UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 11 Machi 2011, Serikali ilichapisha Muswada wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 katika Gazeti la Serikali la tarehe
hiyo. Muswada huo ulipelekwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano kwa Hati ya Dharura. Hata hivyo, baada ya upinzani mkubwa
dhidi ya Muswada huo kujitokeza karibu nchi nzima, Bunge lililazimika
kuondoa Hati ya Dharura na hivyo kufanya Muswada kushughulikiwa kwa
mujibu wa utaratibu wa kawaida wa kutunga sheria uliowekwa na kanuni za
80, 83 na 84 za Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano, 2007.
Katika kufanya hivyo, Bunge – kwa kupitia Spika – liliiagiza Serikali
kufanya mambo yafuatayo kwa mujibu wa Taarifa Rasmi ya Majadiliano
Katika Bunge (Hansard) ya Kikao cha Nane cha Mkutano wa Tatu cha tarehe
15 Aprili 2011:
(a) “Muda zaidi utolewe kwa Kamati na wananchi kuufikiria Muswada huu.
Katika kufanikisha hili, “… iandae Muswada huu kwa lugha ya Kiswahili
ili wananchi wenyewe waweze kusoma yaliyomo kwenye Muswada huo badala ya
kupewa tafsiri tu na watu wengine;
(b) “Muswada uchapishwe kwenye magazeti na kutangazwa kwenye vyombo
mbali mbali vya habari ili kutoa fursa ya kutosha kwa wananchi wengi
kuuelewa na kuutolea maoni;
(c) “Utangulizi wa Muswada huu uwekwe vizuri zaidi ili wananchi waelewe
madhumuni ya Muswada huu, kwani imeonekana wazi wananchi wengi wanadhani
tayari tumeanza kuandika Katiba, kumbe lengo la Muswada huu ni kutunga
Sheria ya Kuunda Tume ya Kukusanya Maoni tu.” (uk. 31-32)
Mheshimiwa Spika,
Katika kutoa maagizo haya, Bunge lilisitiza kwamba “… Muswada huu uko
ndani ya Bunge, hauko serikalini.” (uk. 33) Hii ni kwa sababu, kwa
mujibu wa kanuni ya 84(1) ya Kanuni za Bunge, Muswada ulikwishasomwa kwa
mara ya kwanza na kupelekwa kwenye Kamati inayohusika kwa ajili ya
kuanza kujadiliwa. Aidha, kwa mujibu wa kanuni ya 84(2) Kamati
ilikwishaanza kupokea maoni ya wadau “… kwa lengo la kuisaidia katika
uchambuzi wa Muswada huo.” Kazi iliyokuwa imebaki kwa Kamati ilikuwa ni
kutumia mamlaka yake chini ya kanuni ya 84(3) “… kufanya marekebisho
katika Muswada wa Sheria kwa kumshauri Waziri … anayehusika na Muswada
huo kufanya mabadiliko….” Ni baada tu ya kupata ushauri wa Kamati kuhusu
mabadiliko ndio Serikali ingeweza kuleta Jedwali la Mabadiliko kwa
lengo la kufanya mabadiliko katika hatua hii kabla Muswada haujaletwa
Bungeni kwa ajili ya kusomwa mara ya pili na kwa mjadala wa Bunge zima.
Mheshimiwa Spika,
Hakuna hata moja ya maagizo haya ya Bunge ambalo limetekelezwa na
Serikali. Tafsiri ya Kiswahili ambayo imeletwa Bungeni – pamoja na
kuonyesha imesainiwa tarehe 8 Machi 2011 sawa na Muswada wa Zamani
uliopigiwa kelele sana na wananchi – ililetwa kwenye Kamati wiki mbili
zilizopita, ikiwa ni wiki moja baada ya Kamati kukataa kuujadili Muswada
Mpya kwa vile ulifanyiwa mabadiliko na Serikali bila kupata ushauri wa
Kamati kama inavyotakiwa na kanuni ya 83(4) ya Kanuni za Bunge. Badala
ya kutekeleza maagizo ya Bunge, Serikali imeleta Muswada wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ambao ulichapishwa katika Gazeti la
Serikali la tarehe 14 Oktoba 2011.
Muswada huu mpya una tofauti kubwa na za kimsingi na Muswada wa Zamani
kama nitakavyoonyesha hapa. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, mabadiliko makubwa na ya kimsingi yaliyofanywa kwenye Muswada
wa Zamani yalihitaji na bado yanahitaji mjadala wa kitaifa wa wananchi
kama ambavyo wengi wamedai katika mijadala inayoendelea nchi nzima.
Aidha, Bunge hili tukufu lilihitaji, na bado linahitaji, muda zaidi wa
kuyatafakari mabadiliko haya makubwa nay a kimsingi katika Muswada wa
Zamani. Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini
ni busara na ni sound policy kwa Muswada huu Mpya kusomwa mara ya Kwanza
ili kuruhusu mjadala unaohitajika kufanyika.
TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyokuwa kwa Muswada wa Zamani, Muswada huu unapendekeza kuundwa
kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo, kwa mujibu wa Utangulizi wa
Muswada, itawajibika “… kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi juu ya
Katiba (na) kuainisha na kuchambua maoni ya wananchi….” Kwa mujibu wa
ibara ya 5, Tume hii itaundwa na Rais “kwa kushauriana na kukubaliana na
Rais wa Zanzibar, na kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar….”
Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 6(1), Rais atateua wajumbe wa Tume “… kwa
kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar….”
Ibara ya 6(2) inapendekeza kwamba “… muundo wa Tume utazingatia msingi
wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya
Muungano.” Pendekezo hili linarudia, kwa njia iliyojificha zaidi,
msimamo wa ibara ya 6(2) ya Muswada wa Zamani iliyokuwa imeweka wazi
kwamba idadi ya wajumbe wa Tume itakuwa sawa kwa sawa kwa pande zote za
Jamhuri ya Muungano! Kama ilivyokuwa kwa Muswada wa Zamani, ibara ya
7(2) ya Muswada inapendekeza kwamba “uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti utafanyika kwa msingi kwamba iwapo Mwenyekiti atatoka upande
mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Makamu Mwenyekiti atakuwa mtu
anayetoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano.”
Muundo wa Tume unakamilishwa na Sekretarieti ya Tume itakayoongozwa na
Katibu. (ibara ya 13(1) Kwa mujibu wa ibara ya 13(2), Katibu huyo
atateuliwa na Rais “baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibar.” Watendaji
wengine wa Sekretarieti watateuliwa na Waziri “kwa makubaliano na
Waziri mwenye dhamana ya mambo ya Katiba wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar.”
Muswada unapendekeza kumpa Rais – baada ya makubaliano na Rais wa
Zanzibar – mamlaka ya kutoa hadidu za rejea za Tume na muda wa
kukamilisha na kuwasilisha ripoti. (ibara ya 8(1) Na kama hali itahitaji
kufanya hivyo, Rais – “kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar” – anaweza
kuongeza muda usiozidi miezi mitatu ili kuwezesha Tume kukamilisha na
kuwasilisha ripoti. (ibara ya 8(2) Hadidu za rejea, kwa mujibu wa ibara
ya 8(3), “… zitakuwa ni hati ya kisheria ambayo Tume itaizingatia katika
utekelezaji wa majukumu na utumiaji wa mamlaka yake kwa mujibu wa
Sheria hii.”
Mheshimiwa Spika,
Ibara ya 9(1) ya Muswada inaelezea kazi za Tume kuwa ni pamoja na:
(a) Kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi;
(b) Kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba
yanayohusu mamlaka ya watu, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa
sheria na utawala bora;
(c) Kutoa mapendekezo kwa kila hadidu ya rejea; na
(d) Kuandaa na kuwasilisha ripoti.
Ijapokuwa haijaanishwa hivyo, ni wazi – kwa mujibu wa wa ibara ya
17(1)(d) na (2) ya Muswada – kwamba moja ya kazi za Tume ni kuandaa
Rasimu ya Muswada wa Katiba mpya. Mapendekezo ya Muswada kuhusu Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ni muhimu na yanazua maswali mengi yanayohitaji
mjadala wa kitaifa na maamuzi ya wananchi. Maeneo haya muhimu ni pamoja
na nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano katika mchakato mzima wa
kutengeneza Katiba Mpya.
