchunguzi alisema mradi huo umeathiriwa na tatizo la maji ya bahari baada ya vitako vya nguzo vya zege kuathirika na kusababisha jengo kutitia chini ya ardhi.

Thursday 17 May 2012

Wanasiasa wakongwe: Acheni kupotosha chimbuko la Muungano

 Joseph Mihangwa
MENGI yamesemwa na kuandikwa juu ya chimbuko na kufikiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, 1964; lakini yote yenye kukinzana.
Tumefika mahali tukakata tamaa kuendelea kudadisi ukweli na kuacha kila mmoja wetu ajikite na kile anachoambiwa na kuamini namna Muungano huu ulivyofikiwa.
Wapo wanaodai kwamba Muungano huu ni matokeo na udugu wa miongo na hata karne nyingi wa wananchi wa nchi hizi mbili; na kwamba Rais wa awamu ya kwanza wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipendekeza kwa Rais wa awamu kama hiyo wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, naye akakubali sawia, kuunganisha nchi zao, akitaka Muungano imara wenye Serikali moja, lakini Nyerere akashikilia kuundwa kwa Muungano wenye Serikali mbili – Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.
Wapo pia wanaodai kwamba, Muungano huo ni shinikizo la mataifa makubwa ya Magharibi, enzi hizo za vita baridi, yaliyotaka, Zanzibar imezwe kwenye tumbo kubwa la Shirikisho la Afrika Mashariki kuepusha isikamatwe na kambi ya Ukomunisti wa nchi za Mashariki. Na pale Shirikisho hilo liliposhindwa kuanza, Mwalimu Nyerere, kwa msaada wa Marekani na Uingereza, aligeuka hima kuitia Zanzibar ndani ya tumbo la Tanganyika kwa njia ya Muungano tata.
Lakini imeelezwa pia kwamba, kwa muda mrefu, na hata kabla ya uhuru, Nyerere alikuwa na wasiwasi juu ya Visiwa vya Unguja na Pemba kuwa karibu mno na Tanganyika. Aliwahi kunukuliwa akisema:
“Kama ningekuwa na uwezo wa kukivuta kisiwa kile mpaka katikati ya Bahari ya Hindi, ningefanya hivyo….. Nadhani moja ya matatizo makubwa ya Tanganyika katika siku za mbele litakuwa Zanzibar. Kwa kweli sitanii; ni rahisi sana kuingiliwa na nchi za nje. Nina wasiwasi [Zanzibar] itatuletea matatizo makubwa”.
Je, hii inaweza kuwa moja ya sababu kwa Nyerere kutaka kuitia Zanzibar ndani ya tumbo la Tanganyika, baada ya mchakato wa Shirikisho la Afrika Mashariki kushindwa?.
Kuna ukweli gani baadaye, kwa matamshi ya Waziri wa Ulinzi na Mambo ya kigeni wa Tanganyika na kipenzi cha Nyerere cha wakati huo, Oscar Kambona, kuhusu sababu za Tanganyika na Zanzibar kuungana, aliposema:
“Wasiwasi wetu wa kwanza ulikuwa kuongezeka kwa Ukomunisti Visiwani (ukisimamiwa na kuunganishwa na Abdulrahman Mohamed Babu, kiongozi wa zamani wa Umma Party na baadhi ya makada wa ASP); na pili, hofu ya mataifa makubwa kujitumbukiza Zanzibar enzi hizo za vita baridi, kati ya nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani na Uingereza kwa upande mmoja, na Urusi na China kwa upande wa pili”?
Kuthibitisha hayo, Kambona alibainisha kuwa, mvutano wa mataifa makubwa tayari ulikuwa umeikumba Congo (sasa DRC) hadi kusababisha kuuawa kwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Congo, Patrice Lumumba. Na tayari, Yule Balozi jasusi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) aliyesimamia machafuko nchini Congo, Frank Carlucci, alikuwa amehamishiwa Zanzibar kuongoza machafuko kama hayo, kwa kile kilichoitwa mapambano dhidi ya Ukomunisti Visiwani.
Kwa mantiki hii, wapo wanaodai kuwa tatizo lilikuwa ni jinsi ya kuitenga Zanzibar na nchi za Kikomunisti, na hapo hapo Zanzibar isitumike na nchi za Magharibi kwa faida za nchi hizo.
Kwa hili, Nyerere alinukuliwa wakati mmoja akisema: “China Kisiwani, na Marekani wanasema ninapambana na Wakomunisti; tayari tuna Vietnam katika Afrika, na mimi sitakubali kamwe kuwa na hali hiyo”, akimaanisha kuwa hakutaka kuona Zanzibar ikigeuzwa kitovu cha migogoro Afrika Mashariki.
Inadaiwa pia kuwa, Karume alitia sahihi Mkataba wa Muungano bila kuelewa aina na mfumo wa Muungano aliokuwa akiingia. Na baada ya kubaini kwamba Muungano alioingia si ule aliokuwa akifikiria, aligeuka jeuri, kila mara akitishia kuuvunja akiufananisha na koti kwamba “ukiona linakubana au kukutia jasho, unalivua kwa hiari yako”.
Kuna ukweli gani kwa hili? Kati ya dhana hizi mbili, ya vita baridi na ya undugu wa zamani, ipi iliyozaa Muungano? Wanasiasa wote wakongwe ni wa dhana ile ya kwanza; lakini wasomi na wanazuoni walio wengi ni wa dhana ya pili. Kundi lipi lenye ushahidi usiohojika, kuweza kuthibitisha dhana yake?
Kwa hiyo, tunapoelekea kwenye mchakato wa kupata Katiba mpya nchini, ambapo suala la Muungano na kero zinazoambatana nao zinatikisa mustakabali wa Taifa, ni vyema tukadadisi na kupata ukweli wa jambo hili, utakaosaidia kupata Katiba makini isiyokuwa na ubabaishaji juu ya Muungano.
Tuachane na wanasiasa maslahi, wanaotaka tuamini kwamba Muungano ni “fumbo la imani” ili wao waendelee kunufaika kwa “tufani” wanayozua kila mara, na kujifanya wao “masiya” wa kero za Muungano wenye kuabudiwa. Fuatana nami katika mfululizo wa makala haya kupata majibu ya maswali haya.
Muungano Shinikizo la mataifa makubwa?
Tangu mwanzo, katu Nyerere hakuwa na wazo la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Yeye pamoja na Marais wenzake wa Kenya na Uganda, walipigania Shirikisho la Afrika Mashariki (EAC) kwa ridhaa kubwa ya nchi za Magharibi.
Hili linathibitishwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe kwenye taarifa yake kwa Mkutano wa nchi huru za Afrika, mjini Addis Ababa, mwaka 1960, aliposema:
“Wengi wetu tunakubali bila ubishi kwamba Shirikisho la nchi za Afrika Mashariki litakuwa jambo jema. Tunasema kwa uhakika kwamba, mipaka inayozigawa nchi zetu hatukuiweka sisi, bali iliwekwa na mabeberu; na hivyo tusiruhusu itumike dhidi ya umoja wetu….. Lazima tuwatake wakoloni si kutoa uhuru tu wa Tanganyika, kisha Kenya, na Uganda na hatimaye Zanzibar, bali tudai uhuru wa Afrika Mashariki kama jamii moja ya kisiasa”.
Kwa mujibu wa Nyerere, muungano wa aina ya shirikisho la kisiasa kwa nchi zote tatu za Afrika Mashariki kuunda jamii moja ya kisiasa (single political unit), ulikuwa bora zaidi kuliko muungano mwingine wa aina yoyote.
Miaka mitatu baadaye, Juni 5, 1963, viongozi wa nchi hizo tatu walikutana mjini Nairobi, kuendeleza mchakato, kuona Shirikisho la Afrika Mashariki linaundwa walitoa tamko lenye nguvu juu ya kuundwa kwa Shirikisho hilo wakisema:
“Sisi Viongozi wa watu wa nchi zetu, tunaaazimia kuunda Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki. Mkutano wetu wa leo unaongozwa na dhamira ya Umoja wa Afrika, na si ubinafsi na maslahi ya kikanda… Hii ni siku yetu ya vitendo kwa kuongozwa na maadili, tukiamini katika umoja na uhuru ambao tumesumbukia na kujitoa mhanga kwa mengi” (soma: A Declaration of Federation by Governments of East Africa, Kumb. Na. 13/931/63 DDT/1/1, na kuchapishwa kuwa kijitabu na Wizara ya Habari, Tanganyika, 1964).
Zanzibar, ambayo ilikuwa bado kwenye mchakato wa kupata uhuru miezi minne baadaye, Desemba 10, 1963, haikuwamo katika tamko hili, lakini ilipewa nafasi ya kujiunga itakapopata uhuru, na hivyo Azimio hilo lilisema: “Ingawa Zanzibar haikuwakilishwa katika kikao hiki, tunaweka wazi kuwa, nchi hiyo inakaribishwa kushiriki kikamilifu katika Mkutano wetu wa kuunda Shirikisho. Na mara Zanzibar itakapofanya chaguzi zake mwezi ujao (Julai 1963), Serikali yake itaalikwa kushiriki kwenye Tume inayoshughulikia uundaji wa Shirikisho, na kwenye taasisi yoyote itakayoundwa katika mipango yetu ya kuunda Shirikisho”.
Mpaka hapo, Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa championi na mwanaharakati kiongozi wa kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki, hakuwa na ndoto wala kuonyesha dhamira ya kuunda Muungano wa nchi yake na Zanzibar, mbali na azima pekee kuona Zanzibar inajiunga na Shirikisho la Afrika Mashariki.
Aidha, wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, 1964, viongozi wa Tanganyika, Kenya na Uganda walikuwa mjini Nairobi wakihudhuria Mkutano wa Shirikisho la Afrika Mashariki tarajiwa, na Zanzibar ilikuwa na mwakilishi.
Ilifika mahali kufuatia Mapinduzi ya Zanzibar, Marais Jomo Kenyatta wa Kenya, na Milton Obote wa Uganda, wakajitoa kwenye mchakato wa Shirikisho, huku Kenyatta akidai kwamba hakuwa tayari kupiga magoti kwa Nyerere. Kwa jinsi hii, mchakato wa Shirikisho la Afrika Mashariki ukafa; Nyerere akaachwa njia panda, azima yake ya kuona Shirikisho la Afrika Mashariki likiundwa ikayoyoma.
Hapa tutue kidogo na tujiulize: Je, kama Shirikisho la Afrika Mashariki lingefanikiwa, Muungano wa Tanzania, ambao wanasiasa wengi wanatuambia ni wazo la zama kabla na baada ya uhuru, ungetoka wapi? Na hili wazo jipya (baada ya juhudi za kuunda Shirikisho kushindwa) la Muungano wa nchi mbili – Tanganyika na Zanzibar, lilitoka wapi, na lilianzaje?
Nyerere abuni Muungano mpya
Mapema Februari 1964, huku akiwa amekata tamaa juu ya uwezekano wa kuundwa Shirikisho la Afrika Mashariki, Mwalimu Nyerere alimwita Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Roland Brown, akamwagiza amfanyie “kazi ya siri bila mtu mwingine yoyote kujua”. Kazi hiyo ilikuwa ni kuandaa Mkataba (Hati ya) wa Muungano wa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar.
Hatimaye, asubuhi ya Aprili 22, 1964, Mwalimu alitua Zanzibar akiwa na Hati hiyo mkononi iliyoandaliwa kwa lugha ya Kiingereza, kisha akamwomba Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, aisome na kutafakari, na (pengine) akiridhika, aitie sahihi.
Karume aliiangalia Hati hiyo; na bila kupoteza muda alichukua kalamu; na wawili hao wakatia sahihi zao; wakishuhudiwa na Oscar Kambona (Tanganyika) na Abdullah Kassim Hanga (Zanzibar) na wengine waliokuwapo. Mwalimu alirejea Dar es Salaam siku hiyo hiyo. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ukawa umezaliwa.
Siku mbili kabla ya kutiwa sahihi Mkataba wa Muungano, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Wolfango Dourado, alipewa “likizo” ya siku saba ya lazima, na badala yake aliitwa Mwanasheria kutoka Uganda, Dan Wadada Nabudere, kumshauri Karume juu ya pendekezo la Muungano.
Haijafahamika bado ni kwa nini Karume alifanya hivyo, na matokeo yake akatia sahihi Hati ambayo aliilalamikia baadaye, kwamba amechengwa juu ya Muundo wa Muungano.
Hati hiyo waliyotia sahihi Marais hao wawili ilikuja kujulikana kama “Hati (Mkataba) ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”. Siku tatu baadaye, Aprili 25, Mabunge ya nchi hizo mbili yaliridhia makubaliano hayo na kuwa Sheria ya Muungano.
Aprili 26, 1964 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitangazwa rasmi, umma ukazizima kwa furaha iliyochanganyika na hofu na mashaka, huku wengi wasiweze kuamini kilichotokea; na wengine wakiuliza: ni lini mtoto huyo aliyezaliwa (Muungano) alitungiwa mimba?.
Mazingira na mikakati iliyowezesha kuundwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilizua maswali lukuki, mengi hayajapata jibu hadi sasa, na mengine yanaendelea kuwa kiota cha migogoro ya Muungano hadi leo.
Siku za baadaye, Nyerere alinukuliwa akisema kwamba, alitoa pendekezo la Muungano kwa Karume (kimzaha mzaha) wakati Karume alipomtembelea Mwalimu kuzungumzia suala la “Field Marshal” John Okello, naye Karume alikubaliana na wazo la Mwalimu papo kwa papo, na akapendekeza sawia Mwalimu awe Rais wa Muungano huo.
Wengi wanakubali kwamba, kulikuwa na usiri mkubwa kati ya Nyerere na Karume juu ya suala la Muungano. Kama kuna watu walioshirikishwa mwanzoni, basi watakuwa ni Rashidi Kawawa na Oscar Kambona kwa upande wa Tanganyika; Abdallah Kassim Hanga na Salim Rashid, kwa upande wa Zanzibar.
Je, Muungano huo ni matokeo ya juhudi za hiari za waasisi wake kama baadhi ya watu wanavyodai, au ni matokeo ya shinikizo kutoka nje?.
Chanzo: 