MAMLAKA YA RAIS
Mheshimiwa Spika,
Kama ambavyo tumepata kusema ndani ya Bunge hili, kwa muda wote wa uhai
wetu kama taifa huru, mfumo wetu wa kikatiba na wa kisiasa umejengwa juu
ya nguzo kuu ya Urais wa Kifalme (Imperial Presidency). Hii inatokana
na ukweli kwamba katika mfumo huu, Rais ana madaraka makubwa sana ya
kiutendaji na ya kiutungaji sheria. Vile vile Rais ana kivuli kirefu cha
kikatiba juu ya mahakama kwa kutumia mamlaka makubwa aliyonayo katika
uteuzi wa viongozi wote wa ngazi za juu za Mahakama. Urais wa Kifalme
ndio chanzo kikuu cha kukosekana kwa uwajibikaji katika ngazi zote za
serikali na ndio kichocheo kikubwa cha rushwa na ufisadi wa kutisha
ambao umefanywa kuwa ni sehemu ya kawaida ya maamuzi ya kiserikali. Sio
vibaya, katika kuthibitisha jambo hili, kurudia maneno ya ibara ya 37(1)
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977: “… Rais atakuwa
huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote….” Na kama
alivyowahi kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwenye mahojiano ya
mwaka 1978 na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), kama Rais wa
Tanzania alikuwa na mamlaka – kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi
yetu – ya kuwa dikteta!
Muswada unaendeleza kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme katika mchakato
wa upatikanaji wa Katiba Mpya. Mtu mwenye mamlaka ya kidikteta, kama
Rais alivyo kwa mujibu wa Katiba ya sasa, hawezi kusimamia upatikanaji
wa katiba ya kidemokrasia. Kwa kutumia mamlaka makubwa ya uteuzi wa Tume
yanayopendekezwa na Muswada huu, ni wazi Rais Kikwete, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa chama tawala cha CCM, atateua wajumbe anaowataka yeye na
Rais Ali Mohamed Shein, Makamu wake na pia Rais wa Zanzibar! Ni wazi
vile vile kwamba watu watakaoteuliwa na Marais hawa ni watu wasiokuwa
tishio kwa status quo kwa maana ya kupendekeza mabadiliko makubwa katika
mfumo wa kikatiba na kiutawala na hivyo kuhatarisha maslahi ya CCM!
Mheshimiwa Spika,
Hali ni hiyo hiyo kwa Sekretarieti ya Tume ambayo ndio chombo cha
kiutendaji na moyo wa Tume yenyewe. Kama Katibu, ambaye ndiye mtendaji
mkuu wa Tume ni mteuliwa wa Rais na ni mtumishi wa Serikali; kama
watendaji wengine wa Tume ni watumishi wa serikali walioteuliwa wa
Waziri ambaye naye ni mteuliwa wa Rais baada ya kukubaliana na Waziri
mwenzake wa Zanzibar; na kama watumishi wengine wa Tume nao ni watumishi
wa Serikali kama inavyopendekezwa na ibara ya 13 ya Muswada Mpya, ni
wazi, kwa hiyo, kwamba mapendekezo haya yote ya uteuzi wa wajumbe,
watendaji na watumishi wengine wa Tume yana lengo moja tu: kuhakikisha
kwamba matokeo ya kazi ya Tume hiyo ni yale tu yanayotakiwa na Rais na
Serikali yake na chama chake cha CCM.
Mheshimiwa Spika,
Badala ya mapendekezo haya ya Muswada Mpya, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inapendekeza utaratibu wa kidemokrasia zaidi katika uteuzi wa
Tume. Kwanza, badala ya Tume hiyo kuwa ‘Tume ya Rais’ kama
inavyopendekezwa katika Muswada, tunapendekeza iwe ‘Tume ya Vyama’
(multiparty Commission) kwa maana moja kubwa: wajumbe wa Tume wateuliwe
kufuatana na mapendekezo na makubaliano ya vyama vya siasa vyenye
uwakilishi Bungeni, vyama vingine vilivyosajiliwa pamoja na mashirika ya
kijamii, taasisi za kitaaluma na za kidini. Hii haina maana kwamba
wajumbe wa Tume hiyo hawatatakiwa kuwa na sifa zilizoainishwa katika
ibara ya 6(3) ya Muswada Mpya. La hasha! Wajumbe wa Tume ya Vyama
watatakiwa kuwa na sifa zozote za kitaaluma zinazotakiwa ili kuwawezesha
kufanya kazi ya kitaalamu kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya.
Pili, baada ya uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Vyama, inapendekezwa kwamba
wajumbe walioteuliwa kwa mashauriano na makubaliano kama
tunavyopendekeza watatakiwa wathibitishwe na Bunge la Jamhuri ya
Muungano. Pendekezo hili litahakikisha kwamba wajumbe wa Tume wanakuwa
vetted na chombo kikuu cha uwakilishi wa wananchi. Hili litajenga
kuaminiana baina ya Serikali, vyama vya siasa, mashirika ya kijamii,
taasisi za kitaaluma na za kidini na litaipa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba uhalali mkubwa wa kisiasa, kitu ambacho ni muhimu katika
mazingira ya sasa ya kisiasa.
Mheshimiwa Spika,
Tofauti pekee na muhimu kati ya pendekezo la Muswada Mpya na pendekezo
letu kuhusu mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa Tume ni locus ya uwajibikaji
wao. Wajumbe wanaoteuliwa na Rais wanakuwa na shinikizo la kutoa
matokeo yatakayompendezesha Rais au chama chake. Wajumbe wanaotokana na
mapendekezo na makubaliano ya wadau wengi na wanaothibitishwa na chombo
cha uwakilishi cha wananchi kama tunavyopendekeza hawawezi kuwa na
shinikizo la kutoa matokeo yatakayompendezesha mmojawapo wa wadau hao.
Faida kubwa na ya wazi ya Tume ya Vyama ni kwamba matokeo ya kazi yake
yana nafasi kubwa zaidi ya kukubaliwa, kuheshimiwa na kutekelezwa na
wadau mbali mbali kuliko matokeo ya kazi ya Tume ya Rais. Kwa lugha
nyingine, kazi ya Tume ya Vyama itakuwa na uhalali wa kisiasa (political
legitimacy) mkubwa zaidi kuliko Tume ya Rais.
Pendekezo hili linawahusu Katibu, watendaji na watumishi wengine wa Tume
vile vile. Kutokana na uzoefu uliotokana na historia yetu na mfumo wetu
wa kiutawala na kikatiba, watumishi wa serikali wamekuwa hawana uhuru
wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia utashi wao na uadilifu wa kitaaluma
bali hufanya maamuzi kwa kuzingatia matakwa ya mabosi wao wa kisiasa.
Hii ni kwa sababu, kisheria na hata kivitendo, watendaji na watumishi
karibu wote wa umma hujiona wanawajibika kwa mamlaka zao za uteuzi,
yaani Rais na/au Waziri. Aidha, watendaji na watumishi hawa wanawajibika
kinidhamu kwa mamlaka zinazoongozwa na watendaji wa Serikali ambao nao
ni wateuliwa wa Rais na kwa hiyo wanakuwa na woga wa kufanya maamuzi
yanayoweza kuhatarisha maslahi ya kisiasa ya Rais na chama tawala.
Kwa sababu hizo, ni muhimu kwa watendaji na watumishi wote wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba wawe huru dhidi ya mashinikizo yoyote ya kisiasa
kutoka kwa Rais na Serikali yake na chama chake. Ili Tume iwe na mamlaka
na uhuru unaohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake na ili
isiingiliwe kweli na mtu au mamlaka yoyote kama inavyosema ibara ya 10
ya Muswada, inabidi mamlaka ya uteuzi yaondolewe katika mikono ya Rais
na/au Waziri ambaye ni mdau mmojawapo tu wa wadau wengi wa mchakato wa
Katiba Mpya. Na namna ya pili ya kuhakikisha uhuru huu unakuwepo ni
kuweka utaratibu wa kuwapata watendaji na watumishi hawa nje kabisa ya
utumishi wa serikali kwa kuweka masharti ya kuwataka waombe kazi,
kufanyiwa usaili na kuteuliwa na jopo la wataalamu walio huru.