Hatuwezi kuijadili Tanzania bila kuujadili Muungano

Na generali Ulimwengu
KATIKA muktadha wa mjadala kuhusu kuandika katiba mpya, nimekuwa nikisema kwamba yapo masuala ya kikatiba ya aina mbili: aina ya kwanza ni yale ambayo, hata kama yanaumua hisia kali miongoni mwa wanasiasa, bado yanaweza kupata ufumbuzi wake ndani ya muda mfupi.
Aina ya pili ni ile ya masuala ambayo, hata kama hayaibui hisia kali miongoni mwa wanasiasa na watawala, lakini yana umuhimu mkubwa, ufumbuzi wake hauwezi kupatikana kirahisi au katika muda mfupi.
Aina ya kwanza, kama naruhusiwa kukariri yale niliyokwisha kuyasema, ni ile inayohusu matatizo ya kiutawala na yanayogusa mgawanyo wa madaraka katika ngazi mbalimbali za utawala.
Kuna mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mitatu ya dola (Utawala, Bunge na Mahakama); ukomo wa madaraka ya ofisi za watawala; ukomo wa madaraka ya Bunge; ukomo wa mamlaka ya Mahakama; maingiliano kati ya mihimili hiyo, na kadhalika.
Katika kuyaandikia vipengele vya kikatiba, masuala ya aina hii yatapatiwa majibu kwa kufuata utashi wa kisiasa wa wale walio madarakani pamoja na raia wenzao wenye ujuzi wa mambo na ari ya kuchangia katika maendeleo ya taifa lao.
Mara nyingi maoni yao yatatokana na ujuzi wa kitaaluma katika nyanja za siasa, sheria na historia, na jinsi wanavyoiangalia jamii wanamoishi na mahitaji yake ya wakati huo.
Wajuzi hawa watadurusu mifumo mingi duniani na katika historia, ili kuona kama wanaweza kujifunza namna wenzao walivyoshughulikia hoja zilizo mbele yao. Katika nchi nyingi za Jumuia ya Madola (Commonwealth), mara nyingi wataalamu watajikita zaidi katika historia ya kikatiba ya Uingereza na mfumo unaoitwa wa ‘kibunge”. Lakini wakati mwingine wataenda nje ya mfumo huo na kufanya majaribio ya kuchanganya dhana za mfumo wa kibunge na mfumo unaoitwa wa ‘kirais.’
Ndivyo tulivyofanya sisi kwa kuchanganya dhana hizo mbili, na ndiyo maana tumejenga ofisi zenye utata, kama ile ya ‘waziri mkuu’ asiyekuwa waziri mkuu kwa maana ya mfumo wa ‘kibunge.’
Wanaofuatilia masuala haya watajua kwamba waziri mkuu wa Uingereza ni kiongozi wa wabunge wa chama chake na serikali yake, lakini si bosi wa mawaziri wake. Anaitwa ‘primus inter pares’ (first among equals, ama kiongozi wa walio sawa).
Hata hivyo, inapobidi waziri mkuu achukue uamuzi au abebe lawama, yeye ndiye mkuu wa kufanya hivyo. Hawezi kumwachia malikia majukumu hayo.
Tutaona kwamba hiyo ni tofauti kabisa na jinsi tunavyoendesha mambo yetu kikatiba nchini, na mifano ya hivi karibuni imedhihirisha, kwa mara nyingine tena, utata wa ofisi ya waziri mkuu na mambo mengine yanayotokana na kuchanganya dhana hizi mbili.
Hata hivyo, mimi naamini kwamba haya ni mambo yanayowezwa kurekebishwa iwapo kuna utashi wa kisiasa na uangavu wa mawazo, na utambuzi wa uzoefu wetu kihistoria utakaotuwezesha kuona ni wapi tulipata usumbufu wa kimuundo na ni vipi tunaweza kurekebisha.
Haya ni masuala ya kimpangilio ambayo hayahitaji muda mrefu mno wala tafakuri ya kuchosha kuyapatia ufumbuzi. Utashi wa kisiasa na umahiri wa wajuzi wa mambo vinatosha kuyaangalia, kuyajadili na kuyaweka bayana, kuonyesha njia kadhaa zinazoweza kufuatwa, na hatimaye kuchagua njia mwafaka kwa wote, au kwa walio wengi kwa wakati tulio nao.
Tunaweza kuteua utaratibu wa ‘kibunge’ au ule wa ‘kirais,’ au tunaweza kuteua kuendelea na mseto wetu wa hivi sasa, pamoja na utata wake.
Wakati tukifanya hivyo, tunaweza pia kuamua mambo kama vile mawaziri kutokuwa wabunge; madaraka ya rais kupunguzwa na kukabidhiwa kwa asasi mahsusi; matokeo ya kura za rais kupingwa ndani ya kipindi kilichopangwa, na mambo kama hayo. Haya yote, na mengine kama haya, tunayamudu katika kipindi cha miezi 18.
Sasa tuangalie masuala ambayo ni mazito , nyeti na tata, ambayo yanahitaji tafakuri ya muda mrefu na ambayo hayatatuliki kwa watawala kuwa na utashi wa kuyatatua ama kwa wajuzi wa mambo kuwa na weledi na umahiri uliojipambanua.
Haya ni yala masuala ambayo yanahitaji maridhiano ndani ya jamii ambazo zinaweza kuwa na maslahi yanayokinzana, na wakati mwingine maslahi hayo yakiwa yamejenga uhasama ndani ya jamii hizo, hususan kwa sababu bado jamii hizo hazijapata, au hazijajitengenezea, wasaa wa kuyajadili kwa kina masuala muhimu.
Sina budi kuanza na suala la Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, ambayo ndiyo Tanzania. Juhudi yo yote inayolenga kuwaambia wananchi kwamba wanaweza kuandika katiba mpya kujadili masuala yote yanayohusu nchi yao bila ya kujadili kwa kina sula la Muungano ni kazi bure.
Maana ya juhudi kama hizo ni sawa na kuwaambia watu wajadili kila kitu kadri wanavyotaka lakini wasiijadili Tanzania yenyewe, jambo ambalo halieleweki.
Katiba haina budi kusimama juu ya misingi ya aina ya Tanzania tunayotaka kuijenga, na hiyo ni pamoja na kile kinachoifanya Tanzania kuwa Tanzania, na hicho ni Muungano. Sasa inawezekana vipi kuijadili Tanzania kwa kutoijadili Tanzania?
Sote tunaelewa kwamba yapo maoni yanayopishana mno kuhusu Muungano kama muungano, na pia muungano kwa maana ya mifumo yake na michakato yake. Ni kusema kwamba wapo watu wanaoamini kwamba Mungano, pamoja na kwamba una matatizo kadhaa, ni jambo jema na ambalo linafaa kuendelezwa huku matatizo yake yakirekebishwa ili kukidhi maslahi ya wana-Muungano wote.
Wapo wanaoamini kwamba Muungano hauna haja ya kuendelea kuwapo kwa sababu mbalimbali. Wengine wanazitaja sababu hizo, na wengine hawautaki kwa sababu tu hawautaki.
Kisha wapo watu ambao wanauona Muungano kama kitu kilichopo na ambacho wamekizoea, lakini hawajui kama una manufaa au hauna manufaa, na wala hawaoni ni kwa nini watu wanasumbua akili zao juu ya jambo kama hilo.
Baina ya misimamo hii, naamini kwamba kila mmoja una mantiki yake, na si busara kuenenda kama vile upande mmoja lazima umebebwa na mantiki nzito zaidi kuliko mwingine. Busara inasema tuujadili Muungano, na tuujadili katika marefu na mapana yake na pia kina chake katika kila eneo.
Itakuwa hasara kubwa iwapo tutaingia katika zoezi la kuandika katiba mpya (kama kweli tumedhamiria kuandika katiba mpya, na si kugongagonga iliyopo) bila kujadili kwa kina asasi hii muhimu kuliko zote.
Kitakuwa ni kichekesho cha gharama kubwa iwapo tutajidai tumeandika katiba mpya halafu baada ya miaka miwili au mitatu tuanze kuunda tume, mara “Tume ya Bakari”, mara “Tume ya Yohana” eti “kuangalia kasoro za Muungano na kupendekeza marekebisho ya kuuboresha.”
Tume hizi tumeziona, mapendekezo yake tumeyasoma, lakini hakuna kilichobadilika kimsingi kwa sababu kila mara juhudi zilizofanyika zimekuwa ni za kupoza jazba, kutuliza hisia, “kufunika kombe”, kama wasemavyo Waswahili, ili “mwanaharamu apite”.
Kama kawaida yetu, tumekataa kufanya kazi ya kina, kazi ya kudumu, kazi ya mtazamo wa masafa marefu. Tuna haraka kama vile tuko katika mpito tukielekea kwingine, sijui wapi?
Hakuna sababu ya kukumbushana kwamba huu ni muungano wa nchi mbili zilizokuwa huru kabla ya kuungana. Ingawaje ni kweli kwamba walio wengi katika nchi yetu wamezaliwa chini ya Muungano, bado ni kweli pia kwamba hisia za u-Tanganyika na u-Zanzibari hazijatoweka moja kwa moja.
Zimekuwa zikichomoza mara kwa mara, na kila mara zikizimwa kwa njia ambazo hazikushughulikia masuala ya msingi yaliyojitokeza wakati huo. Tusipoujadili Muungano kwa kina, upana na urefu, kwikwi hizi zitaendelea kujitokeza kama kielelezo cha matatizo yanayofunikwa funikwa kila mara.
Chanzo: Raia Mwema

Sunday 13 May 2012

CCM: Mgombea binafsi haepukiki

KAMATI YA KINANA YAWAAMBIA WANACHAMA WAJIANDAE KISAIKOLOJIAWaandishi wetu
SHINIKIZO la wananchi kutaka mgombea binafsi, limeanza kukilainisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuwataka wanachama wake kujiandaa kisaikolojia kwa kukabaliana na wagombea hao katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Kwa muda mrefu kumekuwa na shinikizo kutoka kwa watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wanaharakati na wanasheria wanaotaka kuwepo kwa mgombea binafsi jambo ambalo pia kiliwahi kupigiwa debe na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mnamo mwaka 1995.

Mwalimu aliwahi kusema: “Mimi nadhani sheria imekosea kuzuia wagombea binafsi. Hili jambo limekosewa ni la msingi. Ndiyo maana napenda kulisema ni la msingi, linahusu haki yangu na yako ya kupiga kura na kupigiwa kura. Hii ni haki ya uraia.”

Jana, katika kikao cha semina ya viongozi ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM, Kamati iliyoundwa na chama hicho kuangalia jinsi kinavyoweza kuwasilisha maoni yake katika Tume ya Katiba, ilitaka wanachama kujiandaa kwa suala hilo.

Suala la mgombea binafsi limekuwa likipingwa na chama hicho kwa muda mrefu kwa hofu kuwa lingeweza kukiumiza pindi wanachama wake wanaposhindwa kura za maoni, kwani wangeweza kusimama binafsi na kushinda.

Lakini, kamati hiyo ambayo iliongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Abdulrahman Kinana, jana ilitoa mapendekezo mbalimbali ikiwamo muundo wa Muungano huku ikiwataka wanaCCM kujiandaa kukabiliana na mgombea huyo binafsi.

Chanzo chetu ndani ya kikao hicho, kilisema miongoni mwa mapendekezo hayo ni Serikali tatu; Shirikisho, Tanganyika na Zanzibar. Pia, kuna pendekezo la Serikali mbili, huku ikitoa manufaa na athari za kila pendekezo.

Mapendekezo mengine ni pamoja na muundo wa Bunge na upatikanaji wa wabunge, ikipendekeza kuwapo kwa mabunge mawili, mojawapo lenye mamlaka ya juu na jingine likiwa na mamlaka ya chini.

Mapendekezo hayo ambayo yataanza kujadiliwa na wajumbe wa Nec, yanaonekana kuwa mtego kutokana na hali ndani ya chama hicho ilivyo hivi sasa.

“Hii inaonekana tumepewa kamba tujimalize wenyewe, maana suala la mgombea binafsi kwa vyovyote vile lazima litakuwa kwenye Katiba Mpya, njia ambazo tumekuwa tukitumia zimefikia mwisho, utashi wa wananchi utachukua mkondo wake, hivyo lazima tujipange,” kilidokeza chanzo chetu.

Katika kikao cha CC juzi, baadhi ya wajumbe walitaka Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa asilaumiwe kutokana na wanachama wa chama hicho kukimbilia Chadema, pia wakipinga George Mkuchika kubaki katika Baraza la Mawaziri.

Moto wa mgombea binafsi
Moto wa kuwepo kwa mgombea binafsi katika chaguzi za kisiasa ulianzishwa na Mchungaji Christopher Mtikila alipofungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma mwaka 1993 akiiomba iruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi.

Katika hukumu iliyotolewa Oktoba 24, 1994 na Jaji Kahwa Rugakingira, Mchungaji Mtikila aliibuka mshindi.

Hata hivyo, Serikali ilikata rufaa Mahakama ya Rufani, lakini wakati rufaa hiyo ikisubiri usikilizwaji na uamuzi, Serikali ilipeleka muswada bungeni na kufanya marekebisho ya kikatiba na kuweka ibara inayotamka kuwa kila mgombea ni lazima awe amependekezwa na chama cha siasa.

Februari 17, 2005, Mchungaji Mtikila alifungua kesi nyingine Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam akipinga marekebisho hayo ya Katiba ya mwaka 1994. Katika kesi hiyo alikuwa akiiomba Mahakama hiyo pamoja na mambo mengine, iamuru kuwepo kwa mgombe binafsi.

Katika hukumu iliyotolewa Mei 5,2006, Mchungaji Mtikila aliibuka mshindi kwa mara nyingine baada ya Mahakama Kuu kukubaliana na hoja na maombi yake na kuwepo kwa mgombea binafsi.

Hukumu hiyo ilitolewa na na jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu wakiongozwa na aliyekuwa Jaji Kiongozi, Amir Manento, Salum Massati na Thomas Mihayo.

Serikali ilikata tena rufaa katika Mahakama ya Rufani, ikipinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu, iliyosikilizwa na Jopo la Majaji Saba wa Mahakama ya Rufani Aprili 8, 2010.

Katika hukumu yake ya Juni 16, 2010, Mahakama ya Rufani ya Tanzania ilitolewa na jopo la majaji hao saba walioongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani, mahakama hiyo ilijifunga mikono baada ya kusema kuwa haina mamlaka ya kutengua ibara ya Katiba.

Wengine katika jopo hilo la majaji walikuwa Eusebio Munuo, Januari Msofe, Benard Luanda, Mbarouk Mbarouk, Nathalia Kimaro na Sauda Mjasiri

Malisa hajafukuzwa
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Benno Malisa, jana walilazimika kutoka nje ya ukumbi wa mikutano na kukutana na waandishi wa habari kukanusha taarifa za kiongozi huyo wa juu wa umoja wa vijana kufukuzwa Kamati Kuu (CC).

Taarifa zilizosambaa juzi na jana, zilidai kuwa Malisa alifukuzwa CC baada ya kuhoji uteuzi wa wakuu wa wilaya ambao Rais Jakaya Kikwete aliufanya hivi karibuni.

Nape alisema hakuna kitu cha aina hiyo na kwamba, hicho ni kati ya vikao vya chama hicho vilivyowahi kufana na kufanyika kwa furaha tofauti na taarifa zilizokuwa zinasambazwa.

Naye Malisa alisema ameshangazwa na taarifa hizo kwa sababu bado ni Mjumbe wa CC na alikuwa akihudhuria kikoa cha Halmashauri Kuu.

Uteuzi Makatibu wa wilaya

Kamati Kuu (CC) ya CCM imefanya uteuzi wa makatibu wa wilaya 32 kujaza nafasi zilizokuwa wazi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo baadhi kuteuliwa kuwa wakuu wa wilaya na kwamba watapangiwa kazi baadaye.

Makatibu hao ni Grayson Mwengu, Abdallah Hassan, Ernest Makunga, Mgeni Haji, Innocent Nanzabar, Nicholaus Malema, Mercy Mollel, Michael Bundala, Elisante Kimaro, Zacharia Mwansasu, Eliud Semauye, Habas Mwijuki, Loth Ole Nasele na Charles Sangura.

Wengine ni Donald Magessa, Fredrick Sabuni, Janeth Mashele, Daniel Parokwa, Zongo Lobe Zongo, Mwanamvua Killo, Joyce Mmasi, Simon Yaawo, Epimack Makuya, Amina Kinyongoto, Asia Mohammed, Venosa Mjema, Augustine Minja, Elly Minja, Ernest Machunga, Seleman Majilanga, Christina Gukwi na Joel Mwakila.

Habari hii imeandikwa na Midraji Ibrahim na Habiel Chidawali, Dodoma na James Magai, Dar