Mheshimiwa Spika,
Namna ya tatu ya kuhakikisha uhuru wa Tume katika kutekeleza majukumu
yake ni kuhakikisha wajumbe wake wanapatiwa ulinzi wa ajira zao
(security of tenure) sawa na wanaopatiwa majaji wa Mahakama ya Tanzania
ili kuzuia uwezekano wa wajumbe kuondolewa kwa sababu zisizotokana na
utendaji wao wa kitaaluma au ukosefu wa maadili. Kwa maana hiyo,
mapendekezo ya ibara ya 10 Muswada Mpya juu ya uhuru wa Tume
hayatoshelezi hata kidogo. Hii ni kwa sababu ibara ya 12 ya Muswada
Mpya, ambayo inazungumzia ukomo wa ujumbe wa Tume, haijaweka utaratibu
wowote wa namna ya kushughulikia nidhamu ya wajumbe pale kunapokuwepo
tuhuma za ukiukaji wa Kanuni za Maadili zinazopendekezwa katika ibara ya
12(2) na Jedwali la Pili la Muswada. Kutokuweka utaratibu huu kuna
hatari kubwa kwani, kisheria, mamlaka ya uteuzi huwa ndio mamlaka ya
nidhamu pale ambapo sheria haijaweka utaratibu tofauti wa nidhamu. Hii
ina maana kwamba bila kuweka utaratibu wa kisheria wa nidhamu ya wajumbe
wa Tume, Rais ndiye atakuwa na uwezo wa kuwaondoa madarakani kwa sababu
yeye ndiye aliyewateua!
Mheshimiwa Spika,
Pendekezo letu la tatu linahusu hadidu za rejea. Hapa kuna hoja za aina
mbili. Kwanza, sambamba na pendekezo la kutompa Rais madaraka ya uteuzi
wa wajumbe wa Tume, Rais asipewe mamlaka ya kutoa hadidu za rejea kwa
Tume. Pili, kwa vile – kama inavyopendekezwa katika Muswada Mpya –
hadidu za rejea ni hati ya kisheria inayotakiwa kuzingatiwa na Tume
katika utekelezaji wa majukumu yake, ni muhimu hati hii iwekwe wazi
katika sheria yenyewe badala ya kubakia kuwa siri ya Rais. Watanzania
lazima wajue Tume inapewa majukumu gani ya kisheria. Aidha, wajumbe wa
Tume wenyewe lazima wafahamu wanapewa majukumu gani ya kisheria na
wafahamu kwamba wanatakiwa kufuata matakwa ya sheria na sio maelekezo ya
mtu mmoja hata kama ni Rais wa Kifalme. Hii itasaidia uwajibikaji wa
Tume kwa wananchi kwani itakuwa rahisi kupima matokeo ya kazi ya Tume
kwa hadidu za rejea zilizowekwa wazi katika sheria.
Ukweli ni kwamba badala ya kumsubiri Rais kutoa hadidu za rejea, tayari
ibara za 9 na 16 za Muswada Mpya zimeshafanya hivyo kwa kuainisha kazi
za Tume, mipaka ya Tume katika utekelezaji wa kazi hizo na utaratibu wa
namna ya kuzifanya. Kwa ajili hiyo, zaidi ya kutaka kuonyesha kwamba
Rais ana mamlaka makubwa katika mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba
Mpya, mapendekezo ya ibara ya 8 hayana maana wala sababu yoyote na
yanaweza kuondolewa bila kuathiri maudhui ya Muswada. Aidha, kwa
kuzingatia mapendekezo ya ibara ya 9, haijulikani Rais atatoa maelekezo
gani ya ziada yanayohusu kazi za Tume na namna ya kuzitekeleza. Kwa
upande mwingine, mapendekezo ya ibara ya 8 yanaweza kuleta mkanganyiko
na mgogoro wa kisiasa na kisheria usiokuwa wa lazima endapo Rais atatoa
hadidu za rejea zinazotofautiana na matakwa ya kisheria kama
yanavyopendekezwa na ibara 9 ya Muswada Mpya. Pendekezo letu, kwa hiyo,
ni kwamba ibara ya 8 ifutwe yote na ibara za 9 na 16 zifafanuliwe vizuri
ili kuweka wazi zaidi hadidu za rejea za Tume na namna ya kuzitekeleza.
Mheshimiwa Spika,
Kuna mapendekezo mengine yaliyoko kwenye Muswada yanayoonyesha hatari za
Urais wa Kifalme. Kama tulivyoona, Tume inatakiwa kuwasilisha ripoti
yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na kwa Rais wa Zanzibar. Baada ya
hapo, kwa mujibu wa ibara ya 18(2) ya Muswada, “baada ya mashauriano na
makubaliano na Rais wa Zanzibar na baada ya kumalizika kwa taratibu za
ndani zinazohusu utungaji wa sera, Rais atamwelekeza Waziri kuwasilisha
Muswada wa Katiba katika Bunge la Katiba kwa ajili ya kupitishwa kwa
vifungu vya Katiba.”
Pendekezo hili ni la hatari kubwa. Kwanza, ‘kumalizika kwa taratibu za
ndani zinazohusu utungaji wa sera’ maana yake ni baada ya kukamilika kwa
utaratibu wa kawaida wa kiserikali unaohusu utungaji sera na sheria.
Chini ya utaratibu huu, rasimu ya muswada hupelekwa kwanza kwenye Kamati
ya Watalaam ya Baraza la Mawaziri (Inter Ministerial Technical
Committee of the Cabinet) kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho na Makatibu
Wakuu kabla ya kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa maamuzi ya
mwisho. Baada ya maamuzi ya mwisho ya Baraza la Mawaziri, rasimu ya
muswada hurudishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya
kuandikwa upya ndipo upelekwe Bungeni la Katiba.
Katika hatua zote hizi, muswada wa sheria huweza kufanyiwa marekebisho
makubwa. Kwa maana hiyo, pendekezo la kuuwasilisha Muswada wa Katiba
Mpya katika Bunge la Katiba baada ya kuupitisha kwanza kwa Makatibu
Wakuu ambao wote ni wateuliwa wa Rais, na kwenye Baraza la Mawaziri
ambalo wajumbe wake wote (ukiacha Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar) ni
wateuliwa wa Rais ni kutengeneza mazingira ya kisheria yatakayoruhusu
uchakachuaji wa Muswada huo kwa lengo la kuhakikisha matokeo yake ya
mwisho, yaani Katiba Mpya, yanakidhi maslahi ya Rais na chama chake cha
CCM. Kwa vyovyote vile, pendekezo hili halikubaliki kwa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni.
SIFA ZA WAJUMBE
Mheshimiwa Spika,
Muswada Mpya unapendekeza sifa zifuatazo wanazotakiwa kuwa nazo wajumbe wa Tume:
(a) Uzoefu katika kufanya mapitio ya katiba na sifa za kitaaluma za
wajumbe kwenye mambo ya katiba, sheria, utawala, uchumi, fedha na
sayansi ya jamii;
(b) Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(c) Maslahi ya umma;
(d) Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbali mbali ya kijamii; na
(e) Vigezo vingine ambavyo Rais ataona vinafaa. (ibara ya 6(3)
Zaidi ya sifa zilizotajwa, ibara ya 6(4) inakataza watu wenye sifa zifuatazo kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume:
(a) Wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, madiwani na
viongozi wa vyama vya siasa wa ngazi zote kuanzia Wilaya hadi Taifa;
(b) Watumishi wa vyombo vya usalama;
(c) Watu waliowahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa au wanaotuhumiwa mahakamani kwa mashtaka ya kukosa uaminifu au uadilifu;
(d) Watu wasiokuwa raia wa Tanzania.
Mapendekezo haya yana athari kubwa kwa mchakato mzima wa upatikanaji wa
Katiba Mpya. Kwanza, kwa kukataza viongozi wa ngazi za juu na za kati wa
vyama vya siasa kuteuliwa wajumbe wa Tume kunaondoa kwenye mchakato wa
Katiba Mpya kundi kubwa la watu wenye utaalamu na uzoefu katika masuala
mbali mbali ya kisiasa, kikatiba, kisheria, kiuchumi, kiutawala, kifedha
na kisayansi jamii. Vile vile, viongozi wa vyama vya siasa
wanawakilisha makundi makubwa ya kijamii yenye mtawanyiko wa watu na wa
kijiografia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wanawakilisha
watu wa umri na jinsia zote kama inavyopendekezwa katika Muswada Mpya.