Chanzo: Mwananchi

Thursday 10 May 2012

Mazingile mwanambiji yanayomkabili Warioba

Na Ahmed Rajab
TUME ya Katiba, chini ya uwenyekiti wa Jaji Joseph Warioba, imekwishaanza kujipanga na kujipangia namna itavyokuwa inafanya kazi. Kwa mujibu wa sheria ya kuundwa kwa Tume hiyo kazi yake kubwa itakuwa ni kupita kila pembe ya Tanzania kwa madhumuni ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya ya taifa, kuyachambua maoni hayo na kuyaratibu.
Hadi sasa hatujui ni mwongozo gani utakaofuatwa na Tume hiyo katika kuendesha shughuli zake. Nielewavyo ni kwamba kwa sasa wajumbe wa Tume wanaipima hali ya mambo ilivyo nchini kuhusu mchakato mzima wa Katiba mpya.
Mengi bado hayajulikani kuhusu namna Tume hiyo itakavyofanya kazi zake lakini nafikiri kwamba kufikia mwisho wa wiki au mwanzoni mwa wiki ijayo Warioba ataweza kutueleza jinsi Tume yake itakavyoanza kuendesha shughuli zake.
Jambo la kwanza la kutiwa maanani ni kwamba itakuwa muhali kwa wajumbe wote wa Tume kufuatana pamoja kwenda kila mahala. Watabidi wagawane sehemu watazokwenda; hawa wende huku na wengine wende kwengine. Vikundi vya Tume vitakuwa vya mchanganyiko wa watu kutoka Bara na wale wa kutoka Visiwani.
Kwa ufupi, Tume ya Katiba ina kazi mbili: mosi, kushauriana na wananchi na kujua wanasema nini kuhusu Katiba na pili, kuyatathmini maoni ya wananchi na kutoa mapendekezo.
Juu juu kazi hiyo inaonyesha kuwa ni rahisi na isiyokuwa na utata. Si jambo gumu kutega masikio na kuyasikiliza maoni ya watu ila labda pale wenye kutega masikio wanapokuwa na masikio ya kufa. Na sidhani kwamba wajumbe wa Tume ya Katiba ni watu wa sampuli hiyo.
Tatizo litazuka katika kuyachambua na kuyaratibu hayo maoni ya wananchi ambayo lazima yatakuwa ni yenye kutofautiana na kukinzana. Tatizo kubwa zaidi litazuka pale wajumbe wa Tume watapokaa kitako wakawaza na kuwazua na kuyatathmini maoni watayoyapata na kutoa mapendekezo.
Hapo patahitajika uadilifu wa hali ya juu kabisa katika kuyapambanua maoni hayo na kuyapanga. Uadilifu huo utahitajika kwa sababu lazima patatolewa maoni ambayo hayatowapendeza wale wenye kujiona kwamba wao ndio wenye uamuzi wa mwisho juu ya mustakabali wa taifa.
Hayo yako bayana zaidi huko Zanzibar ambako tayari tunasikia sauti kubwa zikipazwa kuupinga mfumo wa sasa wa Muungano, sauti ambazo baadhi ya wakubwa wanataka zizimwe. Bado haijulikani lini Tume itafunga safari yake ya kwanza kwenda Zanzibar kusikiliza maoni ya wananchi.
Warioba aliwakuna wengi alipotamka kwamba Tume yake haitofanya kazi kwa shinikizo za mtu yeyote au za kikundi chochote. Ijapokuwa hadi sasa hatujui ni mwongozo gani Tume hiyo itaufuata ni jambo la kutia moyo kuona kwamba Warioba ametoa hakikisho hilo. Ni jambo la kutia moyo kwa sababu endapo atajiachia ashinikizwe basi naye anaweza akawapotosha wajumbe wa Tume yake kwa kuwapitisha kwenye mazingile mwanambiji ya kichaka cha huo mchakato wa kulipatia taifa Katiba mpya.
Nikizungumzia yanayojiri Zanzibar wananchi wengi wa huko wanaisubiri kwa hamu kubwa Tume ya Katiba kwani itawapa fursa ya kutoa maoni yao juu ya aina ya Katiba waitakayo na hususan juu ya mfumo wa Muungano wanaoutaka. Wanaipata fursa hiyo kutokana na ile sheria iliyouanzisha huu mchakato wa Katiba mpya.
Sheria hiyo hiyo inatambua kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni Muungano wa nchi mbili tofauti, yaani Tanganyika (au Tanzania-Bara) na Zanzibar. Utambuzi huo ndio msingi wa Tume ya Katiba yenye wajumbe 32 (tukimjumlisha mwenyekiti na kaimu wake), iwe na wajumbe 16 kutoka Bara (Tanganyika) na 16 wengine kutoka Zanzibar.
Hii ni hatua muhimu sana kwa sababu labda hii ni mara ya mwanzo Zanzibar inawakilishwa inavyostahili katika taasisi za Muungano tangu Muungano wenyewe uundwe miaka 48 iliyopita. Ni matarajio ya wengi kwamba kwa vile Zanzibar inawakilishwa vilivyo kwenye Tume hiyo basi maslahi yake yatalindwa na wajumbe wa Tume watokao Visiwani.
Hayo bila ya shaka yatategemea juu ya msimamo utaochukuliwa na wajumbe wa Katiba – ama wa kila mmoja wao binafsi au wa pamoja kama kundi la Wazanzibari walioteuliwa na Rais wa Tanzania baada ya kupendekezwa na Rais wa Zanzibar na kwa ridhaa yake. Wajumbe hao wataiwakilisha Zanzibar mpaka utapopatikana mfumo mpya wa uhusiano baina ya Tanganyika na Zanzibar, mfumo ambao utapatikana kwa makubaliano ya pande hizo mbili ama juu ya msingi wa Katiba au, kama Wazanzibari wengi wanavyotaka, juu ya msingi wa mikataba baina ya nchi mbili, kila moja ya nchi hizo ikiwa na uhuru na mamlaka kamili ya kuendesha shughuli zake za ndani na ya nje ya nchi.
Wajumbe wa Tume kutoka Zanzibar wana fursa isiyo na kifani ya kuhakikisha kwamba Wazanzibari wanaupata mradi wao na hivyo kujenga msingi madhubuti wa uhusiano wa karibu na wa kindugu baina ya Tanganyika na Zanzibar. Wazanzibari wanataraji kwamba uhusiano huo mpya utaziwezesha nchi hizo mbili ziheshimiane na zitambue kwamba kila mojawao ni sawa na mwenziwe. Kwa lugha ya mitaani wanachotaraji Wazanzibari wengi ni kwamba hakuna nchi itayojaribu ‘kuionea’ nyingine kwa misingi ya ukubwa wa eneo la nchi au nguvu za kijeshi.
Inavyoonyesha ni kwamba wengi wa Wazanzibari wamekwishaamua wanataka nini kitokee utapomalizika mchakato huu wa Katiba. Wanachotaka ni kuiona serikali yao inarejeshewa mamlaka yake kamili yatayoiwezesha kuyatanzua matatizo ya kiuchumi na kijamii yaliyoikumba nchi yao kwa muda wote huu wa miaka 48 tangu ulipoundwa Muungano.
Kwa sasa serikali hiyo imelemaa kwa sababu haina uwezo wa kuyalinda ipasavyo maslahi ya Zanzibar kwa vile wanaamini ya kwamba shughuli zote za utawala zilizo muhimu na za kimsingi zimehaulishwa kwenye Serikali ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano.
Tatizo ni kwamba Katiba hiyo yenyewe haikutungwa kihalali na wananchi hawakuwa na usemi wowote katika utungwaji wake. Matokeo yake, na huu ndio ukweli unaowachoma Wazanzibari, Serikali ya Zanzibar imegeuka kuwa sawa na ‘serikali ya mkoa’ au serikali ya manispaa. Ndio maana hakuna ushahidi kwamba Serikali ya Tanzania inashiriki katika maendeleo ya Zanzibar au kwamba inatenga fungu la fedha za Serikali ya Muungano kwa maendeleo ya Zanzibar. Kwa hakika, tunaweza kusema kwamba hiyo ndiyo sababu moja kubwa inayowafanya Wazanzibari wawe wanaupinga vikali Muungano na wanasubiri tu fursa itayowawezesha kuyamwaga rasmi na hadharani malalamiko yao.
Wajumbe wa Zanzibar katika Tume ya Katiba wameteuliwa kuiwakilisha Zanzibar kama wenzao walivyoteuliwa kuiwakilisha Tanzania-Bara. Uteuzi huo unaainisha kwamba wakuu wa Tanzania wanaelewa wazi kwamba ile iliyokuwa Tanganyika ina maslahi yaliyo tofauti na yale ya Zanzibar. Hivyo, wajumbe wa Bara katika Tume watautetea msimamo wa Tanganyika na haitostaajabisha endapo watataka mfumo wa Muungano uliopo sasa uendelee vivi hivi ulivyo baada ya kutiwa viraka vya hapa na pale.
Wenzao kutoka Zanzibari watakuwa na jukumu gumu zaidi la kuhakikisha kwamba maoni ya Wazanzibari wengi yanaheshimiwa na kuwasilishwa kwa njia itayowaridhisha. Maoni hayo ni yenye kutaka pawepo mageuzi makubwa zaidi na ya kimsingi katika mfumo wa Muungano.
Kadhalika ni wazi kwamba umma wa Zanzibar unaofuatilia mchakato huu kwa shauku kubwa utakuwa unawaangalia kwa macho mawili wajumbe Wakizanzibari walio katika Tume ya Katiba.
Ili waweze kuyatetea maslahi ya Zanzibar, wajumbe Wakizanzibari watawajibika wafanye kazi kwa pamoja na itakuwa jambo zuri iwapo wataongozwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar. Serikali hiyo nayo inawajibika iwe na msimamo ulio sawa na ule wa Wazanzibari wengi juu ya Muungano, hasa kwa vile Zanzibar inajigamba kuwa ni yenye utawala wa kidemokrasia wenye kuongozwa na matakwa ya Wazanzibari.
Chanzo: Raia Mwema