Aidha, kwa kuwa maneno ‘maslahi ya umma’ hayajafafanuliwa katika
Muswada, hakuna anayeweza kudai kwamba viongozi wa ngazi za juu na za
kati wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa kisheria baada ya kutimiza
masharti yote husika ya kisheria, na ambao wanaungwa mkono na mamilioni
ya wananchi wa Tanzania kwa kupewa nafasi za uwakilishi katika taasisi
za uwakilishi za umma kama Bunge, Baraza la Wawakilishi na Halmashauri
za Serikali za Mitaa hawajui wala hawazingatii maslahi ya umma na kwa
hiyo hawafai kuwakilishwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba! Kama
ingekuwa hivyo, Rais – ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM na kwa hiyo
kiongozi wa chama cha siasa – naye pia atakuwa hana sifa za kuteua Tume!
Na wakati haja ya kutoshirikisha watumishi wa taasisi za ulinzi na
usalama katika mchakato wenye ubishani wa kisiasa kama utungaji wa
Katiba Mpya inaeleweka, ni matusi kwa watu waliochaguliwa na wananchi
kuwa Wabunge, Wawakilishi au Madiwani au viongozi wa vyama vya siasa
vilivyowapendekeza watu hao, kuwekwa pamoja na wahalifu na kutamkwa kuwa
hawana sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba!
Inaelekea lengo kuu la pendekezo hili ni kuhakikisha kwamba vyama vya
upinzani, hasa hasa CHADEMA, vyenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya
Bunge havipati fursa ya kuamua muundo na maudhui ya Katiba Mpya hasa
katika hatua muhimu za uundaji wake. Pili, lengo kuu vile vile ni
kuhakikisha kuwa Rais, na kwa hiyo chama chake cha CCM, wanadhibiti
mchakato wa Katiba Mpya katika hatua muhimu ya uundaji wake. Endapo
watafanikiwa katika hili, Rais na chama chake cha CCM watakuwa na nafasi
kubwa ya kuamua aina ya Katiba Mpya itakayotokana na mchakato
walioudhibiti kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya. Hii ni kwa sababu,
kwa kutumia uzoefu wa Tume nyingine zilizopata kuteuliwa miaka ya nyuma,
wajumbe wengi huwa ni watumishi au waliopata kuwa watumishi wa Serikali
na/au taasisi zake. Wajumbe wa aina hii wamekuwa hawana uthubutu wa
kupendekeza mabadiliko makubwa yanayohitajika katika mfumo wa utawala wa
nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Badala ya kukataza viongozi wa vyama vya siasa kama inavyopendekezwa na
Muswada Mpya, na kwa kuzingatia nafasi ya vyama vya siasa katika
historia yetu na mfumo wetu wa utawala, na kwa lengo la kuhakikisha Tume
inakuwa na utaalamu, uzoefu na uhalali wa kisiasa unaohitajika, watu
wanaostahili kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume wawe ni wale wenye sifa
zinazopendekezwa na ibara ya 6(3)(a), (b), (c) na (d) ya Muswada. Kwa
sababu hiyo, hakutakiwi kuwa na vigezo vingine visivyojulikana wazi kwa
wananchi. Kwa maneno mengine, pendekezo la kuwa na ‘vigezo vingine
ambavyo Rais ataona inafaa’ halikubaliki kwani linampa Rais mwanya wa
kuteua marafiki zake au watu ambao hawana sifa zinazojulikana. Kwa maoni
yetu vile vile, badala ya kuwa sababu ya disqualification, uongozi wa
kuchaguliwa na wananchi katika taasisi za uwakilishi au katika vyama vya
siasa unatakiwa kuwa an added advantage pale ambapo kiongozi husika ana
sifa za kitaaluma zinazotakiwa!
MISINGI MIKUU YA KITAIFA
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kuwepo kwa ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ambayo Tume
inatakiwa kuizingatia kwa lengo la kuihifadhi na kuidumisha. Misingi
mikuu inayopendekezwa ni:
(a) Kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano;
(b) Uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama;
(c) Mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
(d) Umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
(e) Uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote kupiga kura;
(f) Ukuzaji na na uhifadhi wa haki za binadamu;
(g) Utu, usawa mbele ya Sheria na mwenendo wa sheria; na
(h) Uhuru wa kuabudu na uvumilivu wa dini nyingine. (ibara ya 9(2)
Kifungu hiki kimefanyiwa mabadiliko kwa kufuta maneno ‘Tume itahakikisha
… kutokugusika na utakatifu (inviolability and sanctity) wa mambo
yafuatayo’ yaliyokuwa katika Muswada wa Zamani, na badala yake yamewekwa
maneno mapya ‘… kuhifadhi na kudumisha mambo yafuatayo….’ Mabadiliko
haya yamefanywa ili kujaribu kuondoa hofu iliyojitokeza wakati wa
mikutano ya kukusanya maoni ya wadau kwamba lengo la pendekezo hilo
lilikuwa kuzuia mjadala juu ya masuala ya kikatiba yenye utata mkubwa
kama vile suala la Muungano. Hata hivyo, hatari ya kuzuiliwa kwa mjadala
juu ya misingi mikuu ya kitaifa bado haijaondolewa kwani, kwa mujibu wa
ibara mpya ya 9(3), “… Tume itatoa fursa kwa watu kutoa maoni yao kwa
uhuru kwa lengo la kuendeleza na kuboresha masuala hayo.” Tafsiri halisi
ya maneno haya ni kwamba mjadala pekee utakaoruhusiwa juu ya ‘misingi
mikuu ya kitaifa’ ni ule ambao lengo lake ni ‘kuendeleza na kuboresha
masuala hayo.’
Kwa maoni yetu, lengo kuu la pendekezo linalohusu kuendeleza na
kuboresha ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ni kuzuia mjadala wenye kuhoji
‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano’ ili kuendeleza mfumo wa sasa wa
Muungano wenye Serikali mbili. Hii ni kwa sababu katika mambo yote
yanayopendekezwa kuwa misingi mikuu ya kitaifa, ni ‘kuwepo kwa Jamhuri
ya Muungano’ yenye Serikali mbili ndio ambayo imekuwa na mgogoro mkubwa
kwa muda wote wa maisha ya Jamhuri ya Muungano. Ukiacha ‘ukuzaji na
uhifadhi wa haki za binadamu’ ambalo lilikataliwa na Serikali ya Mwalimu
Nyerere kwa miaka yote ya utawala wake, mambo mengine yote yanayotajwa
kuwa ‘misingi mikuu ya kitaifa’ hayajawahi kubishaniwa kwa miaka yote ya
uhai wa Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Pendekezo la ‘misingi mikuu ya kitaifa’ linastaajabisha sana kwani, kwa
mujibu wa ibara ya 98(1)(b) ya Katiba ya sasa, ‘kuwapo kwa Jamhuri ya
Muungano, Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya
Kamhuri ya Muungano, kuwapo kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano, madaraka
ya Serikali ya Zanzibar, Orodha ya Mambo ya Muungano na idadi ya Wabunge
kutoka Zanzibar’ ni mambo yanayoweza kubadilishwa na Bunge la Jamhuri
ya Muungano ili mradi tu mabadiliko hayo yaungwe mkono na theluthi mbili
ya Wabunge wote wa kutoka Tanzania Bara na wa Tanzania Zanzibar. Kwa
sababu hiyo, pendekezo la ibara ya 9(3) ya Muswada kwamba ‘misingi mikuu
ya kitaifa’ izungumzwe kwa lengo la kuiendeleza na kuidumisha tu
halikubaliki kwa sababu linazuia uhuru wa kuhoji na/au kupinga mambo
ambayo kwa Katiba ya sasa ni ruhusa kuyahoji, kuyapinga na/au hata
kuyabadilisha! Tunapendekeza ibara ya 9(2) na (3) za Muswada zifutwe
kabisa ili kuwepo na uhuru kamili wa kujadili, kwa kupinga au kuunga
mkono, kila jambo linalohusika na Katiba Mpya.
NAFASI YA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Pengine mabadiliko makubwa yaliyofanywa katika Muswada ni mapendekezo
yanayohusu nafasi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya.
Itakumbukwa kwamba moja ya masuala yaliyozua tafrani kubwa katika
mchakato wa kukusanya maoni juu ya Muswada wa Zamani hasa katika kituo
cha Zanzibar ni kuwepo hisia kwamba nafasi ya Zanzibar ilikuwa imepuuzwa
katika Muswada huo. Muswada sio tu kwamba umetekeleza matakwa yote ya
ushirikishwaji wa Zanzibar, bali umekwenda mbali zaidi kwa kuifanya
Zanzibar mwamuzi wa mustakbala wote wa kikatiba wa Tanzania. Hii
imefanyika kwa njia mbili: kwanza, kwa kumfanya Rais wa Zanzibar kuwa
mshirika sawa wa kikatiba wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; na pili, kwa
kuipa Zanzibar nafasi kubwa ya uwakilishi katika mchakato mzima wa
Katiba Mpya.
NAFASI YA RAIS WA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kwamba utekelezaji wa mamlaka yote ya Rais, Waziri
na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano lazima ufanyike
kwa ‘mashauriano na makubaliano’ na Rais, Waziri au Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar. Kwa mfano, ibara ya 5 inayohusu kuundwa kwa Tume inamtaka Rais
‘kushauriana na kukubaliana’ na Rais wa Zanzibar na kupata ushauri wa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu
wa Zanzibar. Vile vile, ibara ya 6(1) inayohusu uteuzi wa wajumbe wa
Tume; ibara ya 8(1) na (2) inayohusu hadidu za rejea na kuongeza muda wa
Tume; na ibara ya 13(2) inayohusu uteuzi wa Katibu wa Tume, zote
zinataka kuwepo na makubaliano na Rais wa Zanzibar. Aidha, ibara ya
13(5) inayohusu uteuzi wa watendaji wengine wa Tume inalazimu
makubaliano kati ya Waziri na Waziri mwenzake wa Zanzibar ambao nao ni
wateuliwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar.
Mamlaka ya Rais wa Zanzibar hayaishii tu kwenye uteuzi wa wajumbe na
watendaji wa Tume, bali pia yanaingia hata katika uwasilishaji wa ripoti
ya Tume. Kwa mujibu wa ibara 18(1) ya Muswada, mara baada ya kumaliza
kazi yake, Tume itawasilisha ripoti yake kwa Rais na kwa Rais wa
Zanzibar. Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 18(2), mara baada ya kupokea
ripoti hiyo, Rais, ‘baada ya kushauriana na kukubaliana’ na Rais wa
Zanzibar, “… atamuagiza Waziri kuwasilisha Muswada wa Katiba katika
Bunge la Katiba.” Kwa mapendekezo haya pia, Rais wa Zanzibar sio tu
kwamba ana mamlaka karibu sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano bali pia
ana kura ya turufu katika mchakato wa Katiba Mpya. Maana yake ni kwamba
Rais wa Zanzibar asipopatiwa nakala ya ripoti ya Tume au asipokubaliana
na Rais wa Muungano, basi Muswada wa Katiba hautawasilishwa kwenye Bunge
la Katiba!
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo haya yanaashiria kuwepo kwa mtazamo ambao chanzo chake ni
Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri
ya Tanganyika ya tarehe 25 Aprili 1964. Kwa mtazamo huo, Zanzibar ni
nchi huru kama ilivyokuwa mwaka 1964 na kwa hiyo ni lazima sio tu
ishirikishwe kwa usawa, bali pia lazima ikubaliane na mabadiliko yoyote
ya kikatiba yanayopendekezwa na Muswada. Kama Profesa Palamagamba Kabudi
wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alivyosema kwenye
Semina ya Wabunge Juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba
iliyofanyika tarehe 12 Novemba 2011: ‘Katika kuandika katiba mpya, wabia
wa Muungano wanarudi kwa usawa.’
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mtazamo huu sio sahihi. Kwanza kabisa,
Zanzibar sio nchi huru tena kama ilivyokuwa mwaka 1964, kama ambavyo
hakuna tena nchi inayoitwa Tanganyika wala serikali yake. Hii ni kwa
sababu tangu kusainiwa kwa Hati za Muungano mwaka 1964, na kwa mujibu wa
ibara ya 4(3) ya Katiba ya sasa, masuala yote yanayohusu Muungano kama
vile Katiba ya Tanzania yamekasimiwa kwa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano, ambayo pia imekasimiwa mamlaka juu ya masuala ya iliyokuwa
Tanganyika. Masuala haya ya Muungano hayawezi kujadiliwa upya na kwa
usawa kati ya nchi hizi mbili kwa vile moja kati ya nchi hizo haipo tena
na iliyobaki imepoteza sehemu ya uhuru wake kutokana na Muungano huo!
Hii ndio kusema hakuwezi tena kuwa na wabia wa Muungano bila kwanza
kuirudisha Tanganyika kama nchi na bila kuirudisha Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar yenye uhuru na mamlaka kama iliyokuwa nayo kabla ya Muungano!
Pili, kuna dhana kwamba Rais wa Zanzibar hakushirikishwa katika mchakato
wa maandalizi ya Muswada wa Zamani. Dhana hii vile vile ni potofu.
Kwanza, Rais Ali Mohamed Shein mwenyewe ametamka wazi kwa waandishi wa
habari kwamba alishiriki katika hatua zote za maamuzi kwenye Baraza la
Mapinduzi. Pili, mujibu wa ibara ya 54(1) ya Katiba ya sasa, Rais wa
Zanzibar ni mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na kwa hiyo ni mshiriki wa maamuzi yote ya Serikali
hiyo. Kwa maana hiyo, maslahi ya Zanzibar yanawakilishwa ndani ya
‘chombo kikuu cha kumshauri Rais’ katika Jamhuri ya Muungano. (ibara ya
54(3) Hii ni licha ya ukweli kwamba, kwa mlolongo wa madaraka uliopo
katika ibara ya 54(2), Rais wa Zanzibar sio mmoja wa wajumbe wanaoweza
kuongoza mikutano ya Baraza hilo.
Aidha, ndani ya Baraza la Mawaziri, Zanzibar inawakilishwa pia na Makamu
wa Rais ambaye – kwa mujibu wa ibara ya 47(1) ya Katiba ya sasa – “…
ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano….”
Kwa maana hiyo, mapendekezo ya Muswada yanayomfanya Rais wa Zanzibar
kuwa sio tu mshiriki sawa lakini pia mwamuzi wa mustakbala wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano yanaenda kinyume sio tu na Katiba ya sasa bali pia
na Hati za Muungano wenyewe. Kwa mapendekezo haya, endapo Rais wa
Zanzibar hatakubaliana na uteuzi wowote wa wajumbe wa Tume au Katibu
wake au watendaji wake wengine, anaweza kusimamisha mchakato mzima wa
kikatiba hata kama unahusu masuala ya Tanzania Bara yasiyo ya Muungano!
UWAKILISHI WA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Ushawishi mkubwa wa Zanzibar hauishii katika kura ya turufu aliyo nayo
Rais wa Zanzibar pekee yake. Zanzibar ina ushawishi mkubwa vile vile
kutokana na nafasi kubwa iliyo nayo katika vyombo vya maamuzi
vinavyopendekezwa na Muswada. Kwa mfano, kwa mujibu wa ibara ya 6(2), “…
muundo wa Tume utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa
kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.” Hii ina maana kwamba wajumbe wa
Tume na Sekretarieti yake wanatakiwa wawe sawa kwa sawa kati ya
Tanzania Bara na Zanzibar. Ikumbukwe kwamba Tume hii inatengeneza Katiba
inayohusu masuala ya Muungano, ambayo ni haki kwa Zanzibar
kushirikishwa kwa usawa kabisa, na vile vile masuala yasiyokuwa ya
Muungano ya Tanzania Bara ambayo Zanzibar haina haki ya kushiriki.
BUNGE LA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Eneo la pili ambalo Zanzibar ina ushawishi mkubwa kutokana na uwakilishi
wake ni katika Bunge la Katiba linalopendekezwa katika Sehemu ya Tano
ya Muswada. Kwa mujibu wa ibara ya 20(2), wajumbe wa Bunge la Katiba
watakuwa ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano; wajumbe wote
wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar; mawaziri wa katiba na sheria wa
Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar; Wanasheria Wakuu wa Jamhuri ya
Muungano na wa Zanzibar; na wajumbe mia moja kumi na sita wakaoteuliwa
kutoka asasi zisizokuwa za kiserikali, asasi za kidini, vyama vya siasa
vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu na makundi yenye
mahitaji maalum katika jamii. Inaelekea kwamba, kwa mujibu wa ibara ya
20(4), wajumbe wasiokuwa wabunge ama wawakilishi nao pia watateuliwa na
Rais licha ya kutoka nje ya mfumo wa kiserikali!