Zanzibar siyo taifa kamili

Mhariri wa gazeti hili ameamua kuichapicha makala hii kutokana na umuhimu wake nchini wakati huu wa kuelekea kuandika Katiba mpya. Ni makala iliyoandikwa na aliyekuwa Mbunge wa Chunya, Njelu M. Kasaka, miaka 19 iliyopita (1993) na kuchapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Mwananchi.
WAKATI uchunguzi unafanywa na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu uhalali wa Zanzibar kujiunga na Organization of Islamic Conference (OIC) na wakati wa mjadala bungeni kuhusu suala hili mambo mengi yaliyojitokeza. Moja ya mambo yaliyojitokeza kwa nguvu kabisa lilikuwa ni nafasi ya Zanzibar katika Muungano wa Tanzania.
Madai yalitolewa kuwa kwa Bunge kuchunguza suala la Zanzibar kujiunga na OIC ni kuionea Zanzibar kwani hiyo ni nchi huru na taifa kamili (independent sovereign state) lenye uwezo wa kuingia mikataba na mataifa mengine. Viongozi wengi wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na Alhaji Aboud Jumbe, Wolfgang Duarado na Ali Nabwa, mwandishi wa habari wa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, wote walisisitiza kuwa Zanzibar ni nchi huru na taifa kamili.
Hakuna mtu aliyetazamia suala kama hili kuzuka na kupata umuhimu lililoupata. Watanzania wengi hasa Bara, walidhani wanauelewa Muungano na kwamba Zanzibar na Tanganyika zilishaungana na kuwa Tanzania. Lakini hoja zilianza kutolewa ambazo zimeturudisha nyuma miaka 29 iliyopita ili kuangalia upya maana ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni nini.
Kuna swali la kujiuliza. Hivi ni kweli Zanzibar ni nchi huru na ni taifa kamili ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, au ni sehemu tu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyo na uhuru wa kushughulikia mambo yake ya ndani? Ili kupata jibu la swali hili yatupasa kuangalia makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Ibara ya kwanza ya makubaliano ya Muungano (Articles of Union) inasema hivi “Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitaungana na kuwa taifa moja ambalo ni Jamhuri”. Kutokana na makubaliano hayo Jamhuri ya Tanganyika ilitoweka, kadhalika Jamhuri ya Watu wa Zanzibar nayo ilitoweka tukapata Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taifa jipya la Tanzania likazaliwa.
Je, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inasemaje juu ya suala hili? Ibara ya kwanza ya Katiba inasema: “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano,” na ibara ya pili, ibara ndogo ya kwanza inaeleza kuwa, “Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar.”
Katiba hii ndiyo ambayo viongozi wote wa Jamhuri ya Muungano (pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) huapa wanapopewa madaraka, kuiheshimu na kuilinda wakati wote wanapokuwa kwenye madaraka.
Kutokana na maelezo hayo hapo juu ni dhahiri kuwa katika Jamhuri ya Muungano tunayo nchi moja tu na taifa moja tu nalo ni Tanzania. Hakuna taifa jingine ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo kauli ya viongozi wa Zanzibar kuwa Zanzibar ni taifa kamili, ni kauli ya kukana makubaliano ya Muungano (Articles of Union), ni kauli ya kuikana Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kwa hiyo ni kauli ya kutaka kudhoofisha Muungano na hatimaye kuuvunja.
Muungano wa Tanzania ni Muungano wa nchi mbili yaani Tanganyika na Zanzibar. Kuwepo kwa Muungano wa namna hii kunategemea sana nchi zote mbili kubaki kikamilifu ndani ya Muungano.
Nchi moja ikitoka, basi Muungano husambaratika mara moja Kwa maana hiyo basi, iwapo Zanzibar inadai kuwa yenyewe ni nchi kamili, basi Muungano haupo kwa sababu makubaliano ya Muungano hayakutoa nafasi ya Zanzibar kuwa taifa kamili ndani ya Muungano.
Wala Tanzania Bara haiwezi kuwa peke yake ndiyo Jamhuri ya Muungano kwa kujivika jaketi la Muungano. Kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha makubaliano ya Muungano na kinyume cha Katiba inayosema Tanzania ni pamoja na Tanzania Bara na Zanzibar.
Hakuna Rais wa Zanzibar?
Ukisoma makubaliano ya Muungano (Articles of Union) hakuna ibara inayozungumzia juu ya Rais wa Zanzibar, Kulingana na makubaliano hayo hakuna Ofisi ya Rais wa Zanzibar bali Ofisi za Makamu wawili wa Rais. Moja wa Makamu hao wa Rais ambaye kwa kawaida atakuwa mtu mkazi wa Zanzibar, atakuwa ndiye Kiongozi msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa masuala yanayohusu Zanzibar.
Kwa hiyo kuwepo kwa Ofisi ya Rais wa Zanzibar kama inavyofahamika sasa ni moja kati ya mambo mengi yaliyopenyezwa ndani ya mfumo wa Muungano nje ya makubaliano ya Muungano ya 1964.
Moja ya matatizo makubwa yaliyoufikisha Muungano kwenye mgogoro wa sasa ni muundo wa Serikali mbili. Serikali mbili katika Muungano wa nchi mbili una matatizo.
Hivi sasa Serikali ya Muungano ndiyo hiyo hiyo Serikali ya Tanzania Bara wakati Serikali ya Mapinduzi ni kwa ajili ya Zanzibar tu.
Katika kuendesha Serikali hizi kumezuka hisia kwa Wazanzibari kuwa Serikali ya Muungano ni Serikali ya Tanzania Bara. Kwa mtazamo huo, kila utakapoongeza uwezo zaidi kwa Serikali ya Muungano maana yake unaongeza uwezo Tanzania Bara dhidi ya Serikali ya Zanzibar, na Wazanzibari watakataa.
Unaporuhusu Serikali ya Zanzibar iwe na uwezo zaidi katika masuala ambayo Watanzania Bara wanayaona kuwa ni ya Muungano, maana yake unadhoofisha Muungano.
Serikali ya Muungano inapokuwa hiyo hiyo ndiyo Serikali ya Bara inashindwa kuchukua hatua za kinidhamu Zanzibar inapokiuka makubaliano ya Muungano kwa kuogopa itaonekana inaionea Zanzibar kwa kuwa ni nchi ndogo kwa kila hali ukilinganisha na Tanzania Bara. Pia itatafsiriwa kuwa Tanganyika inataka kuimeza Zanzibar.
Hali kadhalika Zanzibar hushindwa kuchukua hatua yoyote Serikali ya Muungano inapokwenda kinyume cha makubaliano ya Muungano kwa vile serikali ile ni ya Muungano. Lakini pia Zanzibar yaweza isichukue hatua yoyote kwa vile haileweki kama kitendo cha Serikali ya Muungano kimefanywa kama Serikali ya Muungano au kama Serikali ya Bara.
Kibaya zaidi ni hisia zilizojengeka sasa kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar ni sawa, hakuna iliyo na kauli juu ya mwenziwe katika jambo lolote. Kwa hiyo mambo inayofanya Serikali ya Muungano huonekana kuwa yanahusu Bara na Zanzibar haijishughulishi nayo.
Madai ya Serikali Tatu
Hivi sasa watu wengi Zanzibar na Bara wanadai Serikali tatu ili mambo ya Muungano yajulikane waziwazi na mambo yasiyo ya Muungano yajulikane pande zote mbili za Muungano. Wasioafiki hoja ya Serikali tatu wametoa sababu tatu:-
  • Kwa vile hakuna muundo usiokuwa na matatizo, basi tuendelee na muundo huu ingawa una matatizo mengi. Wenye hoja hii wanasahau kuwa ingawa muundo wowote ule haukosi matatizo, aina moja ya Muungano yaweza kuwa na matatizo makubwa zaidi. Huu ni muundo ambao hauruhusu hata nchi nyingine kujiunga bila ya muundo wenyewe kubadilika.
  • Muundo wa shirikisho yaani Serikali tatu utaifanya Serikali ya Muungano kutokuwa na nguvu na waweza kusababisha Muungano kuvunjika. Hapa swali la kujiuliza ni kwamba serikali kutokuwa na nguvu kwa upande gani? Kwa hali ilivyo sasa, Serikali ya Muungano ina nguvu Bara lakini Zanzibar haina nguvu kabisa. Afadhali Serikali ya Shirikisho kwa mambo ya Muungano itakuwa na nguvu pande zote ukilinganisha na hali ya sasa ya muundo wa Serikali mbili.
  • Kwa vile Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume walikubaliana kuwa na serikali mbili, basi hakuna sababu ya kubadilisha sasa. Sababu hii haina maana yoyote bali ni ubabaishaji tu na hakuna haja ya kuzungumzia zaidi. Mimi nakubaliana na Muungano wa Serikali tatu ambao ulipendekezwa na Tume ya Nyalali. Muundo huu unaleta usawa na haki kwa pande zote mbili za Muungano. Kudumu kwa Muungano wowote ule hakutegemei muundo wake bali hutegemea nia thabiti ya kisiasa ya kutaka Muungano uendelee. Kama nia haipo bila ya kujali muundo wake, Muungano husambaratika.
Nia ikiwepo nchi shiriki huheshimu makubaliano ya Muungano. Je, makubaliano yetu ya Muungano yanaheshimiwa? Nadhani wakati umefika kwa makubaliano yetu ya Muungano kuangaliwa upya.
Suala la kuhusu uwezo wa Bunge na Serikali ya Muungano juu ya Zanzibar, ibara ya nne ya makubaliano ya Muungano inayataja mambo yafuatayo kuwa chini ya mamlaka ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; Mambo ya Nchi za Nje, Ulinzi, Polisi, Madaraka ya kutangaza hali ya hatari, Uraia, Uhamiaji, Biashara ya Nje na Mikopo, Utumishi katika Serikali ya Muungano, Kodi ya Mapato, Kodi ya Mashirika; Ushuru wa Forodha na Kodi ya Mauzo; Bandari; Mambo ya Usafiri wa Anga; Posta na Telegraphs.
Katika mambo haya makubaliano yanatoa madaraka yote (exclusive authority) kwa Bunge na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa nchi nzima. Ni kutokana na ukweli huu nashindwa kukubaliana na wale wanaosema Bunge halina madaraka kuhoji suala la Zanzibar kujiunga na OIC.
Kadhalika nashindwa kuelewa baadhi ya viongozi wetu wanaposema Katiba ina utata na haikuwa wazi katika kuonyesha yapi ni mambo ya Muungano na yapi ni mambo ya ndani ya Zanzibar. Ninaloliona hapa ni kushindwa kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano na yapi ni mambo ya ndani ya Zanzibar. Ninaloliona hapa ni kushindwa kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano kutekeleza Makubaliano ya Muungano ya 1964, basi.