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(a) ya Katiba ya sasa ya Muungano, wajumbe
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ni pamoja na wabunge wa majimbo ya
uchaguzi. Kwa composition ya sasa ya Bunge, kuna jumla ya majimbo ya
uchaguzi 239 ambayo kati yao majimbo ya Zanzibar ni hamsini. Vile vile,
kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(c) ya Katiba, Baraza la Wawakilishi
Zanzibar linawakilishwa na wabunge watano katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano. Aidha, kama inavyotakiwa na ibara ya 66(1)(b), kuna wabunge
wanawake mia moja na mbili wanaojulikana kama ‘wabunge wa viti maalum.’
Kwa mgawanyo wa sasa wa wabunge hawa, idadi ya wanaotoka Zanzibar ni
ishirini na tano kwa vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni. Na mwisho,
kuna wabunge wasiozidi 10 wanaoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(e). Hadi sasa, Rais ameshateua wabunge
watatu ambao wote ni wa kutoka Zanzibar. Kwa hiyo, katika Bunge la sasa
lenye wabunge 353, wabunge wanaowakilisha Zanzibar ni themanini na tatu
au karibu 23.5% ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Tano ya Katiba ya Zanzibar,
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ni pamoja na wawakilishi wa
majimbo hamsini ya uchaguzi, wawakilishi kumi wa kuteuliwa na Rais wa
Zanzibar na wawakilishi ishirini wa viti maalum na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa hiyo, jumla ya wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi kwa sasa ni themanini na moja. Kwa maana nyingine ni
kwamba endapo mapendekezo ya ibara ya 20(1)(b), (c) na (d) ya Muswada
yatakubaliwa, idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotoka Zanzibar
itaongezeka hadi kufikia mia moja sitini na nne kati ya wajumbe 545 wa
Baraza hilo kwa mujibu wa ibara ya 20(2). Idadi hii ni sawa na 30% ya
wajumbe wote wa Bunge la Katiba.
Idadi hiyo ya uwakilishi wa Zanzibar bado haitakidhi matakwa ya Muswada
kwani ibara ya 20(3) inapendekeza kwamba “… idadi ya wajumbe wa Baraza
la Katiba kutoka Tanzania Zanzibar … haitapungua theluthi moja ya
wajumbe wote wa Bunge la Katiba”! Theluthi moja ya wajumbe wa Bunge la
Katiba ni wajumbe 182. Kwa hiyo ili kukidhi matakwa ya Muswada kuhusu
uwakilishi wa Zanzibar, itabidi wajumbe 18 kati ya 116 waliotajwa na
ibara ya 20(2)(e) watoke Zanzibar ili kufikisha idadi ya wajumbe 182
ambayo ndio theluthi moja ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba.
Mheshimiwa Spika,
Kuna maeneo mengine ya Muswada ambayo pia yanazua maswali mengi juu ya
nafasi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Kwa mfano, wakati
ibara ya 21(1) inapendekeza kwamba Spika na Naibu Spika wa Bunge la
Katiba wachaguliwe kutoka miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo, ibara ya
21(2) inapendekeza kwamba endapo Spika atatoka upande mmoja wa Jamhuri
ya Muungano basi Naibu wake lazima atoke upande mwingine. Sambamba na
pendekezo hili, ibara ya 22(1) inapendekeza Makatibu wa sasa wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano na wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar watakuwa ndio
Katibu na Naibu Katibu wa Bunge la Katiba. Aidha, sawa na ibara ya
21(2), ibara ya 22(2) inapendekeza kwamba endapo Spika atatoka upande
mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Katibu wa Bunge la Katiba lazima
atoke upande mwingine.
Mapendekezo haya yanaonyesha sio tu nafasi na ushawishi mkubwa wa
Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya, bali pia ni mwendelezo wa dhana
potofu kwamba Zanzibar ni mshirika sawa wa Jamhuri ya Muungano. Hii
inathibitishwa pia na pendekezo la ibara ya 24(3) ya Muswada inayotaka
Katiba Mpya ikubaliwe na theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge la Katiba
wanaotoka Tanzania Bara na vile vile theluthi mbili ya wajumbe wanaotoka
Zanzibar. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba iwe ni kwa masuala ya Muungano
yanayoihusu Zanzibar pia, au kwa masuala yasiyokuwa ya Muungano ya
Tanzania Bara ambayo hayaihusu, Zanzibar itakuwa na kura ya turufu kwa
mujibu wa mapendekezo ya Muswada huu.
Mheshimiwa Spika, Uwakilishi mkubwa wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri
ya Muungano umetumika kihistoria kwa lengo la kuwatuliza Wazanzibari
wakati Serikali ya Mwalimu Nyerere ilipokuwa inamomonyoa uhuru wa
Zanzibar kwa kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano kwenye Katiba ya
Muungano. Katika kitabu chake Pan Africanism or Pragmatism? Lessons of
Tanganyika – Zanzibar Union, Profesa Issa Shivji, mwanazuoni mashuhuri
wa kikatiba na mwanafunzi wa historia ya Muungano huu amemnukuu
aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati wa utawala wa hayati
Sheikh Abedi Amani Karume, Bw. Wolfgang Dourado akimnukuu Sheikh Karume
juu ya nafasi ya Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano: “‘Msiwe
na wasi wasi, sisi tuna haki ya kuwakilishwa katika Bunge lao lakini wao
hawana haki ya kuwakilishwa katika Baraza letu la Mapinduzi’”!
Mheshimiwa Spika,
Sababu nyingine inatokana na kuongezeka kwa ushawishi na nafasi ya
Zanzibar katika siasa za ndani ya CCM, hasa hasa katika zama hizi za
vyama vingi na vita za makundi mbali mbali ndani ya chama hicho. Katika
mazingira haya, mtu yeyote anayetaka kupitishwa kuwa mgombea urais kwa
kupitia CCM anakuwa anahitaji kura za CCM Zanzibar ili kushinda katika
kinyang’anyiro hicho. Kwa kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere
mwenyewe katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, “sababu
moja kubwa iliyofanya viongozi wetu wasitake kuwaudhi ‘Wazanzibari’ …
ni umuhimu wa kura za Zanzibar katika kumteua mwanachama wa CCM kuwa
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa kiongozi yeyote anayeliona
jambo hilo kuwa ni muhimu kupita mengine yote, kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ni
dhambi ambayo haina budi iepukwe kwa kila njia.” Kwa maoni ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, hofu hii ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ndio
imepelekea kimya kikuu – ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano – juu ya ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano
uliofanywa na Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, 2010.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba upendeleo wa Zanzibar
unaopendekezwa katika Muswada huu kuhusiana na uwakilishi katika Bunge
la Katiba na katika vyombo vingine vya maamuzi juu ya mchakato wa Katiba
Mpya sio wa haki na haukubaliki tena. Kwanza, ibara ya 64(2) ya Katiba
ya sasa inaweka wazi kwamba Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina mamlaka
ya kutunga sheria katika Zanzibar ‘… juu ya mambo yote yasiyo mambo ya
Muungano….’ Hii pia ndio lugha ya ibara ya 78(1) ya Katiba ya Zanzibar
kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka jana. ‘Katiba ya Tanzania’ ni jambo
la kwanza katika orodha ya Mambo ya Muungano iliyoko kwenye Nyongeza ya
Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwa Muswada Mpya kupendekeza
kwamba Baraza la Wawakilishi Zanzibar liwe sehemu ya Bunge la Katiba ni
kukiuka wazi wazi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ya Katiba
ya Zanzibar. Ni ajabu iliyoje kwamba wale wanaojifanya ni machampioni wa
Muungano wanaweza kunyamazia ukiukaji huu wa Katiba!
Mheshimiwa Spika,
Thomas Paine, mwandishi maarufu wa Marekani ya wakati wa Mapinduzi ya
mwaka 1776, aliwahi kuandika kijitabu alichokiita Common Sense juu ya
uhalali wa Uingereza kutawala Bara la Amerika ya Kaskazini ambako
alisema: ‘… [T]here is something very absurd in supposing a continent to
be perpetually governed by an island [for] in no instance hath nature
made the satellite larger than its primary planet…’! Yaani, ni ujinga
kudhani kwamba bara linaweza kutawaliwa milele na kisiwa kwa sababu
utaratibu wa asili haujawahi kufanya kitegemezi kuwa kikubwa kuliko
sayari yake ya msingi. Hata kama ni kweli kwamba Tanganyika sio bara
kama ilivyokuwa Marekani ya Kaskazini, bado tunakubaliana na Tom Paine
kwamba ni ujinga kudhani kwamba Visiwa vya Zanzibar vitaendelea kuwa na
maamuzi na ushawishi mkubwa katika masuala yasiyokuwa ya Muungano ya
Tanganyika kwa sababu utaratibu wa asili haujawahi kufanya maslahi ya
Visiwa hivyo kuwa bora zaidi ya maslahi ya Tanganyika!
Kwa maoni yetu, wakati umefika kwa Muungano kuwekwa kwenye msingi wa
usawa na imara zaidi. Msingi huo unahitaji kurudishwa tena kwa Serikali
ya Tanganyika ambayo ndio ilikuwa – pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar – mbia mkuu wa Muungano wa mwaka 1964. Kurudishwa huko kwa
Tanganyika kutaiwezesha Zanzibar kujadiliana nayo kwa usawa juu ya
masuala yote yanayohusu Muungano. Haya yote yanawezekana tu endapo
Muungano huu utawekwa mbele ya wananchi ili waamue – kwa kura ya maoni –
kama wanataka kuendelea nao au la; na kama wanataka kuendelea nao ni
muundo gani wa Muungano wanaoutaka.
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya kurudishwa kwa Tanganyika na Serikali
yake sio mapya. Miaka ishirini iliyopita, Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama
Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa (Tume ya Nyalali) ilipendekeza hivyo
hivyo. Miaka saba baadae, Tume ya Kukusanya Maoni Juu ya Katiba, White
Paper Na. 1 ya 1998 (Tume ya Kisanga) nayo ilipendekeza hivyo hivyo.
Kuendelea kupuuza mapendekezo haya wakati Zanzibar inavunja Katiba ya
sasa ya Muungano; kuendelea kukaa kimya kwa hofu ya kuwaudhi
‘Wazanzibari’ wakati wao wanajitwalia uhuru wa kujiamulia mambo yao
wenyewe huku wakiendelea kushiriki katika maamuzi ya mambo ya Tanganyika
yasiyokuwa ya Muungano; kuendeleza kile alichokiita Mwalimu Nyerere
falsafa ya ‘changu ni changu, chako ni chetu’ katika mahusiano ya
Zanzibar na Tanzania Bara, ni kutulazimisha tuipinge dhana nzima ya
Muungano kati ya nchi zetu mbili kitu kinachoweza kupelekea kuvunjika
kwa Muungano wenyewe. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni isingependa tufike
huko lakini ndoa hii ya kulazimishana haiwezi ikadumu muda mrefu kwa
taratibu za aina hii.
UDHOOFISHAJI WA UPINZANI
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya Muswada juu ya uwakilishi katika Bunge la Katiba yana
athari nyingine kubwa katika majadiliano na maamuzi ndani ya Bunge la
Katiba. Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na Profesa Issa G. Shivji kwa
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, endapo mapendekezo ya ibara ya
20(2) ya Muswada yatapitishwa, CCM itakuwa na kati ya wajumbe 350 hadi
400 katika Bunge la Katiba ambalo lina wajumbe 545. Kwa upande mwingine
Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kina Wawakilishi 29 katika Baraza la
Wawakilishi Zanzibar kitakuwa na wajumbe 65 katika Bunge la Katiba. Kwa
maana ya uwakilishi katika Bunge la Katiba, CUF itakuwa ndio chama cha
pili kwa nguvu za kisiasa ndani ya Bunge hilo, licha ya kuwa na wabunge
wawili tu wa kuchaguliwa kwa upande wa Tanzania Bara na licha ya kupata
kura chache sana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Na kama inavyojulikana, tangu Muafaka wa Kisiasa Zanzibar kati ya CCM na
CUF wa mwaka 2010 na kuzaliwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa,
upinzani wa kisiasa Zanzibar umekufa na kwa upande wa Tanzania Bara, na
hasa Bungeni na kwenye chaguzi ndogo kama ule wa Igunga, CUF imekuwa
ikishirikiana na CCM kuipinga CHADEMA. Kwa mapendekezo haya, kambi ya
CCM na CUF katika Bunge la Katiba inaweza kufika hata zaidi ya wajumbe
465 katika ya wajumbe 545 wa Bunge hilo! CHADEMA ambayo kwa sasa ndio
chama kinachoongoza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutokana na matokeo
ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, itabakia na Wabunge wake 48 na vyama vya
kibunge vilivyobaki, yaani NCCR-Mageuzi, TLP na UDP vitabaki na jumla ya
Wabunge sita. Kwa hiyo, CHADEMA itakuwa chama cha tatu kwa nguvu za
kisiasa ndani ya Bunge la Katiba licha ya kuwa ni chama kikuu cha
upinzani chenye nguvu na ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini!
Kwa maana nyingine, iwe ni kwa makusudi au bila ya kujua au kwa kunuia,
athari mojawapo kubwa ya mapendekezo ya Muswada kuhusu uwakilishi katika
Bunge la Katiba itakuwa ni kuiongezea nguvu zaidi kambi ya CCM/CUF na
kupunguza nguvu na ushawishi wa CHADEMA ambayo ndio chama pekee
kinachobeba matarajio na matamanio ya Watanzania wengi wanaotaka
mabadiliko ya kimsingi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu.
Haihitaji kuwa na shahada ya uzamivu kujua kwamba Bunge la Katiba lenye
uwakilishi wa aina hii litapitisha Katiba Mpya ambayo pengine
itatofautiana na Katiba ya sasa kwa jina tu! Na wala haihitaji kisomo
kikubwa kujua kwamba Bunge la Katiba la aina hii halitagusa ‘msingi
mkuu’ uliobaki wa Jamhuri ya Muungano, yaani Serikali mbili. Hapa pia ni
wazi kuwa lengo halisi la mapendekezo haya ni kuhakikisha kwamba
mchakato wa Katiba Mpya utazaa matunda yasiyokuwa tofauti sana na ya
Katiba ya sasa!
‘UWAKILISHI’ WA BUNGE LA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Sio Bunge hili tukufu la Jamhuri ya Muungano wala Baraza la Wawakilishi
Zanzibar lenye mamlaka kikatiba na kisiasa ya kutunga Katiba Mpya ya
Tanzania. Hii ni kwa sababu sisi wote tulioko humu ndani tulichaguliwa
kwa mujibu wa Katiba ya sasa na mamlaka yetu yote yako ndani ya kona nne
za Katiba hiyo. Kama ni kweli, kama anavyodai Profesa Kabudi, kwamba
kitendo cha kutunga Katiba Mpya vile vile ni kitendo cha kuua Katiba ya
Zamani, basi sisi Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar hatuna mamlaka ya
kuiua Katiba ya sasa kwa sababu sisi wote tulikula kiapo cha kuilinda,
kuihifandhi na kuitetea.
Pili, sisi sote ni Wabunge na Wawakilishi wa vyama vya siasa kwa sababu,
kwa mujibu wa Katiba ya sasa sheria zote husika, tumechaguliwa kwa sifa
kuu ya kuwa wanachama wa, na tuliopendekezwa na, vyama vya siasa.
Kuligeuza Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar
kuwa Bunge la Katiba ni sawa na kusema kwamba wasiokuwa wanachama wa
vyama vya siasa hawana haki ya kushiriki katika kutunga Katiba Mpya kwa
sababu ya kuwa na kilema cha kisheria kinachowakataza kuchaguliwa kuwa
Wabunge na Wawakilishi! Ibara ya 20(4) ya Katiba ya sasa inatamka wazi
kwamba “… ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama
chochote….” Sio kosa, kwa hiyo, kwa mamilioni ya Watanzania ambao
wameamua kwa hiari zao kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni haikubaliani, na haiwezi kukubali, ubaguzi wa
aina hii dhidi ya Watanzania walioamua kutumia haki zao za kikatiba ya
kutokujiunga na chama chochote cha siasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni haitakubali Watanzania hao waadhibiwe kwa kunyimwa kushiriki
katika Bunge la Katiba kwa sababu tu ya kutokuwa wanachama wa vyama vya
siasa.