Pia sikubaliani na hoja kwamba kujiunga na OIC si suala la Muungano. Suala hili linagusa Katiba na mambo ya Nchi za Nje ambayo yametajwa na makubaliano ya Muungano kuwa ni mambo ya Muungano. Kwa hiyo iwapo tafsiri ya Zanzibar kwamba mambo haya si ya Muungano itakubaliwa na Serikali ya Muungano, basi hakuna mambo ya Muungano na ndiyo kusema hakuna Muungano!
Ningependa pia kuzungumzia suala jingine ambalo linajitokeza katika makala ambazo amekuwa akizitoa Alhaji Aboud Jumbe aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Katika makala hizo Alhaji Jumbe amelalamikia vitendo kadhaa ambavyo anadai vilitendwa na Serikali iliyoongozwa na Mwalimu Julius Nyerere lakini vilikuwa kinyume na msimamo na maadili ya taifa hili.
Malalamiko ya Jumbe yanachukua sura ya mtu ambaye yeye mwenyewe hakuwepo ndani ya Serikali hiyo. Lakini kama Watanzania wote wanavyojua ni kwamba Alhaj Jumbe alikuwa kiongozi wa ngazi ya juu katika taifa hili tangu Muungano mwaka 1964. Ameshika nyadhifa mbalimbali za juu katika Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kipindi cha miaka 20.
Yeye alishiriki
Leo kwangu mimi linakuwa ni jambo la kushangaza ninapoona Jumbe amekaa kando analaumu vitendo vya Serikali ambavyo yeye mwenyewe alishiriki kwa namna moja au nyingine! Ni vigumu kuamini kuwa Jumbe hakuhusika na uandaaji na utekelezaji wa sera mbalimbali wakati wa Serikali ya Mwalimu Nyerere.
Katika kuzungumzia suala hili, si madhumuni yangu kumshambulia Alhaji Jumbe bali ni kutaka kuonyesha mambo mawili ambayo yamejitokeza katika makala zake. Kwanza ni maamuzi ya pamoja ambayo Serikali yetu imekuwa ikisisitiza kuwa ndiyo msingi unaofuatwa katika kufikia maamuzi muhimu ya kitaifa. Maamuzi ya pamoja mara nyingi hufikiwa kwenye vikao ambavyo Mheshimiwa Jumbe alikuwa ni mshiriki kwa miaka ishirini.
Maamuzi mengi kiserikali hupitia kwenye Baraza la Mawaziri ambako Mheshimiwa Jumbe kwa wadhifa wake kama Makamu wa Kwanza wa Rais, alikuwa anapata nafasi ya kuwa Mwenyekiti wakati Rais hayupo. Ni dhahiri Mheshimiwa Jumbe alikuwa na nafasi nzuri ya kuzuia vitendo vya serikali vilivyoonekana kuwa havifai. Kwa mantiki hii kama kuna vitendo vyovyote vya kulaumiwa katika Serikali iliyopita, basi Jumbe hawezi kuzikwepa lawama hizo.
Pili, inawezekana kweli kwamba mambo yaliyokuwa yanafanywa na Serikali iliyopita Jumbe au kiongozi mwingine yeyote hakuwa na uwezo wa kuzuia au kubadili mwelekeo. Hapo napo inabidi tujiulize kwa nini? Moja ni kwamba Mheshimiwa Jumbe alishindwa kutumia vema madaraka aliyopewa na hivyo kuacha sera mbovu ziendelee kutekelezwa ingawa yeye mwenyewe alikuwa haziafiki. Kama hivyo ndivyo ni kosa la nani?
La msingi ni pale ambapo kiongozi kama Mheshimiwa Jumbe anashindwa kufanya lolote kwa sababu Rais wa nchi ana madaraka makubwa yanayomruhusu kufanya lolote bila kuulizwa na mtu yoyote. Na hili nadhani ndilo tatizo lililokuwepo (na bado lipo) wakati Alhaji Jumbe alipokuwepo madarakani.
Wakati viongozi walikuwa wanahubiri uongozi wa pamoja, viongozi hao hao kwa kupitia chama kinachotawala na Bunge waliendelea kurundika madaraka makubwa kwa Rais wa nchi kiasi kwamba hatimaye vyombo vingine vyote vilibaki bila madaraka kabisa.
Katika mazingira ya namna hiyo ingawa maamuzi mbalimbali huwa ni ya vikao, hali halisi ni kwamba maamuzi yote hufanywa na mtu mmoja. Kiongozi wa namna hiyo baadaye huacha hata kuwasikiliza viongozi wenzake na wao wasiwe na la kufanya kwa kuwa madaraka yote yako mikononi mwake.
Kiongozi mwenye madaraka makubwa hivyo aweza kuliyumbisha taifa bila ya kujijua. Matakwa yake binafsi huchukuliwa kuwa ndiyo matakwa ya taifa. Akimchukia mtu yeyote, basi taifa zima humchukia mtu huyo! Msimamo wake juu ya suala fulani basi huo ndiyo utakaokuwa msimamo wa taifa.
Kwa kifupi ni kwamba kila atakaloamua kulifanya kiongozi wa nchi litafanyika hata kama halifai. Viongozi wenzie ambao ndio waliompa madaraka hayo makubwa, hunung’unikia pembeni lakini hadharani wanamuunga mkono katika kila jambo analolifanya.
Inawezekana Alhaji Jumbe alijikuta katika mazingira ya namna hiyo. Kama kuna mambo ambayo yalikuwa yanafanyika ndani ya Serikali na yeye binafsi alikuwa hapendi, alishindwa kuzuia kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa amepewa kiongozi wa Serikali, yaani Rais.
Wakati huo huenda Alhaji Jumbe hakuweza kutoa malalamiko yake hadharani kwa kuogopa. Lakini leo kwa kuwa hakuna la kuogopa, anatoa malalamiko yake hadharani na kulaumu!
Nimezungumzia suala la Mheshimiwa Jumbe kwa kirefu ili kuonyesha hatari iliyopo kwa taifa kukabidhi madaraka yote kwa mtu mmoja na kuviacha vyombo vingine (Bunge, Mahakama, Halmashauri Kuu ya Taifa) kutokuwa na madaraka.
Rais siyo taifa…
Madaraka yanapaswa kusambazwa kwa madhumuni ya kuleta uwiano wa madaraka na uwezo, kwa taasisi mbalimbali ili kutotoa mwanya wa vishawishi kwa Rais kutawala kwa kadiri anavyopenda. Utaratibu huu huviwezesha vyombo vingine kumzuia Rais kufanya jambo ambalo ni kinyume cha Katiba au hata maadili tu ya taifa yaliyojengeka kwa muda mrefu.
Taifa lazima liwe na uwezo wa kumzuia kiongozi wa nchi siyo tu anapofanya mambo kinyume cha Katiba, bali hata anapotumia uwezo wa Ofisi yake vibaya. Uwezo kama huo unapotolewa kwa taasisi za taifa isitafsiriwe kuwa una lengo la kumwandama kiongozi fulani, bali yote yanafanywa kwa manufaa ya taifa hili la leo, kesho na kesho kutwa.
Jambo jingine ambalo Watanzania wanapaswa kulizingatia ni kutofautisha kati ya taifa na Rais. Rais si taifa lakini taifa si Rais. Tofauti hii ni muhimu kwani ndiyo itakayowezesha Watanzania kujua ni wakati gani vitendo vya Rais havilingani na maadili na matakwa ya taifa. Ni kwa mtazamo huo Wamarekani walikataa vita ya Vietnam ambayo waliiona haina umuhimu wowote kwao.
Kutenganisha kati ya Rais na taifa ni muhimu pia katika kuamua kama kiongozi aliyepo aendelee au hapana uchaguzi unapofika. Vigezo muhimu ni kama vile kutekeleza matakwa ya taifa na si yale anayotaka yeye, mwenendo na tabia zake kuendana na maadili ya taifa na kama Katiba inaheshimiwa.
Kimsingi yaliyomo kwenye Katiba ndiyo matakwa na msimamo wa watu na kwa hali hiyo si suala la kiongozi wan chi kuamka na kusema “Nimefanya hivi kwa kuwa Katiba ina kasoro, tutasahihisha baadaye.”
Mwenendo kama huu haukubaliki. Kila kitendo anachotenda kiongozi wa nchi lazima Katiba iwe inaruhusu. Pale ambapo Katiba hairuhusu lakini ni lazima hatua zichukuliwe, basi hurekebishwa kwanza ili kumpa uwezo halali kiongozi wan chi kutekeleza wajibu wake ipasavyo, mambo ya dharura ni suala jingine.
Uchaguzi unapofika kiongozi wa nchi huchaguliwa tena au kutochaguliwa kulingana na alivyotekeleza majukumu yake kipindi kilichopita. Kiongozi wa nchi aliyeshindwa kutekeleza matakwa ya wananchi na taifa huangushwa. Madhumuni ya kufanya hivyo ni kutaka kumpata kiongozi anayeweza kuliongoza taifa vizuri, kwa mafanikio na bila ya kukiuka Katiba.
Kadhalika, wananchi humchagua kiongozi mpya ili aweze kusahihisha na kurekebisha makosa aliyofanya kiongoziu aliyetangulia. Wananchi hawachagui kiongozi mpya wa nchi ili kuendeleza makosa aliyofanya kiongozi aliyetangulia.
Mwanzo potofu
Kwa mantiki hii sikubaliani na mawazo ya Alhaji Jumbe. Katika makala zake kwa gazeti hili hivi karibuni Alhaji Jumbe alidai kuwa Mwalimu Julius Nyerere alichanganya siasa na dini kwa kuwapendelea Wakristo. Kwa hiyo, na Rais Ali Hassan Mwinyi afanye hivyo hivyo kwa kuwapendelea Waislamu! Mawazo haya ni potofu.
Msimamo wa taifa letu tangu uhuru ni kutochanganya siasa na dini, na Katiba yetu inasema hivyo. Kama kuna ushahidi kuwa Nyerere alichanganya siasa na dini wakati wa utawala wake, hilo ni kosa. Alichofanya ni kinyume cha Katiba na kinyume cha maadili ya taifa.
Tunachokitazamia kutoka kwa utawala wa sasa si kurudia makosa bali kuyasahihisha na kulirudisha taifa kwenye msimamo wake. Kosa ni kosa hata lingetendwa na nani.
Kuna mifano katika nchi kadhaa. Serikali mpya inashika madaraka na ikigundua kuwa viongozi waliopita waliendesha Serikali yao bila kufuata Katiba au walitumia madaraka vibaya, huwa wanakamatwa na kufikishwa mahakamani. Wanapopatikana na makosa huadhibiwa. Itakuwaje basi Serikali ya sasa ya Tanzania badala ya kurekebisha makosa yaliyotendwa na Serikali iliyopita (kama yapo) ijitumbukize katika makosa ya aina ile ile?
Ningependa kumaliza kwa kuwaomba Watanzania wote na hasa viongozi kujiepusha na kauli au vitendo vinavyoweza kusababisha uhasama na vurugu kati ya jamii moja na nyingine ya kitanzania.
Lakini si rahisi kurudisha amani na utulivu kati ya jamii hizo bila ya gharama kubwa kwa maisha ya watu na mali zao.
Na baya zaidi ni kwamba upendo na kuaminiana ambavyo vimejengeka baina ya jamii mbalimbali za Watanzania vinaweza visipatikane tena hata baada ya karne moja kupita. Mifano ya namna hiyo imezagaa ndani na nje ya Afrika, hatuhitaji kuambiwa
Chanzo: Raia Mwema

Friday 4 May 2012

Kikwete atangaza baraza jipya la mawaziri


ORODHA YA MAWAZIRI NA NAIBU MAWAZIRI

MAWAZIRI
1.  OFISI YA RAIS
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu)Ndugu Stephen M. Wasira, Mb.,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Utawala Bora)Ndugu George Mkuchika, Mb.,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (UTUMISHI)Ndugu Celina Kombani, Mb.,


2.         OFISI YA MAKAMU WA RAIS
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (MUUNGANO)Ndugu Samia H.  Suluhu, Mb.,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (MAZINGIRA)Dr. Terezya P.L. Huvisa, Mb.,


3.            OFISI  YA WAZIRI MKUU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri  Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji)Ndugu Mary M. Nagu, Mb.,
Waziri wa Nchi, Ofisi  ya Waziri Mkuu (TAMISEMI)Ndugu Hawa Ghasia, Mb.,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge)Ndugu William V. Lukuvi, Mb.,


4.            WIZARA 
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika MasharikiNdugu Samuel J. Sitta, Mb.,
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Ndugu Shamsi Vuai Nahodha, Mb.,
Waziri wa UjenziDr.  John P. Magufuli, Mb.,
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dr. Hussein A.H. Mwinyi, Mb.,
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya UfundiDr. Shukuru J. Kawambwa, Mb.,
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na WatotoNdugu Sophia M. Simba, Mb.,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa KimataifaNdugu Bernard K. Membe, Mb.,
Waziri wa Katiba na Sheria Ndugu Mathias M. Chikawe, Mb.,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya NchiNdugu Emmanuel Nchimbi, Mb.,
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na UvuviDr. David M. David, Mb.,
Waziri wa Kazi na Ajira Ndugu Gaudentia M. Kabaka, Mb.,
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na TeknolojiaProf.  Makame M. Mbarawa, Mb.,
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof.  Anna K. Tibaijuka, Mb.,
Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe,  Mb.,
Waziri asiyekuwa na Wizara MaalumProf. Mark Mwandosya, Mb.,
Waziri wa  Kilimo, Chakula na UshirikaEng. Christopher Chiza, Mb.,
Waziri wa Uchukuzi Dr. Harrison Mwakyembe, Mb.,
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na MichezoDr. Fenella E. Mukangara, Mb.,
Waziri wa Maliasili na Utalii Ndugu Khamis Kagasheki, Mb.,
Waziri wa Viwanda na Biashara Dr. Abdallah O. Kigoda, Mb.,
Waziri wa Fedha Dr. William Mgimwa, Mb.,
Waziri wa Nishati na MadiniProf. Sospeter Muhongo, Mb.,


5.          NAIBU MAWAZIRI


 OFISI YA RAIS


HAKUNA NAIBU WAZIRI


6.           OFISI YA MAKAMU WA RAIS
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa RaisNdugu Charles Kitwanga, Mb.,


7.            OFISI YA WAZIRI MKUU
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi  ya Waziri Mkuu (TAMISEMI)Ndugu Majaliwa K. Majaliwa, Mb.,
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi  ya Waziri Mkuu (TAMISEMI)Ndugu Aggrey Mwanry, Mb.,


8.          WIZARA MBALIMBALI
Naibu Waziri wa Kazi na AjiraDr. Makongoro M. Mahanga, Mb.,
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na UshirikaNdugu Adam Malima, Mb.,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya NchiNdugu Pereira A. Silima, Mb.,
Naibu Waziri wa Viwanda na BiasharaNdugu Gregory G. Teu, Mb.,
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na UvuviNdugu Benedict N. Ole-Nangoro, Mb.,
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa KimataifaNdugu Mahadhi J. Maalim, Mb.,
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo  ya Makazi,Ndugu Goodluck J. Ole-Medeye, Mb.,
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Ndugu Ummy A. Mwalimu, Mb.,
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Ndugu Philipo A. Mulugo, Mb.,
Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Abdulla Juma Abdulla, Mb.,
Naibu Waziri wa Maliasili na UtaliiNdugu Lazaro Nyalandu, Mb.,
Naibu Waziri wa UjenziNdugu Gerson Lwenge, Mb.,
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Dr. Seif Suleiman Rashid, Mb.,
Naibu Waziri wa Nishati na MadiniNdugu George Simbachawene, Mb.,
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Ndugu January Makamba, Mb.,
Naibu Waziri wa UchukuziDr. Charles J. Tizeba, Mb.,
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na MichezoNdugu Amos Makala, Mb.,
Naibu Waziri wa Maji Eng. Dr. Binilith Mahenge, Mb.,
Naibu Waziri Nishati na Madini Ndugu Stephen Maselle, Mb.,
Naibu Waziri wa Katiba na SheriaNdugu Angela Jasmine Kairuki, Mb.,
Naibu Waziri wa FedhaNdugu Janet Mbene, Mb.,
Naibu Waziri wa FedhaNdugu Saada Mkuya Salum, Mb.,

Chanzo: Globalpublishers

Wednesday 2 May 2012

Necta yapunguzia adhabu wanafunzi 3,000

BARAZA la Mitihani Tanzania (Necta), limepunguza adhabu ya kufutiwa matokeo watahiniwa 3,303 wa kidato cha nne mwaka 2011, waliobainika kufanya udanganyifu na kufungiwa kufanya mtihani kwa miaka mitatu, sasa watatumikia kifungo hicho kwa mwaka mmoja.

Tamko la Necta limekuja wiki chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwaahidi wabunge kuwa Serikali itawasiliana na baraza hilo na kuangalia uwezekano wa kupunguza adhabu hiyo.

Pinda alisema hayo kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo baada ya Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), kuitaka Serikali iwasamehe wanafunzi hao ambao aliwaelezea kuwa kitendo cha kuwafutia matokeo kilitosha kabisa na sasa waruhusiwe kurudia mtihani.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako, alisema jana kuwa baraza limechukua hatua hiyo baada ya kutathmini maombi mbalimbali yaliyotolewa na wakuu wa shule, wanafunzi waliofutiwa matokeo, wazazi wao na wadau wengine.

Hata hivyo, Dk Ndalichako hakueleza iwapo hatua hiyo wameichukua baada ya shinikizo la Serikali.
“Wadau wengi walikiri kosa, lakini waliomba kupunguzwa kwa adhabu ya kutofanya mitihani kwa miaka mitatu… Wakuu wa shule na watahiniwa husika wameahidi kuwa iwapo watapewa fursa hiyo watakuwa makini zaidi kuhakikisha wanazingatia taratibu za mitihani,” alisema Dk Ndalichako.

Kwa sababu hiyo, Dk Ndalichako alisema Necta imewaruhusu wafanye mtihani kama watahiniwa wa kujitegemea mwaka 2013, kwa sababu mwaka huu wameshachelewa katika mchakato wa usajili.

“Uamuzi wa Baraza umezingatia kuwa kitendo cha watahiniwa na wadau wengine walioathirika na adhabu hiyo kuomba msamaha kimeonyesha kuwa wametambua athari zinazoweza kutokea kutokana na kufanya udanganyifu,” alisema.

Necta ilitoa adhabu hiyo kwa wanafunzi hao wa kidato cha nne mwaka 2011, baada ya kufanya kikao Februari mwaka huu na kuthibitisha kuwa walifanya udanganyifu kwenye mitihani mbalimbali waliyofanya.
Licha ya kutoa msamaha, Dk Ndalichako alisema Necta itaendelea kutoa adhabu kali kwa wale ambao itabaini wamefanya udanganyifu kwenye mitihani.

Alisema bado Necta itaendelea kufanyia uchunguzi ripoti ya kamati maalumu iliyochunguza chanzo cha udanganyifu kwenye mitihani na wahusika wote watachukuliwa hatua.

Dk Ndalichako alisema matokeo ya awali ya uchunguzi huo yanaonyesha kuwa, kuna walimu na wasimamizi wa mitihani walioshirikiana kusababisha udanganyifu huo ikiwamo kuwafanyia mitihani.

“Watahiniwa wengine walichelewa kuingia katika vyumba vya mitihani wakisubiri uwezekano wa kupata taarifa za maswali ya mitihani kutoka kwa wasimamizi wasio waadilifu, kuyajibu na kuingia wakiwa tayari na majibu hayo,” alisema Dk Ndalichako.

Kasoro nyingine, ni baadhi ya wasimamizi kupangiwa shule wanazofundisha, wanafunzi kutofanyiwa upekuzi kabla ya mitihani, wanafunzi kusongamana na kutoa mwanya wa kutazamiana, wasimamizi na askari kusafiri kwenda kuchukua mitihani badala ya kupelekewa vituoni na mitihani kufunguliwa ofisini badala ya chumba cha watahiniwa.
Chanzo: Mwananchi