Tatu, wajumbe 116 wanaopendekezwa kuteuliwa kwenye Bunge la Katiba kwa
mujibu wa ibara ya 20(2)(e) na (4) ya Muswada Mpya sio, na hawawezi
kuwa, wawakilishi wa wananchi. Kwanza, hawajachaguliwa na mtu yeyote na
wala taasisi zao kuwawakilisha katika Bunge la Katiba kwa sababu Muswada
Mpya unapendekeza wateuliwe na Rais. Pili, Bunge la Katiba ni chombo
cha uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi na kwa mila na desturi
zinazokubalika na kutumika kimataifa, wajumbe wa Bunge la Katiba
huchaguliwa moja kwa moja na wananchi bila ya kujali vyama vya siasa na
huwa na kazi moja tu: kutunga Katiba Mpya. Kwa sababu zote hizi,
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza wajumbe
wa Bunge la Katiba wachaguliwe moja kwa moja na wananchi na kusiwe na
masharti yoyote kuhusu uanachama wa vyama vya siasa.
UHALALISHAJI WA KATIBA MPYA
Mheshimiwa Spika,
Muswada una mapendekezo ambayo yanaashiria kuachana na utaratibu wa
kihistoria wa utungaji wa Katiba ambao umewaweka wananchi kando katika
michakato wa kikatiba tangu miaka ya mwanzo ya uhuru. Kwa mujibu wa
ibara ya 27(1), kutakuwa na kura ya maoni kwa lengo la kuihalalisha
Katiba Mpya. Kwa mujibu wa ibara ya 30, watu wote walioandikishwa kuwa
wapiga kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Taifa na Sheria ya
Uchaguzi ya Zanzibar, watakuwa na haki ya kupiga kura katika kura hiyo
ya maoni. Aidha, kufuatana na ibara ya 32(2), matokeo ya kura ya maoni
yataamuliwa kwa msingi wa kuungwa mkono kwa zaidi ya 50% ya kura zote
zilizopigwa Tanzania Bara na kiasi hicho hicho kwa Zanzibar.
Mapendekezo ya ushirikishwaji wa wananchi katika kuipa Katiba uhai wa
kisheria ni jambo la maana sana na linaonyesha kuwa tumeanza kuachana na
urithi wa kikatiba wa kikoloni ulioanza na Katiba ya Uhuru ya mwaka
1961. Hata hivyo, mapendekezo haya yamejaa mitego na vichaka vingi vya
hatari. Kwanza, ibara ya 27 inapendekeza kwamba kura ya maoni
itaratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana
na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Tume hizi mbili – kwa mashauriano na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu
wa Zanzibar – ndizo zitakazotengeneza swali litakaloulizwa kwenye kura
ya maoni. (ibara ya 28(1) na (2) Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 31,
utaratibu utakaotumika katika kura ya maoni ni ule unaotumika katika
chaguzi za kawaida katika nchi yetu, yaani Sheria ya Uchaguzi wa Taifa,
Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 na Sheria ya
Uchaguzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia kauli yake ndani ya Bunge hili
wakati wa kujadili Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria
tarehe 24 Agosti, 2011: “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina imani,
sio tu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, bali pia na mfumo mzima wa kisheria
na kitaasisi unaoendesha chaguzi za nchi yetu. Mfumo huu na watendaji
wake wameonyesha wazi kutokuwa huru na kutumiwa na Chama cha Mapinduzi
kuchakachua matokeo ya chaguzi mbali mbali hapa nchini. Kwa maana hiyo,
Tume ya Uchaguzi ya Taifa, na ile ya Zanzibar, haiwezi kuachiwa jukumu
kubwa la kuendesha kura ya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya. Kambi
Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Serikali ilete bungeni muswada wa
mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba na ya sheria husika za uchaguzi kwa
lengo la kuiunda upya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha
inasimamia zoezi la kura ya maoni kwa uhuru na bila upendeleo kwa chama
tawala.”
Kuna maeneo mengine ambayo nayo yanaonyesha kwamba lengo halisi la
Muswada huu ni kupata Katiba ambayo haitabadilisha mambo ya msingi ila
itakuwa mpya kwa jina tu. Kwanza, ibara ya 26(2) inapendekeza kumpa Rais
mamlaka ya “kuliitisha tena Bunge la Katiba lenye wajumbe wale wale
siku zijazo kwa ajili ya kutunga masharti ya katiba kabla ya kuizindua
Katiba inayopendekezwa kwa lengo la kurekebisha masharti yaliyomo kwenye
Katiba iliyopendekezwa.” Maana halisi ya maneno haya ni kwamba Rais
atakuwa na mamlaka ya kuita tena Bunge la Katiba ili lifanye marekebisho
ya mambo ambayo yeye au serikali yake au chama chake hawayapendi katika
Katiba Mpya kabla haijapigiwa kura ya maoni na wananchi! Kama chombo
huru cha wananchi, Rais hawezi kujipa madaraka ya kupingana na kauli ya
wananchi kupitia Bunge la Katiba.
Pili, wakati ibara ya 32(3) inapendekeza kurudiwa kwa kura ya maoni
endapo kura za ‘NDIYO’ na ‘HAPANA’ zitalingana, ibara ya 32(4)
inaelekeza kwamba “endapo wingi wa kura ya maoni utakuwa ni ‘HAPANA’,
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, itaendelea kutumika.”
Endapo pendekezo hili litapitishwa na kuwa sheria, hii itakuwa ni
kualika maasi kwa vile, kwa vyovyote vile, wananchi wa Tanzania – baada
ya kupitia mchakato mrefu wa kutengeneza Katiba Mpya – hawatakubali tena
kuvishwa minyororo ya Katiba ya sasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inapendekeza kwamba badala ya kurudi kwenye status quo ante kama
inavyopendekezwa, mchakato wa Katiba Mpya uanze tena hadi hapo
utakapopatikana muafaka wa kitaifa wa katiba.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 ni Muswada muhimu kuliko
pengine miswada yote ambayo Bunge la Kumi litapata fursa ya kuijadili
na kuipitisha. Ni muswada wa kihistoria kwa vile, tangu uhuru wa
Tanganyika miaka hamsini iliyopita, na tangu Muungano miaka karibu
arobaini na nane iliyopita, Watanzania hatujawahi kupata fursa ya
kujadili na kuamua mustakbala wa taifa letu kikatiba kwa utaratibu kama
unaopendekezwa katika Muswada huu. Hata hivyo, kwa jinsi ambavyo Muswada
huu ulivyoandaliwa na kwa maudhui yake na kwa jinsi ulivyoletwa Bungeni
kwa kukiuka makusudi Kanuni za Bunge, ni wazi – kama utapitishwa jinsi
ulivyo – Watanzania tutakuwa tumekosa fursa ya kuamua mustakbala wa
taifa letu kwa njia ya amani na maridhiano. Bunge hili tukufu lina
wajibu mbele ya historia na kwa vizazi vya sasa na vijavyo, kuhakikisha
kwamba tunapata muafaka wa kitaifa juu ya Tanzania tunayoitaka. Hukumu
ya historia, endapo Bunge hili tukufu litaendekeza ushabiki wa kisiasa
na kufanya maamuzi ya mambo makubwa kama haya kwa kupiga kelele au kwa
kuzomea au kwa kugonga meza kwa nguvu, itakuwa ni kali sana. Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni haiwezi kuwa sehemu ya maamuzi makubwa kama
yanayopendekezwa na Muswada huu bila kwanza wananchi wa Tanzania na
Wabunge wenyewe kupata muda wa kutosha wa kuyatafakari masuala haya yote
kwa uzito unaoyastahili na kuyafanyia maamuzi ya busara.
Kwa sababu hizi zote, Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja chini ya
kanuni ya 86(3)(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge hili tukufu kwamba Bunge
hili likatae Muswada huu Kusomwa Mara ya Pili kwa sababu Serikali
imeleta Muswada Mpya na wenye mabadiliko makubwa na ya msingi bila
kufuata masharti ya kanuni ya 84(3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge; na pia
kwa sababu Serikali haijatekeleza maagizo ya Bunge hili tukufu kuhusu
kutoa muda zaidi kwa Kamati na wananchi kuufikiria, kuuelewa na kuutolea
maoni Muswada huu kinyume na matakwa ya ibara ya 18(a) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano juu ya uhuru wa wananchi kutoa maoni yao; ibara ya
21(1) na (2) juu ya haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wan
chi, na haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi
juu ya mambo yanayowahusu wananchi, maisha yao au yanayolihusu Taifa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
—————————————————————
Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB)
MSEMAJI, KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
&
WAZIRI KIVULI, KATIBA NA SHERIA